Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa mwaka huu 2024 leo ndiyo siku ninachangia mara ya kwanza; namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai. Napenda nichukue nafasi hii kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambazo anazifanya za kuwatumikia Watanzania. Watanzania wote wameona kazi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inavyofanyika kuanzia kijijini mpaka mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, napenda kuunga mkono Maazimio yote ya Kamati yaliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Timotheo Mnzava.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulikuwa hapa, Bunge likatoa maagizo na maazimio yakapitishwa. Kati ya maazimio hayo, Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa na maazimio 10. Maazimio manne yametekelezwa, mawili yanaendelea kufanyiwa kazi lakini manne hayajatekelezwa. Naomba niyasome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maazimio ya mwaka 2023 tuliyokuwa tumeazimia yameshindwa kutekelezwa:-

(a) Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Wanyamapori TAWA.

(b) Kushindwa kutekeleza mchakato wa kupandisha hifadhi ya misitu Tanzania TFS.

(c) Kushindwa kuanzisha mchakato wa sera zilizopitwa na wakati.

(d) Kushindwa kuchukua hatua za haraka kwa wawekezaji wa hoteli na lodge ambao walikiuka masharti ya mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maazimio hayo tuliyoyatoa mwaka 2023 hapa Bungeni na hayajatekelezwa. Sasa ninaanza pale kwenye kushindwa kuchukua hatua madhubuti kwenye hoteli zilizoshindwa kutekeleza mikataba yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliazimia na tukatoa maazimio ndani ya Bunge hili ambayo ni maazimio ya Bunge, kwamba Serikali irudishe zile hoteli ambazo watu walibinafishiwa lakini hawakuweza kuendeleza. Nini maana yake? Kuna hoteli ambazo toka zimebinafisishwa hazijawahi kufanya kazi. vilevile, kuna hoteli ambazo zimebinafisishwa lakini zina-operate kwa kiwango cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa Hayati, Mwalimu Nyerere, alijenga hoteli kila mkoa. Kulikuwa na Mbeya Hotel, Tabora Hotel, Dodoma Hotel, Musoma Hotel. Hoteli hizi zote zina-operate kwa kiwango cha chini. Ni bora zilivyokuwa kabla hazijabinafisishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipitia azimio kwamba, Serikali irudishe hoteli hizo kwa sababu waliopewa wamevunja mkataba na hawakuweza kutimiza masharti ya mikataba. Hata hivyo, azimio hilo halijatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko hotel kama Embassy Hotel, Kunduchi Beach Hotel, Mikumi na Lodge nyingi kule Manyara, zote hizo zipo na zilikuwa za Serikali, zilibinafisishwa na zinafanya kazi kwa kiwango cha chni sana. Embassy imefungwa na ninafikiri takribani miaka 14 sasa pana uzio pale na iko katikati ya Dar es salaam. Vile vile, kuna Agip Hotel pale ziko nyingi. Hivyo, ninaomba Bunge hili labda lije na utaratibu wa kuunda Kamati ambayo itakwenda kufuatilia Mazimio ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa ni kusisitiza kwamba, katika hizo hoteli tulimwita TR wa wakati huo kabla ya huyu wa sasa alikuja kwenye Kamati na tukampa maagizo ya kulifanyia kazi hilo suala. Tunamuomba TR wa sasa alifanyie kazi suala la hoteli ambazo zilibinafsishwa na hazifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumza kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ni suala la miundombinu mibovu iliyopo kwenye mbuga zetu za wanyama. Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, amezungumza hapa lakini na mimi napenda nizungumzie hapo. Mbunga zetu za wanyama zinatuingizia pato la Taifa kama alivyosema Mwenyekiti hapa takribani asilimia 25. Hata hivyo, mbunga hizo za wanyama barabara zake ni mbovu. Nachelea kusema kwamba ni mbovu. Katika mvua hizi za masika tumeona magari yakizama kule Serengeti na watalii wakishuka na kusukuma magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaraja yaliyopo kwenye mbunga zetu za wananyama, kama derava hajui kuendesha vizuri gari linatumbukia kwenye maji. Niombe basi, hii Wizara ya Maliasili na Utalii washirikiane na Wizara ya Ujenzi ili waweze kuweka miundombinu mizuri kwenye Hifadhi zetu za Taifa. Tukianzia na hiyo Serengeti ambayo inafahamika duniani kote, lakini pia Ngorongoro na hifadhi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo madaraja ya Serengeti siyo kwamba ninazungumza kwa kusoma kwenye karatasi tu, tulikwenda Serengeti na nilishuhudia jinsi magari yalivyokuwa yanazama. Ni kitu ambacho nilikiona na ninaweza kuchelea kusema kwamba, vilevile, vidaraja ni vidogo na havifai kuwa kwenye hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara ishirikiane na iangalie itatoa wapi pesa au itafanyaje ili iweze kujenga barabara zetu zilizoko kule kwenye hifadhi zetu, na ukiangalia kwamba Pato la Taifa asilimia 25 linatokana na wageni wanaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi hapo hapo kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii. Mheshimiwa Rais alitusaidia kuitangaza nchi hii kwa filamu yake ya Royal Tour. Sasa hivi wageni wanaokuja kwenda kwenye hifadhi wanakosa vitanda, nikiwa na maana kwamba hoteli hazitoshi. Ndiyo maana natoa msisitizo kwamba, hoteli ambazo zimeshindwa kutekeleza masharti ya mkataba Serikali izichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ni utangazaji wa hifadhi zetu. Hifadhi zetu za Tanzania zinapaswa zipewe uwiano mzuri wa kutangazwa. Nikiwa namaanisha kwamba, tusitangaze Ngorongoro kila siku, Serengeti kila siku, ziko na hifadhi nyingine. Nitoe mfano hifadhi ya kule kwetu Katavi nayo pia inahitaji kutangazwa. Hii ni kwa sababu nayo ni hifadhi nzuri lakini pia ina Wanyama wazuri; ina twiga mpaka mweupe ambaye hapatikani kwenye hifadhi nyingine yoyote. Sasa iwenje unapofungua ile channel ya Tanzania ambayo inatangaza unakuta inarudia hifadhi Serengeti, Serengeti shall never die, Ngorongoro hiyo hiyo, wakati kuna hifadhi nyingine. Tuweke uwiano kama ni mwezi mzima unatangaza Serengeti, mwezi ujao tangaza Katavi National Park mwezi mwingine tangaza Saadani, mwezi mwingine tangaza Gombe ili kuwe na uwiano. Nafikiri hawa waratibu wa haya matangazo wamenisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ni suala la kuweka mazingira rafiki kati ya wale wageni wanaokuja na hoteli zilizopo kwenye mbuga zetu. Kuna hoteli katika mbuga zetu ambazo charge usiku mmoja ni takribani dola 1400 kwa siku. Ina maana mtalii analala kwa dola 1400. Hivyo basi, muone kama mtu binafsi anaweza kujenga hotel akatengeneza dola 1400 kwa siku ni kwa nini Serikali isitengeneze hoteli ya aina hiyo hiyo ikatengeneza dola 1400 kwa siku? Zipo hoteli kama Four Seasons kule Serengeti na nyingine nyingi. Kwa hiyo, kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ninapenda kulisisitizia hilo na lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye Wizara ya Ardhi. Kwenye Wizara ya Ardhi nitakuwa na machache ya kusisitiza, hususani suala la zile fedha, dola bilioni 150 sawa na takribani bilioni 346 ya hela za Kitanzania. Kati ya fedha hizo kuna suala la ujenzi wa ofisi za ardhi katika kila mkoa. Niombe basi, wakati watakapokuwa wanatoa hizi pesa za kujenga hizo Ofisi, basi kwanza ningeomba ile ramani ya jengo ifanane, kwa sababu katika ripoti yao walisema watajenga ofisi za ardhi katika mikoa 25. Niombe, ili kuwe na uwiano wa pesa na ili ile pesa iweze kutumika vizuri na isionekane kuna upendeleo kwa fulani na fulani; kwanza ramani iwe moja ambayo itajengwa hiyo ofisi ya ardhi kwenye kila mkoa. Pili, yale matumizi ya pesa, kama Mkoa wa Tabora utapewa bilioni kadhaa, labda let say bilioni 80, basi na Mkoa wa Katavi upewe bilioni hiyo hiyo na ramani iwe moja ili isije ikaonekana Mkoa mwingine kwamba umeongezewa pesa kwa sababu ramani yake ni kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka kwenye Wizara ya Ardhi, naomba nirudi kwenye Wizara ya Maliasili niende niizungumzie TAWIRI, TAWIRI ni taasisi ya Serikali. Hii TAWIRI ni Tanzania Wildlife Research Institute ambayo inafanya Research kwa ajili ya wanayama wetu nchini Tanzania, kuangalia kama kuna magonjwa Wanyama wamepata lakini pia kuangalia mambo yote ya wanyamapori nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi hii ilianzishwa tangu mwaka 1980, lakini cha kushangaza ndiyo taasisi ambayo inafanya research kwa wanayama wote, sijui kiboko, sijui tembo ameugua, sijui pundamilia wamekufa, sijui nini, wote hao ndiyo wanafanya research kuangalia ni kwa nini wamekufa. Maana yake ni scientific research lakini cha kushangaza taasisi hii haina jengo tangu mwaka 1980. Taasisi hii inapewa bajeti ndogo. Pia, niliona jengo la research kule Serengeti ni kama vinyumba nyumba fulani hivi vimekaa pale ambavyo vimeachwa kwa muda mrefu bila kupakwa rangi. Halafu eti unategemea taasisi kama hii ije na research ambayo itaweza kuboresha mambo ya wanayamapori nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kuboresha mambo ya wanayamapori na kupata research nzuri kutoka kwenye hii taasisi ya Tanzania Research institute (TAWIRI) ambayo ipo Arusha tuna wajibu wa kuwapa bajeti ya kutosha, kujenga makao makuu ya taasisi hii pamoja na kwenda kurekebisha yale majengo yaliyopo Serengeti ambayo kwa kweli nachelea kusema ni majengo ambayo yako kwenye kiwango cha chini kabisa; nimeyaona kwa macho yangu. Hivyo, basi nilikuwa naiomba Serikali itilie mkazo suala hili la hii research ya TAWIRI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuboresha taasisi hii, tutajua ni jinsi gani tunakwenda kupandisha utalii wetu nchini Tanzania kwa faida yetu sisi lakini pia kwa faida ya kizazi kinachokuja. Haiwezekani taasisi mwaka 1980 mpaka sasa ni almost 40 years taasisi haina jengo eti tunasubiri kupata results nzuri kutoka kwenye taasisi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Naomba tu niseme kwamba ninaunga mkono hoja zote za Kamati na Maazimio yote yaliyotolewa na Kamati na ninaomba maazimio ya mwaka jana na maazimio ya mwaka huu Serikali isipoyatekeleza mwakani tutayaleta, na hata mwaka 2030 tutayaleta tena. (Makofi)