Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Khadija Shaaban Taya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata fursa ya kuzungumza, tena kwa ghafla, lakini umenipa fursa hii ya kuzungumza leo ili kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametukutanisha tena leo katika bajeti hii ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya, especially kwenye eneo la watu wenye ulemavu. Mheshimiwa Rais watu wenye ulemavu tunamshukuru sana, tupo pamoja na yeye, tunampenda sana na tunamtakia kila la heri katika majukumu yake yote ambayo anayafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitachangia katika maeneo kadhaa, lakini eneo ambalo ni muhimu sana kwangu kuchangia kila ninapopata fursa ya kuzungumza na naomba msinichoke, ni juu ya masuala ya watu wenye ulemavu. Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi sana kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kufungua vyuo na kutengeneza miundombinu mbalimbali katika maeneo mengi. Sasa hivi ukienda katika shule unakuta miundombinu ya watu wenye ulemavu ipo, ukienda kwenye vyuo tayari kuna vyuo vya watu wenye ulemavu, lakini pamoja na hayo yote naomba kutoa ushauri wa kuboresha katika baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya hivi vyuo ambavyo vinafunguliwa vinakosa vifaa vya kufundishia kwa mfano, kwa wale ambao wanapika keki na vitu kama hivyo. Jambo hili nimelipata nikaona nije kulizungumza ili Serikali iendelee kuweka mkazo katika eneo hilo. Pia, naomba kushauri katika hivi vyuo watu wajifunze namna ya kutengeneza fimbo pamoja na wheel chairs, ili waweze kujisaidia wenyewe kwa sababu, inaonekana kuna uhaba wa vifaa hivi saidizi kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi sasa unasikia kuna harambee kwa ajili ya kupata vifaa vya watu wenye ulemavu. Naamini Serikali ya Awamu ya Sita haijashindwa kutengeneza mkakati mzuri ambao unaweza kusaidia kupata vifaa hivi vya watu wenye ulemavu katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kushauri, kama tunapeleka wanafunzi katika hivi vyuo, basi tuwatengenezee mkakati mzuri ili kujua mwanafunzi akitoka pale anaenda kufanya nini? Akitoka pale atawezeshwa namna gani? Akitoka pale tupate matokeo, ni kiasi gani watu wenye ulemavu wameweza kunufaika na vyuo hivi ambavyo wamepelekwa. Issue siyo vyuo, lakini issue ni hawa watu waweze kunufaika au kujikwamua kiuchumi wao pamoja na familia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itengeneze mkakati mzuri ambao utawawezesha watu wenye ulemavu baada ya kutoka kwenye vyuo hivi. Juzi nimemwona Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika mitandao ya kijamii, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, akisema kuwa 10% imerudi. Kama hii 10% imerudi, basi Serikali ije ituambie kwa sababu, kwa watu wenye ulemavu hili ni eneo ambalo wanalitegemea sana kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi katika zile asilimia mbili ambazo zinatolewa na Serikali. Kwa hiyo, tunahitaji Serikali itusaidie kwenye eneo hili, ili watu wenye ulemavu waweze kujikwamua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2022 tumefanya sensa ya watu wote ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu. Matokeo yamekuja 11.2% ya watu wote Tanzania Bara wana ulemavu na Tanzania Visiwani watu wenye ulemavu ni 11.4%. Hii ni asilimia kubwa sana, natamani sana kuona Serikali inaweka mkakati kwa ajili ya kuwakwamua watu wenye ulemavu ikizingatia idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wanatoka katika familia maskini, nasisitiza wanatoka katika familia maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani kuona Serikali ina mkakati gani wa kuondoa shida za watu wenye ulemavu. Watu hawa wapate shida ya maumbile yao, wapate shida ya changamoto zao za kimwili ila wasipate shida za kiuchumi kama ambavyo nchi nyingine ambazo zinafanya vizuri zina mkakati mzuri wa kunyanyua watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, haiwezi kushindwa. Rais wetu anajali wanyonge, anajali watu maskini, anajali watu wenye ulemavu na ameonesha hilo kwa sababu, ameweza kuwaita watu wenye ulemavu Ikulu na kuzungumza nao, ameweza kutenga fedha kwa ajili ya mafuta, lakini pia ameweza kutenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuwezesha shughuli za watu wenye ulemavu katika Wizara ya Fedha. Mwaka jana tulipata hiyo bajeti na natumaini mwaka huu pia, tutaongezewa hiyo bajeti kwa sababu, shida za watu wenye ulemavu ni nyingi mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi kati niliangalia hizi takwimu na nilitamani sana kupata uelewa zaidi wa hizi takwimu especially kwa sisi watu wenye ulemavu, lakini ikipendeza Bunge zima lipate kujua hizi takwimu. Ni maeneo gani yenye watu wenye ulemavu na ni kiasi gani, au kuna aina gani ya watu wenye ulemavu na wingi wao katika maeneo yao tofauti tofauti kusudi Wabunge wanapokuja hapa kusaidia nchi yao na wananchi wao, watambue katika majimbo yao wana idadi kiasi gani ya watu wenye ulemavu na ni wa aina gani ili ifike mahali nipate kusikia hapa kila Mbunge akizungumzia masuala ya watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kusema masuala ya watu wenye ulemavu, pia naomba nichangie eneo la masuala ya dawa za kulevya kwa sababu hata watu wenye ulemavu wanaguswa na masuala ya madawa ya kulevya. Naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan. Imeweza kufanya kazi kubwa sana pamoja na Kamishna Mkuu wa Madawa ya Kulevya. Serikali tuendelee kumlinda yule baba ili aweze kufanya kazi nzuri ya kukomboa vijana wetu na watoto wetu kwa sababu Mama ameonesha nia ya dhati na thabiti ya kuhakikisha anasaidia vijana wake wasiingie au wasijihusishe sana na matumizi ya madawa ya kulevya au wasipate ule uwanja mpana sana wa matumizi ya madawa ya kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiasi kikubwa sana kimekamatwa mwaka jana Desemba, kiasi cha 3,182, kiasi kikubwa ambacho kwa historia hakijawahi kukamatwa au basi kama kimewahi kukamatwa, hatujawahi kutangaziwa kwamba kiasi kikubwa kama hiki kimeweza kukamatwa. Kwa hiyo, naomba niishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa sababu tunaona kabisa nia yake ya dhati ya kuhakikisha vijana, wanawake, watoto pamoja na watu wenye ulemavu wanajiepusha na matumizi ya dawa za kulevya ambazo zinaharibu akili zetu, utendaji kazi wetu na inaondoa nguvu kazi. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuzingatia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, naomba nichangie na kusisitiza pia kwenye eneo la vifaa saidizi pamoja na ofisi za watu wenye ulemavu. Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kongamano langu la uzinduzi wa NGO yangu alitoa kauli akisema, kila halmashauri itenge chumba maalum kwa ajili ya SHIVYAWATA, wapate ofisi ili watu wenye ulemavu wajue eneo la kufika la kueleza shida zao kwa urahisi na kila halmashauri ipate kujua shida za watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningetamani sana kujua hili suala limefikia wapi kwa sababu namna ninavyosikia, bado kuna maeneo ambayo hawajatekeleza neno hili. Labda sasa tutafute namna ya kutengeneza kama sheria ili kila halmashauri kuwe na ofisi ambazo hazitakuwa zinachangiwa kiasi chochote cha pesa na wenye ulemavu waweze kupata huduma kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia Serikali itengeneze mkakati mzuri wa kupata vifaa saidizi kama nilivyosema hapo awali. Ningetamani sana halmashauri ingetenga pesa ukiachana na hii asilimia mbili ambayo ni kwa ajili ya masuala ya uchumi, lakini nyingine kwa ajili ya kumwezesha mtu mwenye ulemavu. Sasa wheel chairs zimekuwa bei ghali, tunatamani sana kupata vifaa hivi kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Tupate mafuta kwenye halmashauri zetu ili wafikiwe kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo, naomba nikushukuru sana, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya. Tuendelee kumtia moyo, tuzingatie uwezo wake, tufahamu na tuendelee kumsemea Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu tunawiwa kufanya hivyo, kwa sababu tunawakilisha wananchi wale ambao wana shukurani kwa miradi ambayo imepelekwa kule chini, katika kila kata kuna miradi. Kwa hiyo, tumshukuru sana Mheshimiwa Rais na tuendelee kumsemea mazuri...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. KHADIJA S. TAYA: ... na mema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)