Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mola ambaye kwa mara nyingine ametuingiza katika Bunge hili la Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kumpongeza mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika sisi tunajivunia sana kuwa naye, kwa sababu yeye ni kama zile nyavu za wale ndugu zangu, watani zangu Wasukuma, nasema eneo analoongoza kama ni nyavu ni kokolo (ana mambo mengi). Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameendelea kuitendea haki Serikali ya Awamu ya Sita ili kuhakikisha majukumu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwahudumia Watanzania yanaendelea vizuri. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwa kweli dada tunamchosha sana. Hata hivyo, ameendelea kuwa imara akipamba katika eneo lake kama Chief Whip, lakini kuhakikisha mambo yote yanakwenda vizuri na naomba watu wa Peramiho wamwangalie kwa jicho la mara mbili, mbili. Vilevile, nimpongeze sana ndugu yangu Mheshimiwa Deo Ndejembi, kwa kupata fursa hii katika eneo hili jipya, kwa kweli hii ni fursa kubwa sana ambayo imani yangu na imani ya Watanzania ni kwamba, ataendelea kuhudumia na kumsaidia Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba eneo hilo la Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu linatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Katambi, tunafahamiana vizuri sana tokea siku nyingi sana na nafahamu weledi wake katika kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mungu ambariki sana. Vilevile, dada yangu na shemeji yangu Ummy, anaupiga mwingi bila kuchoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya. Katika upande ninaouongoza, niliopewa dhamana ya kusimamia, Ofisi ya Makamu wa Rais, nimeona Mheshimiwa Rais anaitendea haki sana nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaja katika hoja ambayo Wabunge watatu wamezungumza, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu yeye ndiye amepewa dhamana ya kushughulikia sherehe za kitaifa. Jana tulikuwa kule Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, maandalizi aliyoyafanya Mheshimiwa Waziri Mkuu yamekwenda vizuri sana. Pia, nina imani ya kutosha kwamba siku ya uzinduzi wa Kitabu cha Miaka 60 ya Muungano, tarehe 23, halikadhalika siku ya tarehe 26 ya kilele, Watanzania watashuhudia mambo makubwa ya Muungano wetu yaliyofanikiwa katika kipindi hiki, Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika hili kwa kweli namshukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata Mawaziri waliokwenda katika vyombo vya habari kuzungumza mambo makubwa ambayo yamefanyika katika hii miaka 60, hakika kama Serikali uratibu wa Mheshimiwa Waziri Mkuu umetusaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja zilizojitokeza katika upande wa biashara ya carbon. Ni kweli kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nakumbuka mwaka 2022, tulianza kutengeneza Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Carbon. Mheshimiwa Waziri Mkuu, atakumbuka kipindi kile alienda kule Katavi kutoa gawio kwa Halmashauri ya Katavi. Hata hivyo, kipindi kile tulikuwa hatuna kanuni wala mwongozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo yake sasa tumepata kanuni na mwongozo. Naomba nimtoe mashaka ndugu yangu Mheshimiwa Justine Lazaro Nyamoga, kule wana misitu ya kupandwa kwa kiwango kikubwa, lakini, tulizungumzia jinsi gani katika wataalam wa halmashauri wataweza kupata elimu. Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ushirikiano na UNEP, tumeweka mpango kwa ajili ya kufanya capacity building kwa wataalam wetu wa mazingira katika halmashauri zote nchini. Kwa hiyo, katika hili ni imani yetu kwamba, tutaendelea kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika ndugu yangu Sebastian Simon Kapufi, alizungumzia jinsi gani hata Wabunge wanahitajika kupata uelewa wa kutosha. Katika package yetu, tunakwenda kugusa wote kwa lengo la kuhakikisha tunakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu biashara ya carbon.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunaanza mchakato huu, nchi yetu ndani ya kipindi hiki tayari imekwishasajili miradi 42. Katika miradi hiyo, Miradi 22 inahusisha Sekta ya Misitu, Miradi 13 inahusisha Sekta ya Nishati, Miradi minne ni Sekta ya Agroforest na Miradi miwili ya Waste Management. Katika hili naomba niwambie Watanzania kwamba hakika katika hiki kipindi kifupi, haya ni mafanikio makubwa sana. Kwa mfano, Halmashauri ya Katavi siyo muda mrefu watapata gawio lenye wastani kati ya shilingi bilioni 10 mpaka bilioni 14.7, kwa mwaka huu peke yake, haya ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera kule kwa ndugu yangu Mheshimiwa Bashungwa, kule Karagwe, Kyerwa, Muleba na Bukoba, eneo hili zaidi ya bilioni 1.6, kupitia kampuni ya KADERES ambayo inakwenda kuwakilisha katika eneo la agroforest. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, hapa tumejipanga vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika siku za awali kwamba, siyo muda mrefu tumepata mafanikio haya makubwa, haya makampuni takribani 42 yote yatakapokuja kutekeleza ambayo kati yake makampuni 12 yameshapata no objection, yamepata fursa kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi hii ya carbon na mengine yako katika mchakato wa kupitia yale maandiko yao, imani yetu ni kwamba, eneo hilo litakuwa ni fursa kubwa sana ya kupata mapato katika halmashauri, halikadhalika katika nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaombe Watanzania katika eneo hili kuhusu suala kubwa la utunzaji wa misitu. Leo hii tunapozungumza suala zima la mabadiliko ya tabianchi na hata tukiangalia hizi mvua zinazoendelea kunyesha, athari yake imekuwa ni kubwa. Katika hili ni meseji tosha kwamba, Watanzania tuna kila sababu ya kuhakikisha tunaizingatia ajenda ya mabadiliko ya tabianchi kwa kujitahidi sana katika utunzaji wa mazingira. Bila kufanya hivyo madhara yake yatakuwa makubwa sana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba athari ya mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko na mvua zisizotabirika ni kubwa, ndiyo maana leo hii tunaomba Mungu tu, kwa sababu kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka yetu ya Hali ya Hewa, huenda kutakuwa na siku kumi za ziada za mvua kubwa, maana yake madhara yake yatakuwa makubwa sana. Sisi Ofisi ya Makamu wa Rais, tumewatuma wataalam wetu wa NEMC waende nchi nzima ili watupatie taarifa ya kutosha kuhusu mazingira hasa baada ya kujitokeza kwa hali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwaombe Watanzania, kwa upande wetu wa mazingira, waliopo kwenye maeneo hatarishi, waweze kutoka kwenye maeneo hayo kwa sababu hili ni janga kama majanga mengine. Ni imani yetu kwamba, tutaendelea kutekeleza hilo kwa sababu suala la mazingira ni jukumu letu sote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na maeneo machache tu kwa ajili ya biashara ya carbon, kubwa zaidi tumwombee sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, that is my message. Juzi nilikuwa nawaambia watu tulipokuwa tunaelekea katika siku ya Pasaka na Eid, kuna mtu mwingine familia yake alikuwa anapanga awanunulie Abaya “ile Abaya eeh?”

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo, Abaya.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, siku zinaisha abaya haijapatikana. Wewe fikiria kama ni kawaida mtu kupata Abaya ya mama na nguo za mtoto inashindikana, je, kuongoza nchi ni jambo la mchezo?

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu anafanya kazi kubwa, ukiangalia hii investment anayoifanya katika Sekta ya Elimu haijawahi kutokea. Sekta ya Miundombinu for the first time, leo hii ndiyo tumepata athari ya miundombinu na ukiangalia kazi iliyokuwa imefanyika ni kubwa. Hili Watanzania walifahamu, japo miundombinu imeharibika, lakini Serikali ilikuwa imefanya kazi kubwa. Hili ni janga kama majanga mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunatolewa mfano, kwa mfano, katika suala la uwekezaji, tukiwa katika mikutano mbalimbali tunaambiwa; “Tanzania ni nchi ya mfano yenye kutengeneza Mradi wa Green Energy kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Standard Gauge” haijawahi kutokea Barani Afrika. Zaidi ya kilometa 2,100 ni kazi kubwa na ni investment ya fedha nyingi, Watanzania lazima tumwombee Rais wetu, tusipofanya hivyo, tutapata dhambi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwambie kazi aliyofanya Rais wetu imekuwa ni kazi ya mfano. Siyo Tanzania tu bali na nchi nyingine. Tuna kila sababu ya kumwombea sana Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu na yeye ni binadamu, anataka maombi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba anaipeleka nchi yetu katika eneo salama zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilivyoona hii bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, sidhani kama leo hii mtu atashika shilingi, sina mashaka, nimeona bajeti imedadavua mambo mengi na sisi kazi yetu ni kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu, watu waje kushika shilingi katika maeneo yetu na siyo kwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu halali, hapumziki na anahangaika kwa ajili ya Watanzania na ame-present vizuri bajeti yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina imani, tutashirikiana katika Bajeti ya Waziri Mkuu na imani kubwa kwa mtu aliyepewa dhamana na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti yake ipite kwa kishindo. Sisi Wazaramo tunasema hiki ndicho kingilambago. Waheshimiwa Wabunge, ndiyo tumeanza hapo, kwa hiyo, tuanze vizuri. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, ibariki bajeti hii na naunga mkono hoja. (Makofi)