Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya na kunipa kibali cha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya, Watanzania wanaona wana macho. Kwa hiyo, tunaomba tuendelee kumpa moyo sisi wanawake wa Tanzania tupo nyuma yake na tunaamini itakapofika 2025 ni nginjanginja mpaka Ikulu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya, pia, nimpongeze Naibu Waziri Mkuu naye kwa jitihada zake anazozifanya kwa kuungana na Waziri wake Mkuu, nimpongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama, sisi wengine ni mwalimu wetu, lakini niwapongeze na Mawaziri ambao wanafanya naye kazi katika Ofisi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia katika maeneo manne tu, nitachangia kwenye reli, nitachangia kwenye umeme na kwenye kilimo. Nianze kwenye reli; ninafahamu kabisa na naona juhudi zinazofanyika kuhakikisha reli ya kati inajengwa. Reli ya kati itakapokuwa imekamilika itakuwa ni mkombozi mkubwa kwa watu wa Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi, kwa sababu kwa muda mrefu sana tumekuwa tukipata shida katika usafiri wa reli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, reli hiyo itakapokamilika itakuwa ni mkombozi kwa wananchi na hasa kwa wananchi wa kipato cha chini. Wataweza kusafiri kwa gharama nafuu lakini pia wataweza kusafirisha mizigo yao kuitoa sehemu mbalimbali kuipeleka sokoni. Kwa hiyo, naomba juhudi za Serikali ziongezeke ili kumpata huyo Mshauri Msimamizi na Mkandarasi ili kazi hiyo iweze kukamilika mapema iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umeme vijijini; tunafahamu kazi kubwa inayofanywa na Serikali chini ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, kwa kweli anafanya kazi kubwa na sisi tunaona. Tuwaombe wakandarasi wale ambao wapo site kwenye mikoa yetu, wakandarasi wale wa REA waweze kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na kuweza kukamilisha miradi hiyo ili tunapofika mwaka kesho angalau miradi hiyo iweze kuwa imeleta tija. Tunaomba vijiji viweze kuunganishwa lakini pia umeme uweze kufika kwenye Vitongoji wananchi waweze kunufaika na umeme huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye kilimo; tunafahamu kwamba kilimo kimeajiri wananchi wengi sana na hapa nimpongeze Mheshimiwa Bashe kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha kinakuwa ni kilimo chenye tija. Kilimo ambacho kinawaajiri wanawake wengi, vijana wengi ambao mpaka sasa wanajitahidi kufanya kazi japokuwa bado miundombinu siyo rafiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwa mwaka huu angalau kile kilio cha mbolea kimepungua, ukienda madukani unaikuta mbolea. Kwa hiyo, angalau kile kilio cha mbolea sasa hivi kimepungua. Bado changamoto ipo kwenye mbegu tunaomba sasa Serikali iweze kuweka bei elekezi hata kwa mbegu nyingine tofauti na pamba, wakulima wa pamba na wakulima wa kahawa angalau wao wamepata ruzuku kwenye pamba na kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba sasa Serikali iweze kutoa bei elekezi kwa mbolea ili watu wanaolima alizeti, maharage na mahindi waweze nao kupatiwa mbegu kwa ruzuku. Wakipata mbegu bora wataweza kuzalisha mazao mengi sana na wataweza kukuza kipato chao, hatimaye, kuweza kuchangia pato la Taifa. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuliangalia eneo hilo la mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sukari; mwaka huu tumeona jinsi sukari ilivyoleta shida, lakini nampongeza Mheshimiwa Bashe alivyopambana kuhakikisha sukari inarejea kutoka kwenye kuuzwa kwa shilingi elfu kumi, shilingi elfu nane na kisha kurudi na kuwa shilingi 2,500. Kwa kweli, amefanya kazi kubwa sana, kupambana na walanguzi siyo kazi rahisi. Mheshimiwa Bashe nampa maua yake, amewasaidia wananchi na hasa ulipofika Mwezi wa Ramadhani tayari sukari ilikuwa imeshuka bei na kuwa shilingi 2,500. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ilete Sheria Bungeni ili kufanya mabadiliko kwenye upande wa sukari, itungwe Sheria ambayo itafanya wananchi wasirudie tena kupata shida. Sheria ikiletwa Bungeni ikafanyiwa mabadiliko, naamini hakutakuwa tena na kilio cha sukari pia sidhani kama walanguzi wataendelea kuficha sukari kama wanavyofanya siku zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma tunalima zao la muhogo, zao hili ndilo linalochangia kwa kiasi kikubwa wananchi wa wilaya zote za Mkoa wa Kigoma waweze kukuza kipato chao. Mwaka jana zao hili lilikuwa na bei nzuri sana, lakini mwaka huu zao la muhogo Mkoa wa Kigoma limeanguka sana, wananchi wamepata hasara. Tunaomba Serikali ije na bei elekezi ili wakulima wanapolima zao hili wawe na uhakika wa bei elekezi ambayo haitawapa hasara. Vilevile tunaomba kujengewa soko la muhogo ndani ya Mkoa wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)