Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja mbili zilizoko mbele yetu. Moja kwa moja nitajielekeza kwenye Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Naomba nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati yetu Mheshimiwa Sangu kwa kuweza kufanya kazi nzuri sana ya kuweza kuwasilisha yale ambayo tumeyajadili na kuyakubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha niruhusu nimpongeze Msajili wa Hazina kwa sababu kazi yake amaeifanya vizuri sana na lazima tuwe wa kweli. Tumeona changamoto ziko nyingi kama alivyozizungumza Mwenyekiti katika taarifa yetu. Nafikiri ni dhahiri kabisa tunahitaji mabadiliko ya sheria. Ule Muswada ambao Serikali ilikuwa imepanga kuuleta hapa tunafikiria kwamba Serikali ingeharakisha ili uweze kusaidia na kuoko mashirika haya ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitauelekeza katika maeneo mawili makubwa ya kimkakati kabisa. Kwanza, nataka niangalie urejeshaji wa mtaji (return on investment). Pili, nataka niangalie utegemezi wa ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua umuhimu wa taasisi za umma. Taasisi za umma kwa hakika kabisa zinasaidia uchumi wa nchi hii na zinasaidia ajira katika nchi hii. Hata hivyo, hatuwezi kuondoa ukweli kwamba kila anayewekeza iwe ni mtu binafsi au iwe ni Serikali lazima apate rejesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba Serikali imewekeza katika maeneo mawili, katika maeneo ya huduma vilevile katika maeneo ambayo ni taasisi za kibiashara. Mtaji ambao Serikali imeweka kama alivyosema Mwenyekiti ni shilingi trilioni 73.3. Jinsi Serikali inavyowekeza zaidi takwimu za sasa hivi zinafika shilingi trilioni 76. Sasa mnaweza mkaona seriousness ya Serikali katika kuwekeza fedha zake katika masuala yanayohusiana na uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama uwekezaji uko namna hiyo TR anasema nini? TR anatarajia apate angalau asilimia 15 ya uwekezaji wa Serikali iwe ndiyo rejesho. Sasa fedha ambazo Serikali imeweza kukusanya, shilingi bilioni 850, ukipiga hesabu, kwa wale ambao wana calculators utaona kwamba asilimia ambayo Serikali imepata ni asilimia 1.15. Hii ni ndogo sana, ni ndogo mno kwa uwekezaji. Kama ni mfanyabiashara wa kawaida angefukuza hata hizo management. Huwezi ukaweka shilingi trilioni 73 ukapata shilingi bilioni 850,

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna yoyote; najua kuna wengine watasema miongoni mwa hizo taasisi ziko taasisi ambazo hazifanyi biashara, lakini hata ukichukulia computation ya aina yoyote, hesabu ya aina yoyote, kwamba, je Serikali inapata rejesho lake stahiki? Jibu ni hapana kwa sababu angalau basi hata tungepata 5 percent ya hicho kilichowekezwa tungepata zaidi ya shilingi trilioni tatu, na ikasaidia katika bajeti zetu za Serikali. Kwa hali hiyo nikajiuliza hivi ni kwa nini rejesho linakuwa dogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa majadiliano ndani ya Kamati tumegundua kwamba kwa kuwa kuna sheria ya kuleta rejesho pamoja na gawio, ni kwa mujibu wa matakwa ya sheria, taasisi nyingi hazitimizi matakwa ya kisheria. Nataka nikwambie, zipo ambazo hazilipi kabisa. Yaani zinafanya shughuli zake na hazilipi senti tano kwa msajili wa Hazina, zipo. Zipo ambazo zinapojisikia kulipa, si asilimia 15, wanaweza wakalipa wanayoitaka wao na wanayoiamua wao. Hata kama wanaweza wakawekewa madeni lakini hayalipiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama taasisi kwa taasisi zinakwepeshana au zinapeana huduma na hazilipani basi hata hao wengine ambao wanatakiwa walipe asilimia 15 kwa Msajili wa Hazina wanalipa wanavyojisikia na si kwa matakwa ya sheria. Zipo zile ambazo zinatakiwa zilipe gawio, wao nao wanafanya kwa utashi wao. Hakuna sera ambayo inatoa maenelekezo kwamba dividend policy, kwamba huyu mtu au hii taasisi inatakiwa ipeleke gawio kiasi gani baada ya kuweza ku-repair zile hesabu zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naungana mkono na Kamati juu ya hatua gani zichukuliwe, lakini mimi ningependa kwenda mbali zaidi, kwamba kama kuna management ya taasisi ya umma ambayo haitekelezi matakwa ya sheria ya kulipa asilimia 15 Seikalini management hizo zichuliwe hatua ikiwemo kufukuzwa kazi; waondolewe kazini. Hatuwezi kuwa na watu ambao kazi yao wanaendesha taasisi Serikali imeweka fedha na saa nyingine nikiwa huko mbele mchango wangu utaona ni kwa jinsi gani utegemezi uko katika hizi taasisi za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaacha kupewa fedha za kwenye barabara wanapelekewa wao kwenye mishahara lakini hawaleti returns zinazohitajika. Katika jambo kama hilo napendekeza upande wa gawio. Serikali, na bahati nzuri TR nafikiri yupo, waje na kitu kinaitwa dividend policy (Sera za Gawio) ili kila kampuni au taasisi ya umma ambayo inapaswa kulipa gawio Serikalini ije na sera yake na TR aweze kui-approve. Muda wa kulipa policy ukifika policy ile ndiyo iwe sheria ya kufuata ni kiasi gani kilipwe ndani ya Serikali. Tunataka tija na tunataka ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwenyekiti wetu ametoa mfano wa taasisi zinazojiendesha kwa tija lakini bado zinapewa ruzuku. Sasa hapa ndipo ninapopata kichefuchefu. Yaani nachafukwa kweli kweli. Kuna taasisi mapato yao mazuri sana lakini bado wanategemea wapate ruzuku. Ukiangalia hesabu za fedha ambazo, kwa mfano nakupa tu hesabu ya Mwaka 2023/2024 Serikali imetenga kuzipelekea taasisi za umma kwenye uwekezaji shilingi trilioni 2.179 kama mishahara pamoja na OC. Na hapo sasa ndipo ubwetekeji unapopatikana. Watu wanabweteka kwa sababu Serikali itapeleka fedha kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa, kwa sababu pamoja na kwamba hizi taasisi kweli zinasaidia uchumi wa nchi na zina ajira kubwa, zimeajiri watu zaidi ya 900,000 kwa mujibu wa hesabu za mwaka 2021/2022. Lakini, kama mtu anaweza akafanya kazi na akafanya vizuri; nawapa mfano wa taasisi mbili; STAMICO ni moja ya kampuni ambayo inafaa kupigiwa mfano.

Mheshimiwa Mwenyekti, kwanza walikuwa hawafanyi vizuri lakini baada ya kuingia kwa management mpya wao walipandisha faida yao kutoka shilingi bilioni 1.6 hadi shilingi bilioni 76. Hawa ndio sampuli ya watu wa management ambao tunaitaka. Lakini watu wengine…

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

TAARIFA

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji, pamoja na mchango mzuri ambao anaendelea nao hoja alikuwa ameizungumza ni ya msingi, kwamba kuna baadhi ya taasisi haziwezi kupeleka gawio Serikalini kumbe shida ni management. Kwa hiyo, kwa mchango tu huo aliokuwa amezungumzia na alivyoitaja STAMICO shida kubwa kumbe ni management na wala siyo kitu kingine chochote.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abbas unaipokea hiyo taarifa?

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hasa kwa kuwa imetoka Namungo na Namungo tunawadhamini brain zao zitakuwa ni nzuri, namshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe jambo lingine, mimi nimebahatika kufanya kazi Serikalini nikiongoza taasisi inaitwa Gaming Board of Tanzania na sasa hivi mimi ni mfanyabiashara na Mbunge. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie wakati tunaanzisha Gaming Board Serikali ilikuwa ilete subsidy kwa miaka mitano mfululizo, of course, ilikuwa inakwenda inapungua, ndani ya miaka miwili sisi tukasema tunataka kujiendesha sisi wenyewe bila ya kuwepo na ruzuku, mimi nikiwa Director General pale. Board of Directors wengine wakaniambia endapo tutapata hasara tutakufukuza kazi, nikawaambia nipeni challenge nifanye kazi, nikapewa challenge na nikafanya kazi. Ni kampuni ambayo ilikuwa ya kwanza kuanza kupeleka rejesho bila ya Sheria, we started it, sisi tulianza! Wakati ule TR alikuwa Ndugu Mafuru ambaye sasa hivi ni Katibu Mkuu wa Mipango. Hivyo inawezekana na Gaming Board mpaka leo hawachukui ruzuku, hawana mishahara lakini wanapeleka fedha Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Gaming Board of Tanzania na Bodi yake na wafanyakazi kwa sababu tungependa watu katika Menejimenti ambao wanaona uchungu uwekezaji wa umma na wanapeleka fedha Serikalini. Trilioni 2.1 zile ambazo zinakwenda kama mishahara, Waheshimiwa Wabunge tunapiga kelele hapa kwa sababu tunataka fedha sisi za Barabara, kwanini tusizichukue zile kwa wale ambao wanaweza wakajitegemea zikapelekwa zikaondoa hizi changamoto? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kichaka kile cha Mashirika ya Umma yanayopata ruzuku naomba Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Mipango pamoja na TR wafanye uchambuzi wa mashirika ili shirika ambalo linaonekana linaweza kujiendesha wasipewe ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umewasha taa. Nakushukuru sana, naunga mkono hoja zote, ahsante sana. (Makofi)