Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia asubuhi hii, nina yangu machache ambayo ni ya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, natamani kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Mheshimiwa Judith Kapinga ambaye ni Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara hii ya Nishati kwa kufanikisha kupata umeme huu wa megawati 235, sisi kama Taifa kwetu ni faraja. Kumekuwa na stabilization ya umeme kwenye Taifa, zile kelele za umeme zimepungua, kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri. Kwa asilimia 96 ambayo bwawa limefika ni kwamba, zoezi la mgao wa umeme katika nchi hii litaisha kabisa ndani ya muda mfupi, kutakuwa hakuna mgao wa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia natumia nafasi hii kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia Chuo cha VETA pamoja na Chuo cha Watu Wenye Ulemavu katika Mkoa wa Songwe, ni faraja kwetu. Tunaomba wadau wote wa vyuo na vyuo vikuu waje kuwekeza katika Mkoa wetu wa Songwe kwani tunahitaji kuendelea kielimu. Kwa hiyo, natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara ambayo iliona kwamba, upo umuhimu wa kupeleka vyuo hivi katika Mkoa wa Songwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti ya mwaka jana ya Ofisi ya Waziri Mkuu niliuliza kuhusu suala la Sera ya Lishe, nikaambiwa ndani ya miezi sita tutapata matokeo ya kinachoendelea. Mpaka ninapoongea hivi sasa sijasikia, sijapata ufafanuzi na wala sijaona taarifa yoyote inayoonesha sera hiyo imefikia hatua gani, hata kwenye taarifa hii ambayo imetolewa na Waziri Mkuu haimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa kuwa kimya kwenye hii Taarifa ya Waziri Mkuu iliyotolewa hapa Bungeni inaonesha kwamba, katika suala la Sera ya Lishe hakuna kinachoendelea. Kwa hiyo, naomba kupitia Bunge hili, Waziri atakapokuwa ana-wind up aje na majibu ni kwa nini haijaonekana kwenye taarifa hii? Je, inafanyiwa kazi au haifanyiwi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, natamani kutumia nafasi hii pia kuongelea suala la kikokotoo. Tunapoongelea kikokotoo kumekuwa na kelele nyingi sana kwenye jamii, hususani kutoka kwa watumishi. Wengi wame-develop hofu ambayo inawafanya wanapoelekea kustaafu wahisi kama Serikali inawadhulumu. Mimi pia kabla sijapewa mafunzo nilikuwa kama hao wananchi, lakini kwa mafunzo ambayo nimepatiwa kuhusu kikokotoo nimewaza ni wapi, kama Taifa, tunashidwa kuwaelimisha wananchi hususani watumishi kwamba, kikokotoo hiki ni kizuri, kina tija na kinamweka mstaafu katika hali nzuri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokiona ni kwamba, Wizara haijawafikia watumishi na kuwaelimisha vizuri kuhusiana na kikokotoo kwa sababu, kwanza fedha ya mkupuo ambayo wanapewa ni ya kutosha. Sasa wanapewa asilimia 33 kutoka asilimia 25 waliyokuwa wanapewa awali, kwangu naona kuna ongezeko la asilimia nane ambayo huenda wananchi hawana ufahamu mzuri wa tofauti ya walichokuwa wanakipata awali na sasa imekaaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na nilivyoelekezwa, nilivyofundishwa, kwenye mafunzo maalum inaonesha kwamba, mwisho wa mwezi mtumishi huyu ambaye amestaafu anaendelea kupokea kipato ambacho ni karibu na mshahara wake aliokuwa anaupata awali. Kitu ambacho kinawasaidia wastaafu ambao walikuwa wanachoka sana baada ya kustaafu na wengi wanasema walikuwa wanakufa. Kwangu mimi naona kama hali ipo hivi kelele zinatoka wapi? Pia bado kuna fungu la mkupuo kwa familia endapo mstaafu huyu atafariki. Kwa hiyo, kwa hili natamani Wizara iende kutoa elimu hii kwa wananchi, kwa watumishi, ili wajiandae na kustaafu ilhali wakijua baada ya kustaafu watapata faida zipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ambayo ni NSSF na PSSSF bila kuusahau Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi. Kimsingi wanafanya kazi nzuri, wanajitahidi na wanapambana kuhakikisha wanalinda thamani ya fedha kwa kuanzisha miradi ambayo inaendelea kuipatia kipato Mifuko hii, lakini kuna changamoto ndogo ambayo Wizara haina budi kuifanyia kazi. Kwanza ni kuondokana au kuepuka miradi ambayo marejesho yake ya fedha yatachelewa zaidi ya miaka 10. Nasema hivi kwa sababu miradi mingine inayoibuliwa inachukua muda mrefu kurudisha gharama na kuanza kupata faida. Kwa hiyo, namwomba Waziri asaidie, ili miradi isichukue muda mrefu wa marejesho ya thamani ya fedha ambayo inakuwa imewekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu Kamishna wa Kazi na Mkurugenzi wa OSHA, watu hawa wanafanya kazi nzuri. Ombi langu kwa Waziri ni awasaidie kuongeza ofisi katika mikoa mingine. Tunatambua mahali pa kazi ni sehemu inayopaswa kuwa salama, kazi zipo katika mikoa yote, haiwezekani mkurugenzi akawa anateseka kutoka mkoa mmoja hadi mwingine kuhakikisha kazi inafanyika wakati Serikali ingeweza kutengeneza mazingira rahisi ya ufanyaji kazi. Vivyo hivyo Kamishna wa Kazi naye atengenezewe ofisi katika mikoa mingine na pia apewe vitendea kazi vya kutosha pamoja na watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja kuhusu kupeleka fedha kwenye maeneo ambayo Serikali inakuwa imedhamiria. Upo mfano hai, kuna fedha ambayo ilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule fulani katika Mji wetu wa Tunduma, shule ile ina madarasa 36 ambayo yapo na yanahitaji ukarabati. Madarasa 18 yapo yanatumika, lakini Serikali imepeleka fedha kwa ajili ya kujenga madarasa mengine 10 wakati kuna vyumba vingine 18 vya madarasa ambavyo havitumiki. Sasa nawaza na kujihoji kwamba, hivi Serikali inapopeleka fedha kwenye maeneo yetu, inakuwa imefanya tathmini ya kina ya mahitaji ya watu katika maeneo husika?
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hivi kwa sababu, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ziara zake amekuwa mkali sana juu ya matumizi mabaya ya fedha, hata kitendo cha kupeleka fedha ambazo ni kinyume na mahitaji ya eneo husika pia ni matumizi mabaya ya fedha. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie, wanaposambaza fedha kwenye maeneo yetu wazingatie vipaumbele, kama kipaumbele chetu ni ukarabati basi watupatie fedha za ukarabati, kama mahitaji ni madarasa basi watupatie fedha za madarasa, lakini jambo hili la kusambaza hela kienyeji siyo zuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunategemea usimamizi utaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia nataka niongelee kuhusu ukatili wa kijinsia. Kwanza natumia nafasi hii kuwapa pole wananchi na wakazi wa Mji wa Tunduma ambao kwa namna moja au nyingine wameathiriwa na vitendo vya ubakaji na ulawiti ambavyo watoto wao wamekuwa wakifanyiwa. Vitendo hivi vimekithiri sana, kiasi kwamba, sisi Wanatunduma, sisi Wanamomba, hatujisikii vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara, Sheria ya Ukatili wa Kijinsia, hususani juu ya ubakaji na ulawiti, ifanyiwe marekebisho ili hawa watu wakose dhamana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Neema, ahsante kwa mchango mzuri.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba watu hawa wasipate dhamana. (Makofi)