Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na nimeweza kusimama na kuchangia kwenye Taarifa hii ya Kamati ya Ardhi, Msaliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja Taarifa ya Kamati ya Ardhi na Maliasili, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Jerry Silaa kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kwenda kutatua migogoro iliyopo kwa hekima na nidhamu ya ari ya juu kwa sababu migogoro mingi iliyopo inahitaji hekima jinsi ambavyo migogoro inaendelea katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Jerry na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wanafanya ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kuwa salama lakini nimwambie Mheshimiwa Waziri tu kwamba hii migogoro anayokwenda kuitatua leo kesho itazuka migogoro mingine na mingine, kama Taifa hatujaamua kupanga matumizi bora ya ardhi. Kila itwapo kesho tutakwenda kuwa na migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inahitaji kupangiwa matumizi ya ardhi. Mimi nilikuwa mjumbe wa Kamati hii, nilitembea kwenye baadhi ya maeneo ambayo yamepangiwa matumizi bora ya ardhi. Watu hawagusi kwenye eneo ambalo sio la kwao, kama hautapanga matumizi bora ya ardhi hatutafanya kitu. Mheshimiwa Jerry atatatua mgogoro huu leo na kesho utazalika mwingine kule. Hii migogoro haitakwisha kama hatujafanya maamuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Askofu Gwajima, safari hii kama hakutakuwa na bajeti ya kutosha ya Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi na mimi nitakuwa mmoja kati ya watu ambao hatutapitisha bajeti ya Wizara ya Ardhi safari hii. Lazima humu ndani kieleweke, kwa sababu haiwezekani tuwe tunashauri Serikali, tunapiga kelele. Sisi ndio wenye changamoto huko, tunatokanazo kwa wananchi wetu. Haya tunayozungumza sio ya kwetu, haya tunatumwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mbunge wa Viti Maalum, lakini nina Mkoa ambao ninatokea, Mkoa wa Tabora ndio Mkoa mkubwa kwa sasa hivi wenye eneo kubwa katika mikoa yote ya Tanzania na hata tunapozungumza kwamba Mkoa wa Tabora uwe ni miongoni mwa Mikoa ambayo itapunguzwa ili wananchi wetu waweze kupata maendeleo, tunaomba sana hili jambo litekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukubwa wake, ndio umekuwa Mkoa mkubwa pia hata kwenye hii migogoro. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, katika clinic ambazo anaendelea nazo, naomba Mkoa wa Tabora upewe kipaumbele ili mwende kupunguza matatizo na changamoto za ardhi kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro inachosha, pale Tabora ardhi iliyopo ni kubwa sana kiasi kwamba matajiri wachache wanakwenda kununua ardhi sasa wanainunua wanahodhi ile ardhi, hata kama inatokea una jambo ambalo linataka lifanyike, hata kama kuna mwekezaji ni lazima umwone yule mtu ili yeye aweze kukuuzia ile ardhi. Sasa jambo hili ni baya, kama tungekuwa tumeshapanga matumizi ya ardhi kwenye maeneo yetu, tungejua hapa itajengwa shule, hapa hospitali, hapa kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wizara ya TAMISEMI, Mheshimiwa Rais anashusha fedha nyingi sana kwa ajili ya miradi ya hospitali, zahanati na miradi ya shule, lakini unakuta kuna maeneo mengine hatuna maeneo ya kujenga shule kwa sababu tu kuna watu wachache wanahodhi hayo maeneo, kwa hiyo watu wanashindwa kujenga kwa sababu kuna mtu fulani amechukua yale maeneo na anayauza kwa bei anayotaka yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo inasababisha migogoro na mtu anapoona kwamba lile eneo liko wazi anakwenda kufanya shughuli zake na yeye anajimilikisha matokeo yake unakuta tunaanza kukatana mapanga na kuuana. Kwa hiyo, niombe Serikali, tunashauri na kushauri sana tunaomba sana nchi hii ipangiwe matumizi bora ya ardhi ili tuweze kwenda sawa, vinginevyo Mheshimiwa Waziri mtahangaika sana, mnatatua mgogoro, halafu mgogoro mwingine unazaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Mabaraza ya Ardhi, hili jambo bado ni kero kwa wananchi, na mimi nafurahi sana jamani uletwe tu huo utaratibu wa kuondoa mabaraza ya ardhi ama wenyeviti. Huko ni rushwa tupu, hakuna lolote wanalofanya, wanasababisha migogoro tu kila uchwao. Mtu ana haki, ana hati, ana kila kitu, anahangaika mahakamani zaidi ya miaka mitano sita, kwa sababu tu ya Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi aliyehukumu tofauti na hukumu ilivyokuwa inatakiwa. Na hii ni kwa sababu ya kukosa elimu ya ile kazi ambayo yanaifanya pelekeni haya mambo kwenye Mahakama zetu ili kule kuweze kwenda kufanyika vizuri na ili mambo yaweze kwenda sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kwenye suala zima la maliasili, Mkoa wa Tabora ni moja kati ya Mikoa ambayo ni ya kihistoria katika nchi hii. Mkoa wa Tabora katika mapambano ya kupigania uhuru ni moja kati ya mkoa ambao umetoa mchango mkubwa kwa nchi hii katika mapambano ya uhuru wa Taifa hili, lakini cha ajabu mpaka sasa nimekuwa nikizungumza sana maeneo yote yaliyopo Tabora ambayo yangeweza kufanywa kama makumbusho kwa ajili ya vitukuu vyetu watakaokuja wajue kwamba hapa jambo gani lilitokea na lipi lilitokea yametelekezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano mmoja na hili nililizungumza hata kwenye mkutano wa hadhara niulipozungumza Tabora. Tuna eneo moja la taasisi pale Tabora, lipo katikati ya mji. Pale kuna sanamu ya Mwalimu Nyerere pale mwaka 1958, Mwalimu Nyerere alilia machozi akiomba uhuru wa nchi hii, aliombea pale katika eneo lile amepiga magoti analia machozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona eneo lile ni changamoto kubwa, halina umeme, majengo yamechakaa, hiyo sanamu yenyewe ya Mwalimu Nyerere imechakaa. Unajiuliza ninyi kama watu wa Wizara ya Maliasili mna mambo ya makumbusho, mna mambo ya mali kale, mnashindwa hata kututengenezea eneo ambalo Mwalimu Nyerere alilia machozi wakati akiomba uhuru wa Taifa hili? Mnashindwa kuweka kwenye mazingira ya kufanya liwe ni eneo la makumbusho, mnafanya nini kwenye Wizara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea kwa uchungu na nimeongea kwa ukali kwa sababu sio jambo ambalo nimelisema leo, hata Wabunge wenzangu baadhi wamekuwa wakilizungumza hili jambo, linatuchosha Mkoa wetu mnaufanya unazidi kuwa mkongwe. Sasa hivi Mkoa wa Tabora umefunguka. Tuwekeeni ili Wananchi wa Tanzania, watoto wetu, vitukuu na wajukuu waje wajue kwamba Mkoa wa Tabora ni moja kati ya Mikoa ambayo ilichangia katika uhuru wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukurusana TAWA na niseme kwamba, hapa nilizungumza na leo ninaomba. Watu hawa wameongezewa maeneo lakini pamoja na kuongezewa maeneo hawana power ya kutosha yaani hawana watendaji wa kutosha lakini hata waliopo malipo wanayolipwa hayaendani na kazi kubwa wanayofanya. Hali ni mbaya katika taasisi hii na ndio maana tuliomba hapa hawa TAWA, TFS wapewe mamlaka ili waweze kufanya majukumu yao. Mazingira yao ya kazi ni magumu na hata zile ela wanazopata ni kidogo sana haziendani na kazi kubwa wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru TAWA kwamba pamoja na Tabora kuwa na maeneo makubwa ya mapori lakini wameweza kutengeneza maeneo ya vivutio katika Mkoa wetu wa Tabora ili hata mtu anapokuja asikutane na mapori sana ili mwisho wa siku watu waende na waweze ku-enjoy na kuona hali na mazingira ya Tabora jinsi yalivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, sasa hivi tunayo zoo pale Tabora, zamani ilikuwa ni pori kweli kweli, wadudu wote wakali walikuwa pale lakini leo ukifika Tabora utakutana na zoo ambayo iko pale eneo la game ambapo ni kivutio kizuri nani kivutio kikubwa. Ukifika Tabora unahitaji kupumzika unakwenda pale Tabora zoo na mambo yanakuwa mazuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora imefunguka, tunazo barabara, ni Mkoa ambao ni wa kihistoria. Tumechoka kuwa mji mkongwe na sisi tunataka maendeleo ikiwepo vitu vya kihistoria, viwekwe katika mazingira mazuri ili hata na sisi tunapotangaza watalii, watalii waweze kufika katika Mkoa wetu wa Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe sana, Wizara hii haijapelekewa fedha. Fedha zilizopelekwa nimeangalia hapa is almost 17%, 17% kwa Wizara ya Maliasili unafanya nini? Leo ninavyozungumza Watalii wamekuja wengi kweli kweli lakini hizo barabara zinazopita kwenye hifadhi zetu umeziona? Hali ya barabara katika hifadhi zetu ni mbaya, kwa hiyo tunaomba Serikali ipeleke fedha haraka sana ili tuweze kupata fedha lazima tutoe fedha. Mtu hawezi kuja akakutana na hali mbaya namna ile ya barabara akakubali kwenda kufanya utalii wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana hizi barabara zitengenezwe haraka, watalii waendelee kuja ili tuweze kuendelea kuingiza pato ambalo tunalitarajia kutoka katika Wizara hii ya Maliasili. Fedha ndio kila kitu Wizara ikipewa fedha kazi zinaweza zikafanyika vizuri na mambo yakaenda sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi tena kwenye hili suala zima la ardhi na changamoto zake. Changamoto za ardhi zimekuwa ni nyingi sana. Niliona nikimbilie kwanza kwenye Wizara ya Maliasili ili niweze kuzungumzia Mkoa wangu kwa sababu natoka kwenye Mkoa huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema, ardhi ndio kila kitu. Ardhi haiongezeki lakini sisi binadamu tunaongezeka, kwa hiyo, kwa sababu sisi binadamu tunaongezeka ni lazima tutengeneze mazingira ili kila mmoja anapokuja awe ana eneo ambalo atalipata kuliko mtu mmoja kuhodhi ardhi zaidi ya hekari 1,000, 2,000, 10,000, hii kwa kweli sio sawa. Ni lazima mfike mahali mfanye maamuzi kwamba sasa hivi Mtanzania wa kawaida ardhi anayotakiwa kuwa nayo ni kiasi hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu watanzania tunaongezeka na hii ardhi iko vilevile na kila siku watu wanazaliwa, kila siku watu wanakufa lakini bado watu wanazidi kuongezeka na sisi tupo vilevile. Kwa hiyo, ili tuweze kuondoa changamoto hii ni lazima tufike mahali tuamue kwamba, mtanzania unatakiwa uhodhi ardhi kwa kilomita kadhaa ama hekari kadhaa ili mtu mwingine akija, kwa sababu tayari imeshapimwa na imeshawekewa matumizi ataambiwa pale mnaweza mkampimia raia anayetaka ama pale ni kwa ajili ya maeneo ya msingi ambayo tunataka kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili wanahitaji sana fedha kwa ajili ya kuweza kutekeleza haya majukumu yao lakini niwaambie Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, kwamba kazi bado ni ngumu pamoja na kazi kubwa ambayo wanaifanya lakini mwisho wa siku changamoto ni nyingi kuliko hizo ambazo tayari zimeshatatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)