Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia kufika siku ya leo na kutujalia kumaliza salama Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kuipata Iddi vizuri na leo tuko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kubwa kwangu na kuendelea kuchapa kazi. Miaka mitatu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan sote tunaona kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya, tunampongeza sana. Niendelee kuishukuru familia yangu ikiongozwa na mume wangu Rashidi pamoja na wanangu na wasaidizi wangu wote kwa kuendelea kunisaidia na kunipa utulivu ulioniwezesha kuendelea kufanya majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Jenista Mhagama. Naungana na Waheshimiwa Wabunge wanasema ni malikia na mimi ameendelea kuwa ni mlezi wangu. Watu wa Peramiho siku zote nimeendelea kuwaambia nawashukuru sana kwa tunu hii, waendelee kumtunza Mheshimiwa Waziri. Tunampongeza Mheshimiwa Waziri na tunamshukuru kwa malezi, kwa mentorship na kila kitu, Mwenyezi Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro, mabosi wangu kwa kuendelea kuniamini na kuniunga mkono, nawahakikishia tuko pamoja. Mimi ni mtoto wao, nitaendelea kuwa mnyenyekevu kwao. Wanawake wa mikoa mingine ukijumuisha na Zanzibar naendelea kuwaambia nitaendelea kuwa mnyenyekevu na kuwasaidia majukumu, lakini Jumuiya yetu ya UWT chini ya Mama Chatanda na Mama Shomari tunaendelea kuchapa kazi na tunaendelea kuwatia moyo tuendelee kufanya kazi, tusikatishwe tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti na kwa malezi mazuri. Kipekee namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kwa kunipokea katika ofisi yake. Kwa kufanya kazi katika ofisi yake nimeendelea kupata malezi mazuri na miongozo ambayo imeendelea kunijenga kama kijana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na tunawashukuru Wanaruangwa kwa imani kubwa kwake, lakini tunamshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Deo, kaka yangu na Mheshimiwa Patrobass na Makatibu Wakuu wetu wote, Dkt. Jim Yonazi, lakini na Naibu Katibu Mkuu Mutatembwa na Wakurugenzi wetu wote katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kufanya. Niseme tu jambo hapa pia kwa Mheshimiwa Spika, dada yetu Dkt. Tulia tunampongeza sana kwa kazi kubwa na nzuri, ameendelea kuwa role model wa mabinti wengi, hata akinababa wameendelea kumwamini na kumuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakupongeza pia kwa miongozo yako na namna ambavyo umeendelea kutu-lead. Tunawapongeza pia watu wa Ilala kwa imani kubwa wanayoendelea kukuonesha. Sasa niendelee kuwapongeza na Waheshimiwa Wabunge wenzetu wote kwa ushauri, maoni na mapendekezo na Kamati zetu zote zile ambazo zimetupa maoni na ushauri, tumezingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye hoja za Waheshimiwa Wabunge. Niruhusu nianze na takwimu, kwa sasa dunia inakadiriwa kuwa na watu bilioni 7.9, kati ya hao watu milioni 39 wanaishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa mujibu wa Global Trend on HIV, huko unaweza kupata takwimu hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina watu milioni 61, kati ya watu 61 watu milioni 1.5 wanakadiriwa kuishi na Virusi vya UKIMWI. Kwa hiyo, unaona katika janga hili bado tuna kazi ya kufanya. Tunamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu alituzindulia Tanzania HIV and AIDS Impact Survey, mwaka jana pale Morogoro ambayo ilitupa hali halisi na picha kwa sisi kama Tanzania tunaenda wapi kwenye mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye 95% tatu za mapambano dhini ya Virusi vya UKIMWI, kwa Tanzania 95% ya kwanza ya kuhakikisha watu wote wamejua hali, Tanzania tumefikia 82%. 95% ya pili ambapo watu hao wamejua hali zao na wameanza dawa, tumefikia 97%, ya watu ambao wanatumia dawa. Hapa tuendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri. Tunaendelea kutoa dawa za ARV bure katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya. 95% ya tatu watu hawa sasa wawe wamefubaza Virusi vya UKIMWI, hapa tumefika 94%.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini kutokana na takwimu hizo? Utaona 95% ya kwanza ya watu wanaojua hali tuko 82% tunataka kufika 95%. Tunakubaliana na maoni ya Kamati na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wenzetu, tunaenda kufanya programme mbalimbali. Tunaenda kurejesha Kampeni ya Furaha Yangu ambayo mwanzo ilikuwa inafanyika chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na uliona imezaa matunda makubwa. Kwa hiyo, tunaenda kuirejesha Furaha Yangu awamu ya pili ili kuendelea kuwahamasisha wanaume kuendelea kujitokeza kupima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya kazi kubwa na nzuri kwenye eneo la vijana hasa mabinti. Takwimu zilituonesha vijana miaka wa 15 hadi 24 wanapata maambukizi mapya kila mara. Kwa hiyo, tukajielekeza tufanye kwa wasichana, kwa nini? 80% ya maambukizi hayo yalikuwa yanaenda kwa mabinti. Tukaamua kuanzisha programme kwa kushirikiana na wadau wetu. Programme ile inaitwa Dreams katika mikoa mitano, programme hiyo imeendelea kufanya vizuri. Tumepita na Waheshimiwa Wabunge kwenda maeneo mbalimbali tumeona namna ilivyofanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana na Waheshimiwa Wabunge wenzetu kwamba, tunaenda kuiongeza wigo programme hii kutoka mikoa mitano ambayo iko sasa hadi kufikia mikoa 21. Kadri tutakavyoendelea kupata fedha tutaendelea kuiongeza programme hii. Nataka niwaambie vijana wa kiume na wenyewe tutaenda kuwajumuisha katika programme hii na ni kwa mara ya kwanza tutaenda kuwajumuisha kwa ukubwa vijana wa kiume, kwa sababu imeonekana tunawaacha nyuma, tuna-focus zaidi na wanawake. Kwa hiyo sasa hivi tutawajumuisha na vijana wa kiume kwenye programme mpya ambayo itaenda kwa jina la Enabling Dreams. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie vijana hatuwalaumu kwenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ila Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaenda kuchukua hatua kuwafanya washiriki katika miradi hii kama wadau wa kwanza na wanufaika wa kwanza. Sisi kama viongozi, tutawajengea uwezo washiriki.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika programme hizi tutaendelea na programme za kuwawezesha watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI katika maeneo ya kujikwamua kiuchumi. Tutashirikiana na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, liko Ofisi ya Waziri Mkuu. Hivi juzi Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko alizindua makubaliano kati ya PPRA na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwamba sasa twende kufungamanisha maeneo haya mawili ili manunuzi ya umma katika maeneo yetu mbalimbali 30% ya manunuzi hayo yaende kwa makundi ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kuwajengea uwezo ili watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, waweze kupata fursa hii na waweze kunufaika. Nimesema kwenye programme hii ya vijana tutaendelea kuwajengea uwezo kwenye maeneo ya ujasiriamali. Programme hii hatutawaachia njiani, tumepokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge kwa unyenyekevu mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafunzo ya ujasiriamali tutawapa start up kits. Kama mtu amesomea pengine ufundi cherehani anatoka na cherehani yake na ana mafunzo anajielewa na kila kitu na tutaendelea ku-monitor. Niseme Mfuko wa Udhamini na Udhibiti wa UKIMWI Tanzania (ATF), 10% ya fedha za Mfuko zinazotengwa zitaendelea kuwawezesha kiuchumi watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri na maoni yao ambayo kwa kweli yametusaidia kuimarisha eneo hili la mapambano dhidi ya VIRUSI vya UKIMWI. Tutaendelea kufanya kazi kwa ukaribu sana na wao ili tuendelee kupokea maoni kwa sababu janga hili linahitaji approach mbalimbali za namna ya kwenda nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme kwamba mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri wangu Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa unyenyekevu mkubwa, tunaendelea kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi zao na kwa kutuunga mkono na sisi tunasema tuko pamoja nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)