Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Babati Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa ufafanuzi wa hoja chache ambazo zimeelekezwa kwenye Wizara yetu ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na timu nzima kwa hotuba nzuri ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko hoja ilitoka kwa Mheshimiwa Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo ambayo ilihusu changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho vya uraia kwa wananchi wanaoishi kwenye mikoa ya mipakani. Sote tunafahamu kwamba vitambulisho vya Taifa hutolewa kwa raia wa Tanzania, lakini pia kwa wageni wenye vibali vya makazi hapa nchini ambao wanakidhi sifa ambazo zimeainishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto ya mikoa ya mipakani kuwa na wahamiaji haramu pamoja na walowezi wengi, lakini kati ya mwezi Oktoba, 2023 hadi Machi, 2024, kati ya waombaji 802 ambao waliwasilisha taarifa zao katika Ofisi za Uhamiaji Biharamulo, waombaji 112 walibainika kuwa na matatizo ya uraia. Hivyo pamoja na changamoto hizo ambazo tunakabiliana nazo katika mikoa ya mipakani, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba waombaji wote ambao wana sifa zinazostahili wanapatiwa vitambulisho vya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili lilikuwa ni eneo la usajili wa vijana hasa baada ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022. Mheshimiwa Mariam Nyoka, Mbunge wa Viti Maalum alitoa hoja kwamba kuna baadhi ya watu ambao bado hawajasajiliwa. Ni kweli tunakubali kwamba wapo vijana wengi na watu ambao wana sifa hasa baada ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, wanatakiwa wasajiliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanza kwa zoezi baada ya utambuzi na usajili wa mwaka 2012 hadi tarehe 30 Machi mwaka huu 2024, wananchi ambao tayari wametambuliwa na kusajiliwa ni 24,388,715, lakini namba za utambulisho ambazo zimezalishwa ni 20,920,172, vitambulisho ambavyo tayari vimezalishwa ni 20,548,067.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho ambavyo vimesambazwa kwa wananchi kwa tarehe tajwa ni 19,734,367. Kwa hiyo, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba, usajili wa watu takribani 7,000,000 na zaidi ambao tayari wametambuliwa hasa baada ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 utaendelea kufanyika kwa awamu tatu kuanzia mwaka huu wa fedha 2024/2025. kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 tunatarajia kutambua na kusajili wananchi wapatao milioni mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, naunga mkono hoja. Ahsante kwa fursa hii. (Makofi)