Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii leo ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika bajeti hii ambayo imewasilishwa hivi punde. Kwanza kabisa napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya katika kushughulika na masuala mbalimbali ya kiserikali. Pia niwapongeze Mawaziri walio chini yake nikianzia na dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, ndugu yangu Mheshimiwa Katambi, ndugu yangu Mheshimiwa Ndejembi pamoja na dada, Mheshimiwa Ummy Nderiananga kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, kwa kweli ni Mawaziri wa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nataka kwanza nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu zangu wa Rufiji na Kibiti kwa maafa makubwa ambayo yamewakumba, kwa kweli ni changamoto kubwa sana ambayo wameipata. Nipende kuchukua nafasi hii kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inashughulika na Kitengo cha Maafa kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika maeneo ya Kibiti na Rufiji. Kwa kweli wanatutia moyo na wanawapa watu hali na moyo wa kuiona Serikali yao jinsi gani inawathamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitazungumzia suala la miundombinu. Kwa kweli Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mama yetu Samia Suluhu Hassan wanajitahidi sana sana katika suala la miundombinu, lakini bado tuna changamoto kubwa sana ambazo zinatukabili katika suala zima la miundombinu. Ningependa kuzungumzia hasa katika Jimbo langu la Bagamoyo. Leo hii Bagamoyo kuna barabara ambazo hazipo sawa, barabara ambazo zimekumbwa na mafuriko na zimeharibika vibaya sana. Nikichukulia Barabara moja ambayo inatoka Mingoi kwenda Kiembeni, barabara hii ilikuwa katika ahadi ya Mheshimiwa Rais, katika ujenzi wake lakini leo hii barabara hii imekuwa haipitiki. Wananchi wanapambana na kujitahidi kadri siku zinavyokwenda kuhakikisha wanaweka sawa barabara hii kwa nguvu zao, lakini bado barabara ni changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu suala la daraja. Serikali kama inakumbuka mnamo tarehe 3 Januari, 2023, ilitia saini Mkataba wa Ujenzi wa Daraja la Mpiji, daraja ambalo linaunganisha Bagamoyo na Dar es Salaam. Daraja hili kwa kweli tangu mkataba umeingiwa na Wachina wale ambao wanataka kujenga hili daraja wamefika pale, sasa hivi muda mrefu unakwenda Wachina wameweka kambi lakini hakuna chochote kile ambacho kinaendelea kufanyika mpaka sasa hivi. Kwa hiyo niwaombe Serikali, kwa sababu tushaingia mkataba, basi wajitahidi daraja hili ili liweze kujengwa kwa sababu ni daraja ambalo ni kiunganishi kikubwa sana kati ya Bagamoyo na Dar es Salaam. Vilevile ni daraja ambalo litakapokamilika litapunguza foleni iliyopo katika njia ya Bagamoyo na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia barabara nyingine, barabara ya kutoka TAMCO Kibaha kuja Baobab Mapinga. Mkataba wa barabara hii ulitiwa saini tangu tarehe Mosi Julai, 2023 na mkandarasi alishaanza kazi, lakini cha kushangaza kwamba kasi ya ujenzi wa hii barabara ni ndogo sana na hairidhishi. Kwa hiyo niombe Serikali kuhakikisha kwamba wanaongeza kasi katika ujenzi wa barabara hii inayotokea TAMCO kuja Mapinga Baobab ili iweze kuhudumia wananchi katika shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuzungumzia barabara ya Makofia - Mlandizi. Muda mchache uliopita Mheshimiwa Mbunge mwenzangu wa Kibaha Vijijini aliulizia kuhusu barabara hii. Kwa kweli inasikitisha kwamba barabara hii tangu imeingizwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ni miongo miwili sasa hivi, zaidi ya miaka 20 inaingizwa lakini hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali ya Mama Samia, juzi wameanza hatua moja ya kufanya tathmini katika barabara hii, lakini barabara hii bado ni changamoto kubwa sana. Kwa kweli naomba sana Serikali kuitupia macho mawili barabara hii, kwa sababu ni barabara ambayo inasaidia sana katika ukanda huu wa kuunganisha Kibaha pamoja na Bagamoyo. Juzi tu ilitokea ajali ya kuungua kwa mabasi na lori, barabara hii ilitumika sana kupitisha magari mengi ili waweze kufika Dar es Salaam kutokana na changamoto iliyojitokeza katika Barabara ya Morogoro. Niwaombe ndugu zangu wa Serikali, Wizara na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuitupia macho Barabara hii ya Makofia Mlandizi ili iweze kuwasaidia wananchi

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ambayo nataka niizungumzie ni barabara ya Makurunge – Pangani – Tanga. Barabara hii inaendelea kujengwa kwa muda mrefu na kwa kweli bado kasi yake hairidhishi. Naomba hii barabara kama ikiwezekana hawa wakandarasi nao waanze kuanzia kipande cha Makurunge kuelekea Tanga, kwa sababu kipande hiki ni muhimu sana katika uchumi wa Bagamoyo na Taifa kwa ujumla. Watakapoanza kujenga kipande cha Makurunge kuelekea Pangani kwenda Tanga kutasaidia kuifungua Mbuga ya Wanyama ya Saadani. Watalii wengi leo hii wanashindwa kwenda Saadani kuangalia wanyama kutokana na miundombinu mibovu ya barabara. Sasa barabara hii itakapokamilika itasaidia sana kunyanyua uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachilia mbali suala la Mbuga ya Wanyama ya Saadani, bado kuna kiwanda kikubwa sana kinazalisha sukari na kuna mashamba ya miwa ya Bagamoyo Sugar. Bado kinahitaji barabara kusafirishia mizigo yao kupeleka na kutoa mizigo yao kutoka kule, kwa hiyo, niwaombe sana Serikali wahakikishe barabara hii wanaitupia macho. Hata ikiwezekana kuingia mkataba wa kuanza kujenga upande huu nao pia, kwa sababu itawasaidia hata ndugu zetu ambao wanazalisha miwa (out growers) kupeleka miwa katika Kiwanda cha Bagamoyo Sugar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, barabara hii itakapojengwa ya Makurunge kuelekea Saadani, itasaidia hata wazalishaji wa chumvi. Kuna mashamba mengi ya chumvi Kitame pamoja na Saadani ambao wanategemea sana barabara hii. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuitupia macho barabara hii katika kiwango ambacho wanakiona kinafaa. Ukiachilia mbali hilo kuna fursa nyingine vilevile, barabara hii inapotokea Makurunge sehemu kubwa ipo chini ya Serikali, kwa hiyo, Serikali haitapata gharama ya kufidia kwa watu ili kuweza kujenga hii barabara, itakuwa yenyewe imechukua eneo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kidogo katika upande wa afya; niishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kule Bagamoyo tumepata Kituo Kipya cha Afya, tumepata zahanati na vifaa tiba. Tuna changamoto kidogo bado Wahudumu wa Afya katika hiki Kituo cha Afya na hizi zahanati hawatoshelezi. Leo hii Kituo cha Afya ambacho kinakadiriwa kuchukua wafanyakazi 50, kinakuwa na wafanyakazi watano, kwa kweli utendaji kazi wake unakuwa hauridhishi. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali kutupia macho sana katika hili suala la Wahudumu katika Sekta ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umeme; tunatambua Serikali ina mkakati na ina mpango Bwawa la Mwalimu Nyerere litakapokwisha kuzalisha umeme wa kutosha. Leo hii tuna changamoto kubwa sana ya umeme na hasa katika Mji wangu Bagamoyo umeme unakatika mara kwa mara hatujui tatizo ni nini? Kila kukicha umeme unakatika mara tatu, mara nne, mara tano, malalamiko ya watu yamekuwa makubwa sana. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iangalie sana jinsi gani suala zima la uboreshaji wa miundombinu ya umeme linafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la elimu nigusie kidogo nako, kuna suala la upungufu wa madawati katika shule zetu za msingi. Tunatambua mchango mkubwa wa Serikali katika kutujengea madarasa, kutupatia madawati lakini haya madawati yanayokuja mwanzoni wakati madarasa yanajengwa yakishakwisha au yakishaharibika hakuna mbadala. Shule nyingi sasa hivi wanafunzi wanakaa chini kutokana na upungufu wa madawati. Kwa hiyo, tulitupie macho suala hili la madawati kwa vijana wetu ambao wengi wao sasa hivi wameshaanza kukaa chini kutokana na uchakavu wa hii miundombinu ya madawati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nigusie vilevile suala la uvuvi; nimshukuru Mheshimiwa dada yangu Ummy Nderiananga, alikuja Bagamoyo kuja kukagua eneo la kujenga vichanja vya kuanikia samaki, kwa kweli Wizara inajitahidi. Nataka nizungumzie kitu kimoja, bado katika Wizara ya Uvuvi, kuna ahadi zao hawajakamilisha. Pale kwangu Bagamoyo waliniahidi boti ya uvuvi kwa ajili ya wakulima wa mwani katika Kikundi cha Msichoke kilichopo Mlingotini. Boti pamoja na vifaa vyote mpaka sasa hivi bado havijapatikana na huu sasa hivi ni mwaka wa pili. Naomba Serikali ile ahadi waliyoitoa ya boti katika Kikundi cha Msichoke ambacho kipo Mlingotini pamoja na vifaa vyake, basi waitimize ili kuhakikisha kwamba, wananchi wale wanafanya mradi wao kwa kujiamini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naomba niishukuru tena Serikali na niishukuru Wizara. Naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)