Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa nafasi hii, lakini pia nitumie fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia afya njema sisi sote. Pili, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwa na imani nami ya kumsaidia katika kutekeleza majukumu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niwapongeze sana wasaidizi wa Mheshimiwa Rais ambao ni Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Isdor Mpango, Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais na kutusaidia sana sisi katika kutupa miongozo na maelekezo ambayo yanatusaidia kuweza kutekeleza Dira ya Maendeleo na Mpango wa Maendeleo. Pia kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia ofisi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye yeye pia amekuwa akifanya kazi kwa weledi mkubwa kuliongoza Bunge hili pamoja na wewe, lakini pia Katibu wa Bunge pamoja na uongozi wote wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie pia fursa hii kumshukuru sana kwa namna ya kipekee Mheshimiwa Waziri wangu Deogratius Ndejembi na kumpongeza pia kwa uteuzi wake kwa nafasi hii waliyoipata pamoja na Katibu Mkuu wangu kuhudumu katika Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba naye, tunaye Mheshimiwa Jenista Mhagama, amefanya kazi kubwa, Chief Whip tunakushukuru sana kwa miongozo na maelekezo yako. Sisi pamoja na Mheshimiwa Ummy kwa kweli tunanufaika kwa kufanya kazi nanyi za kumsaidia Mheshimiwa Rais, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru Wenyeviti wa Bunge, lakini pia wa Kamati za Bunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa hoja zao ambazo siku zote zimekuwa kiongozi pia kielelezo cha kutusaidia sisi katika kutekeleza majukumu ambayo yamekusudiwa na Serikali kuweza kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze moja kwa moja katika hoja ambazo zimezungumzwa au zilizoelezwa na kutolewa na Waheshimiwa Wabunge katika kutusaidia sisi kutekeleza majukumu yetu. Kwa hoja ambazo zimeelezwa, kwanza nitambue Wabunge ambao wamechangia kwenye ofisi yetu, kwenye maeneo ambayo yametugusa, ni Wabunge zaidi ya 36 na kwa sababu ya muda, naomba uniruhusu kuzieleza hoja hizi kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuunga mkono hoja ya Hotuba ya Waziri Mkuu pamoja na pendekezo hili la bajeti lililoko chini ya ofisi yake. Zaidi niseme maelezo yote, mapendekezo, ushauri na maoni yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge lakini pia na Kamati za Kudumu za Bunge, tunayachukua kwa ajili ya kwenda kuyafanyia kazi ili kuboresha jukumu hili la utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo, lakini pia na Dira ya Maendeleo pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ili wananchi wetu katika makundi hayo ambayo tumepewa fursa ya kuwahudumia, tuhakikishe kwamba tunawahudumia ipasavyo, kwa kuhakikisha tuna mikakati na mipango endelevu ambayo itawasaidia katika kuwahudumia na kufikia azma ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo amejiwekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo ambalo naweza kujielekeza na kwa kueleza kwa ujumla ni kwamba, tumeyachukua maoni na mapendekezo. Lipo eneo la watu wenye ulemavu ambalo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi ya dhati aliyonayo kwa watu wenye ulemavu, alidhihirisha hilo alivyowaita Ikulu ya Chamwino tarehe 16 Machi, 2022 na akasema kwamba; “Leo sina jambo lolote zaidi ya kuwasikiliza na mnieleze changamoto zote zinazowakabili, ziwe za kisera, kisheria, au changamoto zozote,” ambazo yeye kama Mkuu wa Nchi alitaka kuzipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais aliwasikiliza lakini pia akatoa maagizo mahususi kwamba twende kutekeleza. Mbali na mambo mengine ambayo aliyasikiliza, mojawapo ilikuwa ni changamoto ya mafunzo ya watu wenye ulemavu ambayo Waheshimiwa Wabunge wameeleza kama moja ya changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo taarifa kueleza kwa furaha kabisa kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mapenzi ya dhati aliyonayo alitoa fedha zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ukarabati wa vyuo ambavyo zaidi ya miaka kumi vilikuwa havifanyi kazi. Kikiwemo Chuo cha Masiwani Tanga, Sabasaba pale Singida, Lwanzari Tabora na Mtapika kule Masasi Mtwara ambapo tayari vimeshakarabatiwa na vinafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Chuo cha Yombo pale Dar es Salaam vinafanya kazi kwa ajili ya kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ya utengemao na kuhakikisha kwamba hawabaki mitaani bila kupatiwa elimu ili na wao waweze kujitegemea na kuchangia kwenye ujenzi wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais pia alitoa fedha nyingine zaidi ya shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vipya vya watu wenye ulemavu. Hayo ndiyo majibu ya hoja ya Waheshimiwa Wabunge waliyosema kwamba watu wenye ulemavu waangaliwe, sasa hizo ndiyo hatua ambazo Mheshimiwa Rais alizichukua kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 3.4 ambazo tumejenga na tunaendelea na ujenzi wa chuo pale Ruvuma kwa Dkt. Mama Mheshimiwa Jenista Mhagama. Tumesema Dkt ni sahihi, tumwombee kwa Mwenyezi Mungu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia chuo kingine kinajengwa pale Mwanza ambacho ni mbadala wa Chuo kile tulichokuwa nacho cha Milongo. Tuna chuo kingine ambacho tunakijenga Kasulu - Kigoma kwa Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako ambapo tayari ujenzi unaendelea na hali ni nzuri. Tunajenga Chuo kingine cha Watu Wenye Ulemavu kule Songwe. Lengo la Dkt. Samia Suluhu Hassan ni nini? Lengo ni kuhakikisha watu wenye ulemavu pia tunawajumuisha katika ujenzi wa uchumi wa Taifa hili, tunahakikisha watu wenye ulemavu hawawi barabarani tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akasema asilimia mbili za mapato ghafi ya halmashauri nazo ziende kwa watu wenye ulemavu, zaidi ya asilimia mbili za fedha hizi sasa zinakusanywa, zitatolewa kwa watu wenye ulemavu ili waweze kunufaika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa tena fedha shilingi 1,000,000,000, tumefungua akaunti maalum BOT kwa ajili ya ruzuku ya watu wenye ulemavu ambapo watapata vifaa saidizi vya kuwasaidia na pia vifaatiba, zaidi ya hapo hata kuwasaidia kwenye masuala ya elimu na changamoto walizonazo. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha cash na sasa hivi tunasubiri shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu na vikao vinavyohusika viweze kuvipangia matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye eneo la watu wenye ulemavu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi ya dhati ameendelea kuangalia katika maeneo ya ajira, tumetunga mwongozo ambao ameuidhinisha na ametoa ruhusa hiyo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, tayari asilimia tatu ya ajira zote zinazotoka nchini iwe kwa watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, kama ni watu 20 lazima angalau watu wawili au zaidi waweze kupata nafasi hiyo kulingana na masharti na vigezo ambavyo tumeviweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika eneo hilo la watu wenye ulemavu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezidi kuwatendea haki. Tumeenda kwenye miongozo ya ujenzi wote unaofanyika nchini uzingatie mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu. Ukijenga ghorofa lako lazima uzingatie kuna lift au kuwe na ramp ambayo itawasaidia watu wenye ulemavu ili kuweza kupata huduma katika sehemu wanayohitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ameendelea kuupiga mwingi Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa watu wenye ulemavu, yeye mwenyewe kwa kujua kwamba walikuwa hawana ofisi ya kitaifa ya kupata huduma, alitoa fedha zake mwenyewe zaidi ya shilingi milioni 36.7 kwa ajili ya kupata eneo la ujenzi wa Ofisi ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu, ninavyozungumza tayari hati hiyo wameshakabidhiwa watu wenye ulemavu na wanaendelea kwenye hatua ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la watu wenye ulemavu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mengi, pamoja na kuhakikisha kwamba hata kwenye zile kandarasi ambazo zinatolewa kwenye halmashauri na wao waweze kupewa share yao. Tunaendelea kuwaunganisha hata mikopo iliyokuwa ikitoka kwa kikundi cha watu watano, tumebadilisha mwongozo mwaka 2022 na sasa mtu mmoja mmoja mwenye ulemavu anaweza kupata mkopo wa shilingi milioni 10 mpaka shilingi milioni 50. Huyo ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utakuwa shahidi pamoja na Waheshimiwa Wabunge, watu wenye ulemavu sasa hivi wamepungua barabarani. Tulikuwa na kesi nyingi za ombaomba na tulikuwa na kesi nyingi za watu wenye ulemavu kudhalilishwa. Sasa hivi mtu mwenye ulemavu ukimkuta barabarani ni amechagua mwenyewe kwa sababu sikio la kufa wakati mwingine halisikii dawa, lakini kwa sehemu kubwa tayari watu wenye ulemavu tumewaweka kwenye utaratibu wa kupewa nafasi hizi, hata maeneo ambayo yanafanyika ujenzi wa masoko tunawapa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Sekta ya Afya pia hata kwenye huduma zinazotolewa hospitali, watu wenye ulemavu wamepewa kipaumbele pamoja na wajawazito, watoto na wazee katika kupewa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua kuwa rafiki mzuri na mwema kabisa kwa watu wenye ulemavu, tuendelee kumwombea Mwenyezi Mungu, aendelee kudumu ili watu wenye ulemavu waendelee kupata manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliona hatua nyingine ya kuhakikisha tunapunguza ulemavu, kwa sababu wapo wanaozaliwa na ulemavu na wapo ambao wanaupata baada ya kuzaliwa. Tumeweka utaratibu na mikataba ya lishe imesainiwa kupitia Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ili wahakikishe kunakuwa na lishe bora, imekuwa ajenda ya kudumu kwenye Mwenge wa Uhuru ili kuhakikisha watu wakizaliwa wasiwe na ulemavu, hata wale ambao wanapata madhila yanayotokana na kazi katika maeneo mbalimbali na kupata ajali, ameweka Mfuko wa WCF wa fidia kwa mfanyakazi ili kuweza kuhakikisha wanapata huduma pale ambapo wanaweza kupata madhila yanayowapelekea kwenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo lingine ambalo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya vizuri, kupitia Bunge lako Tukufu, ameendelea kutengeneza utaratibu mzuri wa kufanya kaguzi kwenye maeneo ya kazi kupitia Wakala wa Kazi (OSHA) ili kuhakikisha tunapunguza madhila, tunakuwa na kazi za staha na ajali ambazo zinatokea kwenye viwanda zinazosababisha ulemavu wa kudumu na vifo zinafanyika. Amewezesha OSHA kwanza kwa kupunguza tozo na kuwawezesha, amewapa magari zaidi ya 13 ili waweze kufanya kaguzi kwenye viwanda kwa lengo la kupunguza ulemavu na ajali ambazo zinatokana na kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la maendeleo ya vijana, zipo fedha ambazo zinatolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana za SDL ambapo katika fedha ambazo tumekuwa tukipata ni zaidi ya shilingi bilioni moja. Waheshimiwa Wabunge wamechangia hapa fedha hizo zipatikane, ni kweli tunaendelea na mazungumzo na Serikali na ahadi iliyopo ya Serikali kwa sasa kupitia Wizara ya Fedha ni kwamba, fedha hizi watatupatia, tayari hatua ya awali tumekwishakopesha zaidi ya shilingi bilioni 1.7 ambazo zimeenda kwa vijana kama revolving fund. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda kwenye hatua nyingine, katika mikopo hii ambayo imetolewa, miradi zaidi ya 56 ya vijana ilitolewa fedha kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na tayari vijana wanufaika ni 392, walioweza kuunda makampuni kwa ajili ya kuweza kutumia fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia yapo mafunzo ya kukuza ujuzi ambayo fedha hizi za SDL zimekuwa zikisaidia. Pamoja na watumishi wapo vijana ambao wanafanya programu ya uanagenzi, tuliweza kupeleka vijana zaidi ya 9,593 katika mafunzo. mwaka huu wa fedha 2023/2024 ambapo tunaelekea mwaka wa fedha 2024/2025, tayari vijana 6,000 ninavyozungumza wako katika vyuo mbalimbali kwa ajili ya kupata mafunzo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya ajira ndani na nje ya nchi; katika kuzingatia hilo na maagizo mahsusi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na katika utekelezaji wake kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tumekwishaanza kuingia mikataba na nchi mbalimbali za ughaibuni ikiwemo Saud Arabia na Falme za Kiarabu. Tumekwishaingia memorandum of understanding na tayari tumeshaanza kupeleka wafanyakazi kule, lot ya kwanza tulikuwa tumepata nafasi ya vijana 300 lakini walioenda ni zaidi ya 276. Tutaendelea pia kwenye nchi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshakaa na Nchi ya Austria tukafanya makubaliano. Kwa sasa tutaendelea kufungua maeneo haya ikiwa ni pamoja na kusajili mawakala wa ajira za nje ya nchi ili nchi yetu iweze kufunguka na tuweze kupata remittance ya fedha ambazo zinakuja ndani ya nchi ili kuongeza pato la Taifa kwa ajili ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado pia katika eneo hilo la ajira tupo kwenye kutekeleza maagizo mahsusi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara zote za kisekta zimeelekezwa mahsusi ziweze kila mwaka kwa fedha zinazopewa zizalishe ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Kwa kufanya hivyo tayari baadhi ya Wizara zimekwishaanza kutekeleza agizo hilo ikiwemo Wizara ya Mifugo ambapo wana BBT Life, ambapo wajibu wao ni kunenepesha mifugo, Mheshimiwa Ulega anafahamu na ameshafanya kazi hiyo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Katambi, kengele ya pili hiyo.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuwakopesha hawa vijana, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Madini na Wizara nyingine tunategemea kwamba zitafungua fursa zaidi kwa ajili ya kuongeza wigo wa ajira ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aliyoyafanya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mengi, muda hautoshi, lakini naendelea kusema kwamba mchango wangu uweze kuingia katika kumbukumbu, naunga mkono hoja, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya makubwa na ndiyo maana maneno yanakuwa mengi kwa sababu mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan achape kazi, tupo pamoja naye, maneno siyo kazi, kazi ni vitendo. Ahsante sana. (Makofi)