Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wote wawili waliowasilisha taarifa kwa umahiri mkubwa kabisa, akiwemo Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti. Nianze mchango wangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa ya Kamati ya Bajeti, inaonesha kwamba Wizara ya Kilimo iliidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 970.79, lakini mpaka mwezi Desemba, 2023 ilikuwa imepewa shilingi bilioni 311.45 sawa na asilimia 33.45. Ukiangalia eneo lile la Fungu Namba 5, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji nayo iliweza kupewa fedha chache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia sekta ya kilimo ndiyo sekta ambayo inaongoza kwa uchangiaji kwenye Pato la Taifa na ndiyo sekta ambayo imeajiri Watanzania walio wengi sana. Takribani asilimia 26 imekuwa ikichangia kwenye Pato la Taifa. Kwa hiyo, nimwombe sana Waziri wa Fedha, kwa maana ya Serikali, wajitahidi kuidhinisha fedha za Wizara ya Kilimo kwa wakati kwa sababu ni eneo ambalo limeajiri Watanzania walio wengi; na sisi Wabunge wengi humu tumetokana na wakulima. Tunachaguliwa na wakulima ndiyo maana tunawasemea. Kwa hiyo, ni muhimu sana kukuza sekta hii kwa sababu, ukija kuangalia takwimu zinaonesha kwamba, pamoja na kuwa Sekta ya Kilimo inachangia kwa kiwango kikubwa kwenye Pato la Taifa lakini ukuaji wake umekuwa kama umeganda pale pale zile asilimia mchango wake hauongezeki. Sasa, ili mchango uweze kuongezeka nafikiri kazi ya ziada inatakiwa ifanyike. Kwa kuanza, ile bajeti ambayo tumekuwa tumeitenga kama Bunge iweze kupelekwa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa Kamati yetu ya Bunge ya Bajeti tunashukuru Serikali iliweza kutupeleka maeneo mbalimbali kufanya ziara. Tuliona ufanisi mkubwa sana katika uzalishaji wa mbegu hapa nchini. Tulienda kuona maendeleo ya kazi za miundombinu ya miradi ya umwagiliaji ambayo inaendelea kujengwa. Changamoto tuliona ni kwamba, hizi fedha zikiwa zinawahishwa na utekelezaji wa miradi ya kilimo utakuwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, asilimia hii kubwa ya Watanzania ambao wameajiriwa katika Sekta ya Kilimo wanakabiliwa na tatizo kubwa la tija. Sasa tufanye nini ili tuweze kuongeza tija? Ni muhimu sana tukawekeza fedha kwenye tafiti. Nilishawahi kusema kwamba, tuna vyuo vikuu. Tuna Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), tuna Chuo cha Uyole, tuna Nelson Mandela, tuna Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vingine vingi. Sasa, tunavishirikishaje vyuo hivi katika kufanya tafiti ambazo zinaweza zikasaidia katika kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya kazi kubwa. Imetoa vitendea kazi kwa wale maafisa kilimo, ambapo wanapata pikipiki na GPS. Je, tunafuatilia kwamba zile pikipiki wanazitumia, wanapewa mafuta, wanawatembelea wakulima? Je, gharama ya mafuta anabeba mkulima au Serikali inabeba? Kama mkulima hawezi kwenda kupata zile huduma za ugani ataendelea kukosa tija, miaka itaenda na kurudi. Kwa hiyo ni muhimu sana; Serikali inafanya kazi kubwa sana na Waziri wa Kilimo anafanya kazi nzuri. Tumeshuhudia hapa ameanzisha miradi ya kilimo (BBT).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelea mashamba kadhaa na tumeona miradi inakwenda vizuri. Niwapongeze Serikali kwa kuanza kuwapeleka wale vijana kwenye mafunzo ya JKT. Mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao tulikwenda mwaka jana, tulikuwa na kina Jesca Msambatavangu na wengine; tuliona umuhimu wa vijana hawa kupelekwa kule kabla ya kuja kuanza kilimo hiki cha BBT. Kwa hiyo niipongeze Serikali kwa hilo. Niombe pia tuweze kuongeza hizi fedha na zile ambazo hazijapelekwa ziweze kupelekwa kwa wakati ili sekta hii ya kilimo iweze kuongeza kasi katika mchango wake kwenye Pato la Taifa hali kadhalika iweze kutoa ajira nyingi zaidi kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia hata takwimu zinaonesha kwamba sekta ambazo zinachangia sana ukuaji wa uchumi hapa nchini ni zile ambazo Serikali inawekeza zaidi. Kwa mfano, uchimbaji wa madini, bima na utalii, ambazo zinachagizwa sana na Serikali kuweka fedha nyingi, lakini sekta binafsi bado ukuaji wake haupo vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nashauri sana kwamba Serikali iwekeze kwenye kukuza sekta binafsi ili nazo ziweze kuchangia kwenye uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa vijana, kwa sababu nchi yetu ina changamoto kubwa sana ya vijana ambao wanaishi mtaani hawana ajira na wamehitimu vyuo vikuu. Kwa hiyo, tunaweza tukaanza kwa kuangalia zile kozi ambazo zinatolewa kule vyuoni, je, zinahitajika kwenye soko la ajira? Je, zinampa kijana ujasiri wa kuweza kwenda kutafuta masoko nje ya nchi? Je, Wizara inayohusika na viwanda na biashara ina utaratibu gani wa kuwapa elimu wafanyabiashara na watu mbalimbali ambao wanatafuta masoko, wanataka kuyafikia masoko ya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini yule mkulima wa parachichi kutoka Madope Ludewa kuweza kubeba mwenyewe parachichi zake na kwenda kwenye soko la kimataifa. Je, amepewa ujuzi wowote, mafunzo yoyote au tutaendelea kuwa na mtu kati (madalali) ambao wananunua kwa bei ya chini halafu wao wanakwenda kupata faida mara tatu hadi nne?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetoa pendekezo kwamba kuwe na programs za kuwapa wafanyabiashara confidence za kuweza kuyafikia masoko ya kimataifa. Kunaweza kukawa na program kila Mkoa wanakusanywa wale wakulima wanapewa mafunzo. Wapo wafanyabiashara wachache wanatoka kule kwa Mheshimiwa Festo Sanga, Makete. Unakuta wameingia ubia na Kampuni fulani ya Dubai wanazalisha betri, wengine wanazalisha vifaa na wanaandika na majina ya Kikinga. Kuna makampuni ya hivyo, kwa hiyo hiyo model ni nzuri sana tunaweza tukaichukua na kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara wengi zaidi, ili waweze kuyafikia Masoko ya Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za jirani tumeona kwamba wenzetu wanakuja kwetu wananunua hizi bidhaa, wanakwenda kuuza kwenye Masoko ya Kimataifa na kuapata faida kubwa sana. Kwa hiyo, na sisi tunaweza tukaichukua hii model iweze kusaidia katika kukuza uwezo wa Watanzania kuweza kuyafikia masoko ya kimataifa. Hii itasaidia kutatua changamoto ya ajira hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuendelee kuboresha mifumo yetu ya kodi ili wawekezaji kutoka nje wanavyokuja kuwe na mifumo ambayo ni rafiki na tuwape masharti, kwamba uwekezaji wao uwahusishe Watanzania; wajikite katika kuingia ubia na wazawa. Vilevile, zile shughuli ambazo tunawapa mazingira mazuri ya kuja kuwekeza nchini ziwe hasa zile ambazo sisi labda hatuna ujuzi wa kutosha au teknolojia, wenzetu wanayo kubwa zaidi. Lazima tuwape masharti ya kufanya ile tuweze kujifunza hizo teknolojia ili na sisi ziweze kutusaidia katika kukuza sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia sana takwimu za chuma ambacho nchi inaagiza kutoka nje. Tukaona kwamba trilioni 2.6 zinatumika katika kuagiza chuma nje ya nchi. Nikakumbuka kule Ludewa Mheshimiwa Rais ameshalipa fidia kwenye chuma cha Mchuchuma na Liganga kiasi cha shilingi bilioni 15. Tuna chuma kingi sana pale. Nilitamani Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango watembelee wakaone kile chuma, pengine itasaidia na wao kusukuma majadiliano. Maana ni tangu mwaka jana, tangu Bunge lile lililopita mpaka sasa tunakwenda kwenye Bunge lingine. Wanaweza wakasaidia kusukuma majadiliano ya uwekezaji kule uweze kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna tani zaidi ya milioni 126 za chuma ambacho kimechanganyika na titanium na vanadium; madini ambayo yana thamani kubwa zaidi ya mara 20 ya chuma chenyewe na ubora wa chuma ni asilimia 56. Makaa ya Mawe tunayo umbali wa kilomitya 70 tu kutoka pale, ambayo yanaweza yakatumika katika kuyeyusha hiki chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba kwenye lile eneo la miradi ya kimkakati hii Mchumchuma na Liganga pamoja na kuishukuru sana hii Serikali kulipa fidia, sasa twende kwenye uwekezaji. Itaweza kutusaidia kupunguza kiwango cha dola ambacho tunakitoa nje ya nchi wakati kuna changamoto ya upatikanaji wa fedha hii ya kigeni hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache nashukuru sana. Naunga mkono hoja.