Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mungu kwamba wote tuko salama, tuna pumzi ya uhai na tunaweza kuzungumzia maendeleo ya nchi yetu. Ni jambo jema, leo ni siku nzuri, wanasema wenyewe ni Siku ya Wapendanao, na humu ndani nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala tunalozungumza ni mambo ya maendeleo. Nataka kusema wazi, katika jambo lenye appetite kubwa ni maendeleo. Hata ungepata nini, bado unataka kingine na kingine na kingine. Nchi hii imebarikiwa sana kuwa na watu ambao ni wapenda maendeleo, nikianzia na Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wetu wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini timu yote ya Wizara ya Fedha ambayo sasa leo ndiyo tunazungumzia sisi kwenye Kamati yetu ya Bajeti na hiyo Kamati ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Sillo, kwa wasilisho zuri la Kamati ya Bajeti na Mwenyekiti mwenzie wa Uwekezaji. Kwa kweli Taarifa zenu tumezielewa, nasema, naunga mkono hoja zote mbili. Nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, naungana na Mwenyekiti wangu kwa yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi ambayo yanafanyika na hapa ndani wanakiri, wamepokea hela nyingi. Waheshimiwa Wabunge wote wa Majimbo wanasema wamepokea hela, mambo yamefanyika, lakini hakuna siku ambayo hawataendelea kuomba hela zaidi na zaidi kwa sababu baada ya hatua moja, tunakwenda kwenye hatua nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2022/2023, Serikali yetu ilipanga kukusanya na kutumia shilingi trilioni 41.48, lakini hadi Juni, 2023 ilikusanya shilingi trilioni 38.98. Hii ilitoka kwenye vyanzo vya nje na ndani, lakini tuliweza kufikia lengo kwa asilimia 94. Hili ni jambo kubwa na ni jambo la kumpongeza sana. Huko miaka ya nyuma, ilikuwa wakati mwingine tusipokusanya tunasubiri labda misaada, lakini siyo kwa mwaka huu. Nataka niuambie ukumbi huu na pia niwaeleze huko nje kwamba, katika zile shilingi trilioni 13.9 za matumizi ya maendeleo zilizotumika, shilingi trilioni 12.26 zilikuwa ni fedha za ndani. Kwa hiyo, hiyo bakaa ya shilingi trilioni 1.7, ilikwenda sasa kuchukuliwa mkopo kama overdraft ambayo tuliweza pia kuilipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina kila sababu ya kupongeza makusanyo na hawa wanaofanya ni TRA. Pamoja na kuwapongeza TRA kwa makusanyo haya, naomba kuwapongeza Watanzania wote kwa kutoa kodi zao, na kwa kuwa tayari kutoa kodi. Sasa tuendelee kutoa elimu ili wengi zaidi wawe wanatoa kodi kwa hiari, wakiwemo wale ambao tukinunua vitu bila kudai risiti, hawakupi. Hili jambo linatakiwa watu wote tulikubali, tuipende nchi yetu na tutoe kodi kwa hiari ili tupate maendeleo ya miundombinu, elimu, maji, afya, hospitali zijengwe. Bila sisi kutoa kodi, hakuna linalofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote ni mashahidi, baada ya ile corona, hela kutoka nje zinasuasua, lakini tuko tayari kufanya, na Tanzania siyo nchi maskini kabisa. Mimi ni mmojawapo kati ya wale wanaokubaliana kwamba Tanzania ni nchi tajiri sana. Kwa kuwa tunajitambua sisi ni matajiri na tuna vyanzo vyetu ambavyo pia viko vizuri, naomba sana tutoe elimu kila kunapokucha na shuleni waelimishwe. Sensa ya mwaka 2022, ilitufungua akili sana, Sensa hii ilikuwa ya kidijitali chini ya Mtakwimu Mkuu, Dkt. Albina Chuwa. Tumeeleweshwa, tumefundishwa, na tumeona jinsi gani Tanzania tuko katika maeneo tofauti lakini pia tuna vyanzo tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sensa hii imetupa mwanga kuona kwamba kila mmoja anaweza akachangia kutokana na eneo alilopo, na hii ni wazi. Nitachukua chanzo kimoja tu, na labda niende moja kwa moja kwenye Wizara ya Mailiasili na Utalii. Mheshimiwa Rais alifanya Royal Tour, ikatufungua akili kwa wingi sana, lakini hilo ni zoezi ambalo linatakiwa mwendelezo. Kila leo tufundishane, tukubaliane, na pia tuwe wakarimu kwa wageni wanaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko kiasi fulani kwa watu ambao wanaishi tambarare ya Mlima Kilimanjaro. Ule ni katika Maajabu ya Dunia kwa sababu ni Mlima ulio chini ya equator wenye barafu. Ile snowcap siyo kitu cha kawaida kwenye joto kama hili. Mapato yanayopatikana pale walitaraji pia watu walio katika ile tambarare ili waweze kutunza ule mlima, nao wapatiwe kidogo. Wanasema kwenye madini wanapata mrabaha, lakini kwenye mlima, mbona hatupati chochote!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naisema hiyo hapa kadri walivyonituma na bahati nzuri naamini kuwa watu wa Maliasili na Utalii wapo au Mheshimiwa Waziri yupo, aone kwamba kuna haja sasa wapatiwe asilimia kidogo, siyo hiyo ya CSR, hapana, iwe kabisa katika mfumo ili watu wale wawe wananufaika ili waweze kupendezesha ile mandhari, mtu akija kupanda Mlima Kilimanjaro aone Tanzania ilivyo nzuri na watu wale wawe wamenufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulisema hilo, nataka kuzungumzia kidogo kuhusu Benki. Benki zetu ni Benki za kibiashara zaidi na mnufaika ni yule pia ambaye anaweza kukopa na kutumia. Sasa swali linakuja, je, mtu wa kawaida mwenye kipato kidogo, ananufaikaje na Benki? Siku za nyuma alikuwa ananufaika na Benki kwa kuweka Amana na rate ya savings ilikuwa nzuri sana. Mtu anaweka hela yake Benki, anatarajia kiupata interest rate ambayo inamsaidia, lakini sasa hivi gharama za Benki transactions ni kubwa mno kiasi ambacho inafuta ile interest kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, akienda mtu mdogo kuweka hela Benki, hanufaiki, ndiyo maana wamekuwa wajanja. Katika watu wenye akili, ni Watanzania. Wakaamua kufungua vikundi vyao, vicoba, wakafungua SACCOS au kupokezana, lakini mambo kule siyo salama sana. Ndiyo wanakuja hao wengine ambao wana mikopo ya kausha damu. Tumeambiwa hapa, Walimu ndio wanaonyanyasika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu sasa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, hawa watu wa Tier 4 wafikiriwe wananufaikaje na hizi Benki. Benki haimpendi maskini, Benki ni ya matajiri. Sisi wengine ambao tunajaribu kwenda kule kokopa, ndiyo hata unakuta mfanyakazi ambaye mshahara wake unapelekwa na mwajiri kama sisi hapa Bungeni, Mbunge ukikopa, wala hawaji hapa kumfuata Katibu wa Bunge (KB), kwani KB anawapelekea kabla wewe hujauona na umeshakatwa, lakini bado ile interest rate ni double digit, hawajaweza kutuletea ikawa single digit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, aendelee kueleza na kuwaelewesha hawa watu wa Benki, labda waitishe pia kukutana na ninyi Wenyeviti wa Kamati mtusemee tena. Hawa watu wa mikopo ya Staff Loans, tunaita personal loans ipunguzwe mpaka ije single digit. Hii itakuwa more attractive na itasaidia sana watu kukopa wakijua kwamba hata kile alichokopa, anaweza kukitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Tanzania kuwa na wananchi wengi ambao wengine sasa wako idle, yaani hawana kazi. Nitaanza na kundi la akina mama. Wako wamama wenye afya, wanasubiri kusaidiwa startup loans; wako vijana waliomaliza Chuo Kikuu na wao pia wangependa kusaidiwa; pia yako yale makundi maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kwa kuwa tulifundishwa, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne; ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. watu wapo na ninaposema gender ya Ke, wanawake, sisi tuko asilimia 52. Nitatoa tu mfano wa ninakotoka. Wamama wenye nguvu kama mimi, lakini hana namna ya kufanya. Nimekuwa hapa Bungeni kila siku nikiomba wamama hawa waboreshewe startup loans kwenye projects, wapewe ile mitamba ili nao wachangie kwenye kuzalisha. Wapewe vifaranga bora, kwa sababu yule kuku wa kienyeji hafiki hata kilo moja. Ukimkuta hata pale sokoni Majengo mwenye kilo moja, huyo ni crossbreed. Sasa tunataka hao crossbreed. Itawanywe mitamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haina mantiki, tunahesabiwa, tunaambiwa kwenye ranch kuna ng’ombe kadhaa. Tunajua Tanzania ina mifugo mingi, lakini unaponiambia idadi ya ranch, tugaiwe mitamba, lete tufanye crossbreeding. Wale ambao ni zero grazing, waweze kunenepesha na kufanya mitamba mingi, waweze kuwa na maziwa mazuri, viwanda vya maziwa viongezeke na lishe bora ipatikane. Wale wengine ambao wanafuga kondoo, wapewe kondoo bora, wanaofuga mbuzi, wapewe mbuzi bora ili tuondokane sasa na udumavu wa mifugo. Tufuge katika hali nzuri, tufuge wanyama ambao wanaweza kuleta faida kwa nchi yetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuona unashika hapo…

MWENYEKITI: Ahsante sana. Nilikuwa nimekuachia umalizie kuongea.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ahsante sana. (Makofi)