Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwanza kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyetujalia kuifikia siku hii ya leo tunapokwenda kuhitimisha hoja yetu, tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu. Vilevile nachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Spika kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuliongoza Bunge letu Tukufu, tunampongeza sana sana Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kukushukuru sana na wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika. Wewe kwa kweli ni Naibu Spika wa viwango vya hali ya juu. Kwa hiyo tunakushukuru sana na tunakupongeza na hata leo umekalia Kiti tunapokwenda kuhitimisha hoja yetu, tunakuombea kila la heri katika majukumu yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na viongozi Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuwashukuru Wenyeviti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa wale wapya tunawapongeza kwa kuchaguliwa, lakini vilevile tunawapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuongoza Bunge hili na tunawashukuru sana kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tutakuwa hatujatenda haki kama mimi na wenzangu wenye hoja, hatutawashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge zilizojadili Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Joseph Mhagama, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na Makamu Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wote kwa kazi nzuri waliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Nyongo kwa kazi nzuri aliyoifanya pamoja na Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wengine wote. Vilevile naomba kumshukuru aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, ndugu yangu Mheshimiwa Sillo ambaye sasa ameteuliwa kuwa Naibu Waziri na kwa kweli tulifanya kazi nzuri sana. Kwa Mheshimiwa Sillo tulikwenda kupeleka Mfuko wa Bunge. Mwenyekiti wa wakati ule Mheshimiwa Sillo, alisimamia sana kuhakikisha tunaelewana vizuri kwenye Mfuko wa Bunge. Kwa hiyo namshukuru sana sana Mheshimiwa Sillo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi na shukrani za dhati sasa kwa Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa sana na kutoa maoni kwenye Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba kuungana na Mheshimiwa Waziri Mkuu, mara nyingi, kipindi hiki amekuwa akitoa pole kwa wananchi ambao wamepata maafa na hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa letu limekumbana na mvua kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kuwapa pole na naendelea kusema Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya uratibu wa Waziri Mkuu, lakini na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tutajitahidi kila tunaloweza kuhakikisha tunawafikia wale wote waliopata madhara haya. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa kuendelea kutoa taarifa za mafuriko na majanga mengine kutoka kwenye maeneo yao. Ofisi ya Waziri Mkuu iko wazi, nawakaribisha sana watuletee taarifa ili tuweze kuwahudumia Watanzania vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee, namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini kuhudumu ndani ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba kusema kwa unyeyekevu mkubwa, nitaendelea kuyatekeleza majukumu haya kadri ya Mwenyezi Mungu atakavyotusaidia. Nampongeza sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Mpango kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi kwa kazi nzuri anayoifanya na hasa katika kuwatumikia Wazanzibari. Naomba sasa kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, ndugu yetu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa. Kwa kweli namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nimehudumu katika Ofisi yake kwa kipindi cha muda kadhaa, lakini amekuwa ni kiongozi na mlezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusema namshukuru sana na ahsante sana kwa Wanaruangwa kwa kumchagua Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu kuwa Mbunge. Baada ya kuwa Mbunge, Mheshimiwa Rais amemwamini kuwa Waziri Mkuu na kwa kweli anatusaidia. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii pia, kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais. Naomba pia kumshukuru sana, toka ameingia kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, akiwa msaidizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kuwaambia Waheshimiwa Wabunge, tumeanza kuonja karama za uongozi kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakika Ofisi imeongezewa nguvu na Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko ameendelea kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu. Sisi Waheshimiwa Mawaziri ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, pia tumeendelea kukaa na Mheshimiwa Dkt. Doto akitusaidia sana kutuelekeza jinsi ya kutekeleza majukumu yetu sawasawa. Kwa hiyo naomba kumshukuru na nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani za pekee ziende kwa Mheshimiwa Hamza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, tulikuwa naye hapa asubuhi, kwa ushirikiano. Namshukuru sana sana na sasa hivi yuko hapa ndani, Mheshimiwa pacha Waziri Hamza tuko pamoja. Tutaendelea kudumisha Muungano na tutaendelea kuyasimamia majukumu yetu kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pacha wangu mwingine mpya, Mheshimiwa Deo, karibu sana Ofisi ya Waziri Mkuu naomba kumhakikishia ushirikiano. Namfahamu sana Mheshimiwa Deo, tumefanya naye kazi nikiwa Waziri wake Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Naomba kusema Wizara pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na dada yangu Mheshimiwa Joyce Ndalichako ambaye nimefanya naye kazi, namshukuru sana sana kwa kufanya naye kazi vizuri kipindi hicho ambacho alikuwa ameaminiwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwaambia wafanyakazi kwenye Ofisi hiyo ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, mdogo wangu Mheshimiwa Deo mmempata jembe la kutosha ambaye anakuja kuongeza kasi na nguvu katika shughuli zile zilizoanzwa na mtangulizi wake na naamini kabisa atakimbia na atamsaidia Mheshimiwa Rais. Karibu sana Mheshimiwa Deo na niko tayari kwa ushirikiano wa kutosha pamoja naye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Ummy Nderiananga, hakika nimepata Naibu Waziri mwenye karama za kutosha. Wanawake wa Kilimanjaro hawakukosea kumchagua. Anafanya kazi kwelikweli, ananisaidia sana, hachoki na yuko mstari wa mbele kabisa. namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, tuendelee kushirikiana. Hata hivi wanavyotuona leo tukifanana na mioyo yetu na utendaji wetu wa kazi uko pamoja, Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana mdogo wangu Mheshimiwa Katambi. Nimefanya kazi naye pia akiwa Naibu Waziri wangu, najua utendaji kazi wake, namshukuru sana kwa kazi nzuri. Hivyo basi, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu yuko Ofisini kwetu, tunamkaribisha Mheshimiwa Naibu Waziri, Judith kwa kumsaidia Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na tunamtakia kila la kheri na tumeona ameanza kazi kwa ushirikiano mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshukuru Katibu Mkuu wangu Dkt. Jim na Naibu Katibu Mkuu. Hapa kipekee namshukuru Mkurugenzi pia wa Tume ya Uchaguzi ambaye Fungu lake liko kwetu, namshukuru Msajili wa Vyama, Mheshimiwa Jaji Mtungi na timu zao zote na wataalam wote ambao wako kwenye Ofisi yetu. Ahsante Katibu Mkuu kwa uratibu lakini ahsanteni sana Wakuu wa Taasisi na Taasisi zote na watendaji na wataalam wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa siwezi kuacha kuvishukuru vyama vya siasa, na leo Baraza la Vyama vya Siasa wako hapa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa. Nawashukuru kwa sababu wameitikia vyema wito wa Mheshimiwa Rais wa zile 4Rs na wameendelea kuzienzi na kuzisimamia vizuri. Vyama vyote vya siasa nchini, nawashukuru na Ofisi yetu itaendelea kusaidiana na Msajili wa Vyama katika kulea demokrasia ambayo sasa hivi kwenye mikono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, analitendea vema na haki eneo hilo la mfumo wa demokrasia na hasa vyama vingi nchini. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii pia kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Peramiho, ahsanteni sana Wanaperamiho. Mbunge wao nipo nachapa kazi, hakuna kulala. Tunajua mwaka huu tunalo jambo letu la Serikali za Mitaa na mwakani kazi ni ileile hakuna kurudi nyuma. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mbele, Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na mimi Mbunge wao nimo. Kwa hiyo nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Peramiho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutimiza miaka mitatu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi. Waheshimiwa Wabunge wenzangu naungana na nyie, kila aliyesimama amesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni moto kweli kweli. Kwa hiyo naungana nao kumpongeza sana. Tunashukuru sana Serikali zilizotangulia na Marais waliotangulia, wamefanya kazi kubwa lakini miaka mitatu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha mageuzi makubwa sana ya maendeleo kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunasema haikuwa rahisi watu kufanya yale ambayo ameyafanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa muda mfupi. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha uzalendo, ukomavu, umahiri, ubobezi katika kuliongoza Taifa letu na katika maneno hayo hakuna mjadala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tufikirie pale alipoamua kubeba dhamana na kufanya maamuzi magumu kwenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa na kuruhusu mikutano ya hadhara, haikuwa kitu chepesi hata kidogo lakini kwa sababu Mheshimiwa Rais wetu ni mkomavu, ana uwezo, aliweza kufanya maamuzi hayo. Mnafahamu alianzisha mazungumzo ya maridhiano na vyama vya siasa na kuanzisha mijadala huru ya wazi ya masuala ya demokrasia nchini. Tunamshukuru na tunamheshimu sana Mheshimiwa Dkt. Samia kwa jinsi alivyo na anavyoweza kuongoza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakumbuka alipofanya maamuzi ya kuruhusu maandamano ya vyama vya upinzani nchini hakusita, alikuwa na courage ya hali ya juu. Kwa hiyo kwa kweli tunampongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wetu. Ndiyo maana naungana na Waheshimiwa Wabunge na nasema kwamba; sisi kwanza Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutaendelea kumuenzi na kumthamini Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatutasita kufanya hivyo na hatutasita kusema mahali popote. Wote tunafahamu maneno haya tunayoyasema Bungeni yanaungwa mkono na akinamama wa Tanzania waliokuwa hawana mahali pa uzazi salama, leo wana mahali pa uzazi salama. Wanajua alichowafanyia Mheshimiwa Rais wetu, wako nyuma yake, asisite, asonge mbele tuko pamoja naye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wakulima, nitasema hata wakulima wa Jimbo la Peramiho na Mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine nchini, wanafahamu Mheshimiwa Rais wetu alivyoondoa kero ya bei ya mbolea kwa kuipa ruzuku. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Rais, wananchi wa Jimbo la Peramiho na wananchi wa mikoa yote nchini, kwa hili la ruzuku, wako pamoja naye. Wataendelea kumuunga mkono kwa sababu amewaondolea mzigo mkubwa wakulima wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mheshimiwa Bashe amesema hapa, pamoja na kilimo hiki cha mwaka huu na hasa kwenye zao la mahindi, mavuno yatakuwa ni mengi. Mheshimiwa Rais wetu ameshahakikisha masoko ya uhakika, hao wakulima wanamuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu. Safari inaendelea na ushahidi utaonekana mwakani, Mheshimiwa Rais asonge mbele tuko pamoja naye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wa kike ambao walikatishwa ndoto zao kwa kupata mimba, leo wamerudi shuleni na wengine wamekwenda vyuo vikuu, wako pamoja na Mheshimiwa Rais na wanamuunga mkono. Mheshimiwa Rais wetu, asonge mbele na hawa wote wanamwombea na ataendelea kubarikiwa. Amepeleka umeme vijijini, ameleta tiba za kibingwa, wako Watanzania hawakuweza kwenda kutibiwa nje kwenye tiba za kibingwa; Mheshimiwa Dkt. Mollel ameeleza hapa, Mheshimiwa Rais asonge mbele, hawa ndiyo watu wake, wanamuunga mkono na watakufa naye.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko miradi mikubwa ya kimkakati. Hebu fikiria Mheshimiwa Mavunde amesema hapa leo, migodi mipya na mfumo mpya wa uwekezaji kwenye madini unakwenda kuwagusa wachimbaji wadogo wadogo. Hawa ndiyo watu wake Mheshimiwa Rais, asonge mbele na hao ndiyo watakaokuwa naye mpaka mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya kimkakati SGR, meli, viwanja vya ndege, hospitali za rufaa na mambo mengi yaliyofanyika katika Taifa letu. Tuna shida gani ya kuyasema haya hadharani na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan? Haya ninayoyasema nawaunga mkono Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Mawaziri wamesema, kwa hiyo Bunge hili leo linainuka kwa makofi na kumwombea kheri Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba yuko kwenye mikono salama kwa sababu ya kazi anazozifanya na hasa kuwajali wanyonge. Hilo ni jambo kubwa na hata Mwenyezi Mungu atampa baraka tele kwa kazi hii nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza michango mingi wakati Wabunge wakichangia hapa, labda nianze na eneo hili la dawa za kulevya. Kwa takwimu tulizonazo sasa hivi ulimwenguni, 2011 waliokuwa waraibu wa dawa za kulevya walikuwa milioni 240, lakini mwaka 2020 hadi 2022, dunia nzima waliokuwa waraibu wa dawa za kulevya walifikia milioni 296, kwa hiyo kulikuwa na ongezeko. Sasa hapa nchini Tanzania waraibu ambao wana uraibu wa mambo mengi, si dawa za kulevya peke yake, ni pamoja na ulevi na uvutaji wa sigara uliopindukia, kwa mwaka 2020 walikuwa 169,269 na kwa mwaka 2022 walifika 854,134.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kusema nini? Tunataka kusema kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kushughulika na miradi hiyo yote anapoamua kusimama na kushughulikia kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya anafanya kitu cha msingi sana katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1991 Serikali yetu ilianzisha mapambano ya dawa za kulevya kwa kutengeneza Kitengo Maalum ndani ya Jeshi la Polisi; lakini tulivyofanya tathmini tukasema ni lazima tuongeze nguvu zaidi. Mwaka 1997 tukaanzisha Tume ya Uratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya, lakini vilevile tulifanya tathmini tukasema tusonge mbele. Mwaka 2015 tulianzisha sheria ambayo ndiyo imeunda mamlaka tuliyonayo na mwaka 2021/2022, Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema ni lazima tufanye marekebisho kwenye vifungu kadha wa kadha ili tuongeze nguvu kwenye mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Naomba niwaarifu Waheshimiwa Wabunge kwamba mwaka huu 2024 tunakuja na sera itakayotusaidia kutoa matamko makali ya kupambana na matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ziko changamoto ambazo tunaziona. Uzalishaji wa dawa humu nchini unazidi kuonekana upo na unashamiri. Tumeshuhudia mamlaka ikipambana kuteketeza mashamba ya bangi, kemikali bashirifu zikitumika na kuingizwa nchini kwa kificho ili ziweze kutengeneza dawa, vijana wadogo wakiathirika pamoja na matumizi ya digital currency katika kutakatisha fedha hizo ambazo zinatumika katika biashara haramu ya dawa za kulevya. Naomba niwahakikishie, chini ya uongozo mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejipanga kuhakikisha vita hii inakuwa ni vita ambayo tutaiweza na tutafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeamua kuimarisha sheria na kutengeneza sera mpya itakayotusaidia kupambana na dawa za kulevya nchini. Sera na sheria hizo zinatakiwa zitupeleke katika kufanya utafiti, kujitambua tuko wapi hali yetu na kila kitu tunachotakiwa kufanya, udhibiti na kutoa elimu ya kutosha. Waheshimiwa Wabunge tuna kazi ngumu ya kutengeneza kinga kwa watoto wetu kutokujiingiza kwenye tatizo la matumizi ya dawa za kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia biskuti zikizalishwa zina kilevi cha dawa za kulevya na hasa bangi, ni hatari sana kwa makuzi na maadili ya watoto wetu. Kwa hiyo tunahitaji nguvu ya pamoja Serikali na private sector tufanye kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru Mheshimiwa Rais katika kipindi hiki kifupi tumeweza kuongeza MAT Clinics zile Medical Assistants Therapy Clinics kutoka 11 mpaka kufika 16. Hilo ni ongezeko kubwa Waheshimiwa Wabunge na tumeona waraibu karibu 16,000 wameanza kujitokeza ili kupata dawa. Ukiona waraibu wanaongezeka kwenye vituo vya kupata tiba maana yake ni kwamba mtaani sasa hivi dawa za kulevya zimepungua. Hongera sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kuweza kudhibiti jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tuna sober houses 54 na nilimsikia Mheshimiwa Esther Bulaya akitu-challenge, kwamba kwa nini tuwe na hizo sober house na vitu vya namna hiyo. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, historia ya sober house hapa nchini ina maneno yake mengi. Kitu kinachotufurahisha sisi Tanzania tumekuwa ni nchi ya kwanza kuanzisha tiba kupitia sober house katika Ukanda wa South Sahara na hii imetupa heshima kubwa sana. Kwa hiyo ni lazima wakati mwingine tuendelee kusifia mambo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hiyo tumeamua kujipanga kutekeleza mikakati ya kimataifa na mkakati wa kwanza wa kimataifa ni kuhakikisha kwamba tunashughulika na supply reduction, kwa maana ya kupunguza uingizaji wa dawa nchini. Pia tunashughulika na kupunguza uhitaji (demand reduction), tunashughulika na kupunguza madhara (harm reduction) na vilevile tunakwenda kushughulika pia na mahusiano ya kikanda na mahusiano ya kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa mafanikio ambayo tumeyapata kama Serikali, ongezeko la watumiaji hao wa tiba kwenye MAT clinics zetu. Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani tumefanikiwa. Mpaka sasa tumekwishakamata kemikali bashirifu kilogramu 22,143 ambazo zingeingia mtaani zingetengeneza dawa na zingeharibu watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya vilevile ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya za aina mbalimbali. Kwa mwaka mmoja tu wa 2023 mamlaka imeweza kukamata kilogramu milioni 1.9 ya dawa mbalimbali. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba hicho ni kiwango ambacho ni mara tatu ya ukamataji ambao umefanyika nchini kwa kipindi cha miaka 11, hiyo ni kazi kubwa ambayo imefanyika. Wengine wanasema sababu ni ongezeko la uingizaji wa dawa, hapana, ni kwa sababu Mheshimiwa Rais amekuwa na utashi wa kutosha kwenye mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeboresha sheria, na Mheshimiwa Rais ameamua kutoa fedha na kununua vitendea kazi na hapa ninapowaambia tumeingiza boti moja mpya ambayo inaweza kufanya kazi mpaka kwenye Bahari Kuu na kukamata majahazi huko yanakotokea. Tumefanya mafunzo na tunategemea uzalendo walionao watumishi wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti na Dawa za Kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana mwezi Desemba dawa za kulevya zilikamatwa pale Dar es Salaam, zilinunuliwa kwa fedha za Kitanzania zenye thamani kama ya bilioni 40. Kama zisingekamatwa na zikauzwa wafanyabiashara haramu walikuwa wanakwenda kupata bilioni 95, fedha za Kitanzania. Sasa tufikirie ndani ya Taifa bilioni 95, fedha haramu ingeingia humu ndani ingekuwaje? Ingekuwa ni kazi kubwa, lakini kwa sababu ya uzalendo wa watumishi wetu, hilo jambo walifanikiwa, hawakutaka rushwa, walisimama imara, wakafanya kazi zao vizuri. Kwa hiyo tutaendelea kuona ni namna gani tunasimamia eneo hili. Faida za kufanya hii kazi ni kuokoa nguvu ngazi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, vijana wa Tanzania wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni 20,612,566. Hawa tusipowalinda kutokana na madhara ya dawa za kulevya, tutakuwa tumeangamiza kizazi. Masuala ya afya na masuala mengine ni muhimu sana kuyaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea na suala la elimu, Waheshimiwa Wabunge wameniandikia kwamba mnawezaje kuwatambua waraibu wa dawa za kulevya. Tumekuwa tukiangalia tafiti nyingi zinatuongozaje, kwa mfano, wale ambao wamebobea kwenye matumizi ya bangi, macho yao yanakuwa mekundu sana, wanakuwa na tabia za kucheka cheka hovyo, wanakuwa na hasira za haraka, wanaongeza hamu ya kula chakula na wanakuwa wagonjwa wa akili. Kwa hiyo ukianza kutathmini hizi na ukaangalia uhalisia unaweza ukawafahamu. Kwa wale wanaotumia heroine na wenyewe kwa mfano wanakuwa na macho yaliyosinyaa, lakini pua zao zinakuwa nyekundu kwa sababu ya kunusa nusa sana, wanakuwa wachovu, wanapoteza uzito, wanakabiliwa na maradhi mengine. Kwa hiyo, kazi hiyo tutaifanya vizuri na tutaendelea kuangalia namna bora ya kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko eneo lingine la kuunganisha Mifuko, tumeliona na Waheshimiwa Wabunge wamesema, tunaomba tuwahakikishie kwamba jambo hili tunalifanya kwa uangalifu mkubwa. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba Mifuko hii iendelee kutoa huduma na kuwawezesha wananchi wa Tanzania na hasa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Mifuko mingi ilikuwa inashia mijini na sasa tunataka vijijini kwa kuwa kule ndiko kwenye uzalishaji na tunahitaji ibadilishe hali ya hewa mpaka huko vijijini. Tunayo mengi ya kueleza lakini naomba tu… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kengele ya pili hiyo…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: … tunayo mengi ya kueleza, lakini naomba niwahakikishie kwamba tutatoa majibu yetu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba, tunawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri wanayoifanya kwenye Majimbo. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais na sisi tunapokea pongezi za Wabunge. Pongezi hizo walizotupatia zinatupa changamoto ya kuendelea kupambana, kufanya kazi kwa utii na uaminifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)