Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru lakini kipekee niipongeze Kamati kwa taarifa hii nzuri ambayo wameitoa kwa niaba yetu na yale mambo ambayo wameyabainisha. Tuisihi tu Serikali iweze kuyafanyia kazi hususani suala la kushindwa kutekeleza mchakato wa kuifanya TFS kuwa mamlaka na kuitoa kwenye uwakala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la zile sera ambazo zimepitwa na wakati even though kwenye taarifa inaonekana upande wa Serikali au upande wa wasimamizi wao wanasema hazijapitwa na wakati lakini Bunge ambalo ndiyo wawakilishi wa wananchi wanasema zimepitwa na wakati. Sasa saa nyingine najiuliza hawa watu wanamuwakilisha nani? Maana sisi ndiyo wawakilishi wa wananchi; tunaposema kwamba hili jambo linashida na limepitwa na wakati ni vizuri wakasikiliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimeanza na hii? Nataka tu leo niende kwa style ya tofauti kidogo ninataka ku-refer maandiko matakatifu katika Biblia. Ukisoma Mwanzo1: 25 inasema hivi; “Basi Mungu akafanya aina zote za wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa na viumbe vyote vitambaavyo, Mungu akaona ni vyema.” Mstari wa 26 unasema, “Kisha Mungu akasema; tumfanye Mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu akatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimekuwa najiuliza hata maandiko tu yalimpa power mwanadamu dhidi ya hawa wanyama lakini huko tulipo labda kwa sababu Wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wananchi wako tofauti na wote tunakutana humu kwenye Bunge kwa sababu tunawakilisha watu tofauti. Ukienda Ilala pale kwa Mheshimiwa Naibu Spika huwezi kusikia Naibu Spika anaomba josho humu ndani hata siku moja. Maana yeye anawakilisha watu tu ila mimi ninayetoka Biharamulo ninawakilisha wanyamapori maana ninahifadhi, ninawakilisha mifugo maana ninawafugaji na ninawakilisha wananchi sawa na nyie wengine ambao mnatoka kwenye majiji au maeneo mengine makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tulikuwa tunaomba pale tunapoleta mawazo na maoni yetu kama wawakilishi wa makundi haya matatu au makundi zaidi ya nyie ambao mnawakilisha kundi moja moja tupewe nafasi ya kusikilizwa kwa sababu hata maandiko yameelekeza hivyo. Kwa sababu inaumiza sana mimi kwangu sasa hivi wananchi wamekuwa wananyanyaswa. Mtu anakutwa na kuni tu, hivi kweli hata gesi ndiyo tumeanza kugawiwa juzi Wabunge; gesi si ndiyo tunagawana sasa hivi na tunazipeleka kule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea ya ruzuku tumepiga kelele hapa kwamba mbolea zinaishia wilayani hata kule vijijini hazifiki. Gesi tulipewa mitungi hapa sisi wa vijijini nilivyosema tunawakilisha makundi huenda wale tuliowapa baada ya ile gesi kwisha, hawajaenda ku-refill tena maana hata sehemu ya ku-refill hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuta mwananchi ana kuni tu ya kawaida unamnyang’anya baiskeli mwanamke, unamnyang’anya zile kuni; hivi kweli mnataka wapikie nini? Labda nyie mliozaliwa mjini mnajua alternative. Sasa sisi Wabunge wa vijijini tungeomba Serikali mtupe alternative, kwa mwananchi ambaye yuko kijijini ambaye leo hata kituo cha afya au zahanati hana anatembea kilometa tisa, kilometa 10 kutafuta ile lakini anakutwa na kuni ananyang’anywa zile kuni, mnataka hawa watu waende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaumiza and if we are here truly representing people tulione hili. Tumepeleka watu wamesoma wamekuja na sera zao lakini hizi sera mnazoenda huko shuleni mkasoma hebu basi zi-reflect maisha ya watu tunaowawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawafugaji kwangu wananyanyasika kila siku tunaongelea habari za wafugaji. Biharamulo leo ndiyo Jimbo namba 20 kwa wingi wa watu katika Taifa hili, Jimbo namba moja kwa wingi wa watu kwa Mkoa wa Kagera. Nimezungukwa na Hifadhi ya Burigi hiyo sina shida nayo lakini tuna maeneo mengi ya TFS yako pale yale mapori yamehifadhiwa. Watu wangu ng’ombe wanakamtwa kila siku wengine wanalalamika kwamba ng’ombe wanaswagwa wanaingiza mle wanatozwa. Hatukatai hapa Waziri atatetea kwa sababu analetewa ripoti, aliye wilayani atatetea kwa sababu analetewa ripoti lakini je, are we sure kwamba wale watu walioko huko chini wanatenda haki kwa hawa watu? Kwa nini wananchi wanalalamika kila wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wametutuma humu sisi kama sauti yao. Sasa sauti yetu sisi kama Wabunge tunapoongea leo three years niko humu ndani tunaongelea jambo hilo hilo la wananchi kunyanyaswa? Tunaongelea jambo la kuomba maeneo yapanuliwe ili wananchi waweze kupata maeneo ya kuchungia zaidi na kufanya shughuli zao za uchumi lakini tusisikilizwe; sasa anatakiwa asikilizwe nani? Yule mtu aliyeenda kusimamia pale au sisi tunaowawakilisha wale wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe Serikali chonde chonde tunaiomba Serikali kwenye hili itusikilize. Ilani ya CCM iliahidi watatenga maeneo kwa ajili ya wafugaji na kilimo, maeneo hawatayatenga kutoka kwangu mimi kwa sababu mimi sina eneo la kutengwa; yatatengwa kutoka kwenye maeneo ya Serikali yaliyohifadhiwa. Idadi ya watu inaongezeka, kama watu wanaendelea kuzaliana tunawaambia waongeze uzazi halafu maeneo ya kufanya shughuli zao za uchumi hatuwapi, hawa watu ni wa nini kuongezeka? Ni bora tukaanza sasa kufunga speed governor idadi ya watu isiongezeke kwa sababu hatuna maeneo ya kuwapa ijulikane, lakini watu wanaongezeka maeneo hayapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali ilichukue hili ili iweze kutusaidia hususani kwangu Biharamulo wananchi wangu wanateseka. Hili naomba wafugaji wa Biharamulo wanateseka, wananchi wa kawaida wanateseka. Mtu kama hana hata kuni akapikie nini? Kijijini tumezaliwa tunapikia kuni ndiyo nishati yetu ya kupikia. Siku gesi ikifika kule hata wao wataacha, hakuna mtu anayetaka kushinda kwenye moshi lakini for the time being that’s an alternative tuwaache wananchi wafanye shughuli zao za uchumi. (Makofi)

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa kuna taarifa huku; upande gani? Ahaa, Mheshimiwa Pallangyo.

TAARIFA

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Engineer Chiwelesa kwamba siyo kule kwake tu hata kule Arumeru Mashariki Eneo la Momela wananchi wananyanyasika sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Ezra unaipokea hiyo taarifa?

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa naipokea. Sasa nikiondoka hapo liko suala jingine ambalo limepigiwa sana kelele suala la wanyama hawa waliohifadhiwa (wanyamapori). Mimi kwangu Kata ya Nyakahura eneo moja linaitwa Nyabugombe kijiji kimeisha wananchi wote wamehama pale. Kwa sababu tembo wakihama usiku kila siku wanageuza kambi pale. Wanatoka porini wanaingia pale wanavuruga kila kitu siku wakiridhika wanaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaambiwa hapa habari ya kupanda pilipili, hivi kweli mwananchi akaoteshe pili pili kwanza pili pili kwenye buffer zone anaiotesha wapi? Kwa sababu buffer zone ile ya mita 500 mwananchi akisogea tu pale amekamatwa kaingia kwenye hifadhi. Sasa pili pili wananchi wazioteshe wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba kwa sababu wanyama hawa tumeona wanathamani sana na kweli wanatuingizia pesa za kigeni; kwa nini tusitengeneze electric fence tukazungusha yale maeneo ili wanyama wasitoke tuondoe na hii migogoro? Si wanaingiza hela? Tukatafute pesa tuwekeze ili tuweze kutengeneza pesa nyingine zaidi lakini tusitake kutengeneza pesa kwa expense ya wananchi kuendelea kuumia. Kwa sababu kuna mtu mwingine utamletea barabara lakini mazao yake yote yameharibika kwake haoni faida kwa sababu vitu vyote vimeharibika. Hawezi kusomesha watoto wake, hana chakula, hana nini kwake hata hiyo ukienda ukamwambia mambo gani ya maana ya kuhusu hifadhi hayaoni. Kwa hiyo, tunaomba Serikali itafute alternative. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameongea wenzangu habari ya magari lakini mimi ipo kesi nyingine. Unakuta kijiji A kiko hapa kimezungukwa siyo hifadhi hata kusema ni hifadhi ya national park kama hii, hifadhi tu ya TFS. Mwananchi anatakiwa aende kijiji cha pili ambapo labda ni kama kilometa moja au kilometa mbili lakini kwa sababu kuna hifadhi imemzunguka hamna hata njia haruhusiwi kupita. Matokeo yake mwananchi anasafiri kwa kutumia nauli kilometers and kilometers wakati pale; hivi mbona kwenye hifadhi leo watu wanaoenda Iringa, wanaoenda Mbeya mnapita kwenye Hifadhi ya Mikumi? Inakuwaje sisi mtu wa TFS mwananchi tu wa kawaida kupita mule na yenyewe wanaona ni kero? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechunga ng’ombe nikiwa mdogo nyumbani tulikuwa tunafuga. Hivi ng’ombe anayeenda kula majani pale chini kwenye miti ile ukamuacha akala majani anaharibu hifadhi gani pale? Sawa hata mimi nimesoma ingawa sijasomea hayo madude lakini sometimes we have to think. Ng’ombe ameenda amekula majani pale karudi nyumbani hifadhi gani anaiharibu pale? Yaani kuna migogoro mingine tunaitengeneza tu kwa sababu tumeamini watu wengine zaidi the so called wataalamu bila kuweza kwenda na logic. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaache wananchi wafanye shughuli zao maana mimi ukiniambia leo unatengeneza ranch ya Taifa sasa mbolea na maziwa hayo mnayohamasisha watu wanywe ng’ombe tukiwafugia sehemu moja hawa watu wa vijijini watakunywa maziwa lini au wenyewe hawana haki ya kunywa maziwa? Hiyo mbolea ya samadi wataipata lini ili waweze kulima? Kwa hiyo, kuna vitu vingine lazima tukubaliane, kama mtu anafuga ng’ombe wake wachache maeneo yale tangu zamani wametukuta tunafuga hebu wajaribu kuangalia jinsi ya kutengeneza mazingira mazuri na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliongea hapa akasema twende kwenye dialogue tuelewane lakini tukimaliza kuelewana ndani ya Bunge, Wabunge tunaondoka tunasema Serikali imetamka kupitia viongozi wakubwa lakini yanayofanyika kule siyo yale yanayotamkwa hapa ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe Waziri yuko hapa ayachukue, hawa ni watu wake, sauti yetu ndiyo sauti ya wananchi. Yaani hamtaweza kutawala kama Serikali kama wananchi tunaowawakilisha hawasikilizwi mambo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo naunga mkono hoja ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)