Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa ulinzi sasa hivi tuko mahali hapa, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya katika nchi yetu. Naomba nimshukuru sana Waziri wetu wa Maji pamoja na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. Naomba niwashukuru sana kwa kazi kubwa na kuwapongeza kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya katika Wizara ya Maji pamoja na shughuli zote ambazo zinazoendelea pamoja na Wizara zote mbili ambazo tunazisimamia sisi Kamati ya Maji na Mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kupitia Azimio letu la Kamati. Naomba nimpongeze Mwenyekiti wetu wa Kamati pamoja na Wajumbe wote wa Kamati kwa ujumla kwa mchanganuo ambao wameuonyesha kuhakikisha Azimio hili linawatendea haki Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianze kwa kuanza na uchimbaji wa visima vyetu vya maji katika nchi yetu ya Tanzania. Wizara inajitahidi kuchimba visima katika vijiji pamoja na vitongoji; lakini tatizo tunachimba visima vile hatuvijengi hapohapo tunaviacha vinakaa muda mrefu, vingine vinakaa miaka. Sasa nilikuwa naomba Serikali ichukue jukumu la kuhakikisha inachimba vile visima na bajeti yake inakuwepo moja kwa moja, visima vinachimbwa na bajeti yake inakuwepo moja kwa moja ili wananchi wale waweze kupata maji kwa uhakika zaidi kwa wakati ule ule. Kwa sababu, tunakwenda tunachimba visima wale wanachi wanapata hamu ya maji halafu tunafunga matokeo yake wanakaa muda mrefu hawapati maji matokeo yake wanakata tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Wizara safari hii basi tuhakikishe tunatenga bajeti yetu pamoja na gharama za uchimbaji viende kwa wakati mmoja. Ninajua ndani ya nchi yetu ya Tanzania kuna vyanzo vingi vya maji lakini uharibifu umekuwa mkubwa sana na kutengeneza mazingira, mazingira yote ni mtambuka sisi sote tunahitaji mazingira yakae vizuri, tunaharibu vyanzo vya maji wananchi sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninaomba, kwa sababu sisi sote tunatakiwa tulinde mazingira yetu na vyanzo vya maji. Ninaomba Wizara kama ya maji iendelee kusimamia vile vyanzo vya maji vyote kuhakikisha haviharibiwi na wanadamu. Kwa sababu wanadamu na wanyama tunaharibu sana vyanzo vya maji matokeo yake maji yanapotea. Sasa tufanye na sisi kama Wizara ya Maji kuhakikisha vile vyanzo vyote vya maji tunavilinda kuhakikisha tunapata maji safi na salama kwa ajili ya Watanzania wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba nichangie kuhusu masuala ya Wakandarasi. Tunao wa Ndani na Wakandarasi wa Nje. Wakandarasi hawa tunawarudisha nyuma sisi wenyewe, hatuwalipi malipo yao kwa wakati. Nilikuwa naomba sana Wizara, tunajua mnafanya kazi kubwa nzuri sana tunaomba basi hawa Wakandarasi hasa hususani wakandarasi wa ndani, wapewe uwezo mkubwa kuhakikisha wanafanya kazi vizuri zaidi kuhakikisha miradi yote ambayo wanayopewa wanaitendea haki Watanzania wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu uchimbaji wa mabwawa. Mwaka huu tumeona maji ni mengi sana, kama tungekuwa na mabwawa tungehifadhi maji mengi. Na lingine kama haya maji tungekuwa tunayatumia vizuri tungeendelea kuhifadhi maji kupitia mvua zetu hizi. Kwenye sehemu za ukame, katika nchi yetu ya Tanzania kuna sehemu za ukame hazina maji basi kipindi hiki cha mvua kungekuwa kuna mabwawa tungekuwa tunajua kutunza maji ya mvua nafikiri ukame ungepotea katika maeneo yale ya ukame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Serikali ichukue jukumu la kuendelea kuchimba mabwawa na kuhakikisha wanahifadhi maji ili Watanzania waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mita. Kwanza naomba niwapongeze DAWASA, kwa kazi kubwa nzuri ambapo wameanza kuweka mita kwa Watanzania, baadhi, na sasa hivi wako kwenye testing ya kuhakikisha Watanzania wengi wanapatiwa mita ili waweze kulipa kupitia mita. Mimi nilikuwa naomba niishauri Serikali mita ni nzuri kwa sababu tumeona kwa upande wa TANESCO LUKU zinafanya kazi vizuri, na ingekuwa vizuri zaidi kuliko kuhangaika na ulipaji wa maji ilhali kuna walipaji sugu. Wizara, ichukue jukumu la kuhakikisha watanzania wote wanawekewa mita za maji ili waweze kulipa kwa usahihi zaidi. Ile kuhangaika kupeleka bili, kuhangaika kupeleka nini tuache, tuwawekee mita, kwa sasa hivi tuanze miji mikubwa. Tukiweka kwenye miji mikubwa basi itatupa unafuu na kulipa kwa urahisi. na vilevile, kwenye mashirika yanayotusumbua, Wizara zinazotusumbua tuziwekee mita ili ziweze kulipa kupitia mita, wawe wananunua moja kwa moja; hii ni kuhakikisha kwamba maji bili zake zinakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu ya Tanzania tuna mapori mengi. Mapori yale tunaona manufaa kuna Halmashauri zinanufaika kama kwetu Katavi, kuna Halmashauri ya Tanganyika inanuafaika sana na Carbon, na ukizingatia Carbon inatoa manufaa makubwa sana kwenye Halmashauri zetu; na ukiangalia sehemu kubwa ya nchi yetu ya Tanzania tuna mapori. Nilikuwa naomba Serikali ibebe hili jambo kwa uzito wake kitaifa ili wale ambao wenye misitu mikubwa basi tuwekeze uuzaji wa Carbon ili manufaa katika nchi yetu yaweze kuwa makubwa. Kwa sababu tumeona zile Halmashauri ambazo zinauza Carbon zina manufaa makubwa; wana uwezo wa kujenga zahanati, wana uwezo wa kujenga vituo vya afya, wana uwezo wa kujenga shule za msingi na sekondari. Yale maboresho madogo madogo kama Halmashauri wanaweza kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukichukua hili jambo kwa uzito wake kwa ajili ya kuuza Carbon nafikiri tutapata manufaa makubwa sana katika nchi yetu na yale matatizo madogo madogo yanaweza kupungua sana katika jamii yetu. Naomba nikushukuru, naomba niunge mkono hoja katika Maazimio haya ya Kamati. (Makofi)