Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karagwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze na niungane na waliotangulia kuchangia na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri na bajeti nzuri ambayo imesheheni miradi na mambo mazuri kwa ustawi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika pongezi, nimpongeze dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Mheshimiwa Deo Ndejembi kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, bila kuwasahau Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Katambi na Mheshimiwa Ummy. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango yao mizuri na ushauri ambao wametupatia na nitajikita kwenye hoja ya Ujenzi. Niwashukuru sana kwa maeneo ambayo wamechangia hususani yanayohusu Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamechangia Wabunge wasiopungua 37 hasa kwenye masuala ya barabara na madaraja na michango ya Waheshimiwa Wabunge inaonesha taswira ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi ambayo inakuja. Vilevile, inaonesha uhalisia kwa sababu Waheshimiwa Wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wote tunaona namna mvua za El-Nino zilivyonyesha nyingi kuliko namna ambavyo tumezoea kwenye historia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mvua hizi zimeharibu miundombinu, hakuna barabara hata moja iwe ni ya TANROAD au TARURA ambayo haijaharibiwa na mvua za El-Nino. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge michango yao iko kwenye uhalisia na upande wa Serikali pamoja na wananchi, tunaona mvua hizi kubwa ambazo ziko nje ya uwezo wetu na uharibifu mkubwa wa miundombinu ambao zimeufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na changamoto hizi ameendelea kutuwezesha TANROADS na TARURA ili kuendelea kuweka jitihada za kurudisha mawasiliano pale yanapoharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais, katika Bunge hili; Bunge lililopita mwezi Februari, tulikuwa tumeomba bilioni 66, hivi ninavyozungumza Mheshimiwa Rais na Serikali ya Awamu ya Sita anayoiongoza, tayari ametupatia bilioni 66 ili kuendelea kupambana kurudisha mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya nchi hii ambayo yamekatika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema mvua za El-Nino zimeharibu miundombinu nchi nzima. Waheshimiwa Wabunge, wakati tunaendelea na kila aina ya jitihada ili kurudisha hali ya mawasiliano ya barabara za lami na zile za changarawe, naomba kuzungumzia mafanikio makubwa ambayo tulikuwa tumejipanga nayo na tunaendelea kuyafanya. Hata hivyo, kwa sababu mvua hizi zimebomoa madaraja na barabara, zipo changamoto lakini lazima tumtendee haki Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumshukuru kwa barabara 25 ambazo zimekwishakamilika kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Bunge la Bajeti linaendelea pia tuko kwenye maazimisho ya miaka mitatu toka Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameingia madarakani. najivunia kuripoti kwenu kwamba, ndani ya miaka mitatu tumekamilisha ujenzi wa barabara 25 kwa kiwango cha lami, zenye urefu wa kilometa 1198.5. Vilevile, tumekamilisha madaraja makubwa nane, pia sasa hivi barabara 57 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi ambazo mpaka kukamilika kwake tutakuwa tumejenga barabara zenye urefu wa kilometa 3,794. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada hizi yapo pia madaraja matano ambayo yako katika hatua mbalimbali za ujenzi, likiwemo Daraja la Kigongo – Busisi (John Pombe Magufuli Bridge) ambalo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati anaingia madarakani, ujenzi ulikuwa umefikia 25% na hivi sasa uko asilimia 85 na kazi inaendelea. Matarajio yetu, kufikia Desemba, 2024 daraja hili liwe limekamilika ili liendelee kutoa huduma kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali, jitihada hizi na barabara hizi ambazo zimekamilika, barabara 57 ambazo tunaendelea kujenga na madaraja ambayo tunaendelea kujenga, mvua za El-Nino zimeharibu ujenzi huu pamoja na barabara ambazo zilikwishakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti ambayo Wizara ya Ujenzi tutaleta, tutaelezea kwa kina namna ambavyo tumejipanga. Kwa mfano, barabara 49 tayari tulikuwa tumekwishafika hatua ya kusaini pamoja na zile barabara 57 ambazo ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Barabara 30 tulikuwa tuko katika hatua za manunuzi kwa maana ya kupata wakandarasi. Vilevile, bila kusahau barabara ambazo ziko chini ya mikoa yetu (barabara za changarawe) ambazo kila mwaka tunatumia kiasi kisichopungua bilioni 550.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo tutakuwa tunaona jitihada hizi nzuri ambazo tayari tulikuwa tuko kwenye mwelekeo mzuri, lakini tukapata changamoto hii ya mvua za El-Nino ambazo zimenyesha kupita kiasi. Kwa hiyo, mpaka hivi sasa kwa tathmini ambayo tumefanya wakati wa Bunge la Mwezi Februari, tulifanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu. Kipindi kile hasara ilikuwa ni bilioni 200, mpaka kufikia jana miundombinu imeharibika na ili tuweze kuirudisha tunahitaji kiasi kisichopungua bilioni 500 (nusu trilioni).
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ndiyo bajeti ambayo ingekwenda kwenye miradi ambayo iko katika hatua za ujenzi wa kiwango cha lami, barabara ambazo tumesaini na barabara ambazo ziko kwenye manunuzi. Sasa hivi tutalazimika kukaa na kujipanga upya ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuwa na mawasiliano ya hizi barabara ambazo zimeharibika huku tukiendelea na mkakati wa kudumu wa kujenga barabara hizi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania, wote tunaona namna ambavyo miundombinu imeharibika, lakini ndani ya Serikali tunaendelea kujipanga kwa kadri inavyowezekana ili kuhakikisha miradi hii inaendelea. Vilevile, tukiwa tunafahamu kwamba tunaweza tukalazimika ku-review baadhi ya maeneo ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mkoa wa Lindi kuna kipindi Wilaya ya Nachingwea, Liwale pamoja na Ruangwa zilikuwa hazifikiki kwa njia ya barabara. Ililazimika kutafuta fedha za emergence ili kwenda kuhakikisha wilaya hizi zinapata mawasiliano na kuchelewa kwake utakuta bei ya vyakula inapanda, mafuta yanakosekana. Kwa hiyo, yapo masuala mengine ambayo hayawezi kusubiri kesho, lazima tuyafanye sasa hivi ikiwemo suala la barabara hizi ambazo zimeharibika. Pia, tunaendelea kutumia hela za dharura ili kurudisha mawasiliano yake…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bashungwa, ahsante kwa mchango mzuri na tathmini uliyoifanya…
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na tutaelezea kwa kina wakati wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)