Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyoko mezani. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu amenipa uhai wa kufika siku leo, lakini pia nawashukuru wapiga kura wangu wa Urambo ambao wamenipa ushirikiano kila wakati na hali kadhalika naishukuru pia familia yangu, naishukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri waliowasilisha kwa kazi nzuri waliowasilisha leo asubuhi mezani, hongera sana Kamati, Mwenyekiti hongera sana na Wajumbe wote hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli kwa kazi kubwa inayofanya kuleta maendeleo ikiwemo pia kutanganza nchi yetu sasa hivi tunapata watalii wengi, hongera Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati ilikuwa nzuri na nimefuatilia maazimio yao, nayaunga mkono hongereni sana na Kamati hii nimshukuru sana Mwenyekiti kwa sababu nimeshaenda kuonana nao zaidi ya mara mbili kwa suala hili ambalo nalizungumzia sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Urambo sasa na sisi pia tuna hifadhi ya msitu ambayo inaitwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla na niishukuru Serikali kwa sababu walipitisha maazimio hapa ya hifadhi za aina mbalimbali ikiwemo mojawapo ya kwetu ya Urambo inayoitwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna ambaye asingeshukuru kupata hifadhi kwa sababu tunajua yako manufaa yanayotokana na hifadhi kama vile TANAPA sasa hivi wanatusaidia ukiomba madawati unapata tunashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani yetu Wananchi wa Urambo walikuwa wananiuliza, mbona ilitokea ghafla sana? Kwa sababu wao walitegemea pamoja na kufurahia hiyo TANAPA lakini walikuwa wanategemea kwamba watashirikishwa kwenye maamuzi hayo ili wajue sasa ufanyaji kazi utakuwaje, ushirikiano, kulinda msitu wenyewe itakuwaje? Kwa sababu Urambo sisi katika zao mojawapo ambalo tunalithamini sana ni asali na hata marafiki zangu mliomo humu mkitaka kunituma asali ninawaletea tu kutoka Urambo. Ni nzuri sana na watu wanaitaka pamoja na Wamarekani walikuja kuifuata Urambo asali yetu tunayoizalisha pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walipoanzisha tu Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla; la kwanza ni kuzuia marufuku kuingia, marufuku hata kufuata ile mizinga ambayo waliiweka tangu zamani na sisi miaka yote huwa tunauza asali kwa kuweka mizinga kwenye msitu huo. Sasa ghafla ikaonekana kwamba hawawezi kuingia, kama kuna pigo mojawapo ambalo tulilipata; hilo ni mojawapo ni kubwa ambalo limetuathiri sana sisi kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua tunatumbaku lakini huwezi kutegemea zao moja tu, tunategemea na mazao mengine mojawapo likiwa ni zao la asali. Nilikwenda kuiona Kamati nikazungumzia suala hili; la kwanza kwamba mlipokwenda kugeuza kuwa Hifadhi ya Taifa mliongea na wananchi husika? Mliwaelimisha? Mliwaambia wajibu wao ni nini? Mabadiliko yao katika kutumia msituo huo itakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakukuwa na ushirikiano wa aina yoyote wala elimu yoyote. Sasa kata nne zinazozunguka hapo mojawapo ikiwa Kata ya Ugalla, Kata ya Ukondamoyo, Kata ya Nsenda na Kata ya Kasisi wanalia, vijiji kumi hawaruhusiwi kuingia mle kufuga (kuweka mizinga yao) wala kuchukua hata asali ambayo walishaweka mizinga miaka mingi na ng’ombe hawawezi kuwalisha pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba jinsi miaka inavyokwenda watu wanazidi kuongezeka na cha ajabu kimojawapo walipokuwa wanaweka ile mipaka sasa wakachukua mpaka na maeneo ya vijiji. Tukumbukue kwamba hivi vijiji vilipimwa na wao wanajua hata kama ni kesho twende na Waziri muhusika, wao wala hawahitaji jembe wanafukua na vidole tu wanakwambia mawe yetu haya hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwanza mipaka mipya iliingilia mipaka ya zamani lakini pia ikawa kama nilivyosema hawaruhusiwi kuingia kabisa. Hili ni pigo kubwa kwetu sisi na hili suala silizungumzii hapa kwa mara ya kwanza, nililizungumzia tarehe 3 Juni, 2023 nilizungumzia humu Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, walipounda ile Kamati ya Mawaziri nane nilipeleka barua rasmi na Serikali hii pia nilitegemea kwamba baada ya kuwatuma Naibu Mawaziri; Mheshimiwa Ramo Makani alikuwa Naibu Waziri Maliasili alikuja lakini pia Mheshimiwa Josephat Hasunga alikuwa Naibu Waziri alikuja lakini pia Mheshimiwa Dkt. Kigwangala ambaye alikuwa Waziri alikuja lakini bahati mbaya mvua ilinyesha sana akashindwa na Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula aliyekuwa Waziri wa Ardhi pia naye alihusika lakini hatujapata jibu lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani na Serikali yetu kwamba itazingatia maoni ya Kamati lakini pia na ya Wabunge kama hivi ninavyosema sasa hivi. Tuliomba sisi na ninarudia tena kuomba kwa heshima na taadhima Serikali ninayoiamini turudishiwe angalau siyo chini ya eka sita kuzunguka zile kata ili wapate mahali pa kuendelea kuweka mizinga, waendelee kufuga nyuki lakini pia waendelee na kupeleka mifugo yao kuchunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tena kurudia ombi kwa niaba ya Wananchi wa Urambo kata hizo nne kwamba turudishiwe eneo. Sasa ninachoshangaa mimi nitashukuru kama kuna mtu atanipinga hapa; wengine wameomba wamerudishiwa, mimi nimeomba wee sijui mwaka wa ngapi huu. Wanarudishiwa siyo hiyo tu, na sisi tunashukuru kuwa na TANAPA lakini turudishiwe kama nilivyosema siyo chini ya kilometa sita wananchi wetu waendelee kufuga nyuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuja Tabora nakumbuka tarehe 30 Machi, 2022 nililizungumzia hili suala na wenzangu wakaniunga mkono kwamba bado tunahitaji kuweka mizinga kule na kuvuna asali; Mheshimiwa tusaidie. Jambo la ajabu ni kwamba Mheshimiwa Waziri nadhani atakuwepo hapa na aliyekuwa Waziri muda uliopita. Wananchi wa Urambo hawa wafugaji wa nyuki wameunda umoja wao kuna eneo tayari wameshaandaa la kuchenjua asali. Mimi kwa niaba yao na wao wenyewe pia waliandika barua; mimi niliandika barua na wao wakaandika barua tukapeleka Maliasili na Utalii kwenye Wizara. Wakakubali wakamtuma na Naibu Mkurugenzi wa nyuki akaja Urambo akaona lile jengo la wafugaji nyuki akalipenda akaahidi kwamba mimi hapa nitaleta maji na nitaleta umeme na nitaleta mashine; tukashangilia, tukapiga vigelegele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najisikia vibaya kwamba Serikali yetu tunayoithamini na kuiamini iliahidi itatoa mashine ya kuchenjua asali na waliahidi kwamba watatuchimbia kisima na kutuvutia umeme. Sasa hivi imekuwa kimya. Sasa nabaki unauliza; hivi ni mabadiliko ya Mawaziri au ni kitu gani hiki lakini Serikali ni moja? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa heshima na taadhima, Serikali inisikilize tupewe ile mashine tuliyoahidiwa tuchimbiwe kisima cha maji kama walivyoahidi na kutuvutia umeme kama walivyoahidi tuendelee kuheshimu Serikali yetu, Serikali ya Mama Dkt. Samia inaheshima yake. Halafu haya mawili ndiyo ninayasisitizia; kwanza turudishiwe eneo, tunakubali kabisa kuwa na hifadhi lakini turudishiwe eneo ili wanaofuga nyuki ambao wameunda umoja wao waendelee na kufuga nyuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa sababu ya ongezeko la watu waweze kufuga mifugo yao watugawie sehemu hiyo, tunathamini azimio, tunathamini TANAPA lakini na sisi tunaomba maombi yetu hayo mawili; kurudishiwa eneo na kuletewa vile vifaa walivyokubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo napongeza tena Kamati husika imefanya kazi nzuri; ahsanteni sana kwa kunisikiliza na ninaunga mkono hoja. (Makofi)