Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze mchango wangu kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema aliyenijalia afya njema hata siku ya leo nikawepo hapa. Pia, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kulijenga Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu nimeingia hapa Bungeni, mchango wangu mkubwa katika michango mingine ambayo nimekuwa nikichangia, kwa kiasi kikubwa nimekuwa nikichangia sekta hii ya ardhi. Kwa nini sekta ya ardhi? Kwa sababu ya umuhimu wake kwa Taifa letu. Nimeamua kugawanya michago yangu hapa Bungeni, tangu nilipoanza mpaka nitakavyomaliza Ubunge wangu kwa kipindi hiki cha miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimegawanya michango yangu hasa kwenye sekta ya ardhi kwa mfumo wa episode. Nilikuwa na episode one, ikaja episode two na hii sasa ni episode three. Hii inatokana na namna ya Mawaziri kwenye sekta hiyo wanavyobadilishwa. Episode one, episode two, sasa nakwenda kwenye episode three, yuko kaka yangu Mheshimiwa Jerry Silaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee maneno ya Hayati Baba wa Taifa. Alisema maneno haya, wengi wamezungumzia fedha, fedha, fedha. Baba wa Taifa alisema fedha siyo msingi wa maendeleo, bali fedha ni matokeo ya maendeleo. Baba wa Taifa aliendelea kusema kwamba nchi yoyote ili iweze kuendelea duniani; nchi yoyote iliyopiga hatua za maendeleo na inayotaka kupiga hatua za maendeleo, jambo la kwanza lazima liwe na ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina ardhi yenye kilomita za mraba takribani 945,000. Ardhi tunayo ambayo hatuitumii ipasavyo. Jambo la pili, watu tunao idadi ya takribani Watanzania milioni 60. Jambo la tatu ni uongozi bora na la mwisho, siasa safi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza haya kabla sijaenda kwenye mchango wangu, lengo ni kwamba nataka nitoe darasa kidogo hapa. Marcus Garvey alisema, ukitia hofu au shaka kwenye jambo lolote ambalo unataka kulifanya, umeshindwa. Changamoto tuliyonayo sisi kama Watanzania hasa Serikali, ni fikra (mindset), kwamba tunachowaza siku zote ni kwamba tutashindwa, tusaidiwe, tunashindwa. Nchi yetu inaweza kufanya kila kitu. Changamoto ni fikra. Jambo la pili ni commitment. Hali ya utayari wa kuamua kufanya jambo na mwisho ni uzalendo. Tulio wengi Watanzania hasa tuliokuwa kwenye majukumu haya ya nchi yetu, sio wazalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia hapa na nitaanza na hoja ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Ili uweze kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, lazima uwe na mpango kabambe (master plan). Nilikuwa nafuatilia takwimu za sekta ya ardhi nchi nzima na sina hakika sana kama ni kweli zimefika, naambiwa katika halmashauri zote 184, kuna Master Plan 25, sina hakika sana. Katika hizi 25 ambayo nina uhakika ambayo imetekelezwa kwa asilimia kama 90, ni Dodoma, lakini hizi 24 zote hazijatekelezwa. Mfano mzuri ni Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam is a squatter city, na hatuwezi tena, tumeshachelewa. Ili uipange Dar es Salaam na kuipima, ni lazima tuache miradi yote ya maendeleo kwenye bajeti ya mwaka mzima wa fedha, shilingi trilioni zote 15 ziende Dar es Salaam, ndiyo uipange Dar es Salaam. Tumeshashindwa, sasa tusishindwe na mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaenda taratibu, kwa sababu tulitaka tuivunje Vingunguti yote, uvunje ile Buguruni yote, yaani uivunje Manzese sijui wapi kote. Sasa hiyo kitu, na Baba Askofu hapa anatusaidia. Kwa hiyo, Dar es Salaam twende taratibu, tumeshachelewa na hili siyo kosa lenu, ni jambo lamuda mrefu sana, huko nyuma hatukuanza vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia hapa, Mheshimiwa Askofu Gwajima ameeleza kwa habari ya takwimu za vijiji ambavyo vimepimwa na kadhalika. Tuna vijiji takribani 12,318. Katika vijiji hivi vilivyopimwa kwa maana vimepangwa kwa utaratibu mzuri wa ardhi ni takribani 3,681. Nikafanya hesabu ndogo tu, Tume ya Taifa ya Mipango na matumizi bora ya ardhi inasema, inaweza kupima kila Kijiji kimoja kwa Shilingi milioni 15. Hesabu ya kawaida tu ya kujumlisha na kutoa, katika vjiji vilivyobaki 8637 ukizidisha kwa milioni 15, tunahitaji tuipelekee Tume shilingi bilioni 129.5 tu kumaliza kazi ya vijiji vyote. Leo hii mnawapelekea shilingi bilioni mbili, bilioni nne, hii safari ni ndefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, (Naibu Waziri unanisikiliza, wewe ni mtu rahimu sana, ndiyo maana nikasema leo nitakuwa lenient kidogo). Ukipeleka hizi fedha, shilingi bilioni 129 Tume, zile fedha shlingi bilioni 345, mimi mpaka leo nasikitika, au sipati usingizi, hivi zile hela jamani! Tumwombe kibali Mheshimiwa Rais. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani sana naku-address wewe. Naiomba Wizara ya Ardhi imwombe kibali Mheshimiwa Rais kubadilisha mpango wa matumizi ya fedha zile za mkopo wa Benki ya Dunia shilingi bilioni 345 waje kwenye mipango yenye tija. Wewe unapeleka shilingi bilioni 47 kwenye dharura kweli, katika nchi hii ambayo haijapimwa! Sijui, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri ambaye nadhani anasikia, naomba umshauri aende kwa Mheshimiwa Rais aombe kibali, inawezekana. Kubadilisha mpango wa shilingi bilioni 345 waje na mpango wa kupima nchi yetu, inawezakana. Ndiyo maana nikasema ni mindset, commitment na uzalendo that is all, hamna kitu kingine. Hatuhitaji zaidi ya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilieleze hapa ni eneo la kukosekana kwa uratibu mzuri wa sekta ya ardhi na TAMISEMI. Mheshimiwa Waziri TAMISEMI yupo na ningependa unisikilize kaka yangu. Tume-paralyze sekta ya ardhi sisi wenyewe. Leo hii ukisoma Sheria ya Mipango Miji (Na. 8) ya mwaka 2007, inatambua mpaka leo mamlaka ya upangaji ni halmashauri, na tumevunja sheria. Bunge hili hatukuwahi kufanya mabadiliko ya Sheria ya Mipango Miji kukabidhi kazi kwa Wizara ya kisekta. Hatukuwahi Bunge hili, and I stand to be corrected. Ilikuja tu hapa Kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie tu, unajua ni kwa nini? Ah, bwana wee, siwezi kusema zaidi, Mheshimiwa Naibu Waziri ukinitafuta na wenzako nitawasaidia. Alitokea mtu mmoja akaenda kushawishi kwamba unajua hawa Madiwani hawana uwezo wa kuwasimamia watumishi wa ardhi, niletee mimi huku; lakini hakukuwa na nia njema kwa Taifa letu. Ukifanya hivi, maana yake unapoka majukumu ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili nadhani Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI akishirikiana na Waziri wa Ardhi, hebu mtengeneze hapa hii mifumo isomane; sekta ya ardhi na TAMISEMI. Kwa mfano, leo hii Mkurugenzi wa Halmashauri ndio anayesimamia utendaji kwenye mamlaka ya upangaji. Anamwagiza Afisa Ardhi ambaye yupo kwenye ofisi yake akafanye kazi fulani, Kamishina wa Ardhi naye anamwagiza kwa wakati huo huo, anamtii nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesha-paralyze watumishi hawa. Ni mfano mdogo tu, Kamishina wa Ardhi ngazi ya mkoa yupo pale anamwambia sasa wewe Afisa Ardhi nenda kafanye jambo hili, Mkurugenzi Halmashauri, yupo ofisini kwangu nenda kafanye hili, anaenda kwa nani? Kuna ombwe. Mnaliona ombwe hilo? Sasa naomba, kwanza tumevunja sheria. Serikali imevunja Sheria Na. 8 ya 2007 ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi. Sasa tusiendelee kuvunja sheria, wale watumishi warudi TAMISEMI. Kwa sababu, kama hakuna uratibu, kwa sababu Wizara ya Ardhi kazi yake ni sekta, yeye ni msimamizi wa sekta tu. Yeye siyo Mamlaka ya Upangaji, ni msimamizi wa sekta na sera. Sasa sijui kama tunaeleweka! Ndiyo maana nikasema hii ni episode three na episode four itakuja mpaka nione jambo langu linakubaliwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni mfumo wa ILMIS (Integrated Land Management Information System). Nawapongeza Wizara ya Ardhi, all starts well ends well. Mmeanza vizuri katika eneo hili, nimesikia hapa Taarifa ya Kamati kwamba sasa mnakwenda kwenye mikoa mitano katika mkoa mmoja wa Der es Salaam, na Mkoa wa Dar es Salaam nadhani wilaya zote karibu zina ILMIS na ndiyo maana migogoro ya ardhi Kinondoni haipo leo hii. ILMIS ni mfumo wa kuhifadhi taarifa za sekta ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Afisa Ardhi mmoja na nilikuwa sijui gharama inatoka wapi, Mheshimiwa Naibu Waziri utanisaidia, kwa sababu ninachojua kwenye ILMIS hamna jambo jipya. Kuna computer, kuna printer na kuna sever unampa Afisa Ardhi mmoja moja that is all. Sasa tunashindwa nini? Ni jambo la kawaida tu, hatuhitaji ku-invest a will hapa, tumsaidie Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala zima la migogoro ya ardhi. Nampngeza Waziri lakini atachoka, yaani hata Yesu akirudi hapa Tanzania migogoro ya ardhi itaendelea kuwepo. Kwa kweli juzi nimemwona ana mvi kidogo, kashaanza kuchoka, mvi zimeanza. Namwonea huruma sana kaka yangu Mheshimiwa Jerry Silaa, lakini yeye ana-deal na jawabu la tazizo, anaacha ku-deal na tatizo. Lazima u-deal na tatizo, siyo jawabu la tatizo. Ana clean tembezi zile, well and good. Hivi Waziri unaweza kutembea Halmashauri zote 184 na vijiji vyote, si utakufa kesho tu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri Wizara, tengenezeni mfumo. Kauli ya Waziri ikitoka pale juu, hawa wengine wote wanasema shikamoo, halafu yeye anasema marahaba. Very simple, very simple! Yaani wakati mwingine, anyway! Nasikitika lakini... (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama sekta nawaomba, nawashauri mka-deal na chanzo cha tatizo, msi-deal na jawabu la tatizo, hamtafanikiwa kamwe. Migogoro ya ardhi ni matokeo ya failure ya sekta, that is all. Hamna hamna jambo jipya hapa. Jamani eeh, mnajua ninyi mna bahati sana, lakini hizo bahati haziwapati wengine. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini? Kwa nini nimewaeleza haya jamani? Mheshimiwa Naibu Waziri, wewe ni kaka yangu, unanisikiliza, tunashauriana; na Mheshimiwa Waziri juzi umeona tunazungumza vizuri, nia yetu ni njema, na ninakushukuru. Chukueni michango yangu positively. Mimi bado kijana mdogo, ndiyo kwanza nina miaka 38 hapa, huko mbele nitafika tu. Sina nia nyingine zaidi ya kuishauri Serikali hii nzuri ya Mheshimimwa Rais Samia Suluhu Hassan. Nia yake njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashauri kitu kwa watumishi wote wa umma nchini...

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi? Haya Mheshimiwa Gwajima.

TAARIFA

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa mwongeaji, ndugu yangu kwamba ni kweli anachosema, pamoja na mapafu yote ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, lakini migogoro anayokimbiza kutatua ni matokeo ya tatizo ya kushindwa kupima nchi yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jimbo langu unakuta hati moja ya mtu halafu ndani yake kuna hati nyingine 100 ndani ya hati moja lakini yote imetolewa na Serikali. Kwa hiyo, kutokupima na kupanga kama anavyosema ndugu yangu Mheshimiwa Kunambi, ndiyo hasa chanzo cha mgogoro. Tusishughulike na matokeo, tushughulike na chanzo cha mgogoro. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea kwa mikono miwili. Niseme tu kwa dhati, hata ufike mwisho wa dunia, nchi yetu kamwe kama hatuta-deal na chanzo cha migogoro ya ardhi, tukaendelea ku-deal na majawabu ya migogoro ya ardhi, nchi hii migogoro ya ardhi itaendelea kukithiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye enelo lingine la umuhimu la sekta ya ardhi. Wenzetu Walatini, kuna usemi mmoja wa Kilatini unasema, “Quicquid plantatur solo, solo cedit.” Maana yake nini? Anything attached to the land from part of it, permanent attached, na kuna masuala ya fixture huko na fitting, hilo ni somo lingine nitatoa siku nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa umuhimu wa sekta ya ardhi, ukizungumzia madini yako sekta ya ardhi; ukizungumzia kilomo, ni sekta ya ardhi. Kwa hiyo, niwaambie, sekta zote kama hamjashirikiana na Wizara ya Ardhi huko, aah, tunatwanga maji kwenye kinu. Namwona Mheshimiwa Bashe anakimbia kweli kweli, lakini namwangalia, kaka utafika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Watanzania wenye hatimiliki hata za mashamba, ukifuatilia hata 1% hawafiki. Anakopeshekaje. Unakuwaje na kilimo biashara? Unamchukua mwekezaji huko, Mama anafanya kazi kubwa sana, Mheshimiwa Rais kuhamasisha wawekezaji ndani ya nchi, lakini tufanye hesabu kwenye kilimo, kuna wawekezaji wangapi wamewekeza kwenye…

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Karibu. (Kicheko)

MWENYEKITI: Ndiyo.

TAARIFA

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kumpa taarifa mzungumzaji kwa mchango mzuri ambao anaendelea nao kwamba hata hii migogoro inayotokea ya wakulima pamoja na wafugaji chanzo chake ni hicho hicho kwamba hakuna mipango halisia iliyowekwa vizuri. (Makofi)

MWENYEKITI: Unaipokea Taarifa Mhehsimiwa Kunambi?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sana, kwa mchumi bobezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati nazungumza, nasema, hivi nasikilizwa hapa? Ila wajibu wangu ni kusema, nitasema tu. Hii ni episode three, nitaenda episode five, mpaka nimalize Ubunge wangu. Wananchi wa Malinyi wamesema wamenipa guarantee nitarudi tena hapa ili nifanye kazi yao vizuri. Kwa hiyo, nitaendelea mpaka Mungu atakapochukua uhai wangu, mpaka nione Tanzania imepangwa na kupimwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe, nirudi jimboni kidogo, nimezungumza kwa niaba ya watanzania wote sasa nazungumza kwa wananchi wangu wa Jimbo la Mlimba, pale Mlimba, Kata ya Namawala, tuna mgogoro wa ardhi uliochukua takribani miaka 20 na Naibu Waziri tulizungumza, kwa kweli nakusifu sana Kaka yangu, keep it up unafanya vizuri. Hizi changamoto zote, ninyi ni wapya mmekuta zimerundikana lakini anyway tutawasaidia tu, huu mgogoro wa Kambenga kesi yake ni ndogo tu na nitawasaidia kutatua. Huyu bwana Kambenga alipata ardhi hekari mia moja akaongeza sifuri wakati wa miaka ya tisini akapata hekari elfu moja lakini makubaliano ya kijiji ni heka mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Naibu Waziri kama tulivyokubaliana na ikiwezekana tuambatane na Mheshimiwa Waziri kadri mtakavyoona inafaa. Twende kule tukatatue tatizo, ni tatizo dogo sana, lakini niwaambie nimekuwa mtu laini sana leo kwa sababu nimeona mmeanza vizuri. Niwaahidi kama hamjatatua ule mgogoro wa Kambenga nina shilingi ambayo mpaka leo sijairudisha. Kwenye bajeti yenu inayokuja mwezi wa tatu, hii ambayo ninayo nitaongeza tena na ya pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile nyingine ninayo mpaka sasa sikuirudisha sasa sitaki nifike huko kwa sababu najua ninyi ni watu Rahm na Waziri wako twendeni mkatatue migogoro hasa ule wa Kambenga ili wananchi wangu wapate nafuu ya maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ubarikiwe. (Makofi)