Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Jambo la pili, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa Hotuba yake nzuri. Vilevile niseme naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge zaidi ya 21 wamechangia na kutoa maoni mbalimbali. Yale ya ushauri tumeyapokea na tutaendelea kuyafanyia kazi na mengine tutayajibu tutakapokuja kwenye Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya eneo ambalo wameliongelea Waheshimiwa Wabunge ni matumizi ya rasilimali za maji katika Bonde la Mto Rufiji. Nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu, upembuzi yakinifu wa hekta 67,000 wa Bonde la Mto Rufiji umekamilika na tarehe 20 mwezi huu tunatangaza tender ya kwanza ya ujenzi wa mabwawa makubwa mawili ambayo yatakuwa na uwezo wa kukusanya maji cubic meter 269,000,000 na ujenzi wa hekta 17,000 zinatangazwa tarehe 20 mwezi huu na mabwawa mengine yatafuatia katika mwaka ujao wa fedha kadri ambavyo bajeti itakuwa inaturuhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Kilombero Valley tayari mkandarasi ameshapatikana. Kwa hiyo, kazi inayofanyika katika eneo la Kilombero ni ukamilishaji wa upembuzi yakinifu kwa ajili ya flood control na ujenzi wa mabwawa chini ya Kihansi ili maji yanapofunguliwa yaweze kuhifadhiwa na wakulima wa maeneo yale waweze kutumia rasilimali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni kuhusu NFRA. Waheshimiwa Wabunge wa maeneo ya kilimo cha mahindi nataka niwahakikishie na niwaambie wakulima wasiwe na hofu. Serikali itanunua mahindi na tutanunua kwa bei nzuri. Hivi sasa tupo kwenye hatua za mwisho za majadiliano na nchi ya Zambia, Mozambique na Namibia kwa ajili ya kununua mahindi kutoka National Food Reserve Agency. Tunamaliza nao mazungumzo na NFRA itaanza kununua na tutaanza kuuza mahindi tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwatake wakulima wa maeneo ya mahindi ambao baadhi ya maeneo wameanza kuvuna, msikimbilie kuuza mahindi yenu kwa bei rahisi, Serikali itakuja kununua. Nimewaambia wafanyabiashara wa mahindi wote tunawaruhusu kuuza mahindi katika nchi zinazotuzunguka ambazo zimekuwa na matatizo ya chakula. Hatutawaruhusu kwenda kuuza mahindi kwa bei ya kutupa kwa sababu siku ya mwisho atakayepata hasara ni mkulima. Kwa hiyo, tumewaelekeza haya na tumeshaanza kuwapa export permit. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana na WFP ambao wamepata mkataba kutoka Malawi, tutawauzia unga badala ya kuwauzia mahindi, na hivi sasa vinu vyetu vya CPD vimeanza kusaga jumla ya tani 30,000. Kwa hiyo, hizi ni hatua ambazo tunachukua. Nataka niwahakikishie wakulima, msiwe na hofu na bumper harvest mliyonayo. Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ipo na tumeshapata approval kutoka Wizara ya Fedha. Tunachukua fedha kutoka Commercial Bank kuwa ku-supported na mikataba tunayoingia na hizi nchi na tutanunua mahindi ya wakulima yote bila hofu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine Waheshimiwa Wabunge wameongelea suala la BBT. Nataka nirudie tena, BBT ni program ya muda mrefu. Katika bajeti ya mwaka kesho 2025/2026 tutapeleka program ya BBT katika halmashauri, kwa kila halmashauri na tutaanza na halmashauri 100 za kwanza, mtuvumilie. Serikali itapeleka fedha ya kujenga miundombinu ili halmashauri zianze kuandaa maeneo kwa ajili ya vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali katika program ya BBT sasa hivi, jumla ya vijana 118 wamepewa jumla ya shilingi milioni 917 na Serikali ya Awamu ya Sita ambao wanajishughulisha katika shughuli za kilimo katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu. Serikali itaendelea kufanya hivyo na mwaka kesho katika bajeti tutaweka shilingi bilioni 10 ku-support vijana walioko huko vijijini wanaofanya shughuli za kilimo kwa ajili ya kupewa fedha kutoka mfuko wa pembejeo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni la upimaji wa afya ya udongo. Nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tumeshasambaza vipima afya ya udongo 142 katika halmashauri zetu. Sasa hivi mfumo wa upimaji wa afya ya udongo ni real time na wakulima watapewa certificate. Ni huduma ya bure. Ninachotaka kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, wote sisi ni Wajumbe wa Baraza la Madiwani. Twendeni tukawaulize Wakurugenzi wa Halmashauri, umeletewa mashine ya kupima afya ya udongo katika halmashauri yako, umepimia wakulima wangapi? Tupe taarifa na sisi mtusaidie kusimamia katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hoja ya mbegu. Bila kutatua tatizo, kwanza tuna changamoto ya mbegu. Huu ni ukweli kwamba kwa muda mrefu kama Taifa hatujawekeza katika eneo hili. Kwa mara ya kwanza mwaka huu tumeweza kujitosheleza 50% ya mahitaji ya mbegu zetu na zimezalishwa ndani ya nchi yetu jumla ya tani 60,000. Ni matarajio ya Serikali kufikia mwaka 2025/2026 tuweze kujitosheleza kwa 100%, lakini tunawagawia wazalishaji wa mbegu wa ndani, mashamba ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote mashamba yetu yamekuwa yakibaki pori, hayaendelezwi, kwa hiyo tunawapanga Watanzania nao wanazalisha katika mashamba tuliyonayo. Nataka niwahakikishie kwamba tunapokea maoni sasa hivi. Tunashukuru hoja ya wakulima...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Bashe. Kengele ya pili hiyo, mengine jibu kwa maandishi.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)