Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kutupa nafasi ya kuchangia. Pia, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu, wamechangia sana kwenye Eneo la Wizara ya Afya. Wamechangia Waheshimiwa Wabunge nane na sasa hivi amechangia pia dada yangu Keisha amekuwa wa tisa na mambo mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasema kwa asilimia kubwa ni masuala ya sisi kwenda kuyafanyia kazi na wala hayatakuwa na sababu ya sisi kupitia moja baada ya lingine. Tutakwenda kuyafanyia kazi na ninyi mtaona matokeo kule ambako mnafanya shughuli zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme machache. Moja ambalo dada yangu Keisha amelizungumzia sasa hivi lakini pia lile alilozungumzia Mheshimiwa Ester Bulaya, la waraibu kwa maana wenzetu ambao wanatumia madawa ya kulevya. Kwanza niwaambie Waheshimiwa Wabunge, kwa mwaka jana hospitali zetu zote nchini zimetibu waraibu 61,605 na wote wamekuwa wakipata huduma. Kwa kweli tuishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikitusaidia na ikitupa maelekezo, lakini tumshukuru Kaka yetu Kamishna Lyimo, anafanya kazi kubwa sana kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie tu kwenye eneo la waraibu kwa Muhimbili hili niseme tu ni kazi kubwa ya Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo anaifanya na kuboresha kila kitu na ametoa maelekezo. Kwenye eneo la Muhimbili pekee yake kwenye database wako waraibu 5,000 na katika hao waraibu, Hospitali yetu ya Muhimbili haijaishia kwenye kuwatibu tu, wale ambao wamekuwa cleared, wanaajiriwa pale Muhimbili. Kwa hiyo, unakuta sasa hivi tunao zaidi ya 50 ambao wameajiriwa pale wanafanya shughuli mbalimbali za kusukuma wagonjwa, wengine wanafagia na wanalipwa mshahara wakiwa pale. Kwa sababu hao wengine wanaweza wakapona lakini wanapopona wakirudi mtaani wanapokuta maisha ni magumu wanaendelea kuwa waraibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunataka kuanzisha to roll out kwenye hospitali zetu zote, kwamba kila mahali tutengeneze incentive ambayo wale ambao wamekuwa cleared na hawatumii tena madawa ya kulevya wanatengenezewa shughuli za kufanya ndani ya hospitali zetu. Nafiriki kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali tunaweza tukafanya vizuri zaidi. Kwa mfano, kaka yangu Mheshimiwa Bashe hapa ameanzisha BBT, wale wafanyakazi waliokuwa cleared kwenye eneo la vibarua wakaingia pale (BBT) na wakafanya kazi, tunaweza tukafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Muhimbili tunaona zaidi ya 1,000 kwa siku, lakini Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu ametoa maelekezo na tayari ametutafutia wadau pamoja na mbia, ametupa eka 160 kule Vingunguti. Sasa pale kinajengwa kiwanda ambacho kitatengeneza vifaa tiba lakini kita-assemble hizi bajaji. Mle tunategemea waraibu 500 waweze kuwa absolved na kufanya kazi hiyo ndani ya hilo eneo na donor tayari, visibility imeshamalizika sasa ni ujenzi unaanza. Kwa hiyo itakuwa kazi vifaa vya hospitali vinazalishwa, kiwanda kinaendelea, vifaa tiba vinazalishwa lakini hawa wenzetu ambao tunawatibu pale Muhimbili na wanakuwa absolved pale kwa kushirikiana na kaka yangu Lyimo, tuone namna ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wametoa michango mizuri sana sisi tunakwenda kutekeleza lakini niwaombe Waheshimiwa Wabunge, Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi kubwa sana kwenye eneo letu la afya na kwenye majimbo ya Wabunge yamefanyika mambo makubwa sana. Imefanyika revolution kubwa sana ya teknolojia kule kwenye majimbo yao. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge wasisahaulishwe wakati huu na matatizo madogo madogo yaliyoko huko wilayani wakaacha ku-focus kwenye makubwa ambayo tayari yamefanyika na Mheshimiwa Rais wetu amefanya na tukaacha kuwafanya watu wa-focus kwenye yale mambo makubwa, tukaanza ku-focus kwenye madogo madogo yanayoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwa teknolojia aliyoipeleka Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kule chini kwenye wilaya zao, zahanati na kwenye mikoa yao, leo utaona kwamba tulikuwa tukitembea na Kamati zetu kwenye mikoa yetu; tuki-compare na Kamati za Wabunge kwenye mikoa yetu, tukienda Ocean Road tunakuta asilimia zaidi ya 90 mpaka 100 ni wagonjwa wa kansa, wako terminal stage, ni wale wanaongojea kufa. Kwa sababu ya hizo teknolojia wamekuwa wanagunduliwa mapema na wakienda mapema hospitali na wengi wamekuwa wanapona kwa sababu ya teknolojia ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kule kwenye majimbo yetu kila mwaka walikuwa wanakufa akinamama 556. Leo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza vile vituo vimeshuka kwenu, teknolojia imeshuka kwenu na mafunzo yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alisimama hapa akasisitiza kwenye eneo la afya ya mama na mtoto. Leo tunapozungumzia WHO walitegemea mwaka 2025 yaani mwakani walitegemea nchi hii tushushe vifo vya akinamama na watoto mpaka 250, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kushusha teknolojia kwenye vituo na kupeleka huduma karibu na wananchi leo idadi ya vifo vya akinamama imeshuka mpaka imefika 104. WHO sasa hivi wanajiuliza ni nini Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anachofanya. Maana yake ni nini? Naendelea kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba, tusisahaulishwe ni nini kimefanyika kipindi chetu tukiwa Wabunge na ni nini Mheshimiwa Rais wetu amefanya kwenye majimbo yetu na ni nini Rais wetu amefanya kwenye nchi yetu yanapotokea matatizo madogo madogo kama haya mengine yanayotokana na mafuriko na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mheshimiwa Rais wetu amefanya mapinduzi makubwa sana kwenye teknolojia na tiba. Asilimia 97 ya tiba tulizokuwa tunafuata nje na asilimia 97 ya teknolojia tulizokuwa tunafuata India, Ulaya na Marekani, leo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, amenunua tiba hiyo iko Tanzania na tunatibiwa hapa hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wanakumbuka tulipokutana naye wakati wa UVIKO pale kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete, alisema kwa nguvu kabisa; “Nunueni vifaa na teknolojia za kisasa kabisa duniani lakini nunueni vifaa kwenye reputable institute ambazo tunaweza tukawa na future na hivyo vifaa.” Akatuelekeza moja kwa moja, leo nataka kuwaambia tunaanza na Muhimbili. Vifaa vyote na maabara zetu zile za kupima mambo mengi na vile vifaa ambavyo Mheshimiwa Rais wetu ametununulia vina uwezo wa kutumia artificial intelligence. Tunaenda kuanza na Muhimbili, tutaweka software. Kwa hiyo ukifika Muhimbili ukiingia pale anatumika binadamu lakini pia artificial intelligence na ubora wa kuweza kuona magonjwa utaongezeka. Huyo ndiyo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya revolution kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipokwenda Marekani, alikutana na Chuo Kikuu cha South Carolina...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri...

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia hili moja tu la mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu alikwenda Marekani akakutana na Chuo Kikuu cha South Carolina, imefanya revolution kubwa sana. Kesho kutwa tunaanza Muhimbili wagonjwa wote wa sukari hawatatobolewa tobolewa tena. Inakuja teknolojia kwa kushirikiana na South Carolina na sasa wataanza tu kupimwa kwa kuchukua mate, wanaangalia sukari bila kuhitaji kujitoboa kila siku. Tukishafanya hiyo test tunaanza sasa ku-roll out na wagonjwa wote wa sukari watakuwa wanatumia teknolojia ya kisasa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango yao, tutaendelea kufanya kazi, lakini naendelea kuwasisitiza, watu wameamka kule majimboni kwetu na watu wameamka huku Taifani wasitusahaulishwe mambo ya msingi ambayo Mheshimiwa Rais wetu amefanya. Wasitusahaulishe mambo ya msingi ambayo tumefanya kwenye majimbo. Tujikite kwenye makubwa ambayo yametokea kwenye majimbo. (Makofi)