Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi, nimshukuru Mungu kwa kupata fursa ya pumzi, lakini kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu, kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo ameitoa juzi na naamini leo anaenda kuhitimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri ambazo zimefanyika katika Majimbo yetu likiwemo Jimbo langu la Manyoni Magharibi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapompongeza Mheshimiwa Rais, huwezi kuacha kuwapongeza wanaofanya kazi chini yake akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi zake nzuri lakini usikivu ndani ya nyumba hii tukufu na kubwa. Pia niwapongeze Mawaziri wanaomsaidia akiwemo Mheshimiwa Jenista Mhagama, ambaye kwa kweli anafanya kazi za kiwango cha juu sana na usikivu ambao ni wa kipekee katika Mawaziri waliopo katika Serikali hii, pia, Manaibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoipongeza Serikali tunapongeza na kuona namna gani wamefanya kazi katika maeneo yetu. Kwa miaka hii mitatu tumeshuhudia mageuzi makubwa sana katika ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya na maji, ikiwemo miundombinu ya barabara na mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoipongeza Serikali pia kuna changamoto kadha wa kadha ambazo tunapaswa kuzisemea sisi kama Wawakilishi wa Wananchi ambao tumeletwa humu ili kuwasemea watu ambao wametutuma humu. Mimi ni Mbunge ninayetoka katika Majimbo ya Vijijini, watu wetu zaidi ni wakulima, niipongeze Serikali, Wizara ya Kilimo kwa mipango waliyonayo sasa kwa kiasi fulani inaonesha mwelekeo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo ambalo nataka niishauri Wizara hii, ili tuwe hub ya chakula katika ukanda huu, tunapoenda kuwafundisha watu kulima kuna watu ambao siku zote walikuwa wanalima. Bei za pembejeo, bei za mbegu bado siyo rafiki kwa kilimo chetu. Wizara hii ilipoongezewa pesa kwa asilimia 300, nilitarajia wangeweka ruzuku katika pembejeo kwa kiasi kikubwa. Unapopunguza bei za matrekta unamsaidia si yule aliyenunua treka unasaidia walio wengi ambao wako katika eneo lile trekta moja linaweza kuwasaidia wakulima zaidi ya 30, 40, 50 katika eneo moja, maana yake tutaongeza nguvu kazi ya kilimo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya mbegu si rafiki, Mheshimiwa Waziri Mkuu, alihimiza watu wa Singida, Simiyu na Dodoma kulima sana alizeti, lakini bei ya mbegu nzuri za alizeti hazinunuliki, matokeo yake watu wananunua mbegu hizi ambazo ni za kawaida na tija inakuwa ndogo. Niiombe Serikali ione namna gani ya kuweka ruzuku katika mbegu, mbegu za mafuta, mbegu za chakula kama mahindi, bado bei ya mbegu unauza zaidi ya debe moja kupata kilo moja ya mbegu ya kupanda, kwa kweli hii siyo sawasawa na si haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze tena Serikali kwa mara nyingine katika eneo langu tunajenga Barabara ya kutoka Mkiwa kuelekea Mbeya kwa kilomita 56. Kwa kweli barabara ile inajengwa kwa kiwango kizuri sana na mtiririko unaonekana ni mzuri. Tunapojenga barabara upande wa TANROADS hakuna shida, kuna changamoto upande wa TARURA, bajeti yao haitoshi na barabara nyingi za vijijini zinasimamiwa na TARURA pamoja na miji. Kwa hiyo, matokeo ya mvua hizi kubwa ambazo ni neema kwa upande mmoja, lakini upande mwingine zimeleta majanga makubwa ya miundombinu hii kuharibika. Kwa hiyo, niiombe Serikali ione namna gani bora ya kuiwezesha TARURA kuwa na bajeti ya kutosha ili kukabiliana na changamoto hizi nyingi ambazo zipo katika barabara zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Itigi pana mradi wa kilomita 10, unatekelezwa, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja pale nilimwomba taa kidogo kama 200 na kidogo na akatoa ahadi kwamba, zitatekelezwa, lakini hata Mheshimiwa Rais, alipokuja mwaka jana aliwaagiza watu wa TANROADS kufunga zile taa lakini mpaka saivi ni kimya. Naomba majibu ya Serikali lini wanaenda kufunga taa zilizoahidiwa na Mheshimiwa Rais alipokuja Itigi wakati anaweka jiwe la msingi la Barabara ya Mkiwa- Itigi na Noranga, kwa sababu, wananchi wanasubiri na kuona ahadi za viongozi wakubwa kama Mheshimiwa Rais, zinatekelezwa kwa haraka lakini kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto nyingine tunajenga Reli ya kiwango cha Standard Gauge, Itigi ni maeneo ambayo reli hii inapita, lakini inapita maeneo ambayo watu wamechukuliwa maeneo yao yakiwemo mashamba. Wengine wamechukuliwa maeneo ambayo walikuwa wanayatumia kwa maslahi mapana na kufanya maisha. Mimi ni mmoja wa watu waliochukuliwa shamba eneo langu ambalo nilikuwa nalitumia eti unalipwa hekari moja shilingi 200,000, hivi kweli hapa Tanzania kuna eneo linauzwa hekari shilingi 200,000? Jirani uliyepakana naye analipwa kwa square meter.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itende haki kwa wananchi wote bila kuangalia huyu ana rangi gani? Huyu ana ukubwa gani? Huyu yupo eneo gani? Huwezi kumlipa jirani yake kwa square meter na jirani mwingine ukamlipa kwa hekari, naomba Serikali itende haki. Mimi ni miongoni mwa wale ambaye sijachukua cheki yao kwa sababu, unalipwa eti hekari mbili square meter 8,000 unalipwa shilingi 500,000 kitu ambacho hakiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali sikivu ya Mheshimiwa Rais, wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye analipa hata watu waliokuwa wameifuata reli. Leo watu waliofuatwa na reli kwa hekari wanapunjwa. Naomba Serikali iache dhuluma hii ambayo inafanyika kwa watu wa Itigi, ni dhuluma kubwa wapo walioridhia. Basi wale ambao hawajaridhia haraka nao walipwe kulingana na wale wengine ili haki itendeke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wachaguliwa ndio huwa tunalaumiwa kwamba, hatutetei watu wetu, kwa sababu Serikali inapofanya makosa kama haya, inapodhulumu watu hekari shilingi 200,000, Itigi shamba hekari moja linauzwa zaidi ya milioni mbili lakini wao wanalipa shilingi 200,000. Naomba Serikali isikie na ilifanyie kazi jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niishauri Serikali yangu namna gani tunatumia pesa nyingi kununua mafuta ya petroli. Tunayo gesi yetu hapa tumeona Vituo vya Gesi Dar es Salaam. Matumizi ya CNG sasa yameshashika kasi, wakati tunasubiri mchakato wa LNG ambao unaonekana unakwenda mbele nyuma. Basi CNG ichukue nafasi ili haya magari madogo yanayotumia petroli yaweze kutumia gesi kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vilivyopo ni vichahce sana Serikali inashindwa nini kuongeza Vituo vya CNG Dar es Salaam? Serikali inashindwa nini kusogeza pipe ya CNG kufika Morogoro? Serikali inashindwa nini kusogeza pipe ya CNG kufika Dodoma? Serikali inashidwa nini kuifanya CNG ifike Mwanza? Ifike Arusha? Ifike Mbeya? Ili tupunguze manunuzi makubwa ya mafuta ya petroli ambayo yana gharimu pesa nyingi. Mafuta ya petroli kwa kiasi kikubwa hayaja-stabilize kila siku bei hazieleweki mara imepanda mara imeshuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna CNG hapa ambayo kiasi cha lita 10 za petroli manunuzi yake kwenye CNG unanunua zaidi ya lita 30, kilo 30 maana yake ni nafuu. Matumizi ya CNG ni mazuri zaidi pahali ambapo umetumia kilometa 10 za petroli kwenye CNG ungetumia kilometa 30, kwa kilo moja ya CNG. Kwa hiyo, maana yake nini? Naomba niishauri Serikali ione umuhimu hata kama ni kukopa pesa tuwekeze hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuepuke namna ya kutumia pesa nyingi kutoa mafuta kutoka huko Uarabuni. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Massare, kwa mchango mzuri.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)