Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwapongeza nyote, Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri Mkuu mwenyewe, Mawaziri wote wanaomsaidia Mama Jenista Mhagama, Kaka Ndejembi, Dada Ummy na Kaka Katambi pamoja na wataalam wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni pamoja na Makatibu Wakuu wote wawili, Wakurugenzi, Maafisa na watumishi wote; ikiwa ni pamoja na Private Office ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Baada ya pongezi, naomba kutoa maoni na ushauri kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na kazi na ajira, ushauri wangu hususani kuhusu kukuza na kulinda ajira chache hasa katika sekta binafsi, nashauri taratibu za vibali vya kazi ziweze kuzingatiwa. Kwa ilivyo sasa kuna wimbi kubwa la raia kutoka China ambao wamegeuka wachuuzi, siyo Kariakoo tu, bali hata katika miji midogo kama Mafinga, Makambako na kadhalika. Suala hili tusipokuwa makini iko siku litazua tafrani kati ya jamii ya Wachina na Watanzania wazawa japo ni neno lisilopendwa kusikika, kuna kitu kitatokea siyo tu katika nyanja ya uchumi lakini hata kijamii na kidplomasia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa kunajengeka chuki siyo dhidi ya jamii ya Wachina bali wananchi dhidi ya Serikali, wanasema kuwa Serikali kwa nini inaachia Wachina kushindana na Watanzania kwenye ajira za chini ambazo kimsingi zinapaswa kufanywa na wazawa. Ushauri wangu, tukiliacha jambo hili bila kulidhibiti iko siku litaleta mgongano ambao utatuingiza katika shida ya kimahusiano ya kidplomasia na marafiki zetu wa muda mrefu China.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu BBT; programu hii ambayo inasimamiwa na Wizara ya Kilimo inaweza kuwa msaada mkubwa katika kuongeza ajira kwa vijana. Napongeza hatua zote za awali ambazo zimeanza kuchukuliwa, ushauri wangu, washirikiane na Kilimo na JKT katika kuhakikisha kuwa vijana wanaojitolea JKT wanakuwa sehemu ya wanufaika wa BBT. Naamini watakuwa na mchango mkubwa sana si kwao binafsi tu, lakini na kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuimarisha Idara ya Tathmini na Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali; kwanza napongeza uamuzi wa Serikali katika kuanzishwa kwa Idara hii muhimu ambayo itasaidia sana hata katika kupunguza hoja za CAG, lakini zaidi katika kuimarisha utendaji Serikalini hususani katika kukamilika miradi kwa wakati. Hata hivyo ili kuwa na matokeo chanya na kutimia kwa malengo ya kuanzishwa kwa Idara hii muhimu, rasilimali fedha na rasilimali watu ni muhimu sana. Katika kipindi kifupi toka kuanzishwa kwa Idara hii imethibitika kuongezeka kwa umakini wa kiutendaji ndani ya Serikali kwa sababu Idara imekuwa kama watch dog ndani ya Mawizara na Taasisi zetu za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na manufaa haya na kwa faida ya kuokoa gharama kama vile miradi kuchelewa kukamilika ambapo mara kadhaa Serikali imelazimika kuongeza fedha kwa miradi ambayo ilichelewa kukamilika kutokana na kushindwa kufuatilia utendaji wakati miradi inaendelea. Kwa hiyo kuimarisha Idara hii ni sawa na ile tunasema prevention is better than cure kwa maana kwamba kupitia Idara ya Tathmini na Ufuatiliaji tunaweza kuzuia kabla madhara makubwa hayajatokea, ushauri wangu Idara hii itazamwe kwa macho mawili kwa maana ya financing na human resources.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu EPC+F; Serikali ilisaini mikataba kadhaa na wakandarasi wa kujenga barabara kwa kiwango cha lami kwa Mfumo wa EPC+F. Mikataba hii ilisainiwa Juni, 2023 na ni zaidi ya kilometa 2,000, mpaka sasa bado hatujaanza hata kilometa moja. Tatizo tunaambiwa wakandarasi wanaomba kulipwa angalau advance payment ya 10%.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu Serikali ifanye kila linalowezekana ili walau wakandarasi walipwe hii 10% kwa kuwa pamoja na sababu za kiuchumi suala hili kisiasa linaweza kuwa na shida kutokana na ukweli kwamba kama Serikali tulilitangaza sana na kuwapa matumaini wananchi, hivyo kutokuanza kwa miradi italeta ugumu katika chaguzi zijazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.