Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rombo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri wetu Mkuu na vilevile naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na hoja mbalimbali kuhusu Sekta ya Elimu kwa ujumla wake na mapendekezo mbalimbali. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, mapendekezo haya kwa ujumla wake tunayachukua na tutayafanyia kazi. Hata hivyo, ningependa baadhi niyatolee maelezo kidogo na mojawapo ni kuhusu mikopo ya elimu ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma ni kwamba, Serikali ijikite kwenye kuongeza bajeti ya mikopo kwa ajili ya elimu ya juu. Tunapokea ushauri huo na kwenye bajeti yetu tutaona jitihada hizi zikiendelea. Hata hivyo, ningependa tujikumbushe tumetoka wapi katika jambo hili ili vilevile tujipongeze kwa kazi ambayo imeshafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya shilingi bilioni 450 zilitumika kama mikopo kwa elimu ya juu na mwaka wa fedha 2020/2021, fedha ziliongezwa kufikia bilioni 464 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu, lakini Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alivyoingia madarakani mwezi Machi, muda mfupi tu baada ya kuapa kama tulivyoelezwa hapa wakati ule, aliagiza nyongeza kubwa zaidi kupata kutokea kwenye mikopo ya elimu ya juu na hivyo kuongeza kiasi cha fedha kutoka bilioni 464 kwenda bilioni 570 kwa mkupuo. Kwa kweli nyongeza hiyo ni kubwa katika historia ya mikopo ya chuo kikuu na tumeendelea kuongeza kutokana na maelekezo yake kwa sababu tulivyofika mwaka wa fedha 2022/2023 tulitumia bilioni 654. Mwaka ambao sasa hivi tunaenda nao tuna bilioni 731 na katika bajeti ijayo tutaona tena nyongeza ambayo tutaipata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo pamoja na ukweli kwamba bado tunahitaji kuongeza, lakini jitihada iliyofanyika ni kubwa sana. Kwa kweli tumpongeze Rais wetu kwa sababu yeye binafsi ndiye aliyeona umuhimu wa suala hili la mikopo ya elimu ya juu. Si hivyo tu alikutana na viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu, akawasikiliza hoja zao na kuwaongezea kitita ambacho wanakipata kwa ajili ya kujikimu siku hadi siku. Nyongeza hiyo siyo kwamba inaongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mkopo tu, lakini inaongeza kiasi ambacho wanafunzi wanapata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa tuliyonayo ni kuhakikisha kwamba hizi fedha bado tunazigawa kwa haki kwa kutumia vigezo vilivyo wazi vinavyotabirika ili mtu anapokosa mkopo anaweza kukata rufaa, hata ikifika kwa Waziri, kazi yetu ni kuangalia tu vigezo tulivyoviweka kama vimetumika sahihi au siyo sahihi. Bodi ya Mikopo bado ina maelekezo ya kuhakikisha kwamba inazidi kuwa transparent kwa kuweka vigezo wazi, kuvitumia inavyotakiwa na kuondoa aina yoyote ya upenyo wa mtu kumpenyeza mtu kupata mkopo ambaye hastahili ili angalau kama fedha hazitoshi, basi ziwafikie wale ambao wana mahitaji makubwa zaidi kuliko watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo tunaendelea kuwekea mkazo katika marejesho ya mikopo, kwa sababu huu ni mkopo. Waliopata ajira wana wajibu wa kurudisha fedha hizi kwa ajili ya kuhakikisha watu wengine zaidi wananufaika. Mkazo mkubwa unawekwa na mkakati maalum umeandaliwa na bodi ya mikopo kuhakikisha kwamba tunaongeza marejesho.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali ya hivyo, chini ya uongozi wa Rais wetu aliagiza na nakumbuka Bunge lako Tukufu lilipitisha kwamba tutoe scholarship kwa mara ya kwanza. Tangu tuanze cost sharing Serikali ilikuwa haitoi scholarship kwa degree ya kwanza, lakini Rais wetu alipoingia madarakani aliagiza kwamba sekta iandae scholarship kwa ajili ya wanafunzi ambayo hatimaye Bunge lilipitisha na sisi tumeita Samia Scholarship, ambayo inafanya vizuri zaidi na sasa hivi wanafunzi wengi wamenufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka bajeti hii tunayotekeleza tulipewa maelekezo kutoka Ofisi ya Rais kwamba Mheshimiwa Rais amesema anataka kuona mikopo inaongezwa kwa vyuo vya kati. Kwa hiyo tulianza kwa kutenga bilioni 48 kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma vyuo vya kati ili nao waweze kujipatia mikopo na tumeanza ku-administer kwa kuangalia maeneo ya vipaumbele. Tutaendelea kuona utekelezaji wake unaenda vipi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kutoa taarifa kwako na kwa Bunge lako Tukufu kwamba wapo wadau mbalimbali ambao wameiunga Serikali mkono na wengine wamekuja wamesema tunataka kumuunga mkono Rais wetu. Kwa mfano, KCB Bank, yenyewe imeamua kutoa scholarship kwa wanafunzi wanaosoma kwenye vyuo vya VETA. Wanatoa fedha kwa kila mwanafunzi 100%. Wametuambia kwamba wanafanya hivyo kwa sababu wanataka kuunga mkono jitihada za Rais wetu za kutoa mikopo na kuongeza scholarship kwa wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika NBC Bank nao wametoa kitita ambacho kinatoa ufadhili (scholarship) si mkopo kwa wanafunzi wanaosoma kwenye VETA ni kuwasaidia baada ya kusoma ili kuanzisha biashara ambazo zitawasaidia kujikimu katika maeneo hayo. Kama tulivyotangaza katika bajeti yetu wakati ule NMB Bank wametoa bilioni 200; lakini hii ni mikopo kwa watu ambao wana miamala inayopitia kwenye benki kwa ajili ya kusaidia watu kwa ajili ya masuala ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kutoa wito kwa wadau wengine mbalimbali wajitokeze kuunga mkono juhudi hizi nzuri za Serikali na kumuunga mkono Rais wetu kwa ajili ya kusaidia vijana wetu kujenga uwezo wao wa kujisomea na kujiendeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa muda unaenda ningependa nizungumze suala lingine moja muhimu ambalo lilizungumzwa na Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza kuhusu kuangalia school dropout. Kwanza ningependa kutoa taarifa kwamba tunaimarisha sana takwimu za elimu sasa hivi. Kwa mara ya kwanza sasa hivi ile inayoitwa Basic Education statistics of Tanzania, ile basic haitakuwa basic ya education tena itakuwa basic statistics, sasa hivi itakuwa inaanza elimu ya awali mpaka vyuo vikuu. Sasa hivi Tuna kazi kubwa inafanyika kushirikiana na TAMISEMI, TCU, NACTVET na taasisi nyingine zote na kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaosoma shule binafsi ambazo zinatumia mitaala ya nje siyo mitaala ya ndani, nao tunawa-capture. Kwanza tujue wanafunzi wetu wanaosoma ni wangapi, wako wapi na umri wao ukoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo tuna kazi kubwa ambayo tunafuatilia wanafunzi wote ambao waliacha shule kwa sababu mbalimbali. Leo timu yetu iko Geita kwenda kuangalia re-entry programme kwa wale wanafunzi waliopata ujauzito wakati wa kusoma, lakini tunaangalia na boys ambao wametoka shuleni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, mengine utaleta kwa maandishi.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)