Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na nitakuwa na mambo machache ya kuzungumza kwa ajili ya hoja mbili zilizopo mezani, hoja ya Kamati ya Bajeti, lakini pia hoja ya PIC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza niipongeze Serikali, sitakuwa na adabu kama sitaipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo inafanya kazi, lakini pili kwa jinsi ambavyo ukusanyaji wa mapato unaendelea vizuri kupitia TRA lakini na Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipitisha bajeti hapa ya shilingi trilioni 44, lakini hadi kufikia leo tayari Serikali imeshakusanya shilingi trilioni 42.28 sawa na zaidi ya asilimia 50, lakini fedha za maendeleo tayari zimeshakwenda zaidi ya asilimia 62; maana yake nini? Ni maana Serikali inafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa maana Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa ambayo unaifanya licha ya changamoto za kiuchumi ambazo tunazipitia kama Taifa lakini na kama dunia bado unaiyona kazi inafanyika na Taifa letu kuna ustahimilivu kwenye mambo kadha wa kadha. Kwa kweli unastahili na ndiyo maana ni mchumi daraja la kwanza kwenye Taifa letu, kwa hiyo tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri unayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongee zaidi Mheshimiwa Rais kwa sababu amekuwa na political will kwenye kusaidia miradi ya maendeleo kwenye Taifa letu inasonga mbele. Mheshimiwa Rais, ukiangalia tu kwenye TFC kwa maana Kampuni ya Mbolea ilikuwa na mtaji wa shilingi bilioni nne, lakini ameipelekea shilingi bilioni 40, maana yake ana nia ya dhati kabisa na kuboresha kilimo cha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine niipongeze nimeona kazi ambayo inafanyika kati ya TRA na Umoja wa Watu Wenye Viwanda kwamba zile sticker za stamp ambazo tulizipigia kelele hapa ndani tayari zimeshuka bei kwa zaidi ya asilimia 64 hadi asilimia 30, kwa hiyo, naendelea kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambayo inafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zangu ni hoja mbili; hoja ya kwanza ni hoja kwenye Kamati ya Bajeti ukurasa namba 73. Ukurasa namba 73 umezungumzia kuhusu riba kwenye mikopo katika sekta binafsi, nizungumze wazi uhai wa benki za Taifa letu umebebwa na watumishi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza haya kwa sababu asilimia kubwa tu ya mabenki yawe ya commercial, yanayofanya na Serikali na yale ambayo ni ya Serikali yamebebwa na watumishi wa nchi hii, kwa nini nazungumza haya? Nayazungumza haya kwa sababu watumishi ndiyo wenye mikopo mingi kwenye mabenki haya na riba zinazotozwa kwenye mikopo hiyo kwa kweli ni riba ambazo zinawanyonya na zinawakandamiza watumishi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze wazi kwamba watumishi wanaobeba mzigo wa hizi benki ni kwa sababu benki zimewekeza zaidi kwenye maeneo ya mijini kuliko kwenye rural areas, kuna Watanzania wengi bado hawawezi kuweka fedha kwenye benki ili benki at least mzigo wa riba ukashuka ukaachwa kwa ajili ya sehemu kubwa ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ninachotaka kukizungumza ni kwamba kuna haja ya Serikali kukaa chini na mabenki, kuangalia namna bora yakuweza kupunguza riba ili watumishi wetu waweze kukopesheka, watumishi wetu waache kuwa wao ndiyo mzigo au ndiyo mabega ya kubeba hizi benki nyingi ambazo zimekuwa kwa kweli riba zao zimekuwa ni kandamizi. Ukienda kwenye microfinance ni hivyo hivyo, ukienda kwenye commercial bank ni hivyo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi wa Taifa hili hana sehemu ya kukimbilia, ni Serikali ndiyo inaweza ikatusaidia, kama tuliweza kutoa uchumi kwenye double digit kwenye sekta ya kilimo riba tukaishusha hadi kwenye single digit kwenye sekta ya kilimo, ninaamini hili pia linazungumzika kuweza kuwasaidia watumishi ili morale yao ya ufanyakazi iwe ni kubwa kwenye maeneo yao ya kazi kwa sababu riba hii imekuwa ni riba kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati inaripoti hapa kwamba zaidi ya asilimia, kwa wastani ni asilimia 16, lakini kuna benki na kuna microfinance zinaenda hadi asilimia 18 hadi asilimia 20 kwenye hizi riba. Kwa hiyo, nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni vyema akaangalia namna ya kukaa na mabenki na pamoja na Gavana wakaangalia utaratibu gani upya unaotumika kupanga hizi riba, lakini pili jinsi ya kushusha hizi riba ili tuweze kumsaidia mwalimu ambaye yupo kule kijijini Makete, mwalimu ambaye yupo kule Ngorongoro, mwalimu ambaye yupo maeneo ya Iramba, mwalimu ambaye yupo maeneo mengine ambaye zaidi ya asilimia 23 za mkopo wake amekuwa akitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri ni kwamba walimu hawa wana security, security ni kwamba wana pay roll inayotoka Serikalini. Kuna mahali pengine nilisema hizi benki zinafanya kwa ushirika wa karibu sana na Serikali na most of them zina horizontal gain ambazo wanazipata tu kupitia hii mikopo na mishahara ambayo inapita. Ni vyema nazo zikaona tija jinsi gani ya kuweza kumsaidia mtumishi wa nchi hii hususani walimu na watumishi wengine ambao kwa kweli wamekuwa ni wazalendo kwa kulitumikia Taifa letu na wanafanya kazi kubwa sana. Kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali iangalie namna ya kuzipitia upya riba za mikopo kwenye Benki, ili Watumishi wetu waweze kukopesheka na watumishi wetu waone kabisa kwamba Serikali yao ipo pamoja nao. La zaidi…(Makofi)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi?

TAARIFA

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kumpa taarifa mzungumzaji kwa mchango mzuri sana ambao anaendelea nao. Sina shaka hata kidogo kwa faida kubwa tuliyokuwa nayo ya kuwa na Waziri wa Fedha, ambaye ni mchumi. Miujiza mikubwa ameweza kuifanya na mimi sina shaka. Niseme tu, Waziri wa Fedha, ana uwezo mkubwa wa kuweza kuhakikisha kwamba borrowing inakuwa cheaper ili sasa watumishi wale waweze kupata nafuu na cooperate citizen. Katika hili sina shida hata kidogo Waziri wa Fedha, ana uwezo mkubwa wa kulifanya. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Festo, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa. Uzuri anayezungumza pia ni mchumi, kwa hiyo nadhani anatambua uwezo wa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, kwenye Sekta hiyo. Tunaamini, na tuna matumaini makubwa kwako Mheshimiwa Waziri, kwamba utawasaidia Watanzania kwenye hili jambo, hususani watumishi wa nchi hii ambao wamekuwa wazalendo sana. Ukifuatilia…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: … mtumishi wa Serikali…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: …anaacha ATM card kwa mtu ili aweze kukopa mkopo. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri vema tukaliangalia hili. Pili, ni kuangalia kuunda namna kikosi kazi. Tuliona juzi ukizungumza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwamba kuna mikopo ambayo ni kausha damu, mikopo ambayo siyo stahimilivu…(Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Festo, tusikilize taarifa ya Mheshimiwa Musukuma.

TAARIFA

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninampongeza sana mchangiaji kwa uchangiajia wake mzuri. Sisi Watanzania hatuna shida na mchumi jemedari ndugu yetu Mheshimiwa Mwigulu, sisi tunatoa mawazo tu ya kuboresha. Ninataka kumpa taarifa, ninaunga mkono kile anachokisema kwamba ni kweli Wizara ya Fedha na Waziri wetu, ukizibana benki zikashusha riba kwa watumishi hawata-relax tena kutafuta wateja kwa sababu hizi fedha zinazokopeshwa kwa watumishi ni fedha ambazo hazirudi kwenye mzunguko, ni za kula na kununulia magari na kwa sababu zina riba zinalipa fidia benki hawafanyi kazi ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo wadogo, wa kati na wakubwa kwa sababu wale ndio wanarudisha hela kwenye mzunguko. Ninakushukuru nadhani atakubalina na mimi Daktari, Mheshimiwa Sanga. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Festo.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na Dkt. Musukuma kwa sababu ni kweli na ndiyo maana nilizungumza kwamba kuna kitu kinaitwa horizontal gain. Horizontal gain ni mtu amelala tu zinaingia zinatoka zinaingia; na watumishi ndio wana-support hizi benki kuwa na horizontal gain; kwa maana hela yao hawateseki kuhangaika kwenda kufuata watu wengine nje vijiji waweze kuingiza fedha kwenye mzunguko. Kwa hiyo watategemea watumishi wa Serikali waendelee kupokea mshahara na kukopa. Kitu ambacho kwa kweli tunaendelea kumuumiza mtumishi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamuomba Mheshimiwa Mwigulu akae chini benki ili waweze ku-support. Mimi ninawaonea huruma sana wafanyakazi wa Taifa letu jinsi wanavyojitoa lakini asilimia ya riba kwenye mikopo imekuwa ni kubwa sana, inawaumiza kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili lisipofanyiwa kazi hapa kuna siku tutaleta hoja binafsi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunatetea maslahi ya watumishi wa Tanzania ambao kwa kweli wanafanya kazi nzuri na wanaiongezea tija Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusiana na hoja ya PIC. Wamezungumza jambo zuri sana hapa, kuhusu mashirika ya umma, na takribani tuna mashirika 304. Hoja yangu ipo kwenye jambo moja; tuna hii miaka mitatu ambayo tunajipanga kwa ajili ya kwenda kuandaa kwa maana ya kuwa na AFCON kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna haya mambo mawili. Kuna mashirika ya umma ambayo yatakiwa kurudisha gawio, kuna mashirika ya umma, ambayo yanatakiwa kutoa contribution ya 15 percent ya growth revenue. Haya mashirika kwa muda mrefu na hili nimemwambia kabisa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwamba hatuendi ku-disturb bajeti yake kwenye gawio tukipata hatu disturb bajeti yako ya mwaka, lakini pili, kwenye CSR hatu-disturb bajeti yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali, kwa sababu tuna nia ya dhati kwa ajili ya maandalizi ya AFCON, kwa sababu tuna nia ya dhati ya kuendeleza michezo nchini, kwa sababu tuna nia ya dhati ya kujenga viwanja vya mpira. Gawio na CSR zingeelekezwa angalau kwa hii maika mitatu zielekezwe kwa ajili ya kusimamia hicho ambacho tunaenda kukifanya kwa ajili ya mwaka 2027. Ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri ataona tija kwenye hilo, kwa sababu hatuendi kugusa mfuko wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara ya Michezo haina fedha bajeti, yake ni ndogo na tutawalaumu tu akina Mwana FA pamoja na akina Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro. Tuone namna gani tunaweza kuwa-support kwa kutoa gawio na CSR ya kwenye makampuni ikaenda ku-support kwenye kujenga miundombinu ya michezo. Itakuwa ni aibu endapo tutapokonywa kuwa mwandaaji wa michuano hii kutokana na kwamba tumekosa maandalizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kutoa mfano mmoja tu, ninaomba dakika mbili tu. Tuna mradi kama wa SGR, zaidi ya trilioni kumezimwaga kwenye huo mradi. Ukiwauliza hata uwanja wa mpira mmoja, hata kiwanja kimoja cha shule ya msingi hamna kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, tuone tija kabisa wanaojenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, wanaojenga SGR na mashirika mengine, fedha zao zielekezwe kwa miaka hii mitatu kwa ajili ya kujenga miundombinu ya viwanja ili Taifa letu tusiingie kwenye ile aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninazungumza hivyo, Taifa la Zambia walifanikiwa kupitia copper belt; Serikali ya Zambia iliagiza kampuni zinazochimba copper, CSR yote ielekezwe kwenye kujenga viwanja na ikafanikiwa. Sisi kama Taifa letu tukiamua hivyo bila kumsumbua Mheshimiwa Mwigulu kwenye bajeti yake, bila ku-disturb maeneo mengine tunaweza tukawa tumeku-support na kuhakikisha kwamba michezo ya mwaka 2027, tunakuwa na viwanja vya kutosha, hoteli za kutosha. Pili, tunakuwa na academy za kutosha kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupongeza zaidi kwa nafasi uliyonipa. Ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa kazi nzuri ambayo unaifanya hakika yeye ni mchumi wa daraja ya Kwanza. Ahsante sana. (Makofi)