Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi na mimi nianzie alipoishia Mjumbe aliyepita kwa kuwapongeza sana Kamati kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya, lakini naunga mkono maazimio yote yalioletwa na Kamati kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na kwenye eneo la kifuta jasho au kifuta machozi. Kwanza nianze kwa kutoa pole tarehe 27 Januari, 2024 jimboni kwangu mwananchi aitwaye Shija Machenga, mwananchi wa Kijiji cha Itete, Kata ya Itete akiwa anaenda kukamua maziwa alipata changamoto ya kukutana na tembo akakanyaga mguu wake ukawa kama chapati. Ni kwa neema ya Mungu tu kwamba hakufa, lakini mpaka sasa anaendelea na matibabu Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza kwa kutoa pole, mwaka jana tulizungumza kwenye Bunge hili hapa kipindi cha bajeti na kwenye maazimio ya Kamati wameleta tena hilo jambo. Waziri mwaka jana alikuwa Mheshimiwa Mchengerwa ambaye Waziri wa sasa alikuwa TAMISEMI, ukiona changamoto zilizopo tunaamini kutoka kwake hapa migogoro iliyopo huko kwenye vijiji wakisharikiana na Waziri wa Maliasili kuna sehemu tunaamini wanakwenda kufanya utatuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo eneo la kifuta machozi nilizungumza karibia dakika 10 mwaka jana na nitarudia hapa. Kanuni za mwaka 2011 ni kanuni ambazo zinaleta doa kwenye Taifa letu, zinaleta sifa mbaya kwenye Taifa letu, kwa mfano, kwa binadamu pekee yake kwenye hilo eneo la kifuta machozi, mwananchi akipata majereha kutokana na wanyama wakali na waharibifu, akijeruhiwa anatakiwa kulipwa kifuta machozi shilingi 200,000; mkono au mguu ukikatika kabisa analipwa shilingi 500,000 na huyo mtu hawezi kufanya kazi tena; akifa yaani hayupo jamii yake imemkosa kifuta machozi ni shilingi milioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu leo tunaangalia thamani ya mwanadamu ni sawa na shilingi milioni moja, halikubaliki. Tumeshafanya mabadiliko ya vitu vingi sana, kuna shida gani kwenye kanuni hizi? Kuna shida gani? Ukitoka kwa binadamu, njoo kwenye mazao ambayo leo ndio changamoto kubwa. Hawa wanyama wakali na waharibifu, huyu mwananchi ambaye amelima mita 500 kutoka eneo la hifadhi, eka moja…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MHE. AIDA J. KHENANI: … hawa wanyama wakila…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: …analipwa shilingi 25,000 kwa eka moja.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi? Mheshimiwa.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba akipoteza maisha imepangwa alipwe shilingi milioni moja pamoja na hiyo milioni moja kuna watu ambao wamepoteza maisha leo zaidi ya miaka mitatu hawajalipwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Aida unaipokea hiyo taarifa?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa kutoka kwa baba yangu na ninaamini hiki ninachozungumza hatutegemei kuja kwenye Bunge la Bajeti tena mwaka huu kukiwa hakujafanyiwa mabadiliko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ekari moja ambayo leo tunajua mfuko mmoja wa mbole ni shilingi 75,000; shilingi 70,000 mpaka shilingi 69,000 inategemea ni aina gani ya mbolea. Huyu ekari moja ambaye angevuna gunia zaidi ya 25 ambayo maandalizi yake mpaka anakuja kuvuna inakaribia shilingi 750,000 halafu Serikali inasema itamlipa shilingi 25,000. Serikali ituambie ni wapi wataenda kununua gunia 25 kwa shilingi 25,000? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni zenyewe zinawapa umaskini Watanzania, ukitoka kuanzia mita 501 mpaka kilometa moja kama eneo lake liko mbali kutoka eneo la hifadhi, mita 500 mpaka kilometa moja anatakiwa alipe shilingi 50,000 kwa ekari. Hizi kanuni walitunga Watanzania? Tuliwatungia Watanzania? Kweli lengo letu ni kuwasaidia Watanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka kilometa moja eneo la hifadhi mpaka kilometa nne, huyu mwananchi endapo kama hao wanyama wameenda kula mazao yake analipwa shilingi 75,000. Wote tunajua unapozungumzia kilometa nne ni umbali gani kutoka eneo la hifadhi, lakini kilometa nne mpaka tano ikitokea kwamba eneo lake lina umbali kutoka eneo la hifadhi atalipwa kwa ekari moja shilingi 75,000; akitoka shilingi 75,000 kama amekidhi vigezo wanaweza wakampa shilingi 100,000. Halafu ikaenda mbali zaidi, hii kanuni inasema eneo lake lisizidi ekari tano. Kwa hiyo, tunataka Watanzania uwezo wao wa kulima isizidi ekari tano ndio maana yake, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kanuni tumezungumza mwaka jana ziko ndani ya Wizara, Waziri mwenyewe ana mamlaka nayo, kwa nini toka mwaka jana mpaka leo tunazungumzia kanuni hizo hizo zinazowakandamiza Watanzania, zinaleta sura mbaya kwenye Taifa letu, bado tunarudia kuzungumza. Haifurahishi na haipendezi, yaani leo tunataka tuseme hizi kanuni walitunga wakoloni? Hizi kanuni yawezekana zilikuwa zinafaa kipindi hicho kwa sasa zimepitwa na wakati. Mambo yanaendelea kwenye Taifa letu, haya mambo hayafai na hayana sababu ya kuendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni hizi zikiendelea kuwa hivi ina maana tunawaambia watu, tunaiambia dunia kwamba Taifa letu linathamini wanyama kuliko binadamu. Huyu mwanadamu huyu, huyu Mtanzania anapopambana na huyo myama mkali tunayemwita, akimuua tu shilingi milioni 30 inategemeana alikuwa anajihami alikuwa anafanya nini? Kwa nini thamani ya mnyama iwe kubwa kuliko ya binadamu? Haiwezekani, ni aibu kuendelea kujadili kanuni kama hizi ndani ya hili Bunge. Tumejadili mwaka jana vizuri kabisa, tukamwambia Waziri kaanze na hili eneo halileti sifa nzuri kwenye Taifa letu. Toka mwaka jana mpaka leo tunazungumzia kanuni ingekuwa ni sheria ingekuwaje? Na hizi kanuni zipo ndani ya mamlaka ya Waziri mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu naamini na sitaki kuamini kwamba Taifa letu tunaamini wanyama kuliko binadamu, tunategemea Serikali itaenda kulichukua hili jambo kwa umuhimu mkubwa. Najua hata watu hawa wa TAWA kuna wakati wanasema sisi hatuwezi kuvuna hawa tembo, wanakuja wanawasukuma tu wanawaswaga wanawapeleka wanawarudisha hifadhini. Leo tembo anaenda mpaka kwenye makazi ya watu, ndani, halafu huyu mtu akiuawa nyumbani kwake, Serikali yetu ya Tanzania tunasema tutamlipa milioni moja, kweli? Halifurahishi, linatia huzuni, linatia aibu kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri; la kwanza ni lazima mabadiliko ya hizi kanuni yapitiwe haraka ili kuendelea kulinda sifa ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwa sababu tulikuwa na mpango mwaka jana wa kufuta kifuta jasho, kwamba fedha ambazo zinatumika ni zaidi ya zile ambazo tunapitisha kama Bunge kwa kuwa matukio ni mengi, na mimi natamani, Serikali itakapokuja angalau kipindi cha bajeti watuambie ni matukio mangapi yameripotiwa kwao na mangapi yamefanyiwa kazi, kwa sababu pamoja na kwamba hiyo fedha ni kidogo ya kifuta machozi, kwanza inachelewa na wakati mwingine hawa watu wanaikosa hiyo haki ambayo siyo haki kwa namna nyingine, hili jambo si zuri. Kwa hiyo, Serikali ije itueleze ni kesi ngapi zimeripotiwa na kesi ngapi zimefanyiwa kazi kwa Watanzania hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niliwatolea mfano nchi ya Kenya jirani tu hapo waliweka fence na Serikali inaweza kufanya hivyo, Serikali inasema wafugaji inabidi waanze kufuga kisasa, Serikali lazima tuwe mfano na sisi tuanze kuhifadhi kisasa. Eneo dogo lakini uhifadhi ambao una manufaa kwa Taifa letu. Lazima tuwe mfano sisi kama Serikali, hili jambo halikubaliki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine wakati tunafikiri kufuta hicho kifuta machozi ni lazima Serikali iongeze vituo vya askari wa wanyamapori kwenye maeneo yote ambayo yana changamoto na ikipeleka hao askari wawape na magari. Wakati mwingine wale askari ni wachache tembo wamevamia kituo A mpaka waende kule TARI imeshatokea madhara. Kwa hiyo lazima tuwawezeshe tukienda na hili jambo kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hii migogoro inayoendelea, migogoro kati ya hifadhi na maeneo ya wananchi. Huwezi kutumia mfumo uliotengeneza tatizo kumaliza tatizo, nasema hivyo kwa nini? Leo ukiangalia maeneo mengi yenye migogoro yale maeneo wanakuja baadaye kuna makazi ya watu wanasema wamejenga katikati ya hifadhi, wamejenga ndani ya hifadhi. Hilo eneo linakuwa na Mwenyekiti wa Serikali, zimepelekwa taasisi za Serikali, anayehusika na uchaguzi ni Waziri wa TAMISEMI, ni Serikali hiyo hiyo. Wanachagua Mwenyekiti wa Serikali, wanaamua kupeleka shule anayehusika ni Waziri wa TAMISEMI; anakuja Waziri wa Maliasili na Utalii anasema hili eneo ni eneo la hifadhi. Sasa mtueleze hivi kweli hilo eneo linahitaji Malaika Gabriel kuja kutatua tatizo hilo? Lazima tunapoanzisha jambo tushirikiane na taasisi nyingine, hapa unataka kwenda kusajili kijiji lazima tujue ni eneo sahihi? tunakwenda kuanzisha shule mpaka ina sajiliwa ni eneo sahihi? Na wakati mwingine unakuta ina hati, hati miliki hiyo shule halafu unakuja kuwaambiwa wananchi kwamba hilo eneo ni eneo la hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba kuna taasisi za Serikali ziko kwenye maeneo ambayo tunaita sijui maeneo ya wanyamapori, hamjawahi kubomoa lakini wananchi tunawaondoa, tuache hizo tabia. Tuanze kuonesha mfano kama Serikali, kama tumejenga Taasisi za Serikali ziko kwenye maeneo ambayo ni mapito ya wanyamapori tuanze sisi kama mfano. Tunapowaambia wananchi tuwe tumeonesha mfano sisi moja kwa moja, kinachoendelea leo ni uonevu na haukubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo ni vizuri leo maeneo yanayoanzishwa, shule zinazoanza kujengwa zipimwe kwanza kwa mawasiliano ya hizi taasisi zote kujua hili eneo ni sahihi au siyo sahihi; kwa sababu pale mpaka miundombinu ya Serikali inapelekwa pale inakuaje mnakuja kuambiwa baadaye kwamba hili ni eneo ambalo liko ndani ya hifadhi. (Makofi)

Mimi naamini haya mambo yanaanzishwa kuanzia nyumba ya kwanza, ya pili mpaka inajenga shule, anapatikana Mwenyekiti, Serikali haiko likizo Serikali ipo. Tusisubiri matatizo kama hayo, halafu unataka umezalisha matatizo ukienda kwenye huo mgogoro tukupigie makofi, ulianzisha mwenyewe umekwenda mwenyewe, unataka tukushangilie kwa nini? Wakati wewe ndio chanzo cha mgogoro, haiwezekani tusipoteze muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hizi tume/tume zinazoundwa hizi zinatumia fedha za Serikali. Ukiangalia mimi nimekaa hapa sijawahi kuona majibu ya hizo tume yanapokwenda. Ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali, haiwezekani mtu ambaye amesababisha tatizo akalimalize tatizo hilo na tunataka tuone tunapoona mabadiliko ya Mawaziri tunategemea kuna kitu Rais amekiona muende mkafanye mabadiliko, mumshauri Rais mambo ya msingi, haiwezekani turudie mambo hayo kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo tunapozungumza tunategemea tuone mabadiliko na mabadiliko hayo yanawezekana tu kama tunaelewana. Leo tunajua idadi ya vijiji, kama tunajua idadi ya vijiji tuna tume ambayo inatakiwa ihusike, hiyo tume ipo shida ni nini ni dhamira ya dhati. Tumekubaliana hapa kama Bunge fedha ziende, hiyo tume ikafanye kazi ya upimaji, shida iko wapi? Shida ni nini? Ni kwamba hatuna kipaumbele? Ni kwamba hatuoni umuhimu wa mambo haya? Ni kwamba hatuoni umuhimu wa watu wetu wanavyopoteza maisha? Haya mambo hayakubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na nuanga mkono hoja ya Kamati. (Makofi)