Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu na nikushukuru kwa kupata hii nafasi ili niweze kuongea mambo ya kitaifa ambayo yanahusiana na asilimia 38 ya Watanzania ambao ni milioni 23 ya population yetu ya milioni 61 ambao ni labor force ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nataka niongelee kitu kimoja, kuna msemo wa Kiswahili unasema kwamba; chanda chema huvishwa pete, kabla sijaenda huko. Nazipongeza taasisi za NSSF, PSSSF, WCF, OSHA, CMA na taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme na msemo mwingine; ada ya mja hunena, muungwana ni vitendo. Muungwana ukinena unatakiwa utende. Katika Mpango wetu wa Taifa umezungumzia kwamba utazidi kuhamasisha kukuza ajira na ujuzi, hii iko katika paragraph ya mwanzo katika mpango mpya. Pia kuna makubaliano ya Association of Tanzania Employers (ATE), waajiri wa Tanzania walikubaliana na Serikali kwamba zikusanywe skills development levy na one third ipelekwe kama ni investment katika kukuza ujuzi kwa vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa agenda yangu ni moja tu, ni Mradi Na. 6581 ambayo ni Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi. Hii programu walikubaliana, Serikali na Waajiri kwamba, itatoka one third ya skills development levy ili kutazama gap of skills ambayo inakosekana katika viwanda vyetu, katika maeneo yetu ya kazi na ndio maana hawa wamechangia, badala yake sasa muungwana amenena lakini hajatenda kwa sababu mpaka sasa hivi hiki kitu bado hakijafanyika na tumezoea kupeleka shilingi bilioni tisa katika bilioni 300 zinazokusanywa za skill development levy. Tunapata gap of skills kwa sababu hatufuati haya makubaliano yaliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nazungumzia investment katika ujuzi, investment katika ujuzi kwa Tanzania, mwaka jana kwa Watanzania milioni 61 tuliwekeza bilioni tisa. Mwaka huu tumeshuka tumewekeza bilioni 7.8 katika nchi ambayo sasa tunakwenda katika kipato cha kati, nchi ambayo ukiitazama tuko nyuma kiujuzi, halafu katika mipango yetu tunasema kwamba hiki ni kipaumbele. Naomba tutende yale tunayoyasema. Kipaumbele hiki kweli katika hawa vijana milioni 23 tunaweza tukakuza ujuzi kwa bilioni saba? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mpango Mkuu wa Miaka Mitano umezungumzia kwamba tutakuza ujuzi kwa vijana 681,000. Hapa ina maana kwamba kila mwaka tungekuza ujuzi kwa vijana 136,200, lakini kwa bahati mbaya msimu uliopita tulikwenda na vijana 10,000 tu ambao ni sawasawa na asilimia saba ya hii 136,000 ya mwaka. Mwaka huu plan yetu kukuza ujuzi kwa ajili ya kupata ajira kwa vijana 12,280, ni sawasawa na asilimia tisa ya mwaka. Kwa maana hiyo hii asilimia tisa ndio itakayokwenda kukuza ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimemsikiliza vizuri Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye paragraph ya 163 na 164 ya hotuba yake ukurasa wa 81 na 82 alielezea kwamba tutatengeneza fursa za ajira 470,257, lakini Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi imetaka tutengeneze fursa za ajira 8,000,000 na hii itakuwa ni sawasawa na asilimia 29 kwa mwaka. Milioni nane kwa mwaka maana yake ni sawasawa na kupata fursa za ajira 1,600,000, badala yake tunapata 470,000, ina maana hapo bado tunaenda kuanguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, isitoshe uwekezaji katika program hii ni mdogo tena ni mdogo mno, ni sawasawa na kusema kwamba hakuna kitu. Waarabu wana kitu wanasema kwamba kuna kitu kinaitwa Mudahala, Mudahala ni kumpaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa. Maana yake anaona anapakwa mafuta, lakini kumbe mafuta yako ndani ya chupa, kwa maana hiyo tunakuwa tunamdanganya na kwa kuwa tunajidanganya wenyewe ni sawasawa na kujitekenya halafu tunacheka. Sasa hapa hatufikii malengo ambayo tumeyaweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninazo statistics hapa, nchi yetu ina watu milioni 61, labor force yetu ni milioni 23, lakini pia skilled labor ni asilimia 3.6 peke yake, lakini inatakiwa tufikie asilimia 12. Ni sawasawa tunafikia labor force ya watu 828,000 ambao ndio waliosoma katika milioni 61, ndio skilled labor, hapa tuko chini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija ukatazama katika hotuba ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu amesisitiza kwamba itolewe one third kama tulivyokubaliana na tusipofanya hivyo ina maana kwamba hii program inaweza ikafanyika lakini isilete tija. Tumebaini katika ziara yetu ya Kamati watu wanasomeshwa lakini inakuwa kama anakwenda na kurudi shule, hana kifaa chochote, anarudi mtaani anasahau kila kitu. Ina maana bado elimu hiyo ya ufundi huo tunayowapa inakuwa haileti tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa Kamati pia umesema kwamba, ni lazima ipelekwe hii, lakini kuna Sheria ya Mafunzo Mheshimiwa Mwigulu alikuja nayo hapa kwenye Finance Act katika Finance Bill, alikubali kuweka one third kama iwe ring fenced, lakini tunashangaa mwisho Serikali haikupitisha. Hapa ninayo Hansard ya tarehe 26 Juni, Mheshimiwa Mwigulu alisema hili jambo litaletwa mwaka huu kwa sababu mwaka jana halikuweza kufanikishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuzungumza hivi hivi isipokuwa bora labda tujilinganishe na wenzetu ambao na wao wako katika hizi nchi za Afrika, wao wanawekeza vipi na wamefanikiwa vipi? Tutazame Botswana, Botswana imewekeza dola milioni 11.35 ambayo inakuwa ni sawasawa inakaribia kwenye shilingi kama bilioni 25 za Tanzania, lakini Mauritius imewekeza karibu ya bilioni 70. Sisi Tanzania tunawekeza shilingi bilioni 9.0, Mauritius population yao ni 1,301,636, lakini vijana ambao ni labor force, ni sawasawa na watu 532,000, sisi ukitutazama tuko wengi milioni 23 tunawekeza fedha kidogo kuliko ya wao. Botswana labor force yao ni 1,145,000 lakini fedha walizowekeza ni nyingi kuliko sisi na ukitazama population yao ni ndogo kuliko sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa labda tutazame katika skilled labor au labor force ambao ipo. Wenzetu, watu ambao wamekuwa employed ni 400,000 katika labor force ya 500,000, vijana 400,000 wamekuwa employed, vijana 100,000 ndio wako nje ya ajira, lakini bado wamewekeza vizuri. Hiyo ni Mauritius.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija Botswana katika 970,000 waliokuwa wamekuwa employed ni 732,000 na 232,000 pekee ndio ambao wamekuwa unskilled. Hii inatokana na maamuzi ya makusudi na utashi wa kisiasa. Sisi tuna vijana wengi lakini hatutaki kuheshimu makubaliano. Sasa tatizo linakuja wapi? Tatizo linakuja kwamba bado hatujakubali kubadilika na kama hatutakubali kubadilika ina maana kwamba hatutoweza kufikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huu ni wakati wa kufanya mageuzi katika kutazama ufundi unaohitajika katika soko. Hawa employers wanatoa hizi fedha ili tuangalie required force inayotakiwa pale. Kwa hiyo zile skills zinazotakiwa na hawa waajiri ni lazima sisi tuweze kuzi-produce lakini hatuwezi kutoa zile skills kwa sababu tunaangalia vitu vingine. Hizi fedha zimekosa clarity, hazina uwazi na uwazi wenyewe kwamba hatujui kiasi gani kimekadiriwa kwenda kule, sisi tunasema iende one third kwa makubaliano, lakini inakwenda bilioni tisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwigulu alituahidi kwamba atafanya liwezekanalo ili aweze kukidhi haja ya kupeleka hizi fedha kule ili ziwe nyingi, lakini mpaka leo hatujaona mid-year review. Kwenye hii mid-year review ingeonesha kwamba kuna fedha zimekwenda kwa ajili ya ku-train watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanachangiwa kutokana na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa King, ahsante.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: …msimamo katika kutazama vijana. Naweza nikasema neno moja ambalo niliwahi kulisema…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa King muda wako umekwisha.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: …Mungu anasema; famaa amalali Mussa ila dhuriya, waliomuamini Musa ndio maana akashinda walikuwa ni vijana, lakini sisi vijana tunawatelekeza, hatutaki kufanya kama Musa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)