Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi, na nianze kwa kuunga mkono taarifa hii ya Kamati yetu ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Naipongeza Kamati kwa taarifa nzuri na maazimio waliyoyatoa; na zaidi nishukuru kwa ushirikiano ambao wanatupatia mimi, Naibu Waziri pamoja na uongozi mzima wa Wizara pamoja na taasisi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao mmeweza kuchangia hoja hii. Utaweza kuona ni kwa namna gani hoja hii au Wizara hii inavyogusa wananchi wetu huko, na tunawashukuru ninyi kama wawakilishi wa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kujibia au kutoa ufafanuzi katika maeneo machache napenda tu kusema kwamba tutaendelea kutekeleza majukumu ya Wizara, na napenda kusema kwamba Mheshimiwa Rais amekuwa akifuatilia kwa ukaribu na kutuelekeza katika maeneo mbalimbali. Kubwa ikiwa ni suala zima la kulinda na kuimarisha uhifadhi wetu; lakini vingine kuendele kuhamasisha na kutunza utalii tulionao na tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote na wajumbe wa Kamati kwa namna ambavyo wameendelea kutupa uongozi, lakini vilevile, kwa namna ambavyo wameendelea kutushauri katika kusimamia maeneo hayo makuu kama mlivyowaeleza kama tulivyokasimiwa na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo napenda sasa kutoa ufafanuzi katika maeneo kadhaa ambayo yameelekezwa na Kamati kupitia taarifa. Vilevile, maeneo mengine ambayo wamegusia Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kuhusiana na zoezi zima la uhamishaji kwa hiari kwa wananchi wa eneo la Ngorogoro ambao wanahamia Msomera, kwa wale ambao wako tayari kuhamia Saunyi, lakini vilevile wengeine ambao watahamia Kitwai D kule Simanjiro na wengine pia watahamia katika maeneo ambayo watayachagua. Niishukuru Kamati ilitembelea Msomera na waliweza kutoa maoni mbalimbali walipofika huko. Maelekezo na ushauri ambao kweli tunaendelea kutekeleza na tunaamini yatatuletea tija kubwa pamoja na ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea maelekezo ya kuendelea kuunda timu ya Wizara za Kisekta. Niwahakikishie tu waheshimiwa wajumbe wa Kamati na Wabunge tumeunda timu ya Wizara za Kisekata na wataalamu wetu wamekuwa wakiendelea kufanya uratibu kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge. Namshukuru dada yangu Mheshimiwa Jenista na wengine wpte chini ya Ofisi ya Waziri mkuu ambao wamekuwa wakishirikiana nasi lakini na Wizara zile nyingine; kwa sababu bila wao kutekeleza matakwa mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu, upelekaji wa huduma ya maji na barabara tusingeweza kufika hapa tulipofika na kuweza kukamilisha ujenzi huu wa nyumba. Kipekee nashukuru sana. Mimi na wenzangu tunashukuru Wizara hizo za kisekta pia kwa namna ambavyo wametimiza wajibu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya utekelezwaji wa bajeti kwenye miradi ya maendeleo, tunashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati na Wabunge wote ambao wameweza kutoa ushauri wa bajeti yetu kuweza kutoka kwa wakati na hasa ile ya maendeleo pamoja na Matumizi Mengineyo (OC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kufanya mashauriano na Wizara ya Fedha ili kuweza kuongeza kasi ya utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo, na bahati nzuri Jumanne tutakutana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake na tunaamini tutaweza kupiga hatua kubwa lakini tunashukuru na tunapokea ushauri huu ambao mmeweza kuutoa na tunaamini tutakapokutana, lengo letu, na Waziri wa Fedha pamoja na Serikali kwa ujumla ni kuona ni kwa namna gani tunaendeleza zaidi miundombinu ndani ya hifadhi zetu, vilevile kuona ni kwa namna gani tunaunganisha barabara kati ya Wilaya moja na nyingine na kwenye hili tutaendelea kupata ushirikiano mkubwa wa TARURA. Pia zile ambazo zinavuka Mkoa na Mkoa ili tuhakikishe kwamba na hata zile hifadhi nilimsikia dada yangu Mheshimiwa Taska, za Katavi na kwingineko ambako unakuta labda huoni zikitangazwa sana au zikipata watalii wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii wa Kusini na maeneo mengine tunaamini tukiweza kupata miundombinu ya kuunganisha Wilaya zetu vizuri basi itakuwa rahisi hata tunavyofanya uhamasishaji na watalii waweze kufika katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya ile account ya ESCROW lakini vilevile kuona ni kwa namna gani taasisi zetu zitapata retention. Ni eneo ambalo vilevile tumeendelea kufanya mashauriano na Wizara ya Fedha, watakopokuwa wakiandaa ule Muswada wa Fedha ambao unakuja kila mwaka basi kuweza kuona ni kwa namna gani taasisi zetu zitawezeshwa kubaki na makusanyo yake moja kwa moja badala ya kuzipeleka Mfuko Mkuu wa Hazina na kurudi ili tuweze kuzitumia katika kuendeleza taasisi zetu. Vilevile, pale itakapohitajika kuendeleza miundombinu na kufanya shughuli nyingine kwa ufanisi, tuweze kufanya hivyo huku tukitambua pia bado tuna jukumu la ulinzi pamoja na suala zima la uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo kubwa ambalo ukiliangalia kwa leo lilikuwa ni changamoto la wanyama wakali na waharibifu, limesemewa kwa kiasi kikubwa sana. Kwenye hili kwa kweli napenda kusema kwamba tunaendelea kutoa pole kwa wananchi wetu ambao wameathirika na wanyama hawa. Hatuwezi kusema kwamba tunajali wanyama kuliko binadamu. Obviously binadamu ni namba moja, ndiyo sisi tupo. Mheshimiwa Mbunge wa Biharamulo mpaka ameamua kutoa na maandiko kabisa ya Biblia, wakati huo huo na hifadhi zetu tunazihitaji kwa hiyo lengo letu kubwa ni kuona kunakuwa na hiyo balance kuhakikisha kwamba utajiri tuliopewa huo wa wanyamapori basi usije ukaathiri na wananchi wetu wakaona hakuna umuhimu kabisa wa kuweza kuwa na uhifadhi na uwepo wa wanyama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea kuchukua hatua za dhati kabisa na bahati nzuri mtakumbuka hata Mheshimiwa Rais alipofanya ziara katika Mkoa wa Lindi alielekeza Kamati zetu za ulinzi na usalama lakini alituelekeza pia na sisi tuweze kutafuta muarobaini wa changamoto hii ya muingiliano kati ya wanyamaporti na binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba tulishafanya tathmini hasa kwa Wilaya ambazo zimeathiriwa sana takriban Wilaya 44, tayari ukiangalia kwa Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Lindi na kwingineko tunaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba kwa wale ambao walitoka nje tunawarudisha ndani. Pia, kama kuna wengine wanafanya vitendo visivyo ndani na wenyewe kuweza kuwatoa nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ukiangallia chanzo kikubwa, tunahangaika na chanzo. Wanyamapori wengi wanatoka nje hasa wakati wa kiangazi wanapokuwa wanatafuta maji, kwa hiyo kwenye eneo hili kama Serikali tunaendelea kufanya kazi kwa kuchukua hatua kuona ni kwa namna gani tunaongeza kasi ya uwekezaji zaidi, kuhakikisha tunachimba mabwawa mengi zaidi katika hifadhi zetu ili kuhakikisha kwamba wanyama hawa hawalazimiki kutoka nje ya hifadhi kuweza kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaanza katika hifadhi yetu ya Mkomazi na nyinginezo na tutaendelea kuongeza bajeti ili kuhakikisha tunatekeleza katika hifadhi zote kwa idadi inayojitosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni matumizi ya teknolojia, mmeeleza vizuri sana Waheshimiwa Wabunge. Tumeshaanza kuangalia ni kwa namna gani tutatumia drones ili kuhakikisha kwamba zinatusaidia katika suala zima la doria, udhibiti na ulinzi. Tumeshaanza mafunzo kwa wanafunzi wetu, askari wetu ili waweze kuzitumia kwa suala zima la doria pamoja na kuhakikisha tunadhibiti Tembo wetu na wanyama wengine wakali na waharibifu wasiweze kutoka ndani ya hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, nimesikia kulikuwa kuna hoja ya kuweka fensi za umeme, watu wametoa mfano wa Botswana na Afrika Kusini. Ni kweli na sisi tumefanya kwa kiasi kidogo kwa upande wa Grumeti kwa Serengeti na tunaona mafanikio. Kwa changamoto tuliyonayo kama Tanzania ukilinganisha na nchi zingine, wenzetu wengi zaidi hifadhi zao wanamiliki watu binafsi. Wengine pia kwa nchi hizo maeneo hayo ni madogo kwa hiyo hata akiweka fensi ya umeme unajikuta pia inawezekana na wala hamiliki eneo kubwa sana. Kwa upande wetu tutafanya kwa maeneo kwa hali ya uwezo wetu wa kiuchumi utakavyoruhusu. Pia, tunatumia mfumo mwingine wa kielektroniki wa geo-fencing ili kuweka parameters ambazo ikitokea mnyama ametoka amevuka kiasi kadhaa kitakachokuwa kimekuwa set basi iweze kutoa alert na kuweza kujua mapema ameelekea wapi kabla ya hajafika mbali kutoka nje na kuleta madhara ili aweze kurudishwa ndani hifadhini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba tunaendela kuongeza vituo vyetu vya askari. Tayari kwa miaka miwili tumejenga zaidi ya vituo vya askari 16 na mwaka huu pia tunajenga vingine 16 katika bajeti hii ya 2023/2024 na tutaendelea kufanya hivyo mwaka hadi mwaka ili kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo yanapakana na hifadhi zetu basi tunakuwa na vituo ambavyo vitakuwa na askari. Tayari kwa mwaka huu wa 2023/2024 tutakuwa na askari tutakaoajiri zaidi ya 350 na tumeendelea kupata vibali kutoka Ofisi ya Rais, Utumishi, kwa ajili ya kuweza kuajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja nyingine ilijitokeza ya kuwawezesha TAWIRI na TAFORI, tunapokea ushauri tukitambua kwamba taasisi zetu za utafiti hizi ni muhimu sana katika suala zima la maendeleo ya uhifadhi, menejimenti, uendelevu na usalama wa uhifadhi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla muda wangu haujaisha najitahidi kuongea kuhusu suala zima la masuala ya fidia na hasa eneo la kifuta jasho na kifuta machozi. Waheshimiwa Wabunge mmelieleza vizuri sana, na kwa kweli kama nilivyosema tunaumia tunapoona binadamu, tunapoona wanyama wengine wanaumizwa, tunapoona ndugu zetu mazao yao yanaathiriwa na wengine kumalizika kabisa na wengine kufilisika hata kupelekea kuingia katika njaa kubwa kutokana na mazao yao kuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge tumeendelea kufanya uhakiki, tunaendelea kufanya malipo na hata mwezi Januari mwaka huu tumeweza kufanya uhakiki kwa ajili ya kuweza kulipa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kanuni za kifuta jasho na kifuta machozi, tayari tulishafanya mapitio na tulishayakamilisha. Tumepeleka Wizara ya Fedha kwa wenzetu ili nao waweze kuangalia tathmini, waweze kuona ni athari kiasi gani za kiuchumi zitakazoweza kujitokeza na kuona uwezo wa nchi katika kulitekeleza suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Sheria ya Uendeshaji wa Mamlaka ya TAWA na TFS, yenyewe bado ni maeneo ambayo tunayatekeleza, Nawahakikishia Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati na Wabunge wote waliochangia hoja hiyo, tunaendelea kulifanyia kazi ndani ya Serikali na pindi litakapokamilika basi litaweza kuwasilishwa Bungeni sambamba na kuhuisha sera mbalimbali na sheria nyingine zinazosimamia wanyamapori, misitu na sera nyingine chini ya Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vivutio vya utalii tutaendelea kutangaza na tutaendelea kubuni mikakati mbalimbali kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini sambamba na kuongeza uwekezaji katika ujenzi wa vyumba vya malazi ili watalii hao wanaokuja nchini waweze kupata maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa pendekezo lile la kuunda mfuko wa maendeleo ya utalii ambalo Kamati mmelitoa. Napenda kusema kwamba tumeunda Kamati ya kimkakati ambayo nayo pia itaendelea kufanya uchambuzi wa eneo hilo ili kuona endapo linaanzishwa lianzishwe kwa namna gani lakini ni eneo ambalo kwa kweli tunaliunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kabla muda haujaniishia ya WMA, nisipoeleza nitakuwa sijatenda haki. Tunazo WMA takribani 22 na tunaendelea kufanya nazo kazi vizuri sana. Tunawategemea sana katika suala zima la uhifadhi na maendeleo na lengo letu ni kuona ni kwa namna gani tunaendelea kushirikiana nao kwa karibu zaidi ili kuhakikisha kwamba wanatusaidia katika ulinzi. Vilevile, kuona ni kwa namna gani masuala ya utalii kupitia WMAs hizo zinaweza kutuletea ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa fedha ambazo zinadaiwa, tunaendelea kushauriana na Wizara ya Fedha zitoke haraka, lengo letu kubwa ni ikiwezekana kile kilicho chao wapewe mapema halafu zile zingine za taasisi za Serikali ikibidi kama itahitajika ndiyo ziende Serikalini badala ya kuchanganya na zile za WMAs pamoja na Halmashauri zetu za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kulikuwa kuna hoja kuhusiana na utekelezaji wa Azimio la Bunge la kuridhia mapendekezo ya kurekebisha mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Napenda kuwashukuru Kamati hii ni hoja ambayo kwa kweli azimio wamekuwa wakilifuatilia sana kwa niaba ya Bunge. Tunaiona hoja ya Kamati kama Wizara na kama Serikali, kama Serikali tumeshafanyia kazi suala hili tulirekebisha mpaka, GN iliweza kutoka 754 lakini bado haijaweza kukidhi kama vile ambavyo Kamati au Bunge liliweza kuelekeza katika Azimio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba tunaiona hoja ya Kamati na tunaiona hoja ya Bunge na ni Azimio halali la Bunge ambalo linapaswa kutekelezwa. Hata hivyo, wiki iliyopita tuliweza kuitishwa na Waziri wetu wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mawaziri Nane kuweza kufuatilia utekelezaji wa maagizo yote kuhusiana na migogoro ile ya vijiji 975 lakini tukabaini pia kuna shauri limefunguliwa, Shauri Namba 46 la mwaka 2023, lilifunguliwa mwezi Disemba katika Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika Mashariki, takriban wananchi 855 wamefungua shauri hilo kuweza kupinga baadhi ya utekelezaji wa maeneo. Kwa hiyo bado tunaendelea kuhangaika lakini napenda kusema kwamba hiyo bado haituzuii kufanya hatua za kiutawala sisi ndani ya Serikali, kuweza kuendelea kuangalia Azimio lilitutaka nini, tufanyeje tathmini uwandani tutaendela nayo, lakini wakati huo huo kuweza kuona endapo tutatoa ardhi basi tutoe ardhi kwa kiasi gani bila kuathiri masuala mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu kwa namna Azimio lilivyowekwa sasa kama ikiwaridhia Wajumbe wa Kamati maana hili ni Azimio lao na hii nii taarifa yao, tulikuwa tunaomba marekebisho kidogo kwenye lile Azimio mwishoni pale kama ilivyowekwa ili kuweza kuona ni kwa namna gani sasa basi wakati tunaendelea na hatua zingine, itakapohitimishwa ile kesi, basi tutekeleza kwa mujibu wa hukumu itakavyokuwa imetoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nawashukuru sana Wajumbe wote wa Kamati yetu pamoja na Wabunge wote waliochangia katika taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. (Makofi)