Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote naishukuru sana Serikali kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Mlimba. Wananchi wangu wa Jimbo la Mlimba ni miongoni mwa wananchi ambao wamepata maafa ya mvua hizi za El-Nino. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa sababu Serikali imechukua hatua mara moja baada ya wananchi wangu kupata changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wananchi wa Kata ya Masagati, takribani kaya 391 na wananchi 1,486 wanatafuta chakula. Serikali iliweza kunisaidia usafiri wa helikopta na sisi wananchi wa Mlimba kwa kushirikiana na wafanyabiashara tuliweza kupata chakula tani nne tukawapelekea chakula kiwasaidie kwa muda huo mfupi. Sambamba na hilo, Mheshimiwa Rais alielekeza timu ya Mawaziri wanne na Manaibu watatu, ikiongozwa na Mama yangu Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, walifika Masagati, walifika Mlimba. Jambo hili naendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, kwa kweli naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye sababu za maafa. Sababu za maafa ziko mbili; moja ni mabadiliko ya tabianchi, mbili ni ukosefu wa matumizi bora ya ardhi (mipango ya matumizi bora ya ardhi). Mabadiliko ya tabianchi yametokea baadhi ya maeneo kama vile Manyara halikadhalika na kule kwangu Mlimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia pia kwa habari ya ukosefu wa mipango na matumizi bora ya ardhi kwa sababu Taifa letu lina changamoto hiyo. Katika maeneo mengi wananchi wamekuwa wakijenga maeneo ambayo ni hatarishi, (hazardous areas). Sasa kama tungekuwa na mipango ya matumizi bora maana yake ni nini? Tungeweza kuchukua tahadhari haraka wananchi hao wasijenge maeneo hayo, wakajenga maeneo ambayo kimsingi yanafaa kwa kujenga makazi yao, mathalani Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiutazama Mkoa wa Dar es Salaam hauna Infrastructure Masterplan, hata kama ipo basi haijatekelezwa, kwa sababu, Infrastructure Masterplan inaeleza wapi maji ya mvua yanaelekezwa. Sasa, katika mazingira hayo maafa haya yametokea na nimesema tu kwa sababu ya muda nieleze kwa ufupi kwamba, sababu kuu ni mbili. Ni mabadiliko ya tabianchi, ya pili ni ukosefu wa mipango na matumizi bora ya ardhi na kwa kuwa sasa hivi Waziri wa Ardhi ni Waziri anayeshaurika tutampa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nieleze madhara yaliyotokana na maafa haya hasa katika Jimbo langu la Mlimba. Huduma ya usafiri wa barabara haupatikani, Barabara yote ya kutoka Ifakara – Mlimba – Madeke – Njombe haina mawasiliano, imekatika. Upande wa huduma ya usafiri wa reli, nayo imekatika katika eneo hili. Kwa hiyo, wananchi wangu wa Jimbo la Mlimba wapo kisiwani. Leo hii ili ufike Mlimba hakuna mbadala zaidi ya kwenda na helikopta. Kwa hiyo, naiomba Serikali, Wizara husika, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi waone namna ya kuchukua hatua za haraka kurejesha mawasiliano ya barabara na reli.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iwasaidie TAZARA. Reli imekatika, leo hii mwezi mzima umepita lakini hakuna jitihada za makusudi zinazofanywa pale na TAZARA kurejesha mawasiliano ya reli. Hivyo, naiomba Serikali hata kwa kutumia vikosi vyetu hivi kama SUMA JKT na hata Jeshi lenyewe, wachukue hatua pale. Ni jambo la kutoa tu ule udongo uliolala kwenye reli ili ile reli ipitike.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu lingine kwa niaba ya wananchi wa Mlimba, tunayo ile Treni ya Mwakyembe pale inayosafirisha watu kutoka Dar es Salaam kuja Mlimba. Ombi langu iongeze safari zake, badala ya kusafiri mara mbili kwa wiki, basi safari zile zifanywe angalau mara nne kwa sababu sisi wananchi wa Mlimba kwa kiasi kikubwa tunatibiwa hapa Ifakara. Kwa hiyo, leo hii akitokea mgonjwa wa Mlimba anatakiwa aende Ifakara Saint Francis Referral Hospital, hawezi kufika kwa sababu hakuna mawasiliano ya reli. Kwa hiyo, maombi yangu kwa kuwa najua na naamini Serikali ni sikivu, hivyo itakwenda kuwatendea haki wananchi wa Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu eneo lingine, Serikali ijitahidi kuharakisha zoezi la kuwapatia chakula wananchi wa Mlimba. Tunafahamu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa inafanya kazi zake vizuri, tunafahamu Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatuma timu kule ya kufanya tathmini. Ombi letu wananchi wa Mlimba, watusaidie kile chakula kitufae sisi wananchi wa Masagati.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, eneo lingine nigusie Shirika la Reli la TAZARA. Shirika hili la Reli la TAZARA, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa utashi wa Marais wawili. Rais wa Zambia na Rais wetu Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mahusiano aliyoyajenga na watu wa Zambia wamekubaliana kufanya maboresho ya Shirika letu la Reli. Maombi yangu, kuna shida kwenye upande wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria iliyoanzisha Shirika la Reli ina changamoto zake, hasa kwenye eneo la uwekezaji wa mtaji. Kwa hiyo, kwenye mabadiliko hayo, hofu yangu tusiachie tu utashi, tumwombe Waziri wa Uchukuzi atuletee mabadiliko ya sheria ya TAZARA. Sheria iliyoanzisha Shirika la Reli (TAZARA) wafanye mabadiliko kwenye eneo la uwekezaji wa mtaji. Kwa muda mrefu Serikali imeshindwa kuwekeza kwenye Shirika la Reli la TAZARA kwa sababu ya ombwe kwenye sheria yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake nini? Leo hii Sheria inasema, Zambia na Tanzania hisa ni 50% kwa 50%. Kwa hiyo, leo hii kinachofanywa na Waheshimiwa Marais hawa wawili ni utashi tu. Kwa hiyo, hatuna uhakika kwamba Rais mwingine atakayekuja atakuwa na utashi wa namna hii. Ili kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji wa Reli ya TAZARA, ni muhimu sasa Waziri wa Uchukuzi atuletee Bungeni hapa mabadiliko ya Sheria ya TAZARA ili kuweka mgawanyo wa hisa. Yule anayewekeza mtaji zaidi, basi awe na hisa nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, labda watu hawafahamu umuhimu wa Reli ya TAZARA. Reli ya TAZARA ilianzishwa mwaka 1975. Ni kwa sababu ya kurahisisha huduma ya usafiri wa reli kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda New Kapiri Mposhi Zambia. Hii ilisaidia kuunganisha mahusiano ya kibiashara baina ya nchi zetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa kuwa kengele imegonga, nawaomba Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Ulinzi na hata Wizara ya Ujenzi, washirikiane kutusaidia kurejesha usafiri wa Reli ya TAZARA, kwani sasa hakuna mawasiliano ya reli kwa upande wa Mlimba kwenda Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)