Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na awali ya yote ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa, kwa uzalendo kwa nchi yake na kulitumikia Taifa letu. Ninaomba nizipongeze Kamati zote mbili kwa taarifa zao mzuri. Ninampongeza Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Deus Sangu, Mwenyekiti wa Kamati (PIC), tumefanya naye kazi vizuri na nimekuwa nikishiriki katika vikao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja moja tu ya Shamba letu la Mzindakaya, ambalo lipo kule Sumbawanga. Shamba lile lilikuwa ni mkopo kupitia Benki Kuu. Shamba lile alilisimamia Mheshimiwa Mzindakaya kwa muda mrefu sana. Kwa kweli ninachukua nafasi hii, kwanza kumpongeza kwa uzalendo wake na kwa nia njema katika kuendeleza Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzee yule alihangaika sana kuhakikisha shamba hili linapata mafanikio. Kwa bahati mbaya ametangulia mbele ya haki na Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema huko alipo. Ninataka usema jambo moja tu, kwamba shamba lile baada ya mkopo limekwenda mpaka limefika shilingi bilioni 28 pamoja na riba na penalty mbalimbali. TIB wakaazimia kuliuza shamba lile. Wamekaa chini wametoa penalty, zote wametoa interest zote na hatimaye likashuka mpaka bilioni 14. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumuomba Mheshimiwa Waziri, baada ya kufika shilingi bilioni 14 Wizara ya Kilimo ikaamua ukiandikia barua Benki ya TIB, kwamba sisi Wizara tupo tayari kununua shamba hilo kwa shilingi bilioni 14. Mazungumzo yakaenda na Waziri wa Kilimo akakubali kuiandikia barua TIB kwamba tupo tayari kulipa fedha hiyo. Hoja yangu ipo hapo; naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha anisikilize kidogo. Baada ya kubainika kwamba Serikali inataka kununua Shamba lile ali maarufu la Mzindakaya kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu na kilimo cha ngano. Sasa wajanja wametokea, sijui wametoka wapi? Wamekwenda kufanya mazungumzo na Benki ya TIB wameenda kununua shamba lile kwa shilingi bilioni mbili na balance itakayobaki, bilioni 12, zitalipwa kidogo kidogo. Uhamisha mfuko huu au unaruka mkojo unaenda kukanya kule kwingine kuchafu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajiuliza kama nia ilikuwa ni hiyo. Kwa nini, msimwachie Mzee Mzindakaya na familia yake wakaendeleza hivyo wakaanza kulipa taratibu taratibu? Kulikuwa na haja gani ya kuuza shamba lile kwa shilingi bilioni mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli wakati mwingine tukisimama hapa tunasimama kwa uchungu. Tukihoji kwenye Kamati kuna maneno yanakuja, kwamba, unajua kuna maelekezo; nani anayetoa maelekezo hayo? Mtuambie. Kama Serikali imeandika barua Wizara ya Kilimo imesema sasa hivi tutalichukua shamba lile, tutalipa shilingi bilioni 14 kutoka kwenye fedha za EP4R. Shamba lile tutalitumia kuzalisha mbegu pamoja na kulima ngano. Sasa, kati ya Serikali na huyu mtu aliyekuja kutoa bilioni mbili; na mimi simjui; lakini akili hainijii, jamani ninyi ni wasomi, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wewe ni mzalendo wa nchi hii, hebu kaeni chini. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu upo hapa, mawaziri mkae chini muangalie hili lina uhalali gani? bilioni mbili, bora angelipa hata bilioni 10, then akalipa zote. Sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Mzindakaya alikopa na huyu amekuja kukopa tena yaani mnahamisha faili mmoja la mkopo mnalitoa kwa Mheshimiwa Ezra hapa unalipeleka kwa Mheshimiwa Aeshi, deni lipo pale pale. Huyu ninataka kukuhakikishia huyu hatalipa deni litakwenda vile vile ambavyo tumetoka kwa Marehemu Mzindakaya tunakuja kwa huyu bwana ambaye simjui ametoka wapi, amekwenda kununua shamba lile kwa shilingi bilioni mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninahoji kwenye Kamati hivi jambo hili mlifikiria vipi kuliuza shamba hilo wakati huo Serikali inataka kulilipia kwa shilingi bilioni 14? majibu hawana. Mkikaa pembeni wanaanza kukuambia tu, ujue hili jambo hili liache, sasa tunaacha mangapi? Mimi namuona Mheshimiwa Rais ana dhamira njema kabisa na nchi hii, ana uchungu na nchi hii, ninaamini akilijua jambo hili hatokubali shamba hili liende sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha utusaidie, kule Rukwa tunakutana na vitu viwili, kuna Shamba la Efatha lina mgogoro, watu wanauana, tunakuja tunakaribisha mgogoro mwingine, hivi Rukwa wapi tumelogwa? Mimi sijui lakini nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kaa chini ita TIB, waulize hoja waliyotumia na vigezo walivyotumia ni vipi? Pia uombe barua ya Wizara ya Kilimo ipo? Je, mazungumzo ya Wizara ya Kilimo na TIB yapo? Kama yapo kwa nini waliyavuruga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona hivyo Wizara ya Kilimo hakutokuwa na rushwa, wakaona wachezecheze huku ili wachukue percent zao. Hili jambo halikubaliki! Nikuombe sana, tulisema leo tutasimama kwa hoja moja tu. Mwenyekiti wangu anafahamu, Kamati nzima ya PIC inafahamu, na sisi tuliwahoji karibu masaa mawili mpaka ilifika wakati tulitaka kuwafukuza kule ndani. Sasa mimi sipati picha lakini naamini kwa uzalendo wako, uzalendo wa Naibu Waziri Mkuu, uzalendo wa Mama na Kiti kilichokaa pale Mheshimiwa Najma Giga, hili jambo lifuatiliwe na majibu tuletewe. Mimi siungi mkono hoja kabisa shamba lile kununuliwa na mtu binafsi, lirudi Serikalini, hatuwezi kuuza mashamba yote. Kila tulichonacho tunauza, watoto wetu watakuja kurithi nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba ya mbegu hatuna, uzalishaji wa mbegu. Mashamba ya ngano hatuna, ndiyo tunaenda kuuza kila kitu. Nikuombe sana na nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, najua hapa nitakuwa nimeeleweka nilichokisema. Nikisema sana nitakuwa naenda zaidi. Lakini hoja yangu ni kwamba, hili jambo la kutaka sisi tuhoji kwenye Kamati tunaambiwa subirini hili jambo ni zito halafu mwisho wa siku tunakuja tunadanganywa kuwa kuna maelekezo, nani huyo anayetoa maelekezo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha watu wanatumia mwanya wa kupiga na kusema kuna maelekezo. Mimi siamini! Nikuombe lichukue na mimi ninaamini utatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja Kamati zote mbili. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)