Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa hotuba nzuri kutoka katika ofisi yake. Pia niwapongeze Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mheshimiwa Jenista Mhagama; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi; pamoja na Manaibu wao Mheshimiwa Ummy Nderiananga na Mheshimiwa Patrobass Katambi kwa kazi kubwa wanazofanya kulijenga Taifa letu. Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake wanafanya kazi kubwa kwenye majukumu yao ya kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita kwenye tatizo la ulevi kwa vijana na mchezo wa kamari katika sehemu nyingi hapa nchini Tanzania na hususan Mkoani Kilimanjaro. Vijana ni nguzo ya Taifa katika nyanja za uchumi, michezo, maadili na uongozi na wakiachwa kujitumbukiza katika ulevi na utumiaji wa dawa za kulevya kama ilivyo sasa hivi tutalifanya Taifa letu kuangamia siku za mbeleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la ulevi kwa vijana na kuongezeka kwa mchezo wa kamari Mkoani Kilimanjaro katika maeneo ya vijijini limekuwa kubwa na linaua kabisa uwezo wa kundi hili kuchangia kuijenga nchi yetu kupitia nguvu kazi yao kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukosefu wa ajira rasmi Serikalini kwa vijana wetu, sehemu kubwa ya vijana wamejiingiza katika ulevi wa pombe kali zilizotapakaa mitaani na kuvuta bangi na kutumia dawa za kulevya za aina mbalimbali. Kudhihirisha tatizo hili, akiongea katika hafla ya kuzindua Mbio za Mwenge tarehe 2 Aprili, 2024 katika Viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa alisema: “Siku za hivi karibuni imeibuka aina mpya ya bangi inayotumiwa na vijana wetu yenye kiasi kikubwa cha kilevi inayofahamika kama 'cha Arusha' na 'Skanka'.” Alieleza kuwa aina hii ya bangi yenye sumu nyingi huchanganywa kwenye sigara na wanaoitumia hubadilika na kuwa kichaa na kupoteza mwelekeo kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko Mkoani Kilimanjaro, viongozi wa dini mbalimbali wamelalamikia tabia ya vijana wengi wa kiume vijijini kubugia pombe kali, dawa za kulevya na bangi kitu ambacho kimesababisha athari mbalimbali. Vilevile, vijana wengi hushiriki kwenye kucheza kamari. Matokeo ya kamari hizi ni kwamba hela zote huishia kwenye kamari. Mabonanza ya Wachina yako hadi huko vijijini, mabonanza haya yamefilisi vijana wetu huko vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla pombe kwa vijana wetu hawa ni sumu. Hatari zake hujumuisha vijana wetu kukosa nguvu za kiume na kushindwa kushiriki tendo la ndoa na kushindwa kuzaa watoto. Kasoro hii imelalamikiwa na viongozi wa dini na wale wa Serikali kwenye Mkoa wetu wa Kilimanjaro katika maeneo ya Rombo, Vunjo na Moshi Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, athari nyingine kubwa za pombe, dawa za kulevya na bangi ni ajali mbaya zinazosababishwa na ulevi, magonjwa ya ini, UKIMWI na aina nyingine nyingi za saratani. Pombe, bangi na dawa za kulevya husababisha umaskini na vinapelekea vifo vya haraka kwani vijana waathirika, kuwa maskini na huishi katika mazingira magumu na mara nyingi hushindwa kumudu matibabu. Vilevile, vilevi huwa ni chanzo cha magomvi yasiyo na msingi, ajali za uzembe, kujeruhiwa na kuuawa na vibaka na msongo wa mawazo. Tabia hii ya vijana wetu kujiingiza katika vilevi ni ya kusikitisha kwani nchi isipokabiliana nalo kwa nguvu zote, sote tutaathirika kwa namna mbalimbali ikiwemo usalama wa Taifa na familia zetu na mali tulizonazo huku nyumbani na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hii, zinahitajika jitihada za pamoja kati ya wazazi, viongozi wa mila, jamii, vitongoji, vijiji, kata, wilaya mkoa na madhehebu ya dini na Serikali kwa ujumla katika kulishughulikia na kulimaliza tatizo hili la ulevi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la wazazi kuhakikisha kwamba katika umri wa kijana kuna mambo ya msingi yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini na kwa ungalifu mkubwa. Vijana wafundishwe na kutayarishwa namna ya kuishi katika jamii, namna ya kupambana na umaskini kwa kufanya kazi na mfano mzuri wa malezi ya vijana uko kwenye jamii ya Kimasai. Mpaka sasa vijana wa kabila hili ni mfano wa kuigwa kwani wamedumisha mila zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla tatizo la ulevi kwa vijana wetu vijijini (Mkoani Kilimanjaro na maeneo mengine nchini) ni kubwa sana na jambo hili ni letu sote. Ni vyema tukaweka nguvu pamoja ili kuitokomeza shida hii na kunusuru maisha yao kwani linatishia nguvu kazi ya Taifa letu ambayo inatokana na kundi la vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kupitia Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, iwasaidie vijana wa Kitanzania wawe na programu za kuweka vipaumbele katika mambo makuu matatu katika maisha yao ya kila siku ambayo ni utaifa, uchumi na kushiriki katika fani mbalimbali za kujipatia kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie mchango wangu kwa kusema kwamba Tanzania yetu ya leo na kesho inawategemea sana vijana. Hivyo basi ni vyema nchi yetu ikawekeza nguvu kubwa katika malezi ya vijana kwa kuhakikisha kuwa wanaachana kabisa na ulevi wa aina yoyote ile kwa sababu vijana ni tunu, hazina na thamani katika Taifa letu. Ni vyema jambo hili likasaidiwa na michakato ya kisheria katika ngazi za vijiji, kata, wilaya na Taifa. Uwepo wa sheria kali katika maeneo hayo kutasaidia sana kukabiliana na ulevi uliokithiri kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.