Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Kwa upekee kabisa niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa namna ambavyo wamegusia katika Sekta yetu ya Maji, nasimama hapa nikiwa naelewa kabisa kwamba Sekta ya Maji, inagusa nyenzo muhimu sana katika uhai wa binadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia ni zaidi ya sita, lakini wote kwa umoja wao wameonyesha namna ambavyo wanataka kuharakisha miradi ya maji na kuboresha namna ambavyo Wakandarasi wetu wanafanya. Miradi ya maji inayoendelea nchini iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, lakini vilevile ipo katika hatua ambazo zinaenda kuleta huduma ya maji kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba miradi hii itakamilika kabla ya muda, kwa sababu wiki iliyopita Serikali imetoa fedha bilioni 60 kwa ajili ya kuanza kulipa Wakandarasi ambao wanatekeleza miradi ya maji vijijini. Leo asubuhi nimejulishwa na Katibu Mkuu, Mfuko wetu wa Maji pia tumeweza kupata bilioni 18. Kwa hiyo, kwa ujumla tuna bilioni 78 kwa ajili ya kuhakikisha miradi yetu ya maji huko vijijini inaendelea kutekelezwa na ili iweze kukamilika kwa wakati. Hizi ni dalili tosha kabisa za kuonesha kwamba tunaye Rais, ambaye anajali Watanzania, tuna Rais ambaye amejikita katika utoaji wa huduma za msingi kabisa kwa Watanzania, hivyo tuendelee kumuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika yale ambayo yameongelewa na Waheshimiwa Wabunge, naomba nigusie jambo ambalo ameongea Mheshimiwa Issa, Mbunge wa Kibamba kuhusu bwawa la Kidunda. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Mheshimiwa Rais, ametoa fedha takribani bilioni 49 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba bwawa hili ambalo ndilo linaenda kutoa uhakika wa maji katika Mto Ruvu ambao ndiyo chanzo cha maji yanayopatikana katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa hili limefikia katika 20% ya utekelezaji wake na litakapokamilika litaweza kutoa lita bilioni 190 ambapo zitakuwa zina uwezo wa kuhudumia mikoa ya jirani pamoja na Dar es Salaam. Vilevile katika ujenzi wa bwawa hili, kuna ujenzi wa kituo cha kufua umeme ambapo takribani Megawatt 20 zitazalishwa pale. Pia kuna njia kuu ya msongo mkubwa wa umeme kutoka Kidunda mpaka Chalinze takribani kilometa 101. Maana yake ni kwamba tunaenda kuwa na uhakika wa huduma mbalimbali unaotokana na bwawa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuongelea Bwawa la Farkwa. Mheshimiwa Kunti amejaribu kuligusia katika kuchangia kwake na ameonyesha hofu yake, lakini nimhakikishie kwamba Serikali iliingia makubaliano na Benki ya Maendeleo ya Afrika na takribani dola za Kimarekani 125 zilitolewa. Tunafahamu kabisa kwamba bwawa hili limekuwa na changamoto kidogo kwa sababu ya kubadilika kwa mahitaji ya maji na kubadilika kwa wingi wa watu katika Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumepata mtaalamu mshauri ili aweze kupitia ule usanifu wa bwawa na kuhakikisha kwamba anapitia mpango wa kulinda na kutunza mazingira ambayo ndiyo chanzo cha maji kitakachokuwa kinapeleka katika lile bwawa. Kwa hiyo, tunaamini kwamba akishapitia huu usanifu, maana tumempatia muda mpaka mwezi wa Tisa awe amekamilisha ili ujenzi wa bwawa hili uanze mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Waheshimiwa Wabunge tunafahamu kwamba miradi ya maji ni miradi muhimu sana. Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kama ambavyo imepangwa na hili bwawa pamoja na mabwawa mengine, kwa sababu mabwawa yapo mengi ambayo yanaendelea katika hatua mbalimbali. Tuna uhakika kwamba kwa sababu tunaenda kwenye bajeti ijayo, Waheshimiwa Wabunge watatuunga mkono ili tuweze kuhakikisha kwamba miradi hii tunaisimamia ili iweze kukamilika na iweze kutoa huduma ya maji kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba changamoto ya maji katika Jiji la Dodoma inaendelea kuwepo, lakini tuna miradi 15 inayoendelea katika Jiji la Dodoma. Vilevile tuna miradi 78 ambayo inaendelea katika Mkoa wa Dodoma ambapo miradi hiyo ina takribani shilingi bilioni 54 na watu takribani 400,900 wanaenda kunufaika na huduma hii ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba changamoto ya Dodoma hatuwezi kuitatua kwa mpango wa muda mrefu peke yake. Serikali imejipanga katika mpango wa muda mfupi, muda wa kati na vilevile muda mrefu. Mpango wa muda wa kati kwa Jiji la Dodoma, tayari tuna miradi midogo midogo 15 ambayo inaendelea kujengwa katika maeneo ya Nzuguni, Nala na maeneo mengine ili kuhakikisha angalau wananchi wanaokuja katika Jiji la Dodoma na wananchi wanaoishi katika Jiji la Dodoma hawapati changamoto yoyote ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo tunaomba muwe na subira, pale ambapo kutakuwa na changamoto, tunaamini kwamba kila changamoto tutaichukua kwa uzito wake kwa sababu tunaamini kutatua changamoto na kuhakikisha huduma zinazidi kuimarishwa na kuboreshwa, ndiyo mafanikio ya Taifa letu na ndiyo mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, na Waheshimiwa Wabunge, niwahakikishie kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Maji ameendelea kufungua kapu lake na ameendelea kuonesha kwamba kumtua ndoo mama kichwani...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, muda wako umekwisha.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo kipaumbele katika kuhakikisha kwamba...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, mengine yajibu kwa maandishi.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.

NAIBU SPIKA: Yaliyobakia jibu kwa maandishi.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)