Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie Wizara hii ya Maliasili, Kamati ya Maliasili na Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tunayozungumza hapa wala hayahusu Mawaziri, yanahusu Serikali yetu ya CCM. Haya mambo ambayo tunayaangalia miaka nenda rudi, miaka nenda rudi wananchi wanafilisika. Wanafilisika kwa kunyang’anywa ng’ombe zao, wanafilisika kwa mazao yao kuliwa na tembo, wanafilisika watoto wao hawasomi, wanafilisika hawana chakula miaka nenda rudi tunaongea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama ni Mawaziri, mimi nadhani tatizo liko kwenye sisi Wabunge kabisa. Sisi Wabunge tunaotoka kwenye maeneo haya tuna matatizo. Kwa nini tunapitisha Bajeti ya Maliasili na Utalii na Ardhi wakati sisi wananchi wetu wanaenda kuumia? Sisi ndiyo wenye matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukubaliane bajeti ijayo na bajeti zinazokuja kama Serikali haina mpango wa kuweka fensi kwenye maeneo yetu, haina mpango wa kuzuia wanyama kwa mkakati tuzungumze mambo haya. Kuna haja gani ya kuwa Mbunge wakati watu wanakufa kila siku? Kuna haja gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi mama mmoja ameuawa na tembo pale, watoto wake wanauawa pale. Kila siku ni kuua watu, kila siku ni nini? Maeneo yangu yote ya vijiji 15 watu hawana chakula, hawana hata sasa hivi hamna kitu. Jana wanyama wote walishindia pale, kuna haja gani? Leo mtu wa Maliasili akipigiwa simu kwamba ng’ombe wako hapa dakika moja amefika lakini akipigiwa simu tembo wako hapa haji kuona hao tembo. Kuna nini kinachoendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani; sidhani kama kuna watu wanafanya vizrui. Pengine mimi nataka kuzungumzia mambo miwili; la kwanza pengne fedha zilizokuwa zinakwenda maana yake sasa hivi na huko nyuma kumekuwa tofauti. Baada ya Corona zile fedha za TANAPA, fedha za TFS, Ngorongoro na TAWA zilipoenda Serikalini hazirudi kwa wakati. Kwa hiyo, watu kila mkiwaambia hawana mafuta, hawana nini na kila kitu na hapa nimeona Kamati imesema vizuri, kweli kabisa tukubaliane kwamba fedha hizi zilizokuwa zinakusanywa kwenda Serikalini wawaachie wenyewe ili tuone udhibiti wao unaendaje kwenye mambo haya.

Mhehimiwa Mwenyekiti, lakini mimi siamini kama tunaweza tukazungumza miaka 300 watu wanakufa, watu wanafilisiwa tupo hapa Bungeni, siamini mambo kama hayo, siamini kama Serikali hatuwezi kuamu jambo, siamini kama wanyama walioumbwa na Mungu akatupa sisi wanadamu akili tuwatunze leo wanatuzidi akili, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiria Wabunge tulioko humu ndani tukubaliane kwamba hatuwezi kuongoza watu wanakufa, wanafilisiwa, watoto hawana madawati na kila kitu hakipo kwenye maeneo yetu, na tupo Wabunge humu tukafanye hiyo kazi. Kwa hiyo nafikiri kwamba hiyo ndiyo message inatakiwa iende eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vinginevyo kuna suala la fidia; fidia ya Vijiji vya Nyatwali, Serengeti na Tamau jamani kuna mambo ya ajabu sana. Nilizungumza Bunge lililopita hapa, Ngorongoro watu wamehama wamepewa maeneo mazuri ya kuishi wamepewa na fidia wamepewa na umeme wamepewa na mashamba. The same leo wakati wa Nyantwali wale nao wanapisha wanyama. Ngorongoro wanapisha wanayama ni kweli tunataka wananya wapite kwenye maeneo mazuri, wanapisha wananyama. Nyatwali, Tamau na Serengeti ni vijiji ambavyo vina registration zake vinapisha wanayama unawapa shilingi milioni mbili. Unawahamisha unasema mwezi wa tatu utawalipa, mpaka leo hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawalimi na hawafanyi chochote. Haya mateso ni ya nini. Haya mateso watu wanakula kwenye nchi hii ni ya nini sasa? Kwa hiyo, nawaomba wanaohusika na mama anasikia haya maneno tunazungumza anasikia nendeni mkawalipe. Nimeongea na Waziri asubuhi hapa amesema wako tayari kulipa wakati wowote, basi nendeni mkalipe. Nendeni mkawalipe wale watu angalau wajue wanaenda wapi. Mpaka leo hawalimi na hawafanyi kazi yoyote. Kwa hiyo, nafikiri kwamba nalo hilo mlichukue muende mkalifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimesikia Wabunge hapa wanasema kifuta machozi na kifuta jasho. Sasa wakasema kilomita tano kilomita ngapi. Kuna sheria za ajabu na zimetungwa 2004 sijui 2009. Maana yake ni kwamba ukienda zaidi ya kilomita tano ukikuta shamba la hekari 20 limelimwa huyu mtu analipwa hekari tano tu. Hekari tano kwa kipimo cha kawaida analipwa shilingi laki tano; ndivyo sheria ndiyo inasema hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake kwa hekari moja ambayo anapata gunia 30 ukizidisha kwa shilingi laki moja kwa gunia anayoweza kupata shilingi laki tatu, anapata shilingi laki tano kwa heka tano. Heka 15 nyingine ni sadaka kwa tembo. Haya maneno gani haya? Kanuni hiyo inasema hivyo, sasa ni maneno gani haya? Kanuni ambayo unaweza kuleta hapa kesho tukaibadili, haiji. Mheshimiwa Waziri aende alete hiyo kanuni ili tuibadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kusema kweli mimi nasema, Wizara ya Maliasili na Utalii, hii bajeti inayokuja mjiandae mtusaidie, itusaidie kwenye haya mambo. Hatuwezi kuwa tunakaa hapa kila siku tunapiga kelele watu wanaumia, haiwezekani. Kama fidia imeleta shida kwa nini South Africa, Botswana, Kenya wameweka fence wamefaulu, kwa nini Serengeti wameweka fence sehemu nyingine wamefaulu? Kwa nini tusikubali fedha zote hizi za fidia ziende kwenye fence? Shida iko wapi? Watu wanahangaika kila mwaka tunaangalia. Kwa hiyo, hilo nalo tulizungumze tuone linaenda maeneo gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la migogoro ya ardhi, migogoro ya ardhi tunaisababisha sisi. Waliunda hapa Kamati ya Mawaziri sijui 10 wakazunguka wakawa sijui na interest zao. Yaani huku ndani unashindwa kuelewa hiki ni kitu gani? Hivi kweli kwa mfano watu wa Bunda, Eneo la Nyatwali, Eneo la Serengeti, Eneo la Tamau mmechukua kwa ajili kuwapa wanyama wetu. Watu wamehamia Kijiji cha Mekomariro ambako kulikuwa na eneo; kijiji hicho hicho mnaenda mnatengeneza eneo kwamba kuna mwekezaji atakaa hapa. Mwekezaji hajulikani, yuko mfukoni mwa mtu; watu wanateseka maeneo hayo kila siku. Kijiji cha Mekomariro wameteka eneo la wafugaji, kuna mtu ameenda amejenga mule ndani, hatoki, Mkuu wa Mkoa anajitahidi sana kumtoa, hatoki. Sasa nashindwa kuelewa ni nini hiki, mtu hana hati hana nini, hatoki. Sasa Serikali hii tunakuwaje? Haya ni mambo gani haya yanaonekana? Nimemuomba Waziri Mchengerwa na nimemuomba Waziri wa Ardhi waende pale basi watusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaamini kama leo Mawaziri wa Maliasili na utalii, TAMISEMI na Waziri wa Ardhi tukikaa pamoja na Wabunge wote wenye matatizo tunaweza kutatua matatizo. Hivi ardhi ni ya nini? Hivi kweli ardhi ni ya Nani, si ni ya kwetu sisi? Hivi ukisema wewe sita una kashamba, chukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi watalii wanahitaji tembo wangapi ili tupate hela? Hivi ili tupate hela kwenye hii Wizara tunahitaji tembo wangapi? Sasa mbona ardhi ni kubwa na bado tunanyanyasika, watu tunanyanyasika ili hali ardhi ipo. Pale kwenye matatizo gawa ibaki. Tuna mapori sijui mapori sijui mapori ya akiba, yale mapori hifadhi za Taifa 22. Zinazofanya kazi ziko tano tu. Nyingine zipo tunatunza tu. Hivi maana ya akiba ni nini? Maana ya pori la akiba ni nini? Maana yake ni kwamba wanadamu wakizidiwa wasaidiwe. Sasa haya ni maneno gani? Naona mambo haya yananishinda sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana jamani wala hamna mgogoro na Waziri, watendaji wetu wanafanya kazi vizuri na hawa TANAPA wanfanya kazi vizuri, isipokuwa wanazidiwa. Maamuzi tufanye sisi Wabunge. Maana sisi ndio tunatunga sheria. Si kila mtu amegawana? Tukubaliane kwenye maeneo haya ambayo ni hatari Wabunge tujikusanye tuandike matatizo tuliyo nayo kwenye maeneo yetu tuje hapa tukae na Mawaziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na wa TAMISEMI, tukubaliane bwana haya yatoke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake imefikia wakati sasa sisi Serikali ya CCM tukiwajengea watu madarasa, Barabara na tukiwapa watu umeme lakini wamekaa na nyongo za maisha hivi wanatupigiaje kura? Kwa nini watupigie kura. Lazima CCM tukubaliane hii hali, tutaendelea kutawala, tutoe au tuwatolee watu nyongo kwenye roho zao. Tutoe nyongo, watu wanatapika nyongo. Leo mnaona Mwenezi anatembea mahali watu wanaenda na makaratasi wamejaa kila mahali. Wamejaa nyongo, tuondoe hizi nyongo. Nakushukuru.