Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na napenda kutumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya tulizonazo humu ndani. Pia kwa niaba ya wananchi wa Mafinga, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru Serikali na Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake wote kwa jinsi ambavyo tunaendelea kuijenga Mafinga. Hivi karibuni tulikabidhi gari la kubebea wagonjwa pale kwenye Kituo cha Afya cha Ifingo, kama hatua za kuboresha huduma za afya kwa wananchi wetu wa Jimbo la Mafinga Mjini ambalo pamoja na kuwa lina hospitali ambayo ni kama vile inahudumia Wilaya nzima na wilaya za jirani, lakini pia ipo kando ya barabara kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kupata ambulance ile maana yake ni kwamba inaenda kutusaidia kurahisisha utendaji. Hata hivyo, natumia nafasi hii kuomba gari kwa ajili ya kufanya tathmini. Nilizungumza na Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Festo Dugange, alinihakikishia kwamba tutapata wasaa wa kulijadili jambo hilo na kuona ni kwa namna gani watatusaidia watu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga kupata gari kwa lengo lilelile la kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia pia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na wasaidizi wake kwa Hotuba nzuri ya Bajeti. Naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla, kwa kuja na hii Idara inaitwa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali. Idara hii nimeona hapa kulikuwa na watu wa CAG, kwa namna fulani Idara hii inaisaidia Serikali kufanya monitoring ya utendaji wa kila siku wa shughuli za Serikali, hususan katika kufuatilia utekelezaji wa miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba, tofauti na siku za nyuma ambapo tungesubiri pengine mpaka mwisho ndiyo mradi uje ufanyiwe tathmini, lakini idara hii inafanya ufuatiliaji wa kazi kadri zinavyoendelea. Kwa hiyo, kama kuna mapungufu maana yake ni kwamba yatafanyiwa kazi wakati ile kazi inaendelea ili kuipunguzia Serikali hasara ambayo pengine ingekuwa imejitokeza. Kwa maana nyingine, hii ni kama vile tunasema prevention is better than cure, yaani kwamba hii badala usubiri kutibu, basi yenyewe inaanza kuchukua tahadhari mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo naomba kuishauri Serikali. Kwa sababu hii ni Idara muhimu sana ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utekelezaji wa Shughuli za Serikali, naomba mambo mawili muhimu. Kwanza, ili itimize wajibu wake kiufasaha na malengo yaweze kutimia, lazima tuiongezee nguvu kazi. Nguvukazi ya watu kwa maana ya watendaji, nguvukazi ya vitendea kazi na nguvukazi ya rasilimali fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kusisitiza jambo hili kwamba, ili iwe na thamani na maana halisi ya kuanzisha Idara hii, basi tuifanye kwa vitendo kwa maana ya kuiongezea watendaji, kuiongezea vitendea kazi na kuiongezea nguvu ya fedha. Kwa sababu, kazi inayofanya ni kuokoa mamilioni na mabilioni ya fedha za Serikali ambazo kama isingekuwepo, kama ingekuwa haifuatilii na kama itashindwa kufuatilia kama lengo lilivyo, maana yake ni kwamba tutashindwa kuokoa hizo fedha za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo ningependa kushauri na kulizungumzia ni kuhusu kazi na ajira. Mojawapo ya kitu muhimu ambacho kinaweza kuimarisha suala zima la upatikanaji wa ajira ambazo ni rasmi na za kujiajiri, ni pamoja na uwepo wa miundombinu madhubuti. Kwa hiyo, nashauri sana, pamoja na kazi nzuri ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu imeifanya katika hizi siku za karibuni kukabiliana na maafa kutokana na mafuriko, kutokana na miundombinu ya maeneo mbalimbali ya barabara kuharibika, naomba na kushauri, hili liwe kama funzo na fundisho kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba huwa tunakuwa na fedha ya dharura na inawezekana bajeti yetu ikawa ni finyu kiasi kwamba tusiwe na fungu kubwa la dharura, lakini maafa yaliyojitokeza mwaka huu, yawe funzo kwetu na tujielekeze kwa kiwango kikubwa kuwa na fedha za dharura especially kwa ajili ya miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi? Sasa hivi ilivyo kama sehemu ya watu kujiajiri, nchi yetu asilimia kubwa ni wakulima. Leo hii miundombinu maeneo mengi hakuna mawasiliano. Nitatoa mfano tu, pale Mafinga Barabara ndogo tu ya kutoka Uguta kwenda Kikombo kalavati limezolewa na maji. Maana yake ni nini; wananchi kutoka Mafinga kwenda Kikombo kupeleka bidhaa watashindwa kwenda ama itabidi watumie safari ndefu kuzunguka maeneo ya Rungemba na Kitelewasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, wananchi hawa kutoa mazao yao kuyapeleka sokoni Mafinga Mjini, ama watashindwa kama mazao yao ni mali mbichi zitawaharibikia au itabidi wazunguke kwenda Rungemba ili wafike sokoni, maana yake tunawaongezea gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, maeneo kama kwenda Bumilayinga, maeneo kama ya Mtula ambako kuna Skimu ya Umwagiliaji, kama hakuna miundombinu ya uhakika maana yake ni kwamba kuhusu kipengele kizima cha kazi na ajira, hakitakuwepo kwa sababu hakuna movement, kutakuwa hakuna ajira kwa sababu hakuna movement.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, hata matengenezo ya magari leo hii watu wa vibasi kama hiace wanaokwenda Mufindi kwa pale Mafinga, anatumia masaa mengi kufika kwenye kituo anachokwenda, lakini akienda akirudi atakuwa na gharama kubwa sana za ku-service chombo chake. Kwa hiyo, hata kile alichokipata kama sehemu ya kujiajiri na chenyewe chote kinapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu; tuwekeze katika miundombinu na ikiwezekana sijui kama nitaeleweka, lakini katika bajeti ya mwaka huu, kama kuna kitu ambacho inabidi tukiwekee macho mawili ni sehemu ya kuimarisha miundombinu. Leo hii Mafinga, Mufindi hata maeneo ya Njombe, watu wanaofanya shughuli zao za msitu hawawezi kwenda msituni kusomba magogo au kufanya shughuli zao kwa sababu miundombinu na barabara hazipitiki kwa namna inayotakiwa. Kwa hiyo nguvu yetu na akili yetu kama Taifa tuwekeze sana katika miundombinu kwa sababu kwa kuwepo miundombinu imara maana yake ni kwamba tutakuwa tumejitengenezea ajira kwa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, yawezekana kabisa huu ukawa ni mzigo mkubwa sana kwa Serikali; ushauri wangu, tulipitisha hapa Sheria ya PPP, hebu tujaribu kuitumia sheria hiyo kuona kwa namna gani tuta-engage private sector katika kuimarisha na kujenga miundombinu. Nchi yetu ni kubwa, Serikali kwa hakika kama tutasema ijenge peke yake itachukua miaka mingi kuweza kuwa na miundombinu ya uhakika. Kwa hiyo tutumie utaratibu shirikishi wa kutumia sekta binafsi kujenga miundombinu katika baadhi ya maeneo. Naamini ni salama zaidi kwa wananchi kuongeza gharama kidogo, lakini wakafika kwa wakati na kwa usafiri wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la mwisho kwa kumalizia katika hili hili la ajira na kazi, naomba kuishauri na kuipongeza Serikali kwa mpango wa BBT. Sasa, kwa sababu hii ni programu, ushauri wangu bado naendelea kusisitiza ndani ya Serikali kushirikiana, JKT, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo tuone kwa namna gani tunaweza tukawashirikisha vijana ambao wanaenda JKT kwa nia ya kujitolea, wanapata mafunzo ya uzalishaji mali, mafunzo ya nidhamu na kwa namna gani tutawa-incorporate kwenye mpango wa BBT, naamini watakuwa na tija kwao kama sehemu ya kujiajiri, lakini pia watakuwa na tija kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni kuhusu Mradi wa TACTIC. Huu ni mradi wa kuboresha miji, manispaa na majiji kama ilivyo DMDP katika Jiji lako la Dar es Salaam. Mimi Mafinga na baadhi ya miji tupo awamu ya tatu. Ushauri wangu na ambao nimeutoa na nimeusema kila siku, kwa sababu mpango huu upo chini ya Benki ya Dunia na kwa sababu ni mkopo nashauri kwa kushirikiana na TAMISEMI Wabunge ambao tunatoka awamu ya tatu na ya pili tukutane ili tuweze kushauri kusudi mradi huu uweze kwenda kwa mapema na kwa haraka. Hii ni kwa sababu mradi huu pamoja na ujenzi wa barabara, lakini pia tunakwenda kujenga vitega uchumi ambavyo vitakuwa vyanzo vya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano sisi Mafinga tunaenda kujenga Stendi pale Kinyanambo, tunakusudia kujenga soko kubwa la mazao ya misitu na pia tunakusudia kuimarisha na kuboresha soko letu. Hivi vyote vinakuwa ni vyanzo vya mapato ambavyo hatimaye vitaipunguzia Serikali mzigo. Kwa mfano, zile fedha ambazo zingeenda TARURA kama miradi itatekelezwa hii ya DMDP II na TACTIC maana yake kuna portion itatoka TARURA itaenda kufanya kazi sehemu nyingine kwa sababu miradi hii itakuwa tayari imetekelezwa chini ya mpango wa Benki ya Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, Mungu atubariki wote, Mungu aibariki Mafinga, Mungu aibariki Tanzania na nawatakiwa wote mchezo mwema siku ya Jumapili kati ya Simba na Yanga. (Makofi)