Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba ya bajeti ya Ofisi yake ambayo ameiwasilisha, ambayo imetoa mwelekeo kwa Wizara nyingine zote ambazo tunakuja baada yake. Pia niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri chini ya Ofisi yake kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia kwenye hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambao waligusa Wizara yetu ya Viwanda na Biashara. Naomba nikiri kwamba tumepokea mawazo yao, miongozo yao pamoja na ushauri wao na tutakwenda kuifanyia kazi, tunapokuja na bajeti yetu ya Wizara ya Viwanda na Biashara tutayasema yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kwa sababu ya muda niruhusu niseme mawili tu. Nianze na suala la siku zote ambalo ni suala la Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mheshimiwa Yustina Rahhi aliuliza ni wapi tumefika kwenye utekelezaji wa mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na hasa kwa kuonesha mwelekeo chanya kwenye utekelezaji wa Mradi huu wa Mchuchuma na Liganga. Mheshimiwa Rais alitupatia shilingi bilioni 15.42 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wetu 1,142 ambapo mpaka leo tayari tumeshalipa shilingi bilioni 15.38 kwa wananchi 1,129 na hakuna malalamiko yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshalipa 98.86% ya wafidiwa wote ambao walifanyiwa tathmini na wamebaki 13 tu. Hawa 13 hawajajitokeza na sisi kama Wizara tunaendelea kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa kuwatafuta hawa 13 ili tuweze kuhitimisha kuwalipa fidia yao na mradi wetu uweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishahitimisha ulipaji wa fidia ndipo sasa tunaweza kusema eneo hili ni la Serikali. Nimshukuru tena na kumpongeza tena Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miongozo yake anayoendelea kutupatia. Tayari tunafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Ardhi, ambapo sasa tunakwenda kutwaa lile eneo baada ya kuwa tumeshawalipa wananchi wetu wote kwenye hili eneo, ili sasa mwekezaji yeyote yule anayepatikana aweze kutekeleza mradi huu kwa kuwa eneo sasa ni la Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu majadiliano; kama nilivyosema Bunge la bajeti lililopita, tunaendelea kujadiliana na mwekezaji yule wa Sichuan kwa umakini mkubwa ili tusiliingize Taifa letu kwenye hasara yoyote kutokana na mikataba ambayo ilishasainiwa kabla. Kwa hiyo tunaendelea kushughulika pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Mambo ya Nje ili tuwapate watu sahihi na tuhitimishe majadiliano na mwekezaji wa Sichuan Hongda na ardhi ile iweze kurejea mikononi mwetu na tuweze kupata mwekezaji mwingine atakayefanya kazi nzuri au yeye kama atarudi atakuwa amejipanga sawasawa, basi afanye kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili eneo la Mchuchuma na Liganga, naomba kusema maneno yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo linaloshindaniwa ambalo tuko kwenye majadiliano ni asilimia 15 tu ya eneo kubwa la Mchuchuma na Liganga lenye madini. Hivyo, sisi kama Wizara kupitia miongozo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tumeamua eneo lingine 85% lililobaki tumetangaza ili waje wawekezaji tufanye utafiti na tuweze kuchimba makaa ya mawe pamoja na chuma kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwaambia Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu taarifa njema kabisa, kwamba tayari tumepata wachimbaji ambao ni wazawa watano, tumeshasaini nao mikataba kwa ajili ya vitalu vidogo na wawili wameshakamilisha utafiti wa kijiolojia, wanaanza uchimbaji wa makaa ya mawe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeimba sana kuhusu Liganga na Mchuchuma na sasa Serikali imeamua kutekeleza mradi huu na tunakwenda kuutekeleza na wanaanza Watanzania wazawa wenyewe ambao wameshamaliza utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye hoja ya pili, napenda kuitolea ufafanuzi, nayo ilitolewa na Mheshimiwa Kunti Majala kuhusu mikakati ya kulinda wakulima wa alizeti ikiwa imepunguza tozo ya mafuta yanayotoka nje ya nchi ili kulinda wakulima wa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliweka sawa jambo hili. Serikali haikupunguza kodi yoyote. Waheshimiwa Wabunge naomba niwakumbushe, mwezi Desemba, 2022, mwezi Januari, 2023 mpaka tulipofika mwezi Februari hali ya bei ya mafuta ilikuwa ni ya juu sana ndani ya Taifa letu, ni kwa sababu tulifanya mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2021. Jambo hili lilipoonekana kwa dhamira njema ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema turudi pale tulipokuwa ili Watanzania wasiumie na bei kubwa ya mafuta ya kupikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwaambia Waheshimiwa Wabunge, dhamira ya dhati ya Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni njema sana na nimpongeze sana hasa uwekezaji wake kwenye kilimo. Anawekeza kwenye kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ametoka kusema hapa. Tunachotakiwa kukifanya ni wazalishaji wetu ambao ni wakulima wa mbegu za mafuta kuzalisha kwa ufanisi ili ziweze kuchakatwa kwenye viwanda vyetu ambapo kwa sasa viwanda vinazalisha kwa muda wa miezi miwili tu na mbegu zote zinakuwa zimekwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweza kuongeza ufanisi kwenye uzalishaji wa alizeti, nina uhakika hata bei yetu kwa wakulima itakuwa nzuri na bei ya mafuta nayo itakuwa nzuri, tutakuwa tunawalinda watu wetu wote…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri ahsante, mengine yajibu kwa maandishi.
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)