Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri na ninaunga mkono hoja. Moja kati ya hoja ambazo zilizungumzwa wakati wa kuchangia bajeti hii ni hoja ya mradi wa Nyanzaga pale Sengerema ambapo Mheshimiwa Mbunge alichukua fursa hii kutamka mbele ya Bunge hili kutaka Serikali itoe ufafanuzi wa hali ilipofikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Tabasam kwani amekuwa ni sehemu muhimu katika mradi huu ambao utawanufaisha wananchi wa Sengerema na Tanzania kwa ujumla. Mradi wa Nyanzaga upo chini ya Kampuni ya Ubia ya Sotta Minning ambapo Kampuni ya Ore Corp ina 84% na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina 16%.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo katikati ilijitokeza kampuni ambayo ilikuwa inaitwa Silver Corp ambayo walionesha nia ya kununua hisa za Ore Corp na hatua hii ilisababisha kufungua scheme of arrangement katika nchi ya Australia kwa mujibu wa Sheria za makampuni ya Australia katika kuzipata hizo hisa za Ore Corp. Katikati ya mchakato ilitokea kampuni nyingine ya Perseus ambao wao walikuja na superior offer na wakanunua hisa za kampuni ya Ore Corp ambayo mchakato wote huo hauathiri hata kidogo ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Ore Corp katika Kampuni ya Sotta Minning.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niwatoe hofu Watanzania kwamba baada ya kukamilika mchakato wote huo wa Ore Corp, Silver Corp na Perseus, hivi sasa kampuni ya Persus wao ndiyo wamekuwa na offer kubwa nao ndio watanunua hisa za Ore Corp na itakuwa sasa ni Serikali 16% kama ilivyokuwa awali na Ore Corp 84%.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hivi sasa, tayari wale ambao wameshinda offer Kampuni ya Perseus wanaingia nchini tarehe 18 na tarehe 19 nitakutana nao hapa Dodoma kwa ajili ya mazungumzo. Nchi itanufaika kama ifuatavyo na ndiyo ilikuwa hoja ya Mheshimiwa Tabasamu: Kwanza, kabla ya mchakato wote huu sisi kama Wizara ya Madini tuliwaandikia TRA kuufuatilia mchakato huu na nchi itapata capital gain tax baada ya mchakato huu kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa sababu Sheria inataka kampuni yoyote ya Australia ambayo inafanya acquisition ya shares lazima ipate approval ya taasisi muhimu ya nchi husika na hapa ilikuwa ni FCC, kwa mujibu wa Sheria ya Madini, kifungu Na. 10 kinasema, “Serikali itakuwa ina hisa zisizopungua 16% ambazo hazififishwi;” baada ya kampuni ile Perseus kuja hapa nchini tulikaa nao na kuzungumza nao. Katika majadiliano Serikali inatoka katika umiliki wa hisa 16% mpaka 20%, yaani tumeongeza hisa nne. Haya ni manufaa makubwa sana katika uchumi wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho katika hoja hii ya Mheshimiwa Tabasam ilikuwa, ni lini mradi unaanza? Kwa mujibu wa timeline, nusu ya pili ya mwaka 2025 Kampuni ya Perseus wanapaswa waanze kutoa dhahabu ya kwanza katika mgodi pale Sengerema. Kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Mbunge mahususi kwamba jambo hili linakwenda kufanyika na litafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ambayo ilizungumzwa hapa ndani, ni kuhusu utafiti wa Helium ambao unaendelea katika Bonde Rukwa. Ni kweli katika Bonde Rukwa tuna utafiti wa kampuni kubwa mbili ya Helium One na Noble Helium. Wamefanya utafiti katika eneo hili na imepatikana Helium nyingi na ya kutosha sana na Helium hii inakwenda kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kati ya nchi chache ambazo zitakuwa zina uwezo wa kuzalisha Helium ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwaondoa Marekani na Urusi, Tanzania sisi, tunafuatia kwa kuwa na kiwango kikubwa cha Helium. Kwa hiyo, ni jambo ambalo kama Serikali tumelichukulia kwa uzito mkubwa na kama inavyofahamika kwamba katika Helium hii ni mahususi sana kwa ajili ya vifaa vya kielektroniki na MRI, kwa hiyo, nchi itakuwa imepata faida kubwa kutokana na jambo hili ambalo linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mwisho ni kuhusu maeneo kwa wachimbaji wadogo. Nataka niwaondolee wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa na changamoto ya watu wengi hasa wawekezaji wakubwa kushikilia maeneo makubwa pasipo kuyafanyia kazi. Wiki tatu zilizopita nimefuta maombi na leseni 2,648 kwa ajili ya kuyafanya maeneo haya yabaki wazi na tutayapanga vizuri na tutawapatia wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuja na program kama ile ya kilimo ya BBT, lakini ya kwetu ni MBT (Mining for a Brighter Tomorrow) ambapo tutawapanga vizuri akina mama na vijana na maeneo haya watayafanyia kazi na mwisho wa siku nchi yetu itanufaika na program hizi. Sambamba na hilo, pia tumejipanga kukamilisha ule utafiti wa kina kabisa kwa maana ya High Resolution Airborne Geophysical Survey ili tuweze kufahamu ni kiasi gani cha madini tulichonacho chini ya ardhi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi cha bajeti yangu nitasema hatua ambayo tumeifikia, ni hatua ambayo inapendezesha sana. Ni hatua nzuri, kwani tunakwenda kuikomboa nchi yetu katika rasilimali ya madini na Watanzania hawatachimba tena kwa kubahatisha, tutawaongoza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)