Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuungana na wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu wa Rehema ametupa nafasi hii leo kuweza kujadiliana masuala mbalimbali kwa ajili ya watanzania wetu. Pia, niipongeze Serikali kwa kazi kubwa inayofanya kupitia Wizara hizi zilizo chini ya Kamati hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kwa ujumla kutoa na kuchangia kwa sehemu Taarifa ya Kamati. Kwanza nizungumze tu kwamba ni karibu miaka kadhaa sasa tukisubiri hizi Kanuni za Mwaka 2011 zilitwe Bungeni ili tuzitazame upya. Kanuni hizi ambazo zinazungumzia fidia pamoja na kifuta machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni karibu miaka saba, kanuni hizi sio rafiki kwa watanzania kwa sababu unapozungumza kifuta machozi shilingi laki tano na fidia ama tunasema fidia kwa wale waliopoteza maisha kile kiasi cha shilingi milioni moja. Hebu tutazame kwa upana, kwanza hakuna fidia wala hakuna kifuta machozi kwa mtu ambaye tayari amepoteza maisha. Mimi ushauri wangu ni kwamba jambo hili lifanyiwe kazi na Serikali halafu mtuletee tulijadili tutazame kwa upana wake na athari zake kwa jinsi ambavyo tunapata madhara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni madhira makubwa kwa wananchi kwa sehemu hii ya fidia ya wanyama wakali, lakini pia wanaokuja kuleta madhara makubwa katika maisha ya watanzania. Hali hii inafanya Serikali kulalamikiwa lakini pia watanzania kuona kwamba sisi tunathamini zaidi wanyama kuliko maisha ya watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo hili linakabiliwa sana na changamoto nyingi hasa kwa sisi tunaopakana na hifadhi. Mojawapo ni ile ya wanyama kutoka kwenda kuharibu mali za watanzania kwa muda mrefu na hakuna namna ya kuwazuia wala kuwarudisha kwenye yale maeneo. Pia hatua za haraka zinashindikana kwa sababu eneo hili linakabiliwa na changamoto kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto mojawapo ni ukosefu wa wa wataalam, wale askari game lakini pia na vitendea kazi. Ni hali ambayo inasikitisha sana pale ambapo tunashindwa kuchukua hatua za makusudi ili kunusuru usalama wa wananchi na mali zao na hatimaye madhara yanakuwa makubwa. Pia, mahusiano ambayo sio mazuri kati ya wenzetu wa TANAPA na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu mji sio mji kama tunavyozungumza, lenyewe lina kata saba ziko mjini na kumi ziko vijijini, na kule kwenye kata za vijijini kuna hifadhi za TANAPA za Manyara na Mara, ambako kuna wanyama wakali na wanyama waharibifu, lakini unakuta Tembo anatoka msituni anaharibu mazao ya mwananchi, matokeo yake yule mwananchi anaambiwa tutakufidia laki tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa akili ya kawaida ama hali ya kawaida, hatua ya kwanza ni kuwazuia na hatua ya pili ni kuchukua namna ya kuweza kuzuia majanga yanayotokea. Lakini unapozungumza madhara ya laki tatu wakati ng’ombe tu akiingia msituni ni shilingi laki moja, laki mbili. Hebu jambo hili litazamwe na tukijifunza kwa umbali zaidi tunaona madhira makubwa pengine wale wanyama wanafuata maji na chakula na kwa asilimia kubwa chakula huwa kipo msituni na suala kama ni maji si twendeni Serikali yetu ikafanye tafiti maeneo ya kujenga mabwawa ili kuweza kupatikana huduma ya maji katikati ya hifadhi zetu kuliko ambavyo wanatoka nje wanaharibu mazao ya wananchi, usalama wa wananchi na maisha ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hali hiyo imesababisha mahusiano ya wenzetu wa TFS na wale wa TANAPA kuwa mabaya sana na wananchi katika maeneo ya vijiji, hali ambayo baadaye Serikali ndiyo inalaumiwa, kumbe sisi ndio tunatakiwa kuchukua hatua, na kadri tunavyochelewa kuchukua hatua basi wananchi wanaichukia Serikali, ningeomba yale yanayowezekana yawekwe kwenye mpango na utaratibu ufanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna matumizi makubwa na yasiyorafiki kati ya Askari wa TANAPA na wananchi wetu hasa katika hifadhi hizi ambazo zinapakana na wananchi. Nini kifanyike? Vikao vya ujirani mwema, mahusiano mazuri, kuweza kutafsiriana majanga yanayotokea na namna ya kukabiliana nayo na uwazi kwa mambo yanayotokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengine ni magumu, ya wananchi kupotea msituni na hata hawafahamiki walipo. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili nilikusihi sana ufanye ziara Mbulu. Mbulu siyo salama kama tunavyofikiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe, mimi kama mwakailishi wa wananchi siwezi kuzungumza kitu ambacho hakina ukweli ama hali ikoje. Kwa hiyo, mimi naomba sana kama inawezekana, upande wa Serikali na upande wa wachaguliwa wote tunajenga nyumba moja. Nia yetu ikiwa ni kujenga taswira nzuri ya wananchi kuipenda Serikali yao. Kwa hiyo, mimi nadhani jambo hili lina umuhimu mkubwa, ulichukulie hatua na uweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie eneo la upimaji; hii KKK kwa maana ya kupanga, kupima na kumilikisha. Nia ya Serikali ilikuwa njema sana, na tunaipongeza sna Serikali kwa kuja na mpango huu, lakini mpango wowote unapoanzishwa inafika mahali tuje tukae chini ili tufanye tathimini ya mapungufu yaliyoonekana na namna ya kuyarekebisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili fedha zinatumwa halmashauri, unakuta halmashauri hatuna wataalamu, kampuni inatafutwa inakwenda kufanya upimaji, inafanya upimaji ambao haujakamilika. Pengine eneo fulani limepimwa lakini upimaji haujaainishwa kwa mipaka halisi na malalamiko ya wananchi hayajafanyiwa kazi. Matokeo yake yale makusanyo ya fedha yanakosekana, na hata uendelezaji wa ule mpango unakwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa na ushauri, kama itawezekana tukubaliane na baadhi ya wajumbe waliochangia, kwamba tuangalie sasa suala la kupanga, kupima na kumilikisha liwe suala la Wizara ya Ardhi. Pia, lifanywe na maafisa wa ardhi kwenye ngazi za halmashauri, kama hawapo waazimwe kwenye halmashauri nyingine. Wakati huo ukusanyaji wa maduhuli yale ya upimaji, pia ufanywe na maafisa wa ardhi. Ni kazi ngumu sana inapokuwa anayepima ni mwingine, anayekusanya fedha ni mwingine, mpango kabambe wa master plan unaandaliwa na mwingine. Matokeo yake mradi huu na mpango huu utakwama na mwisho wa siku hautakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini napendekeza jambo hili? Majukumu ya upimaji, upangaji na umilikishaji, sasa hivi tumekwenda kufanya tathmini katika nchi nzima hakuna hati zilizotolewa inagawa tunazungumza ni KKK. Je, kama “K” ya kwanza ya kupanga ilifanywa na afisa ardhi, “K” ya pili ikafanywa na afisa ardhi, kwa maana ya kupima, na “K” ya tatu ya kumilikisha anatakiwa afanye afisa ardhi; na fedha za makusanyo katika eneo hili inatakiwa ikusanywe na afisa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yanawezekana. Niipongeze sana Serikali kwa hatua hizi inazochukuwa. Kuna athari kubwa sana sasa hivi kwenye maeneo ya miji na yale maeneo ambayo yanafikiwa na upimaji, hasa yale ya miji. Tunakosa maeneo ya vituo vya afya, tunakosa maeneo ya ujenzi wa shule, tunakosa maeneo ya huduma nyingine mpaka za mazishi kwa sababu mipango ya ardhi, au ule mpango kabambe wa master plan haujaweza kuingiza hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Ni kwamba mipango hii iwekwe wakati wa kupanga master plan (mpango kabambe wa eneo linalokusudiwa kwa mradi huu) ili uweze kukidhi mahitaji ya wakati huo na kwa jinsi ambavyo itawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuna maeneo, kwa mfano watu wa Wizara ya Ardhi. Waziri wa Ardhi na timu yake hebu tuangalie sasa hivi. Kwa mfano National housing wanajenga kwenye miji mikubwa lakini kwenye miji ya halmashauri kuna nyumba zao zilikwishakuwa chakavu, kama kule Mbulu, hzaifai hata kuona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini waipange kwa mwaka kwa yale maeneo ambayo yana nyumba zao zilizo chakavu, wakatenga fedha wakajenga hata ghorofa moja, wafanyakazi na watu wengine wakanunua majengo kwenye yale maghorofa na mengine yakapangishwa kwa watu wenye uhitaji, ili kuweza kujenga miji yenye taswira nzuri lakini pia kwa miji ambayo hatima yake inakuwa imepangika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nilikuwa nadhani wafanye tathimini katika maeneo ya miji ambayo tayari ni miji kongwe ya zamani na wamekwishakuwa na maeneo. Hayo maeneo yajengwe nyumba za kuuzia wananchi, watumishi lakini pia kujenga majengo yale na kuibadilisha sura za miji. Vilevile waweze kutembelea hayo maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango kabambe wa upimaji wa vijiji. Huu mpango tusipouchukua kwa mfano Mkoa kama wa Manyara una kesi nyingi za ardhi. Maana upimaji ungekuwa umepima Kijiji, tukatoka ngazi ya upimaji wa Kijiji, tukasogea upimaji hata wa kila mwananchi kote nchini, itawezekana kuondoa migogoro ya ardhi, vile vile wananchi wanaomiliki zile ardhi watakuwa na manufaa makubwa na thamani ya zile ardhi itakuwa imeonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mpango huu ambao tunakwenda tu tunaanzisha mabaraza ya ardhi siyo njia ya kuzuia kesi za ardhi. Maana yake baadaye tutapata mabaraza ya ardhi ngazi ya kata na gharama za kuyahudumia kwa sababu mahitaji yatakuwa makubwa kulingana na hali halisi ambayo tatizo linazidi kujitanua na linakuwa kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nilikuwa nashauri, kama itawezekana, katika bajeti tuwe walau tunatoka katika ngazi za upimaji wa mipaka ya vijiji halafu, ndipo tuje na mpango wa kwenda kwenye upimaji wa mwananchi mmoja mmoja. Na kwa kuwa sehemu kubwa wananhi ndio wanaogharamia, na hata hizo za vijiji wanaweza kugharamia baadhi ya gharama, tuangalie namna ya kuingia ubia wa hizo gharama ili kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya upimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije tena kwenye eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie kwa namna ya pekee sana; eneo la mapato; fedha hazikusanywi kwa nini? Tunapozungumza asilimia 22, sasa hivi tumebakiza miezi minne. Hebu kwa akili ya kawaida hatupaswi kukaa chini na kutafakari kama Serikali? Ina maana miezi minne iliyobaki tuta-cover hiyo asilimia 76. Hatuoni kuwa hata tukipambana kwa vyovyote vile tna kwa namna yoyote ile hatuwezi kukusanya hizo fedha asilimia 70 na kitu katika miezi minne iliyobaki kuelekea mwaka mpya wa bajeti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hali hii inasbababishwa kwanza na mkanganyiko uliopo wa upungufu wa watumishi kwenye kada hiyo pamoja na uwajibikaji usiokidhi haja. Watu tuko katika nafasi hizo kwa kukaa tu bila kufanya majukumu yetu ya kila siku na usimamizi ambao unakidhi haja na kuweza kufikia hatua ambayo inastahili na itafanikisha sana kwa jinsi ambavyo fedha hizo zinahitaji kukusanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ama mamlaka yoyote ile inayoshindwa kukusanya, itakaposhindwa kukusanya ni lazima itashindwa kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kadri ilivyokusudiwa na hii inachangiwa na wachache ambao pengine hawazitendei haki nafasi zao lakini pia kufanikisha na kufanya kazi kubwa inayoweza kuleta tija ya kuwahudumia wananchi na jamii kwa ujumla. Vilevile kwa upande wa majukumu yetu tuliyoomba kwa wananchi, iwe mtumishi au mchaguliwa kwa kadri ambavyo kila mmoja tunatakiwa atimize wajibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niishukuru Serikali, na niombe sana katika ajira zinazokuja tuangalie zile kada muhimu kwenye halmashauri, hasa Wizara ya Ardhi lakini pia kwenye halmashauri. Kwa sababu ukizunbgumza Wizara ya Ardhi na Wizara ya TAMISEMI ni wizara mbili zinazoshabihiana katika majukumu ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapokuta katika halmashauri huna watumishi wa idara ya ardhi katika eneo lile la halmashauri huwezi kutekeleza mipango hii kabambe inayokusudiwa na Serikali. Kwa hiyo, niishukuru Serikali lakini kwenye bajeti tusi-base tu upande mmoja wa kuajiri sekta moja na tunaacha upande wa pili tunakwama na mwisho wake hatuna vitendea kazi lakini pia hatuna watumishi ambao wataweza kutufanyia hizo kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi naunga mkono hoja. (Makofi)