Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa ya kusimama siku hii ya leo kuzungumza machache yanayotokana na majadiliano kwenye Kamati yetu ya Bajeti ambapo mimi ni Mjumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anaongoza Serikali yake na namna ambavyo amewezesha Serikali hii kufikia yale malengo makubwa ya kiuchumi ambayo tulijiwekea kwenye mwaka huo 2022/2023 na kwenye nusu ya mwaka huu wa 2023/2024. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli malengo mengi yamefikiwa. Ukienda kwenye upande wa mapato tumefikia lengo kwa asilimia takribani 94, upande wa matumizi of course inatumika ikipatikana fedha. Niseme uzuri mwingine kwamba ukiangalia overall nakisi ile ya bajeti ambayo tulitarajia iwe around 3% bado iko kwenye 3.6%, siyo mbaya kwa sababu ni ndogo sana ukilinganisha na za wenzetu hapa jirani wanazungumzia 7%. Ni kweli kwamba ukitaka kuwa na uchumi tulivu sana basi unataka kuwa na nakisi ya bajeti ndogo maana yake hufanye deficit financing kubwa na hiyo ni njia moja ya kudhibiti mfumuko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho nikizungumzie zaidi ni suala zima la ukuaji wa pato letu la Taifa ambalo kwa bahati mbaya bado tuko around asilimia 5. Tunatarajia sasa mwaka huu wa 2023 tufikie asilimia 5.3 lakini ni chini ya lengo lililokuwa kwenye dira ya 2020 ambayo ilisema iwe ni zaidi ya asilimia 8 na tuliweza kufikia fikia kule hapo nyuma tukafikia around 6%, 7%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba tulivyofika kwenye growth ile nilishangaa kwamba kuna taasisi za kimataifa hazikutupongeza lakini sasa hivi tuko 5% wanatupongeza basi kuna mahali kitu kimejificha. Niseme hivi, tatizo la ukuaji wa pato la Taifa hapa nchini hatujapata ufumbuzi wake na hatujajua chanzo chake ni nini hatujabaini sawa sawa. Ngoja mkinipa fursa nielezee kwa nini nasema hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunasema mambo ya blueprint tukifanya blueprint ile tukatekeleza basi Sekta Binafsi itaibuka. Tukasema kwamba tukifanya kuboresha miundombinu Sekta Binafsi itachangamka lakini hili jambo halijatokea, kwa nini? Niseme hivi ili Pato la Taifa likue, kichocheo kikubwa licha ya kuwa na rasilimali ya watu na rasilimali ya resource ya land ambayo ni very rich, tunahitaji financial resources. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, financial resources zipo; watu tuliowapa jukumu la kukusanya akiba zote za watu binafsi hapa nchini ni benki. Sasa tuseme kwamba tumeona kwamba kweli benki zimeweza kuongeza mikopo kwa Sekta Binafsi kwa 16% na mwaka juzi ilikuwa 20% na ushee. Sasa lakini tunasema kwa nini hili ongezeko halichochei ukuaji wa pato la Taifa? Kwa nini halichochei?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niwasilishe kwamba ukweli ni kwamba haliwezi kuchochea kwa sababu benki zimeondoka kwenye commercial banking proper (kwenye kukopesha kwa business sector) wanaenda kukopesha kwa sekta ya consumption (sekta ya watu binafsi). Ndiyo sasa unaona benki zinakimbizana na watu walioajiriwa kukopesha watu wenye mishahara ili wasifanye risk yoyote. Maana yake ni kwamba kwa mfano sisi hapa Bungeni kwenye Kamati yetu tulisema wapunguze riba wanayotoza kwa fedha hii ambayo wanakusanya kwa urahisi bila kuingia kwenye risk. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa issue iliyojitokeza hapa ninasema kwa nini benki zifanye hivyo? Kwa sababu tulipokuwa sisi tunaanza benki pale, nilivyokuwa pale tunaanzisha ile benki tulikimbizana na wateja kwenye corporate sector lakini kilichokuwa kimetukuza tukaanza kukua haraka ni kwamba corporate banking (mikopo kwa wateja wakubwa kwenye biashara na kwenye uzalishaji) tulikuwa tunakimbizana nao na tulikuwa tunawafanya wao wanakuwa ni marafiki zetu, siyo tupate hongo ila tuweze kuwakuza wawe wateja ambao ni endelevu kwa benki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi badala ya kukimbizana na hiyo corporate sector ambayo ndiyo inazalisha, ndiyo inafanya biashara, kwenye utalii ndiyo ipo, unakuta benki zinakimbizana kufanya michapalo huku na kule ili sisi tukachukue mikopo kwao kwa bei ambayo ni ile ile ya corporate sector, kwa hiyo ukweli ni kwamba hatuwezi kukua. Sasa kilichopo ni hivi, kilichofanya benki wafanye hivyo siyo kwamba ni wao wenyewe. Benki Kuu imeweka hii limit ya kwamba mikopo chechefu isizidi 5%, ok ni nani atadanganya kwamba atafanya biashara kuanzia mwaka wa kwanza aweze ku-limit ile risk yake ya kutokuweza kulipa au default risk yake kwa 5%? Mtu aliyefanya biashara yoyote atasema it is impossible kabisa tena wengine watasema the dream was impossible. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulikuwa tunachukua mikopo tukijua kwamba tutafanya restructuring, tutafanya nini lakini unajua kwamba unachukua risk above 5%, nachukua 10%, 15% benki inachukua. Inaweza ikachukua mwaka wa kwanza lakini baada ya miaka miwili yule mtu ana turn around anakuwa mteja mzuri. Kwa hiyo, hapo tunakopesha wale watu. Sasa hivi kwa sababu huwezi kufikia hiyo limit ya 5% ya mikopo chechefu, the only thing you can do ni kutafuta wakopaji ambao wana-cashflow ambayo ni guaranteed ambao ni wafanyakazi kwenye Serikali, Bunge na kwenye mashirika makubwa lakini siyo kukopesha business kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tatizo ni hilo na mimi nasema kwamba ukiangalia kwamba benki zimekuwa overcapitalized sasa hivi kwa sababu risk ile ya kwao risk premium zao zimeshuka sana. Kwa hiyo, wanafanya faida bila kutumia earn ya ile capital, wako overcapitalized unakuta badala ya kuwa na capital minimum ya about 14.5% ambayo ndiyo required wako kwenye 20% wame-accumulate capital kwa sababu they are not taking risk but they are getting a lot of profit sasa tatizo ndiyo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwamba kama hatuta address hiyo issue kwamba sekta hii ya benki ambayo imekusanya akiba zetu ikopeshe private investors kwenye business, hata kwenye biashara ndiyo sawa lakini mnyororo mzima wa biashara basi tusipofanya vile hatutaweza kuona tumeepukana na hili tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme cha pili ni hivi; utaona pia kwamba tumeweza ku-maintain very low inflation. Tujiulize; je, kwa nini basi tusiweke target ya inflation ya sifuri kama tungetaka low inflation basi iwe sifuri lakini tunaweka lengo kwamba target iwe tatu na kwa nini iwe tatu? Ukikaa kwenye TV unaangalia … utakuta kwamba watu kila wakati wanasubiri takwimu inapokuwa released ya inflation rate Marekani kwenye Nchi zote mtu anasema inflation imeongezeka ngapi? Je, kwa hiyo Federal Reserve itaongeza riba au itafanya nini kwa sababu inflation ikipanda riba inatakiwa ishuke, ipande na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tumekuwa na 3% constant, figure ambayo ni constant sasa hivi kwa miaka mingi ni lengo letu. Sasa nauliza what do you do when you have a low inflation ambayo iko very low? Faida yake ni nini? Utakuta kwamba faida ni ndogo sana. Maana yake ni kwamba tumezuia kuingiza fedha kwenye mzunguko kwa mikopo kwa sababu fedha kwenye mzunguko inaingia kwa mikopo. Hutaweza kukuta mtu anaenda kuchukua pale Benki ataipataje hiyo fedha ya Benki Kuu bila kuchukua mkopo benki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, benki ndiyo zina-create money, inavyo-create money ndiyo inachochea uchumi. Sasa maana ya kusema kwamba umekandamiza kwenye 3% maana yake ni kwamba unasema kwamba mikopo isitoke na fedha isizunguke. Issue ni kwamba hakuna mtu yeyote ambaye aliwahi kuja hapa mchumi akasema optimal inflation ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa optimal inflation kwa Marekani inaweza ikawa ni 3% kwa sababu wako almost full employment, unemployment yao ni around 5% - 6%. Unemployment yetu kwa kipimo ambacho yaani sijui ni kipimo cha ngapi inasema ni 14% lakini ukihesabu partially employed people (mtu anayefanya kazi masaa mawili) halafu anaenda kunywa chai na kahawa huko kijiweni pengine unemployment yetu iko 20% - 30%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuonyesha kwamba unemployment ni kubwa ni kwamba kuna watu wako tayari kufanya kazi bure. Mimi watu wamenifuata wananiambia tutafutie tu tukajishikize pale hata temporary halafu tutakaa tu pale usinipe chochote. Sasa mtu unaogopa inflation kwamba itakuwa driven kama resources ziko full employed lakini sisi tuna resource ambazo haziko employed; watu, ardhi sijui na kitu gani kingine hicho na hizo financial zote ambazo haziendi the right place.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima tumuombe Gavana kwamba kwanza aangalie hiyo issue kwamba you don’t just want to bank, they don’t lend; actually, watu wanasema hizi benki zetu hapa ni saving banks, they are not commercial banks at all, katika nadharia ya finance hizi benki zetu ni saving banks basi. Kwa hiyo, hazisaidii na hazitakaa zisaidie kwa sababu wanachukua hela wanaweka, wanawapa watu zinaenda hovyo hovyo halafu hazisaidii kwenye kutengeneza ajira, kufanya nini na nini. Ni lazima tuangalie hili. (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kusema kweli…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma muda wake umeisha nimemuongezea lakini nakupa ruhusa utoe taarifa.

TAARIFA

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. nilikuwa napenda kumpa taarifa mzungumzaji anatoa somo zuri sana kwa leo mpaka na mimi Daktari nime-appreciate. Sasa nilikuwa nakuomba umuongeze walau dakika tano tu ili somo lituingie vizuri. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Charles naomba uendelee kidogo.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Musukuma nakushukuru sana kwa taarifa yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio nasema hivi kwamba katika hilo ni kwamba kuna mikopo ile tunaizungumza itakayoenda kwenye private sector yes, lakini wakati private sector inakuwa kwamba inasuasua haichukui ile mikopo na kuiingiza kwenye miradi Serikali pia ina-widen ile nakisi ya bajeti wanafanya deficit financing. Wanaweza wakachukua mikopo pia kwenye benki zetu wakaipeleka hata kwenye ile mifuko ya uwezeshaji kama ikiwa imeundwa sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya uwezeshaji ni ile ya 10 ambayo ina 4:2:2 na ukatumia njia nyingine ukaiweka hizo zote mahali pamoja ukaunda hata guarantee fund ambayo itakuwa inawa-guarantee watu wote na pesa itakuwa ni nyingi halafu Serikali sasa ikaweza kutumia hiyo hela ikaingiza kule watu wanakopeshwa hata kama kwa masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii TIB tunayoambiwa hapa kwamba ina matatizo, TIB waambiwe wa-focus kwenye kitu kimoja tu. Wawachukue vijana wajasiriamali wawaweke kwenye incubation (viatamishi). Wakishawaweka kwenye incubation wanawapa mitaji wanaenda kuwasimamia huko mtaani wanafanya kazi kwa kutumia agency, ni hawa watu ndiyo wataanza kuibua uchumi tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unawaambia TIB sijui ikagawe mafuta sijui wapi, ikagawe majiko ya gesi; what are you doing? Kwa nini tusiwape kazi hiyo kwamba nyinyi haya makubwa mmeshindwa, hizo corporate landing wameshindwa, sasa kama wameshindwa corporate landing nenda kule kwa wale ambao tunahitaji, startups hapa nchini hamna mkopeshaji, siyo commercial bank siyo nini. Kwa hiyo, lazima hizi benki zetu ambazo tumeziunda kwa mitaji ya Serikali basi ndiyo zifanye hiyo kazi ya kuatamisha startups na hiyo itasaidia sasa kuibua vitu tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ukienda kwenye benki kitu wanachoumiza sana, corporate banking departments zilizokuwa tumezikuza yaani ndiyo zinazunguka, wateja wengi wako hapa wanajua wanawakumbuka wale vijana wangu wakina Mlabwa, akina Alfred Philipo Alfred na wengine wanakimbizana nao wanaenda kuwasadia halafu hii miradi mikubwa tunayoiona sasa hivi mingi imetokana na corporate landing basi. Wakati ule niliona tukimbizane na consumer landing, consumer landing ni hii personal landing ambazo sasa hivi zina-occupy more than 35% ya mikopo yetu hapa nchini na mingine itakuwa iko kwenye Serikali. Nataka kuomba kwamba kweli tujaribu kuangalia upya na tubuni upya. Namba ya blue print naona haisaidii sana hivyo lakini yale ni madogo sana lazima tuibue mambo mapya haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niseme, kwa sababu naona nisije nika nani hii. Natumai kazi kubwa tuliyonayo hapa Bungeni ndiyo hii ya kuwezesha Pato letu la Taifa lianze kukua kwa haraka zaidi. Linakua lakini likue kwa haraka sana kwa sababu we have the windows za kufanya hilo Pato la Taifa likue haraka. Kwa hiyo, kama tunazo tufanye hivyo, hiyo ndiyo njia pekee ya kuboresha maisha ya Mtanzania. Ndiyo njia pekee ya kufikia lengo na dira yetu, ya kwamba tunataka tuboreshe maisha ya Mtanzania. Lazima tufanye hayo na mengine ambayo sasa kwa sababu ya muda naomba niishie hapa, ahsante sana. (Makofi)