Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mwenyekiti Ndugu Mnzava pamoja na Kamati kwa ujumla kwa utayarishaji mzuri wa taarifa hali kadhalika na uwasilishaji wa taarifa yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Allah Subhanahu Wa Taala kwa kutujalia uzima na kutupa kibali cha uhai na wale ambao kidogo afya zao zina mgogoro basi allah awajalie wapone haraka ili waungane na Watanzania wenzao kuja kulijenga Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu kwanza ningependa kumshukuru sana na kumpongeza Mama Samia kwa juhudi zake ambaye ni mwanamazingira na mhifadhi nambari moja ambaye amejitolea siku yake ya kuzaliwa kwenda kupanda miti katika eneo la Donge Muhanda, hii inatupa sisi wanajamii wa Tanzania kwamba kama kiongozi mkubwa kama yeye amejitolea siku yake kubwa ya kuzaliwa kwenda kupanda miti, na siku hiyo amepanda miti karibu miti 5,400, sasa kama ingekuwa kwa viongozi wetu wote kuanzia ngazi za Taifa, ngazi za Mkoa, Wilaya hadi Vijiji basi kama siku zao za kuzaliwa wanapanda miti namna alivyofanya Mheshimiwa Rais basi sijui Tanzania ingekuwa na miti kiasi gani. Hali kadhalika nafikiri tunafahamu kwamba Watanzania tupo milioni 60, sasa kama kila mtanzania siku yake ya kuzaliwa angepanda miti basi ingekuwa kila mwaka tunakwenda kupanda miti milioni 60 mbali zile jitihada za TFS na jitihada za wadau wengine katika kupanda miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiria tu hii iwe ni chachu kwa viongozi hali kadhalika na kwa wadau wengine kufuata nyayo za Mheshimiwa Rais kuweza kutukuza siku zao za kuzaliwa kwa kwenda kuhifadhi mazingira. Nafikiri wale wasanii akina Diamond, Harmonize, kina Nandy, akina Ali Kiba na kadhalika sasa badala ya kwenda kwenye majukwaa kama kwenda Serena Hotel kwenda kusheherekea siku zao za kuzaliwa basi nafikiri wameshapewa mafunzo mazuri ya mazingatio sasa walekeze siku zao za kuzaliwa katika kuhifadhi mazingira na itaacha legacy katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu pia ni utangulizi nafikiri Mheshimiwa Rais ametoa dira kwamba hali ya uhifadhi, hali ya misitu yetu Tanzania siyo nzuri sana, kwa sababu wataalam wanatuambia kwamba kila mwaka tunapoteza karibu hekta zaidi ya laki tatu za misitu. Hii inatujulisha kitu gani? Hii inaonyesha kwamba maji ambayo yallitakiwa yatiririke kutoka katika misitu yetu ya jamii au misitu yetu ya asili kwa uharibifu wa misitu inakwenda kupungua, lakini nishati ambayo inategemea sana maji katika maeneo tofauti ya misitu yetu inakwenda kuathirika, hata shughuli za utalii ambazo vivutio vingi vinapatikana katika maeneo ya misitu vinakwenda kuathirika, hii nafikiria tunaweza tukapima Tanzania tunaathirika kiasi gani kwa uharibifu au upoteaji wa misitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama jitihada hazikuongezeka za kupanda na kuhifadhi misitu yetu ya asili na tukaelekeza jitihada zetu katika kulaumu zaidi na katika kuji-defend, kwa sababu utaona kuna hali halisi ambayo inajitokeza mara nyingi kwamba oooh wananchi wanataka eneo la kulima, wananchi wanataka eneo la mifugo, wananchi wanataka maeneo tofauti tofauti kwa shughuli mbalimbali lakini bila kuangalia thamani ya mazingira yetu, thamani ya misitu yetu kama ikitoweka hizi sekta nyingine za kilimo, mifugo, uvuvi, nishati na kadhalika zitakwenda kuathirika kwa kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ningependa kutoa wito kwa maliasili lakini hata kwa Mheshimiwa Rais, nafikiri sasa ilishafika hatua kwamba tuje na semina elekezi ambayo itajumuisha watendaji wote wakubwa wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu na vyombo vingine mbalimbali ili tuje tujadili hali halisi ya uharibifu wa mazingira, hali halisi ya uharibifu wa misitu Tanzania na kila mtu aondoke na jukumu lake pale. Kwa sababu tunajua kwamba kuna jitihada mbalimbali zimefanyika au zimewekwa, kwa mfano wenzetu wa mazingira wamekuja na mpango kabambe ambao unategemea kila sekta i-play its part, our part. Ukiangalia uhalisia kila sekta imejifungia upande wake haifanyi vya kutosha, sasa nafikiria katika semina elekezi itatusaidia kuweza kila taasisi kuweza kuelekezwa upande gani ikafanye shughuli zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningeomba nichangie kidogo kuhusu suala zima la bajeti, nafikiri Kamati imetufahamisha hapa kwamba bajeti hasa upande wa maendeleo, nafikiri mpaka sasa hivi kuna asilimia 17. Tumebakisha nafikiri kama miezi mitano ama sita hivi tuweze kufika mwisho wa utekelezaji wa bajeti hii. Sasa hii inatoa picha gani? Kwamba hali ya mtiririko wa fedha hauko vizuri. Ningependekeza turejee katika maazimio ya miaka miwili iliyopita. Tumezungumza hapa kwamba ni vema suala la retention ambalo lilikuwepo huko nyuma tulirejeshe, yaliwekwa maazimio mwaka juzi, mwaka jana lakini azimio hili halijatekelezwa katika hali yake ya ukamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeliomba tu kwamba Wizara ya Fedha hivi kuna kigugumizi gani kuweza kupanga retention au kurudisha retention ya asilimia 30 siyo asilimia 100 ni asilimia 30 na asilimia 70 tuka-retain tukafanya kazi za maendeleo katika mambo mengine. Kwa sababu dunia nzima masuala ya uhifadhi basi yanaendeshwa kwa retention, kwa kutegemea fedha za OC, fedha zitoke kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ndiyo zitumike zirudi si rahisi, kwa sababu mambo mengi ya uhifadhi ni mambo ya dharura. Moto ukitokezea hausemi utatokezea kesho, keshokutwa, hali kadhalika uvamizi umetokezea hausemi utatokea lini. Sasa kama hatukuweka retention jamani wa are very hypothetical, hatuhifadhi maliasili katika hali ya kisayansi tunahifadhi katika hali tunayojua sisi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ningeliomba hili nasikia kwamba tumeanzisha utaratibu wa escroll kwamba kutakuwa na account maalum ambayo tutaweka fedha asilimia sita, na asilimia sita hii asilimia tatu itakwenda kwenye hifadhi na asilimia tatu itakwenda kwenye masuala mengine ya kutangaza utalii lakini mimi naona hili siyo suluhisho ambalo lina afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeliomba Waziri wa Fedha akafuata maelekezo ya Bunge lako Tukufu ya kwamba tuende tukaweke retention ambayo itakwenda kusaidia hizi hifadhi TANAPA, WMA na wenzao kuweza ku-retain hizo fedha na kutumia katika maeneo mbalimbali badala ya kutegemea ruzuku kutoka Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka hapa kipindi kile Mheshimiwa Mchengerwa alikuwa nafikiri alikuwa ndiyo Waziri, aliahidi kwamba kila mwanzo wa mwaka basi watatenga bajeti mbili zitapelekwa kwa miezi miwili ili hizi bajeti hizo moja ikae kama standby na moja ndiyo itumike, hata hilo halikufanyika! Tutakuwa tunakaa hapa tunapitisha mambo halafu wenzetu wa Serikali wakishafika Wizarani huko wanayafumbia macho nafikiri hili halina afya na ningeliomba likafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine kuna maazimio ambayo wenzetu hapa mwaka jana tuliyapitisha unakumbuka wewe, kuna maazimio kumi tuliyapitisha na tumeambiwa kuna maazimio manne yametekelezwa kwa vizuri na maazimio mawili yako kwenye mchakato, maazimio manne hayakutekelezwa kabisa, maazimio haya ukiangalia ndiyo afya ya uhifadhi wa maliasili zetu. Mfano, kama Azimio la kuweza kuipandisha hadhi taasisi ya TFS kuwa mamlaka, tumelipigia kelele sana lakini naona katika Azimio ambalo limefeli kutekelezwa ni hili la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, azimio la kuweza kuhuisha sheria ambazo zimeshapitwa na wakati au sheria ambazo zilishakaa muda mrefu na ni sera lakini mpaka hilo nalo halikufanyiwa kazi na inasemekana kwamba wenzetu wa Serikali wamejitetea kwamba hizi sera ziko vizuri. Jamani nafikiri mwezi mmoja uliopita tulikuwa huko Dubai tumeona mabadiliko ya sayansi, mabadiliko ya teknolojia, mabadiliko ya kidunia yanavyokwenda kwa kasi, ndani ya miaka 15 tunasema kwamba sera hii bado iko rafiki na inafaa kwa mazingira ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiria siyo haki wenzetu wa Serikali hawalifanyii haki hili Bunge kwa sababu kama kuna mambo tunayapitisha tu pamoja halafu tena wakishajifungia Wizarani huko wanasema Hapana, tunakwenda hivi ni vyema tukaa kitako wakati tunakubaliana kwenye Kamati na tunakuja kupitisha hapa basi haya maazimio yatekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna azimio la WMA kutayarisha sheria yake independent badala ya kuongozwa na Bodi mpaka leo nafikiri ni zaidi ya miaka saba Wabunge wanapiga kelele, sheria hii haijaja bado hapa, hili ni tatizo, kwa hiyo ningeliomba wenzetu hawa tunapokaa pamoja tukapanga basi ni vyema tukafanya mambo kwa pamoja na makubaliano yakatekelezwa kinyume chake inakuwa hawalipi heshima Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni suala zima la Jeshi la Uhifadhi. Tumekuwa tukizungumza mara nyingi hapa kwamba Jeshi la Uhifadhi maslahi yake bado yako duni. Vijana hawa wanafanya kazi nyingi ambazo zinahatarisha maisha yao, kwa hiyo ningeliomba tu tuende tukawasaidie kutayarisha maslahi mazuri, package nzuri kama yalivyo Majeshi mengine Jeshi la Uhifadhi nalo waweze ikiwezekana kupata mishahara na marupurupu yanayofanana Majeshi mengine ili kuwatia moyo na mazingira magumu wanayofanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kengele imelia naunga mkono hoja (Makofi)