Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa jinsi ambavyo wamechangia kwenye eneo la Sekta ya Maliasili na Utalii kupitia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nawashukuru kwa sababu michango hii imezidi kuboresha yale ambayo tunakusudia kuyafanya katika Wizara yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kama wanavyofahamu, tumejitahidi sana katika kipindi hiki kuwa karibu nao, kufungua milango kwa kila mmoja wao ili tuweze kusikia kutoka kwao nini changamoto wanazokabiliana nazo kwenye Majimbo yao ili nasi tuweze kukidhi mahitaji na matarajio yao. Niwaahidi tutaendelea kuwa karibu nao na kuwasikiliza ili kuweza kutatua changamoto zinazotukabili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda hoja zilizoibuliwa ni nyingi, lakini nitajibu chache kwa ujumla na kwa sababu tunaelekea kwenye hotuba ya bajeti yetu huko mbele ya safari, basi majibu mengi tutayapata kule, vilevile tutaandaa majibu ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie hoja chache ambazo zimejitokeza. Eneo la kwanza ni jambo kubwa linalofanywa na Serikali yetu la kufanya uhamishaji wa wananchi kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda kwenye maeneo mengine ya nchi yetu. Jambo hili ni muhimu kwetu sote, ni jambo ambalo linakwenda kuboresha au kuimarisha utu wa Mtanzania, kwa hiyo sisi sote kama viongozi tuna wajibu wa kuliunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa sababu jambo hili linafanyika kwa umakini mkubwa na amekuwa karibu sana kutoa miongozo na maelekezo ya jinsi ya kuliendea jambo hili. Kazi kubwa imefanyika kwa wale ndugu zetu ambao wamehamishwa kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda Msomera na maeneo mengine, uhamasishaji mkubwa sana unafanyika wa kuwaonesha ndugu zetu faida ya wao kukubali kuondoka kwa hiari kwenye eneo hili na kwenda kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Msomera wote tunafahamu kazi kubwa imefanyika ya kujenga makazi ya wananchi, ya kujenga nyumba, ya kuwapatia wananchi wanaokubali kuhama ardhi ekari tano kwa kila kaya, lakini vilevile wamekuwa wakipewe fedha takribani shilingi 10,000,000 kwa ajili ya maendelezo waliyoyafanya kwenye maeneo wanapoondoka. Nafurahi kusema kwamba mwitikio wa wananchi kuhamia Msomera ni mkubwa na sisi ndani ya Serikali tunapata faraja kwamba jambo hili litakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwepo hofu kwamba pengine wapo watu hawatakubali kuhama. Sisi tunaolisimamia jambo hili faraja tunayoipata ni kwamba kuna mwitikio mkubwa, kwa hiyo hakuna sababu ya kuwa na hofu kwamba watu hawatahama. Wananchi wanaelezwa, wanaelewa na mwitikio ni mkubwa. Niwaombe viongozi wenzangu tujitahidi kuhakikisha kwamba tusiwe na tamaa ya kuvuka mto kabla hatujafikia daraja, tusubiri tufikie daraja, tutajua namna gani tunavuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hoja zilizojaribu kuonesha kwamba wananchi waliopo kule wamesahaulika, hawapati huduma za kijamii, jambo hili siyo kweli. Zipo hoja zimejaribu kujengwa hapa kwamba kuna baadhi ya shule hata vyoo havijengwi, nataka niseme nini kinachotokea. Serikali kwa umuhimu wa eneo lile ilipata ushauri wa kitaalam kwamba pengine siyo busara kuendelea kujenga vyoo kwenye maeneo yale. Kwa hiyo, nini ambacho Serikali imefanya? Serikali tulichofanya ni kuja na utaratibu mahsusi wa kuhakikisha vyoo vyote vinavyotumika sasa kuwe na utaratibu wa kuvinyonya ule uchafu uliopo ili uende ukahifadhiwe kwenye shimo moja pekee yake ili vyoo vile viweze kuendelea kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza zoezi hili limefanyika katika Shule ya Msingi ya Endulen limekamilika kwa 80%. Tunaendelea na zoezi hili kwenye shule za msingi, tunaendelea na zoezi hili kwenye vituo vya afya, tunaendelea na zoezi hili na kwenye zahanati zetu. Niwasihi sana Waheshimiwa kama kuna jambo halieleweki milango yetu ipo wazi, waje tutapeana maelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo limejaribu kuoneshwa hapa kwamba hata lile jambo la kutoa misaada ya kielimu kwa wanafunzi wanaotoka kwenye eneo hili, ambao wanatoka kwenye kaya ambazo hazina uwezo sasa limesitishwa. Jambo hili nalo siyo kweli. Tangu tumeanzisha utaratibu huu, Serikali imekwishalipia ada wanafunzi takribani 14,000. Hivi ninavyozungumza kwa mwaka huu wa fedha mpaka kufikia mwezi Machi, tayari Serikali imelipa zaidi ya shilingi 925,051,120. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nini kinachoendelea sasa? Kinachoendelea sasa ni kwamba utaratibu wa kuwalipia wanafunzi hao unasimamiwa na Baraza la Wafugaji wenyewe...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, ahsante, mengine utatoa taarifa ya maandishi.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)