Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mimi leo ndiyo mara yangu ya kwanza kusimama na kuzungumza mbele ya Bunge lako hili Tukufu tangu kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, napenda kutumia nafasi hii mbele ya Bunge lako kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake na afya njema ambayo anatujalia sote na kuweza kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kubwa aliyoionesha kwangu na kunipandisha kutoka kuwa Naibu Waziri ambapo aliniteua kuwa Naibu Waziri katika Ofisi mbili tofauti, Ofisi ya Rais, Utumishi na Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, sasa amenipandisha kumsaidia kazi kama Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee namuahidi Mheshimiwa Rais, wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wabunge wote hapa ndani kwamba nitajitahidi kadri ya uwezo wangu na alivyonijaalia Mungu kuhakikisha najituma kuweza kufikia malengo ambayo yanategemewa kutoka kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru sana Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, nawaahidi kwamba miongozo yao na maelekezo yao tutayasimamia na kuyatekeleza kama vile ambavyo wanatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee natumia nafasi hii vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mabunge yote Duniani IPU, Rais wa 31, vilevile kwa kuliongoza Bunge letu hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa viwango vya hali ya juu. Aidha, nakupongeza wewe mwenyewe Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge na Wenyeviti wa Kamati kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee vilevile natumia nafasi hii kumpongeza na kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati. Bahati nzuri Mwenyekiti wa Kamati hii ni Mbunge mwenzangu kutoka Wilaya ya Chamwino ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dodoma, Mama yangu Fatma Toufiq. Nakuahidi Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati na Wabunge wote kuwapa ushirikiano wa hali ya juu na pia maoni yenu, miongozo yenu na ushauri wenu tutauzingatia katika utekelezaji wa majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ofisi hii ambayo naihudumu kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu chini ya Waziri Mkuu ni ofisi ambayo inafanya kazi kwa utatu kwa maana ya Serikali, Waajiri na Wafanyakazi. Natumia fursa hii mbele ya Bunge lako Tukufu kuwaahidi Muungano wa Waajiri (ATE), vilevile Vyama vya Wafanyakazi kupitia Shirikisho lao la TUTCA kwamba tutakuwa pamoja, tutashirikiana katika kuhakikisha utatu wetu unafanya kazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijikite kwenye hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge katika michango yao waliyokuwa wanachangia kwenye bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza ni suala ambalo ametoka kumalizia hapa Mheshimiwa Naibu Waziri, suala la ajira, kutafuta fursa za ajira kwa Watanzania. Nawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba katika hili tutafanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya kumsaidia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutafuta fursa mbalimbali ambazo zinaweza zikapatikana kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari ofisi hii imeshaingia makubaliano na Serikali ya Saudi Arabia na Serikali ya UAE katika kuhakikisha Watanzania wanapata fursa mbalimbali, skilled na unskilled labor katika nchi hizi, vilevile tunaendelea kutafuta fursa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tumeona Serikali ya Japan imetangaza ajira zaidi 12,900 kwa wageni hasa wanaotokea Afrika. Tutahakikisha tunafanya kazi usiku na mchana kuweza kupata fursa hizo kwa ajili ya Watanzania kwenda kufanya kazi katika mataifa hayo. Tumeshuhudia South Korea ikitangaza ajira mbalimbali kwa ajili ya wageni, tutahakikisha tuna tap-in katika ajira hizo ambazo zimetangazwa ili vijana wetu wa Kitanzania waweze kufanya kazi zote za skilled na unskilled. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Ofisi yetu hii ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha tunaratibu fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vijana na watu wenye ulemavu, nawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba tutafanya kazi kwa karibu sana pamoja na wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhakikihsa 4:4:2 zile fursa ambazo zipo kwa vijana basi zinawafikia na vijana wanaanzisha biashara ambazo zina tija. Tumezoea kuona zile 4:4:2 saa nyingine kila mmoja anakimbilia kwenye trend iliyokuwepo pale wakati huo, hawaangalii fursa nyingine zilizopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, unakuta vijana wa Kagera kule kwa Mheshimiwa Bashungwa, wote wanakimbilia kuwa na bodaboda ilihali ukienda kilomita chache unaweza kukuta kuna Ziwa pale. Tunaweza kuangalia ni namna gani ile 4:4:2 inawasaidia kwa ajili ya kwenda kuwa wavuvi na kuzalisha katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta katika maeneo kama ile Mikoa ya big five, vijana wote wanatafuta fursa za mikopo za kwenda kuendesha bodaboda wakati kuna fursa katika mashamba, wana uhakika wa mvua. Serikali hii kupitia Wizara ya Kilimo imejitahidi katika kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima katika maeneo hayo. Tutakwenda kuratibu ili fursa hizi ziweze kuwafikia vijana kulingana na maeneo ambayo wanatoka ili ile 4:4:2 iweze kuleta tija na ikaonekane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna nafasi kubwa ya kuweza kunyanyua entrepreneurs kwenda kuwa mamilionea kutokana na fursa mbalimbali ambazo zinatolewa na fedha za Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ukiacha fedha hizi za 4:4:2 vilevile tumeona wenzetu wa Wizara ya Kilimo wakija na BBT. Tutahakikisha tunatoa fursa nyingi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kwa vijana wengi zaidi kuweza kuingia katika BBT ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni nimekuwa nikizungumza na Mheshimiwa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Antony Peter Mavunde, wanaenda kuanzisha MBT, Mining for a Brighter Tomorrow, ambayo tutahakikisha vilevile tunaratibu vijana wengi zaidi waweze kwenda kwenye fursa hizo. Hizo ndizo kazi ambazo zinaenda kufanywa na Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha fursa hizi zinawafikia vijana wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hapa Waheshimiwa Wabunge walichangia kuhusu Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii. Kuna changamoto kubwa ambayo ipo, unakuta michango hukatwa kwa mwajiriwa lakini haifiki katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii. Mwajiriwa pale anapokuwa amestaafu ama ameacha kazi anakwenda kwenye ile Mifuko ya Hifadhi ya Jamii anakuta asilimia yake aliyokatwa yeye ile 10% ilifika, lakini asilimia ya mwajiri haikufika, saa nyingine unakuta zote mbili zile 20% hazijakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nasema mbele ya Bunge lako Tukufu, tutakuwa wakali kwa waajiri wote ambao hawatapeleka michango ya pensheni kwenye Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii. Ile ambayo inatakiwa kwenda NSSF na ile ambayo inatakiwa kwenda PSSSF ambayo inatoka kwenye halmashauri zetu na kadhalika, tutahakikisha waajiri wote wanapeleka michango ili wale Watanzania ambao wanafanya kazi waweze kupata fedha yao kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kuwahakikishia kwamba hoja zote ambazo zimetolewa hapa tumezichukua, tumezipokea na tunakwenda kuzifanyia kazi. Majibu tutaleta kwa niaba ya Mheshimiwa Spika kwenye Kamati yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Fatma Toufiq juu ya yale yote ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge hapa na namna gani ambavyo tunakwenda kuyafanyia kazi. Nawaahidi ushirikiano wa hali ya juu Waheshimiwa Wabunge wote na Ofisi yetu na sisi ambao tunamsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu tutahakikisha yale malengo ambayo ameyaweka na yale atakayokuja kutuelekeza tunayatekeleza kwa haraka zaidi na kwa ushirikiano mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii vilevile kumshukuru sana Mheshimiwa Chief Whip Jenista Joachim Mhagama, Mbunge wa Peramiho kwa ushauri wake. Nimepata bahati ya kuhudumu kama Naibu Waziri wake. Nina imani yale aliyonilea na kunifundisha, ndiyo ambayo yamenisaidia kuweza kufika hapa nilipofika leo. Kwa hiyo namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Jenista Joachim Mhagama, kwa ushirikiano mkubwa ambao ameendelea kunipa na hata sasa bado ananipa on the job training huku tunaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wote, Waheshimiwa Naibu Mawaziri wote akiwemo Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Katambi na Mbunge wa Shinyanga Mjini, kwa ushirikiano na ukaribisho ambao amenipatia kwa muda ambao nimeripoti katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Waziri, mwisho kabisa na si kwa umuhimu, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Chamwino kwa imani yao kubwa ambayo wanayo kwangu. Mpaka sasa, Jimbo liko salama, liko shwari na naendelea kufanya kazi kwa sababu wamenipa utulivu huo. Kwa hiyo nawashukuru sana Wanachamwino na nawaahidi nitaendelea kuwatumikia kadri ya vile ambavyo Mungu atanijaalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, naomba kusema kwamba naunga mkono hoja iliyo mezani ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba kuwasilisha na Ahsante sana. (Makofi)