Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuhitimisha hoja hii ya Kamati ambayo tuliianza mapema asubuhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, kwanza, kwa kukubali kupokea hoja hii ya Kamati lakini kuijadili na kuiunga mkono. Tumepata bahati ya kuwa na wachangiaji wengi, hoja yetu imechangiwa na wachangiaji karibu 16, siwezi kuwataja wote kwa sababu ya muda lakini tunathamini na kutambua sana michango ambayo Waheshimiwa Wabunge wameitoa katika kuchangia hoja yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pia, namshukuru Mheshimwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa michango yao ambayo imesaidia kwa sehemu kubwa kutoa ufafanuzi wa yale yote ambayo yamesemwa kwenye taarifa ya Kamati na ambayo yamesemwa na Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu hiyo wamenirahisishia kazi yangu ya kuhitimisha hoja itakuwa fupi. Naomba kutumia nafasi hii kuongeza ufafanuzi kwenye maeneo machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, katika eneo ambalo limechangiwa sana na Waheshimiwa Wabunge karibu wote ni migogoro ya ardhi na suala la kupanga, kupima na kumilikisha pamoja na jambo zima linalohusiana na mipango ya matumizi bora ya ardhi. Lazima tukubaliane, nchi hii ni ya kwetu sisi sote, nchi yetu ni ya amani yenye utulivu wa kutosha, tunaweza kuchukua mfano wa amani na utulivu wa nchi yetu kama shati zuri jeupe lakini migogoro ya ardhi inaweza kuwa sehemu au naweza kuifananisha na kidoa kidogo chekundu kinachokuja kwa kasi kwenda kuchafua shati letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tusipochukua hatua za haraka kwenye eneo hili, huko tunapokwenda hatma yake siyo nzuri. Kama tulivyosema kwenye taarifa ya Kamati tunaiomba Serikali iendelee kuangalia namna ya kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee tunaipongeza Wizara, kama tulivyosema asubuhi tunaamini sehemu kubwa ya utatuzi wa migogoro hii ya ardhi kwanza ni mfumo wa kidijitali wa kusimamia ardhi yetu. Mfumo ambao mtu anaweza kuingia, akakaa mahali alipo, akaangalia akajua kila kipande cha ardhi katika nchi hii kinasimamiwa na nani? kinamilikiwa na nani? na kipo kwa ajili ya kazi gani? Tukifanya hivyo tutakuwa tumefika pazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia nyingine ya kutatua migogoro hii ya ardhi ni hili zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha lakini hasa kutengeneza mipango ya matumizi bora ya ardhi. Ziko tafiti zimefanyika duniani kote na nyingine zimefanyika ndani ya nchi yetu. Mimi nimefanikiwa kuona tafiti mbili zimefanywa na Chuo chetu Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi. Walifanya moja kwa nchi nzima lakini moja walifanya kwenye Wilaya za Kilombero, Mvomero pamoja na Kilosa. Moja ya njia bora inayoshauriwa kama sehemu ya utatuzi wa migogogro ya ardhi ni kutengeneza mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye nchi yetu. Ndiyo maana kama Kamati tumeweka msisitizo kwamba Serikali iendellee kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kusema kidogo ni kuhusu suala la kodi ya ardhi (land rent). Waheshimiwa Wabunge wamechangia vizuri, ni kweli sisi Bunge ndiyo tulipitisha Sheria ya Fedha na ilikuja na pendekezo la kuhamisha makusanyo ya land rent yakafanyike kwenye Halmashauri. Changamoto ya jambo hili, moja ni mifumo yote ya kiutumishi na mifumo yote ya kusimamia ardhi iko Wizara ya Ardhi. Mwenye database ya wamiliki wa ardhi wanaopaswa kulipa kodi ya ardhi iko Wizara ya Ardhi. Zaidi ya yote changamoto nyingine kubwa sisi kwenye nchi yetu ardhi ni mali ya umma na iko chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Rais. Kila mmoja anapopewa hati masharti makubwa mawili ya kuwa na hati ni kulipa kodi na kufanya maendelezo. Mtu asiyelipa kodi Sheria inaruhusu kufanya revocation ya hati yoyote ambayo hailipiwi kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anayesimamia ardhi ni mwingine, anayeweza kufanya revocation ni mwingine lakini mapato au kodi anakwenda kukusanya mtu mwingine, jambo hili haliwezekani! Tunaomba Serikali ikubali kama siyo kubadilisha basi tunakokwenda kwenye Sheria ile ya Fedha tutoe jambo hili tuwaachie watu wa Wizara ya Ardhi kazi ya kuendelea na jukumu hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limekuwepo hapa jambo kuhusu watumishi wa sekta ya ardhi. Jambo hili lina mjadala mpana, kwamba waendelee kubaki Wizara ya Ardhi au warudi Halmashauri. Waheshimiwa Wabunge tukumbuke, kabla ya mfumo huu wa sasa Watumishi wa Ardhi walikuwa chini ya Halmashauri zetu na tumeona ndiyo sehemu kubwa ya changamoto hizi za ardhi kwa sababu Wizara ilikuwa haina nguvu ya kuwasimamia moja kwa moja. Kamati tumeliona lakini tumeliacha kwa Serikali, Bunge tunaendelea kulitafakari zaidi, huu ni mjadala mpana namna gani ya kwenda na jambo hili, lakini kwa hili tunaona kama Kamati watumishi hawa wakiendelea kuwa chini ya Wizara ya Ardhi itasaidia kuwasimamia vizuri na kwa ukaribu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo moja Mheshimiwa Kunambi alilisema kwamba kwa Serikali kuwapeleka watumishi Wizara ya Ardhi imevunja Sheria ya Mipango Miji, naomba niliweke hili sawasawa. Sheria ya Mipango Miji kwa asilimia zaidi ya 70 mtekelezaji wake ni Wizara ya Ardhi. Sheria ya Mipango Miji ni kweli inatoa jukumu, planning authority kuwa ni Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwa watumishi hawa kutokuwa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa hakuathiri chochote kwenye sheria, kwa sababu hata wakati wakiwa kwenye Halmashauri, tunaposema Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwenye Halmashauri ni Full Council. Hawa watumishi kazi yao ni kuwa-facilitate Madiwani ili waweze kufanya kazi vizuri, jukumu ambalo wanaweza kulifanya hata wakiwa chini ya Wizara ya Ardhi kwa sababu wanafanya kazi kule kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwenye upande wa ardhi ni kwenye eneo la fidia. Limesemwa sana na kwa kirefu na Waheshimiwa Wabunge naomba Serikali ilisikie. Changamoto kubwa kwenye fidia ni tatu, moja, kuna kuchelewa kwa kulipwa fidia hasa kama ardhi inatwaliwa. Changamoto ya pili kumekuwa na malalamiko ya fidia ambayo ni kidogo na ya tatu mara nyingi Serikali inafanya uthamini halafu baadaye inaahirisha kuchukua yale maeneo na kuwarudishia wananchi. Jambo hili linawakwaza wananchi linawarudisha nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoa ushauri mzuri na mapendekezo mazuri kwenye taarifa yetu ya Kamati namna ya kuhakikisha kwamba uhakika wa fedha unapatikana kabla Serikali haijafanya uthamini na kuchukua ardhi za wananchi. Naamini mapendekezo tuliyoyatoa yakifanyiwa kazi na Serikali yatatufikisha mahali pazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwenye upande wa sekta ya ardhi ni Kamati ile ya Mawaziri Nane wa kisekta, jambo hili limesemwa muda mrefu, binafsi natambua na kukiri kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Kamati ile ya Mawaziri Nane, tunachokiomba kwa Serikali ni jambo hili lifike mwisho. Tumelisema muda mrefu lakini hatma yake ni nini? Kwenye kila eneo tumeamua nini, tumetekeleza nini? Tunaomba Serikali ifikishe mwisho jambo hili ili matunda ambayo yalitarajiwa na Mheshimiwa Rais wakati wa kuunda Kamati hii yaweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa hoja za Wizara ya Maliasili na Utalii, pia yamesemwa mengi na siwezi kuyasema yote na Mheshimiwa Waziri amenisaidia, amesema vizuri, ntasema machache tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ni kuhusu utendaji kazi wa Taasisi zetu za Uhifadhi; kwanza natumia Bunge lako Tukufu kukiri na kuwapongeza watumishi wetu, askari wetu wa Jeshi la Uhifadhi kwenye Taasisi zote, kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana kwenye mazingira magumu. Kama Bunge na kama viongozi, lazima tuwatie moyo askari wetu hawa, wanafanya kazi nzuri kupambana na ujangili, wanafanya kazi nzuri kutunza maeneo yetu ya uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tumesema vizuri kuna changamoto nyingi, tunampongeza Mheshimiwa Rais ametangaza utalii kwa mfano, watalii wameongezeka. Kutangaza utalii, utalii ni biashara, kwenye biashara kutangaza ni hatua ya kwanza kwa maana kuisema na kuizungumzia biashara yako, lakini matangazo ya pili ambayo ni ya msingi, ni huduma anayokuja kupata huyo mteja wako unayemkaribisha kwenye biashara. Bila kuweka mikakati mizuri ya kukarabati miundombinu kwenye maeneo ya uhifadhi, watalii wanaokuja hawatapata huduma nzuri watakasirika, wataondoka na wengi wao hawatarudi na hawatatusemea vizuri kule wanapokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuiomba Serikali tumeweka azimio lile, tuunge mkono tukalitekeleze, tuwape taasisi za uhifadhi fedha ili waende wakatekeleze majukumu yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekiri, eneo kubwa ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelisema na kwa kweli kama kuna jambo ambalo pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini kama kuna eneo ambalo linawakwaza wananchi kwa sasa ni athari za wanyama wakali na waharibifu, jambo hili ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali, tunaiomba ilione kwa ukubwa huo, ilione kwa upana wake, lakini kubwa pia na kile kifuta jasho na kifuta machozi kwa muda mrefu tumesema tumeweka azimio, tumeomba Serikali ikatekeleze kufanya marekebisho ili kiendane na maisha na hali halisi ya uchumi ya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la WMA; namshukuru sana Mheshimiwa Olelekaita, amelisema vizuri na ametoa darasa zuri sana kuhusu Jumuiya za Hifadhi za Jamii. Tunaiomba Serikali, pendekezo letu lina nia njema sana na pendekezo hili hata wenyewe watu wa TAWA linawakwaza, TAWA anapotengenezewa ceiling kwenye bajeti, wana-include mpaka na hela za WMA wakati TAWA hana kazi nazo wala siyo sehemu ya mapato yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inafanya ceiling inakuwa chini, wakipata fedha zinakwenda kwenye WMA, wanapunguza mapato kwa ajili ya kufanya wao kazi zao za uhifadhi. Tunawaomba pendekezo hilo mlichukue, tuweke utaratibu, inawezekana, kama mwekezaji anataka kulipa, kwa sababu kwenye kanuni inajulikana, alipe hela ya Serikali, alipe hela Halmashauri, alipe hela WMA tuachane, kusiwe na haja kubwa ya watu kusubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo hili la TAWA na TFS; kwa kweli kama kuna eneo ambalo tumesema sana kama Bunge, ni eneo hili. Tunaposema leo TAWA ina Bodi ya Ushauri, ilianzishwa kwa Amri ya Serikali ambayo ilitengenezwa chini ya kifungu cha 8 cha Sheria ya Wanyamapori. Jambo hili linapunguza ufanisi kwenye utendaji kazi wa TAWA. Tunaiomba Serikali ituelewe kwenye eneo hili, na kwa kuwa tumelipigia kelele muda mrefu, tunaomba itoke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wako katika hatua mbalimbali, lakini mara ya mwisho alivyokuja kwenye Kamati walisema kwamba wao kama Serikali kwa sasa hawaoni umuhimu. Bunge lako Tukufu liliona umuhimu na ndiyo maana tuliweka azimio. Tunaiomba Serikali ikatekeleze azimio hilo ili mambo yakae vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni azimio lile kuhusu hoteli na lodge ambazo zimetelekezwa. Mtu mwingine anaweza akasema kwa nini Kamati inazungumzia hoteli na lodge hii ni mara ya pili. Malazi ni eneo muhimu sana katika shughuli za utalii, leo tunapozungumza, kwa mujibu wa Taarifa ya Wizara yenyewe ya uthamini wa maeneo hali ya malazi nchini ya mwaka 2021, kwenye nchi hii tuna maeneo ya malazi 10,432 ambayo yana vitanda 132,676. Katika hivyo vyote, maeneo ambayo yana hadhi ya juu ambayo watalii wanayapenda na yanawafaa ni maeneo ya malazi 1,437 ambayo ni sawa na asilimia 13 ya maeneo yote ya malazi. Katika haya maeneo ambayo yapo ndani ya hifadhi au yanamilikiwa na Serikali, ni maeneo 261.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunasema kuhusu hizi hoteli, ziko hoteli ambazo zilikuwa kwenye maeneo ambayo ni potential kabisa kwenye hifadhi zetu ambazo watalii walipenda kukaa kwenye hizo hoteli zilikuwa zinafanya kazi. Tunajua Serikali ilizibinafsisha, iliziuza. Tumeenda mbali kwenye Kamati, tumeona mpaka na sehemu ya ile mikataba, maeneo mengine pamoja na kwamba ziliuzwa, lakini ziliuzwa kwa masharti. Lazima kuwe na sharti la kuendeleza, kulikuwa na kiwango cha fedha cha kuwekeza, lakini lazima ulete na mpango wa masoko na mpango wa uwekezaji. Serikali ilipewa nafasi ya kuendelea kufuatilia utendaji kazi wa hizi hoteli. Tunaiomba Serikali ilifanyie kazi eneo hili ili mambo yaweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni mahitaji ya ardhi kwa ajili ya matumizi mengine. Amesema vizuri Mheshimiwa Margaret Sitta na ni kweli alikuja kwenye Kamati, tulisema wakati ule na leo amesema tena. Hakuna anayepinga kuanzishwa kwa hifadhi; mwaka 2019 bahati nzuri ilikuwa ndani ya Bunge hili, tulianzisha Hifadhi za Taifa mbili; Hifadhi ya Taifa ya Kigosi na Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maeneo sehemu kubwa yalikuwa ni maeneo ambayo kwenye misitu hiyo wananchi wengi walikuwa wanafanya shughuli za kufuga nyuki. Baada ya kuanzisha haya maeneo, wananchi wale wameshindwa kuendelea kufanya shughuli zao. Baada ya kelele nyingi Serikali mmeona na kwa moyo mzuri wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwaka jana tumeishusha hadhi Kigosi ili kuruhusu wananchi hawa wafanye kazi za kufuga nyuki. Tunaiomba Serikali, ilione na hili la Ugala tuwasaidie Watu wa Kaliua, watu wa Urambo na watu wa maeneo mengine ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho, ni hili eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na urekebishaji wa mipaka. Jambo hili lina historia ndefu na nikiri kama kuna jambo mojawapo gumu tumewahi kukutana nalo kwenye Kamati yetu ni jambo hili. Hata baadhi ya Wajumbe wangu walipata kashkash kidogo, wengine wakiambiwa maneno haya na yale lakini katika kufanya kazi ya Kibunge vizuri na kuitendea haki nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote tunaupenda uhifadhi, nchi hii ni ya kwetu, na asiwepo mtu wa kutudanganya kwamba tutaondoa maeneo yote ya hifadhi yakawa ni maeneo ya kutumiwa na watu eti kwa ajili ya kuchunga au kufanya shughuli nyingine, maeneo ya hifadhi lazima yawepo, lazima yaendelee kutunzwa na huo ndiyo uhai wa hii nchi yetu na lazima tuungane kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili pamoja na kuwa na historia ndefu, sitaieleza sana, lakini nasema tu kidogo, baada ya Serikali kumaliza kufanya ile kazi kwenye Kamati ya Waheshimiwa Mawaziri nane, walipokwenda kuchambua wakagundua migogoro 975; katika migogoro 975, migogoro 35 ilikuwa inaangukia kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Katika hii migogoro ya vijiji 35, Kamati ya Mawaziri ikafanya kazi, ikamaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yakatoka maazimio matatu; eneo la kwanza wakasema Ranchi ya Usangu, lakini kuna shamba la madibira ile phase one na vijiji 14, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, ikakubali virudishwe kwa wananchi ili wafanye shughuli zao. Jambo hili ni kubwa sana la kupigiwa mfano, lazima tuipongeze Serikali kwa moyo huu na kwa uamuzi huu ambao umefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo Serikali ilifanya, kuna vijiji vitano walisema kwa namna yeyote kwa maslahi ya nchi hii, vijiji hivi vitano haviwezi kuvumilika lazima wananchi wahame, na sisi tuliunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, kulikuwa kuna vijiji 16 kwenye baadhi ya vitongoji walikuwa wanataka kutoka nje na vingine vibaki hifadhini, kwa hiyo jumla ya vitongoji 47 vilitakiwa kubaki hifadhini. Baada ya Kamati ya Mawaziri nane kumaliza kazi yake, wakaenda kuandaa azimio kwa ajili ya kuleta Bungeni. Wakati wa kupitisha maazimio, yakaibuka malalamiko kwamba haya maeneo wanayoondolewa wananchi, wako wawekezaji wanalima kama wanavyolima hao wananchi, wao wameachwa, lakini wananchi wanaondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukasema kama Kamati lazima tujiridhishe, Mheshimiwa Spika akatupa kibali, tarehe 22 Juni, 2023 tulikwenda Mbarali. Tulifanya ziara angani, tulifanya ziara ardhini, tukajionea. Ukiachana na maeneo mengine yote ambayo tunajua Serikali inayashughulikia kwa namna ya tofauti, lipo eneo moja linaitwa Mpungamoja; hilo eneo, shamba la wananchi na shamba la wawekezaji vimefanana, viko sambamba, wanatenganishwa na barabara, lakini wanaambiwa wananchi wanarudi hifadhini, lakini wanaambiwa huyu mwekezaji yeye anakuwa ni nje ya hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukasema jambo hili ni gumu, inawezekanaje kwamba wananchi wanatoka nje ya hifadhi, lakini hawa wengine wawekezaji wanaambiwa wao siyo sehemu ya hifadhi. Tukakaa na Wizara, tukazungumza na Wizara, tukakubaliana vizuri na tarehe 27 Juni, 2023 tukawasilisha Bungeni hapa. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alitoa commitment ya Serikali kwamba wako tayari kufanyia kazi ushauri wa Serikali na kwa sababu ya muda, sitasema lakini ninayo Hansard ya tarehe hiyo, ukienda ukurasa wa 136 na ukurasa wa 137.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati na kama Bunge, tukawa tunasubiri utekelezaji wa jambo hili. Tulikutana na Wizara mwezi wa Agosti, 2023, hatukuwa na majibu ya utekelezaji, tulikutana na Wizara mwezi wa Oktoba, 2023, hatukuwa na majibu ya utekelezaji, tumekutana na Wizara Januari, 2024 hatukuwa na majibu ya utekelezaji. Katika mazingira hayo lazima turipoti kwamba azimio hili halikutekelezwa ndiyo maana tulileta Bungeni na kuliomba Bunge lako Tukufu liazimie na kuitaka Serikali ikatekeleze jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa, ni jambo hili moja, siyo hayo mengine yote yanayohusiana na Mbarali tunajua Serikali ina utaratibu wake inaendelea nao hatuna shida, liko eneo moja ambalo sisi wote Serikali na Bunge tulikubaliana, tulipoona halijatekelezwa ndiyo maana tumekuja kuliambia Bunge kwamba jambo hili halijatekelezwa. We have nothing, nothing and nothing personal kwenye jambo hili, ni shughuli za Kibunge, ni utendaji kazi wa Kibunge na tulichokifanya sisi, tumefanya sehemu yetu kama Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo lakini busara inatuongooza, lazima tutafute namna ya kwenda mbele na kukubaliana kwenye mambo hayo. Pamoja na michakato yote hiyo na kukaa muda mrefu pasipo kukamilika kwa azimio hilo, tumetaarifiwa hapa, amesema Mheshimiwa Waziri kwamba ipo kesi imefunguliwa kwenye Mahakama ya East Africa (East African Court of Justice) kuhusu eneo hili la Mbarali. Bahati mbaya hatujapata nafasi kama Kamati kujua nini kesi inasema, nini maelekezo ya kesi hiyo, nini madai ya kesi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungeijua pengine tusingekuwa tumeweka kwenye jahazi hilo kwa sababu tunajua sisi kama Wabunge na Bunge letu, tunao wajibu wa kulinda utawala wa sheria kwenye nchi yetu ikiwemo kuheshimu vyombo vyote vya kimahakama. Sasa kwa sababu hatukupata nafasi hiyo ya kujiridhisha na kwa sababu Mheshimiwa Waziri amelisema hapa na tunamwamini kama Waziri aliyepewa dhamana na Serikali na Mheshimiwa Rais, sisi kama Kamati, tunaomba Bunge lako Tukufu tukubaliane twende vizuri kwenye eneo hili, kwenye eneo la azimio hili ambalo ni Azimio Namba 3.2.8, naomba Wabunge turidhie, tuongeze maneno ili ku-take consideration ya hiki kilichosemwa ili kama kipo kweli na kina madhara kwenye jambo hili, tusifanye Bunge kama tulivyokuwa tunataka kufanya mwanzoni ikaonekana kwamba Bunge tumedharau kile kinachoendelea kwenye Mahakama au Bunge hatujasikiliza kilichokuwa kinaendelea kule mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu hiyo, tunaomba tuongeze maneno machache tu kwenye lile azimio, baada ya maneno; “Bunge linaazimia kwamba, tuseme; “kwa kuzingatia hatma ya shauri lililoko mahakamani.”

Kwa hiyo, azimio hili naomba lisomeke hivi; “Azimio la Bunge kuridhia mapendekezo ya kurekebisha mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha:-

Kwa kuwa, Taifa linahitaji uhifadhi wenye tija ambao ni endelevu usiokuwa na migogoro ya mipaka kati ya maeneo ya hifadhi na ardhi za vijiji;

Na kwa kuwa, utekelezaji wa Azimio hili la Bunge ulilenga kusaidia kulinda mifumo ya ikolojia katika Bonde la Usangu ili kurejesha uoto wa asili kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kuimarisha mtiririko endelevu wa maji katika Mto Ruaha Mkuu ambao unategemewa katika uzalishaji wa umeme wa maji katika Vituo vya Mtera, Kidatu na Mwalimu Nyerere;

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba kwa kuzingatia hatma ya shauri lililoko mahakamani, Serikali itekeleze Azimio la Bunge na masharti yake kama ilivyowasilishwa na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Taarifa ya utekelezaji huo italetwa Bungeni kazi hiyo ikikamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba tukiliweka hivi jambo hili, itatusaidia kuwa tumejiweka vizuri na wenzetu wa Mahakama, lakini pia isionekane kwamba tumedharau hicho kinachoendelea kwenye upande huo wa mihimili mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, narudia tena kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuwasilisha lakini pia na kuhitimisha hoja hii. Nawashukuru sana Wabunge, sisi kama Kamati tuko tayari kuendelea kufanya kazi hii ya kuishauri na kuisimamia Serikali kwa maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia haya marekebisho kwenye lile azimio moja ambayo nimeyasema, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako lipokee Taarifa ya Kamati na likubali Maoni na Mapendekezo yote kama yalivyowasilishwa ikijumuisha na marekebisho yale ambayo tumeyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)