Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. DEUS C. SANGU – MWENYEKITI WA KAMATI KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuhitimisha hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ambayo tumewasilisha leo asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao mmetupa pongezi kwa kazi nzuri tuliyoifanya ya uwasilishaji wa taarifa ya Kamati, mimi kama mwenyekiti na Kamati yetu kwa ujumla. Kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuyawezesha mashirika yetu ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha miaka mitatu amewezesha uwekezaji wa mtaji wa takribani trilioni 8.6 na kufanya uwekezaji katika mashirika 304 kufikia trilioni 76.56. Hii ni kazi kubwa ya kizalendo na ameendelea kutoa maelekezo mengi yenye nia ya kufanya mabadiliko. Katika zile 4R hasa katika kipengele cha reform na rebuild ambayo kimisingi imejikita katika mabadiliko ya kiuchumi. Kazi hii tumeiona ya Mheshimiwa Rais na kubwa zaidi hivi karibuni kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii alileta Muswada Bungeni mwezi Novemba Mwaka jana, Muswada wa Uwekezaji wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni Muswada ambao Waheshimiwa Wabunge wameuzungumzia kwa uzito mkubwa na mimi kama Mwenyekiti wa Kamati hii ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma niendelee kuisisitiza Serikali, amesema hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba, Muswada huu haujapotea utarudi. Kamati tulifanya kazi kubwa kuupitia huu Muswada, matatizo yote tunayopitia, shida nyingi zinazoongelea juu ya udhaifu na uendeshaji wa mashirika ya umma ni kukosekana kwa chombo madhubuti cha kusimamia mashirika yetu ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, reform ambayo ilikuwa inakuja na hii Public Investment Authority na ambayo inaenda kuanzisha Public Investment Fund itakuwa ndiyo mwarobaini wa matatizo haya. Niwashauri wenzangu, muswada huu una players. Upande wa kwanza ni sisi Bunge, upande mwingine wa player katika muswada huu ni watu wa Serikali. Sote tujitathmini wala tusiwe na hofu yoyote, wala tusiogope kwamba where shall I fit in kwenye huu muswada au baada ya reform nabakije? Tutafakari kwa nia njema ya kizalendo kwamba muswada huu unaenda kutengeneza mustakabali wa uwekezaji kwenye mitaji ya umma na mashirika yetu ya umma kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo. Nilitaka nilisemee hili jambo kwa msisitizo wake kwa sababu limechangiwa kwa hisia kali na Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia katika jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, niongelee jambo lililozungumzwa sana hapa na kwa hisia kubwa juu ya Benki yetu ya Maendeleo (TIB DFI). Benki yetu ambayo tangia historia ya nchi hii tukianzia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kweli amekuwa mstari wa mbele, si kupigania tu maslahi ya ukombozi wa nchi zilizopo katika ukanda huu wa Bara la Afrika pia amekuwa ukombozi wa Kifikra na Uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mambo aliyoyafanya baada ya kupata uhuru pamoja na kwamba nchi yetu ilikuwa na Sera ya Ujamaa na Kujitegemea, alifikiri namna gani tunaweza tukakomboa hasa Ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Alikuwa ndiyo muasisi wa kwanza mwaka 1967 kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (East African Development Bank 1967); na baadae Mwalimu Nyerere alivyoona kwamba hii ina tija baada yaku-finance miradi mingi ya maendeleo iliyopo hasa katika ukanda huu wa East Africa, ambao wenzetu Kenya kwa kiasi kikubwa walifaidi hii miradi wakaamua mwaka 1970 kupitia Sheria ya Benki ya Maendeleo mwaka 1970 akaanzisha Benki ya Maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, benki hii sasa ina takribani miaka 50, lakini ufanisi wake umekuwa ukipata changamoto nyingi mno. Lengo kubwa la benki hii siyo benki ya kibiashara (commercial). Ni benki ambayo ilianzishwa ili kuweza ku-finance miradi ya maendeleo ambayo ni medium term na long term investment. Miradi hii ilikuwa na lengo moja tu la kwenda kuchagiza ukuaji wa uchumi katika Taifa letu. Badala yake hapa, mambo yamepita mengi na hadithi zinazosimuliwa ndani ya Bunge leo, ni hadithi za kusikitisha. Ni jambo la aibu sana kuona Benki ya Maendeleo imefikia hali iliyopo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapa historia kidogo ya nini kinachoendelea pale? Nitaanzia tu miaka mitatu ya hivi karibuni. Mwaka 2019 benki ilikuwa na mtaji wa shilingi bilioni 242.8. Huu mtaji ukashuka kidogo, mwaka uliofuata ukafika shilingi bilioni 219.7. Baada ya hapo kufikia mwaka 2020 wanapofunga hesabu zao, mtaji wa benki hii ukashuka toka shilingi bilioni 219 mpaka ikafika shilingi bilioni 24, sawa na kushuka kwa mtaji kwa asilimia 89. Maana yake ni nini? Hatujui hesabu zitakazofungwa mwaka huu wa fedha ambazo mkaguzi amezikagua. Yawezekana shilingi bilioni 24 ikapigwa kwa kiasi kikubwa mpaka ikaenda kuwa negative core capital. Maana yake ni nini? Hapo benki hamna, biashara imeisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ninachotaka kusema? Sababu ya haya mambo yote kutokea ni nini? Sababu kubwa iliyosababisha matatizo haya, moja ni kutokujali na utoaji holela wa mikopo. Mikopo chechefu imetolewa. Mwaka 2023 kwenye vitabu hivi vya TIB imeondolewa shilingi bilioni 302.2, wamei-charge off. Ninaposema ku-charge off kihasibu maana yake ni nini? Kama mna mkopo ambao upo kwenye loss category kwa quarter nne mfululizo, Sheria ya Benki Kuu inakuhitaji mkopo huo uuondoe kwenye vitabu, weka pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii yote inaenda kumomonyoa mtaji, unaendelea kwisha. Kuna hadithi moja ambayo siyo nzuri sana, tumeipitia kama Kamati. Kuna wateja wawili katika portfolio ya mkopo wa Benki ya Maendeleo. Wateja wawili tu; mmoja ana shilingi bilioni 83 na mwingine ana shilingi bilioni 104. Jumla wana shilingi bilioni 187, watu wawili. Sasa benki iliyoanzishwa kwenda kuchagiza uchumi na kusukuma uchumi wa miradi ya maendeleo, leo tunaongelea habari ya kwenda kuchukua mkopo BADEA kwa ajili ya kuja kuwekeza kwenye umwagiliaji. Wakati jimboni wanalalamika miradi ya shilingi bilioni tano, sita au tisa, tunaona kama ni hela nyingi, wakati watu wawili wamechukua shilingi bilioni 87 wapo, biashara zao zipo, collateral zao zipo na hawalipi na hawana mpango wa kulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba baadaye tuki-write off na hii, tukiingiza kwenye vitabu vya benki, tayari hadithi imeishia hapo. Ninachoomba ni nini? Yameongelewa mambo mengi, uweke mtaji shilingi bilioni 118, ndiyo utaweka, lakini unaweka, ikifika inapigwa, inaondoka. Sasa si umeona! Kama shilingi bilioni 219 ilishuka ikaja kuwa shilingi bilioni 24, kwani hapo kwenye shilingi bilioni 219 na milioni 24, shilingi bilioni 118 haimo humo? Ukiiweka ndiyo inaenda kutoa tiba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kutokana na nature ya namna kodi zinavyokuwa charged TRA, ukitoa mkopo, wewe una-recognize kama ni mapato ya riba utakayoyapata. Kule TRA wana-charge kodi. Leo hii kuna malimbikizo ya kodi ya shilingi bilioni 68.42 yanayodaiwa TIB na yanaendelea ku-accumulate day to day mpaka sijui hapo yatafikisha hata shilingi bilioni 200. Kwa hiyo, hili jambo naliongelea nikiwa na jicho la tofauti kabisa kwa namna benki hii tunavyoi-preserve. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri tulipata fursa ya kuhudhuria kwenye moja ya jambo kubwa lililokuwa linafanyika pale Morena, la kutia saini mradi wa kwenda kuzarisha megawatt 49.5 kwenye mradi wa Malagarasi kule Kigoma. Nilifurahi sana kusikia habari njema kwamba ule mradi siyo tu kwamba tutapata umeme ndani na kuongeza kwenye Gridi ya Taifa, pia, tutapata advantage hata muda mwingine kuuzia hata nchi jirani kama Burundi na kadharika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ndiyo development yenyewe ilitakiwa tu-finance, lakini kuna kitu kikanifanya nijiulize maswali, mkopo ule tumechukua dola milioni 140 toka kule Benki ya Maendeleo ya Afika. Sisi kama Serikali ya Tanzania tumeweka dola milioni 4.4 kwenye mradi ule. Nikawaza hii TIB yetu si ndiyo ilikuwa kazi yake ya kufanya hivi! Hii TIB yetu si ndiyo financing ya miradi ilitakiwa iwe! Kwa hiyo, hapa kunatakiwa kufanyike mambo yafuatayo: Ikafanyike due diligence ya uhakika na Serikali ihamishie akili, macho na nguvu zote kwenda kuinusuru hii benki. Kwa hiyo, inavyochukua mradi kama alivyowaahidi hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, haiendi ku-function chochote. Itaenda itamezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIB mmeiongezea majukumu mengi, amesema Mheshimiwa Aeshi. Ule Mkopo wa Shamba la Safi la Hayati Mzee Mzindakaya, ule mkopo ulikuwa Benki Kuu, baadaye ukarudishwa uje usimamiwe na hii hii TIB Development. Kwa sababu kuna michezo michezo, Serikali kupitia Wizara ya Fedha wamekwambia watakupa shilingi bilioni 14. Kwa sababu wamezoea kuipigisha short Serikali na kuiingiza kwenye hasara, mnaenda kumpa mtu kwa shilingi bilioni mbili. Tupo, tunaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, jambo la Benki ya Maendeleo ya Taifa, ni jambo very sensitive. Tuungane mkono wote, tulipigie kelele leo, kesho na kesho kutwa mpaka tuone reforms zinafanyika, na ndiyo itakuwa suluhu pekee ya kuisaidia benki hii ika-survive. Otherwise, hakuna tutakachokuwa tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ameongelea suala la VAT refund, nashukuru kwa ufafanuzi wake, lakini kwa kesi tuliyo-build kama Kamati, VAT refund tunazozilalamikia ni kwa Taasisi za Serikali. Nimeongelea habari ya STAMIGOLD ambayo naamini Taasisi ya Serikali haiwezi kufoji risiti wala kufanya mambo haya. Pengine kwenye private wanafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMIGOLD ilianza mwaka wa kwanza ikadai VAT ya shilingi bilioni nne, hawakupewa. Mwaka wa pili shilingi bilioni tisa na sasa mwaka huu wana shilingi bilioni 12.3 wanadai Serikalini VAT refund. Ukiangalia networking capital, mtaji wake ule wa STAMIGOLD ambayo ni state mining company inadai ina mtaji hasi (negative core capital) ya shilingi bilioni 11. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba, hizi VAT refund ukizirusha zinakuja ku-offset hii negative 11, tunapata positive core capital, inaanza ku-operate katika mtaji chanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana maswali yanakuja: Je, hiyo kodi inayotamkwa na TRA ina usahihi? Kama kule kwao wana-recognize hizo shilingi bilioni 12.3, hizi zinazotoka STAMIGOLD kama ni mapato na huku tukija kwenye hesabu za STAMIGOLD tunakuta wanai-compute kama receivable, kwamba ni deni wanalodai. Ukweli uko wapi katika ku-reconcile hesabu hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, haya mambo ni mazito ambayo kama Taifa tusipochukua hatua za haraka yatatugharimu sana. Mashirika yetu katika nchi yetu, giant public spender is the Government. Mtu ambaye anatumia sana kupita institution zote is the Government na investor mkubwa katika nchi yetu ya Tanzania ni Serikali. Sasa investor huyo aliyewekeza takribani shilingi trilioni 76.56 kwenye uwekezaji wake lakini anapata kagawio kiduchu ka shilingi bilioni 850, watu wanawashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna makampuni yanayofanya commercial, achana na haya ya huduma, karibia 66, zote hizi ni sleeping giants, zimelala, hizi ndiyo zilitakiwa zi-drive uchumi wa nchi. Tutoke hapa tulipo, zianze ku-contribute kwenye GDP yetu. GDP yetu ingeweza kupata pato kubwa zaidi hata ya shilingi trilioni tano kutokana na uwekezaji huu wa shilingi trilioni 76 ambayo ni fedha ya bajeti yetu ya miaka miwili. Bajeti yetu miaka miwili imewekezwa kwenye mashirika hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, mambo mengi yamejadiliwa. Hayo mengine ya kampuni tanzu ni mambo ambayo kidogo yanasikitisha. Mnaanzisha kampuni tanzu inakuwa kama a department, yaani hata maana ya kusema ni kampuni tanzu haipo. Mkifika pale mkijisikia wawafanyie kazi fulani mna-divert fund, kafanya huyu hapa. Halafu maana yake ni nini? Hakuna clear line, lazima muweke demarcation, kwamba hii ni subsidiary na hii ni parent company. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, parent company iwe imewapa wale uhuru wa kutosha wa kufanya kazi zake independently, hapo ndiyo tutaona tija. Unless otherwise katika subsidiary zetu tulizonazo kwenye makampuni yetu 57 tukazifanyie analysis tuone, je, hizo zote zinahitajika kuwepo au nyingine ni sehemu ya watu ku-divert mambo yao? Au ni sehemu ya watu kupeleka mambo yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mnasema leo tunaanzisha kampuni ya kwenda kujenga nguzo za zege, ten years iko kwenye archive. Baadaye mnaibadilisha kuwa ni dalali. Anaenda anamwambiwa bwana wewe Dem Constructions jenga nguzo leta hapa, utanipa asilimia nne tu ili niweze ku-survive. Hatuwezi kufanya business kwenye state owned enterprises kwa namna hiyo. Lazima tu-change mindset. Mindset ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyokuja nayo ya kufanya reforms kwenye mashirika ya umma, tum-support kwa nguvu zetu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tutasimama imara kuyatazama kwa kina na tutayapokea na kuyakumbatia mambo pekee yaliyo na maslahi mapana kwa mustakabali wa Taifa letu. Nje ya hapo tutakuwa tunapiga mark time, tunakuja hapa na ni bora tukakaa kimya kwa sababu watu wote watakuwa wanatushangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa Bunge lako Tukufu liyapokee mapendekezo yetu 11 yaliyotolewa na Kamati yetu ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, yawe ni maazimio ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)