Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia kwenye taarifa hizi mbili. Taarifa ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), vilevile taarifa ya Kamati ya Bajeti. Ninawashukuru Wenyeviti wote kwa kuwasilisha, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PIC na mchango wangu leo utajikita zaidi kwenye Kamati ya PIC. Nina maeneo matatu ambayo nitachangia, eneo la kwanza ni kuhusu utendaji wa mashirika ya umma, lakini eneo la pili nitachangia kuhusu STAMICO na STAMIGOLD na muda ukiniruhusu nitachangia kuhusu Benki yetu ya TIB (Tanzania Investment Bank).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuhusu utendaji wa mashirika ya umma. Kamati yetu inasimamia zaidi ya mashirika 300, katika yale mashirika 300 kuna mashirika ambayo yamewekeza mitaji, kuna mashirika yanatoa huduma na kuna mashirika ambayo ni taasisi za elimu ya juu. Kitu gani tumejifunza tunapofanya chambuzi za haya mashirika na tunapokutana nayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, tuna tatizo kubwa sana, tunayo mashirika mengi hayana tija. Pili, tuna tatizo kubwa sana, ukiangalia vile vigezo ambavyo vimewekwa na Msajili wa Hazina kwa kweli, mashirika mengi haya-meet vigezo vilivyowekwa na Msajili wa Hazina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashirika mengi, hususan haya mashirika ambayo yanawekeza mitaji ya umma, yana tatizo kubwa sana la jinsi ya kukuza mapato. Mengi yanasuasua, lakini hata ile mitaji yao ambayo wanawekeza mashirika mengi hayana uwezo wa kuirudisha. Vilevile tumesikia kwenye taarifa yetu kuna mashirika mengi hayana hata uwezo wa kukusanya madeni, lakini hata kulipa madeni yao ambayo yanawaathiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa kuna mashirika kazi zao zinalandana sana, zinafanana. Nitakutolea mfano, hivi kuna haja gani ya kuwa na Chuo cha IFM, Chuo cha Dar-es-Salaam Institute of Accountancy na Arusha Institute of Accountancy? Maana yake ni nini? Hivi vyuo vyote vina bodi tatu, vina wakuu wa vyuo watatu. Imagine labda kila chuo kinamlipa Mkuu wa Chuo milioni sita, maana yake vyuo vitatu vinalipa milioni 18. Tuna Wenyeviti wa bodi watatu, tuna bodi tatu, ukiangalia hawa wote hawa wanatoa huduma inayofanana. Chuo cha Uhasibu cha Arusha, Chuo cha Uhasibu cha Dar-es-Salaam na Chuo cha IFM, kwa nini tusiwe na chuo kimoja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo hoja yetu Kamati. Tuna utitiri wa mashirika ambayo yanafanana shughuli zake, tulitakiwa tuyafanyie harmonization. Hili ni eneo mojawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna mashirika yamepewa mitaji ya umma, lakini yanasuasua sana katika usimamizi wa hiyo mitaji. Tumeona kuna mashirika hayana hata investment plan, yanajiendesha tu yanaendaenda. Mashirika hayana hata business modal, yanajiendesha tu yanaendaenda, hili ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lipo kwenye utendaji wa mashirika ya umma na Mheshimiwa Charles Kajege amesema, mashirika mengi yanategemea ruzuku kutoka Serikalini. Tunamsumbua Mheshimiwa Mwigulu hapa alete bajeti, lakini hawa watu wamepewa mitaji, tulitegemea ifike muda sasa wajiendeshe, walipe mishahara wenyewe na wa-reinvest ile faida inayopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa. Mashirika mengi yamepewa mitaji na Serikali lakini yameshindwa kuwekeza na yanashindwa kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni nini? Kwanza, tunahitaji kufanya functional review, tuangalie mashirika gani tunayahitaji, mashirika gani hatuyahitaji, mashirika gani tunahitaji kuya-harmonize. Hili ameshaanza kulifanya na nilisikia Kamati moja hapa walilalamika kwamba kuna shirika moja limevunjwa. Ushauri wangu ni kwamba, tunahitaji kufanya functional review. Tuyapitie haya mashirika tuone, lipi tunalihitaji, lipi hatulihitaji? Hilo ni eneo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tumeanzisha mchakato wa kuja na Sheria ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Katika ule mchakato, vilevile tuna-propose kuanzisha mamlaka ya kusimamia mashirika ya umma na pia kuanzisha mfuko wa uwekezaji. Naiomba Serikali, hii sheria ni ya muhimu sana kwa sababu tayari tumeona haya mashirika yetu hayafanyi vizuri. Naomba Serikali iharakishe mchakato wa kuleta Muswada wa Sheria wa kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ambayo itatusaidia kuhakikisha kwamba tunaboresha mashirika yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili napenda kuchangia kuhusu STAMICO na STAMIGOLD. STAMIGOLD ni kampuni tanzu ya STAMICO. STAMIGOLD wanafanya kazi Kanda ya Ziwa na wamejikita kwenye maeneo mawili; kuchimba dhahabu na kuchenjua dhahabu. STAMIGOLD walirithi mitambo ya Kampuni ya Barrick ambayo iliondoka takribani miaka 10 iliyopita, lakini STAMIGOLD ni kampuni ya Kitanzania na kwa kweli inafanya viizuri sana. Matatizo ni nini? Tangu warithi ile mitambo ya Barrick, ile mitambo haijarekebishwa, haijapewa technology mpya. Kwa hiyo, STAMIGOLD wana shida kubwa sana. Wana mitambo ambayo imechakaa lakini hawana mtaji wa kununua mitambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni la kikodi. Tunapopeleka dhahabu nje, ni zero rated. Tunapouza dhahabu ndani, ziko VAT exempted. Inapotokea hawa STAMIGOLD wanahitaji ku-claim zile VAT returns zao, inachukua muda mrefu sana. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Mwigulu ni nini? Tunahitaji ku-harmonize. Tunapo¬-charge kodi, tunapouza dhahabu Tanzania, tuna-inflate bei ya dhahabu Tanzania. Tunaenda ku-distort market ya dhahabu. Kwa nini tu-standardize, tuitumie ile ile bei ya global ili kama tunapeleka nje, ipo zero rated, kwa nini na ndani tusiiache iwe zero rated. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, hata ndani tuiache iwe zero rated (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya mwisho ni Benki yetu ya TIB. Wenzangu wamechangia. Kwa kweli, katika benki ambayo ni ya muhimu sana kuisaidia ni Benki ya TIB. Tulitegemea wafanyabiashara wakubwa, wawekezaji wakubwa, wakandarasi wakubwa wapate mitaji kutoka Benki ya TIB. Tatizo ni nini? Viwango vya Benki Kuu ya Tanzania ili iitwe benki inatakiwa iwe na mtaji angalau wa shilingi bilioni 200. Sasa hivi TIB wanaendesha kwa shilingi bilioni 24. This is so risk. Shilingi bilioni 24 lakini hapo hapo wana madeni zaidi ya shilingi bilioni 160. Katika yale madeni shilingi bilioni 160, waliokopa hawazidi watano. So risk! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni tatizo kwenye benki yetu. Tunahitaji kui-rescue. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, kwenye bajeti iliyopita aliwaahidi kuwapa TIB shilingi bilioni 118. Ushauri wangu ni kwamba, tunahitaji kui-rescue Benki ya TIB. Hizi ni benki za Kitanzania ambazo zitawasaidia wakandarasi wetu wanaohangaika kutafuta mitaji. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tuwape fedha Benki ya TIB ili tuweze ku-raise ile capital yao. Wana 24 billion shillings, tukiwapa around 120 billion shillings watafikia hiyo hiyo shilingi bilioni 200 ili waweze ku-operate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni ombi kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. Mheshimiwa Mwigulu, nina mradi wangu wa maji wa Kintinku – Lusilile wa shilingi bilioni 13. Yule mkandarasi (Halem Contractors) amefanya kazi nzuri sana. Ameshanunua mabomba yote, lakini kuna fedha anakudai Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, shilingi bilioni 3.6. Naomba tuimalizie. Ameshatoa zaidi ya shilingi bilioni nane, lakini anadai shilingi bilioni 3.6 na amenunua mabomba yote. Tuimalizie. Huu mradi ni wa vijiji 11. Naomba tuimalizie na anafanya kazi nzuri sana. Kwa kweli naishukuru RUWASA na Waziri wa Maji. Wame-push sana huu Mradi wa Maji wa Kintinku na upo kwenye hatua nzuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni Daraja la Sanza. Mheshimiwa Rais alikuja Manyoni mwaka jana 2023, na bahati nzuri Waziri wa Ujenzi alikuwepo. Wananchi waliomba Daraja la Sanza lijengwe na Rais alimwagiza Waziri kwamba akamilishe mkataba wa ujenzi wa Daraja la Sanza. Namwomba Waziri naye ananiangalia hapa, Mkataba wa Sanza usainiwe ili basi ile ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa pale, wananchi waweze kumwamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Rais alipokuja Manyoni vilevile tulimwomba Kilometa 10 za lami Manyoni Mjini na alimwagiza Waziri wa TAMISEMI alifanyie kazi. Nalo niikumbushe Serikali kwamba hii ni ahadi ya Rais, aliwaahidi watu wa Manyoni, basi watuletee hizo Kilometa 10 za lami pale Manyoni Mjini ili wananchi waweze kufurahia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, narudia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambazo anazifanya. Sisi watu wa Manyoni tuna imani kubwa sana na Mheshimiwa Rais. Amefanya mambo makubwa sana. Ile shule ya wasichana ya shilingi bilioni nne imeshaanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)