Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kuungana na wenzangu wote waliotangulia kuipongeza hotuba hii ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Vilevile naomba nichukue fursa hii kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa pole kwa mafuriko yanayoendelea nchini kote ambapo tumeshuhudia na kwa upande wa Mkoani kwetu Pwani Wilaya ya Rufiji na Wilaya ya Kibiti zimepata changamoto hii kwa mapana sana. Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa zoezi kuratibiwa vyema na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tumeshuhudia namna ambavyo Serikali imekuwa imara katika kusimamia vyema changamoto zozote zinazotokea katika Taifa letu. Ni wazi na sote tumeshuhudia kwamba kipimo cha uongozi ni wakati wa changamoto, na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelithibitisha jambo hili kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, sisi kule kwetu tumepokea misaada ya kiutu ya kutosha ambapo mpaka hivi sasa wananchi wa wilaya hizi wako salama wakiendelea kutazama hali inavyoendelea. Ni ukweli usiopingika kwamba mvua zimenyesha mfululizo na hata sasa zinaendelea kunyesha. Kila siku inayokwenda tunapata mvua. Kwa hiyo tunashukuru Wilaya yetu ya Mkuranga hatuna mafuriko lakini tunajua kwamba iko changamoto kubwa ya uharibifu wa miundombinu. Tunaomba tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu inapoangazia jambo hili kwa ukaribu sana. Mheshimiwa Rais amethibitisha ucha Mungu wake, amethibitisha umahiri wake, amethibitisha uchapa kazi wake. Nasi tunaendelea kumwombea aendelee kuwa na afya njema aendelee kulijenga Taifa letu bila ya kikwazo chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepata michango kadhaa, takribani Wabunge 10 wamechangia hoja za mifugo na hoja za uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jambo lililochangiwa hapa ni juu ya uhitaji wa majosho na chanjo kwa ujumla wake. Katika bajeti yetu tunayotarajia kwenda kuisoma hapa Bungeni tutakuwa na majosho ambayo tumeyaweka tena kama ambavyo tumekuwa tukiyaweka katika bajeti zilizopita. Ni matarajio yetu kwamba halmashauri zetu ambazo zimeleta maombi ya majosho zitapata majosho hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mpango kabambe ambao sasa badala ya kuacha wafugaji wawe wanafanya zoezi la kuchanja mifugo wao wenyewe kwa utaratibu ambao wamejipangia, sasa tunakwenda na zoezi la pamoja. Tutakuwa na ratiba maalum ambayo itasimamiwa vyema na Wizara na hatimaye chanjo ikachanjwe kwa pamoja. Hii itatuepusha sana na wale makanjanja ambapo hata leo asubuhi nimemsikia Mheshimiwa Mbunge mmoja akiuliza swali juu ya dawa fake. Kwa hiyo sasa tunataka tuliratibu suala hili sisi wenyewe kama Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema; kwenye uratibu huu itatusaidia hata kutoa ajira za muda mfupi kwa vijana wengi sana wa Kitanzania waliosoma masomo haya ya mifugo na wako mtaani. Vijana hao tutawachukua na watakuwa ni part and parcel ya programme hii ya uchanjaji wa mifugo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Waheshimiwa Wabunge wametupa ushauri juu ya kunenepesha mifugo ili kuongeza chachu ya biashara ya mifugo ndani na nje ya nchi yetu. Ni ukweli usiopingika kwamba, sote tunashuhudia biashara ya nyama inakwenda vizuri sana na hasa wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Sita, tunafanya vizuri mno katika uuzaji wa nyama nje ya nchi yetu na record ziko wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni biashara ambayo inavutia na tunawakaribisha wawekezaji mbalimbali kwenye eneo hili na sisi Serikali tumejiweka mguu sawa, ndio maana tunayo programme yetu ya BBT ambayo inafanya vizuri na tunakwenda kuongeza vituo katika Mwaka huu wa Fedha wa 2024/2025. Miongoni mwa vijana watakaotoka katika programme hii ya BBT tayari tumewaandalia vitalu katika maeneo yetu ya mashamba ya Serikali ya NARCO ambayo yatasaidia kuwafanya vijana hawa wawe ni wafanyabiashara proper wa mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa uvuvi kilichozungumzwa ni suala la maboresho ya sheria. Tuko katika mkakati wa kuhakikisha kwamba sheria na kanuni zetu tunaziboresha na tunapokea maoni ya wadau wote kusudi tuzifanyie marekebisho zile sheria ambazo zinaonekana kuwa ni tatizo kwa wavuvi wetu ili tuweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia iko rai ya kulitumia Bwawa la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya upandikizaji wa samakiā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili hiyo.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)