Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia taarifa hizi mbili za Kamati ya Uwekezaji Mitaji ya Umma pamoja na Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia katika Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Naomba kuanza kwa kuwapongeza Wenyeviti wote wawili kwa kuwasilisha vizuri taarifa lakini nampongeza zaidi Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Sangu kwa jinsi anavyoiongoza Kamati vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kuhusu mashirika ambayo yanashindwa kujiendesha kwa sababu ya mashirika mengine ambayo yanakopa na kushindwa kurejesha kwa wakati. Nilisimama hapa Bungeni mwaka jana nikaongelea kuhusu TEMESA, nikasema TEMESA imeshindwa kujiendesha kwa sababu Serikali inapeleka magari yao kutengenezwa lakini hawalipi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo pia naendelea na hoja yangu hiyo hiyo. Katika taarifa imeonesha kuna mashirika mengi ambayo yanashindwa kujiendesha kwa sababu baadhi ya mashirika wanakopa nyenzo za kufanyia kazi na kushindwa kulipa kwa wakati. Nitataja baadhi ya mashirika, kwa mfano, Kampuni ya Usambazi na Usafirishaji Umeme (ETDCo) inadai TANESCO na REA shilingi bilioni 44.782. LATRA inadai Shirika la Reli shilingi bilioni 1.81 na Kampuni ya UDART inadai shilingi bilioni 1.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kuna baadhi ya mashirika mengine ambayo pia sijayataja hapa, Serikali isipoangalia kufanya kazi ya ziada kusimamia mashirika haya ambayo yanakopa mashirika mengine kiasi kwamba yanashindwa hata kugawa gawio la Serikali na kujiendesha yenyewe, hii tunaelekea pabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu, naomba Serikali isimamie mashirika yote ambayo yanadaiwa yarejeshe fedha zinazodaiwa katika mashirika husika ili yaweze kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee Benki ya Maendeleo. Tukiangallia benki hii ni kama imeshakufa, kwa sababu Benki hii mpaka sasa hivi imeshindwa kujiendesha, benki hii ina hasara ya shilingi bilioni 129 kati ya mwaka 2021 na mwaka 2022. Ukiangalia hasara hii inatokana na madeni chechefu ambayo kuna watu wanadaiwa na benki hii ambayo hawajalipa. Tukiangalia Sheria ya BOT ili benki iweze kujiendesha inatakiwa iwe na shilingi bilioni 200 lakini TIB ina shilingi bilioni 24 tu. Haiingii akilini kwamba hii benki inaweza ikaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inatambulika wazi kwamba wako wengi ambao wamekopa benki hii lakini hawakurejesha kwa wakati. Mimi naiomba Serikali ihakikishe kwamba inasimamia kwa umakini na kwa ukaribu zaidi ili wadeni hawa waliokopa katika benki hii waweze kurejesha fedha hii ili benki hii iweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea pia kuhusu suala zima la uwekezaji. Uwekezaji umekuwa ni tatizo kwa kuwa hatuna chombo kinachotuongoza ambacho kinaweza kikaangalia mashirika yanayofanya vizuri ili Serikali iweze kuongeza fedha pale ili Serikali iweze kupata gawio. Mashirika ambayo hayafanyi vizuri kama kuna uwezekano yaweze kufutwa, kwa kuwa wananchi wengi wanaona mashirika ambayo yanasuasua na kusuasua kwa mashirika hayo ni fedha za walalahoi Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uwekezaji uweze kusimama vizuri naiomba Serikali iweze kuhakikisha kwamba inaleta Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Mashirika ya Umma katika Bunge hili ili uweze kupitishwa uwe sheria kamili. Kwa kufanya hivyo, tukipitisha sheria hiyo, kutakuwa na usimamizi mzuri katika sekta mbalimbali hasa katika utendaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kuna baadhi ya mashirika mengine Bodi zao hazifanyi vizuri lakini wanalindana kwa kuwa hakuna chombo kinachowasimamia. Tukipitisha sheria hii ya uwekezaji patakuwa na chombo kinachosimamia masuala yote hayo na tunaamini uwekezaji katika Taifa letu utaimarika na utaleta tija katika Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi ya kuongea naunga mkono hoja, naomba sana Muswada wa Sheria ya Uwekezaji uletwe hapa Bungeni upitishwe uwe ni sheria. Ahsante sana. (Makofi)