Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. Kwanza kabisa naomba nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan; na mimi nimekuwa nikisema ni Daktari bingwa duniani, kwa nini? Ni kwa sababu azma ya kumtua Mama ndoo kichwani ni ya kwake tangu alipokuwa Makamu wa Rais, na sasa anaendelea kuitekeleza akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, ni yeye kama Mama anawiwa kuona kabisa adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa akina Mama wa Kitanzania, inaendelea kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Sita kama nilivyotangulia kusema. Pia nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu, mdogo wangu, Mheshimiwa Aweso, Mheshimiwa Maryprisca na Watendaji wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Taarifa ya Kamati umeona yapo mafanikio; nitaje machache; kwa mfano, upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa sasa imefikia vijiji 9,670 kati 12,318, sawa na asilimia 77. Tunajua Ilani inataka kuwa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama vijijini hadi mwaka 2025 kufikia asilimia 85, ni imani yangu Wizara hili inalimudu kama ambavyo Mheshimiwa Aweso, amesema yeye anaisikia ile mihemo ya wagonjwa kwa hiyo hili atalimudu kuhakikisha asilimia hiyo inafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika taarifa ya Kamati imeonyesha pia kwamba Wizara imeanza kushughulikia vizuri miradi mikubwa ikiwemo Uchimbaji wa Bwawa la Kidunda, ambao umefikia asilimia 15, kwa fedha bilioni 329 ambazo ni fedha za ndani, lakini Ujenzi wa Bwawa la Farkwa umeanza, lakini mahususi Mradi wa Makonde, kule Mtwara ambao umekwamuliwa tangu mwaka 1972 kwa bilioni 84.7 unaendelea vizuri; niombe Wizara kuongeza kasi ya ufuataliaji. Pia na Mradi wa Mangaka, maji kutoka Mto Ruvuma wa bilioni 38 unaotekelezwa na Wizara unaendelea vizuri, tunaona na mabomba yameshafika. Kwa hiyo, hiyo kwa kweli ninakupongeza Mheshimiwa Waziri, kwa kazi nzuri. Hata hivyo, ni jukumu letu sisi kuisimamia Serikali lazima tukupe maeneo ambayo unahitaji kuongeza msuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwa upande wa Sera ya Maji. Sera ya Maji ya Mwaka 2002, inaelekeza kuwapatia wananchi maji kwa umbali usiozidi mita 400. Sasa ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wakati wa bajeti kila mmoja alikuwa anaomba hii Sera itekelezwe, lakini naiona changamoto ya utekelezaji wa hii, ni kwa sababu pia kuna uhuru wa wananchi kwenda kujenga makazi kwenye maeneo ya mbali pengine hata na vile Vijiji vya Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pengine hapo ndipo tuna ile hoja ya mifumo kusomana. Serikali za Mitaa inapotoa vibali za uanzishwaji wa vitongoji izingatie. Kwa kweli nchi yetu ni kubwa unakuta kuna nchi nyingine za jirani hapa zinaingia mara tatu, mara nne. Kwa hiyo, Serikali kuhakikisha inapeleka mahitaji haya ya maji kwenye maeneo yote ambako wananchi wanajenga pengine itakuwa ni ngumu, lakini mimi naamini Wizara, zikisomana hili litarahisisha sana kuona upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama unapatikana kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja za Kamati ya Maji na Mazingira. Kama ambavyo Kamati imewasilisha Maazimio na mimi naomba niunge mkono hoja na nisisitize kwenye maeneo machache yafuatayo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, mitambo 25 ya kuchimba maji iliyopelekwa Mikoani. Kamati imeeleza vizuri sana, kwamba kama hii mitambo 25 imeenda kule tulikuwa tunaamini itafanya kazi na upatikanaji wa maji sasa utaongezeka kwenye maeneo yote lakini inaonekana baadhi ya majimbo ama wilaya hawajachimbiwa kisima hata kimoja. Kamati imeeleza vizuri sana Serikali ifanye tathmini kupitia majimbo yote ili ionekane bayana; yale majimbo ambayo visima havijachimbwa kupitia hii mitambo basi wapewe kipaumbele na hivyo tunaweza kuwa na uwiano ulio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo Kamati pia imeliomba Bunge, likubali kuazimia ni mchakato wa uanzishwaji wa Grid ya Taifa ya Maji. Hili Kamati ya Maji na Mazingira imekuwa ikilisema mara nyingi na pengine niombe sasa, kwa kuunga Azimio hili, Wizara iharakishe huu mchakato wa uanzishaji wa Grid ya Maji ya Taifa, itarahisisha sana. Sasa pengine tunaweza tukaanza kuweka tu msingi wa kuona; kwa mfano Serikali imeweka nguvu kubwa katika kutupatia maji kutoka Ziwa Victoria, yanakuja mpaka Ukanda wa Kati, lakini tunalo Ziwa Tanganyika upande wa Magharibi, kule Kusini tunalo Ziwa Nyasa, na Mto Ruvuma uko kwenye master plan, Pwani lipo Bwawa la Kidunda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikiweka msingi na kuweka Grid italeta usawazishwaji, uwiano wa upatikanaji wa huduma ya maji. Hivyo, itarahisisha sasa maeneo yote yanaweza kwa wakati mmoja ikaona ina unafuu wa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama na hasa kwa kuzingatia maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, Kamati imeeleza wazi kwamba hakuna Mwongozo wa Kitaifa wa Uvunaji Maji. Naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Anna Lupembe na sasa hivi mvua nyingi zinanyesha kila eneo ukipita kuna maji yametapakaa. Ni muhimu Serikali ikaweka Mwongozo wa Kitaifa wa Uvunaji Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mara nyingi wataalam ukiwauliza wanasema ni gharama kubwa kuchimba malambwe ya kukusanya maji. Sasa lazima tusikimbie hizo gharama kuna gharama ya kutafuta maji chini ya ardhi kwenye maeneo ambayo maji hayapatikani, ni rahisi kutumia maji ambayo Mwenyezi Mungu, ametupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kila siku hapa majibu yanakuja tumeanza kwenye taasisi za Serikali. Tuanze kwa kuangalia hata yale maji ya kuyavuna ya mvua ya juu ni taasisi ngapi imeweka na ni lita ngapi zinakusanywa? Kwa hiyo ni muhimu ili likawekewa Mwongozo ili nchi nzima sasa badala ya haya maji yakaendelea kupotea huko chini tukawa tunayavuna na tukaondokana na hii adha ya upatikanaji wa maji safi na salama wakati wa kiangazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba, Kamati imeeleza vizuri, kwamba hakuna msisitizo wa utumizi wa wakandarasi wa ndani. Naunga mkono maelezo yote ya Mheshimiwa Anna Lupembe, mimi naomba nisisitize; pamoja na wakandarasi wa ndani ambao kwa sasa hivi kwa kweli hatuwezi kulalamika kwamba hawapewi kazi, wanapewa; changamoto ni upatikanaji wa fedha kwa haraka ili watekeleze hiyo miradi na ili waweze kwenda kutekeleza kwenye maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi liliulizwa swali hapa kwamba Serikali inasemaje kwamba kama Benki inaamua sasa, kwa sababu hawa wakandarasi wengi wamekopa na hivyo wasipolipwa inakuwa ni changamoto nyingine na wenyewe kufilisiwa, lakini mimi naomba niongeze hapa pamoja na kutumia wataalam wa ndani. Katika kazi zetu za Kamati tulitembelea kule Manyara tulikuta mradi mkubwa kabisa umetekelezwa na Wataalam wa Ndani. Juzi tuliona Tabora kuna bwawa limekarabatiwa lilijengwa mwaka 1958 limetimiza miaka 60 limekarabatiwa na watalaamu wa ndani. Hapa tunaiomba Serikali kusisitiza kutumia wataalam wa ndani ili waweze kuanzisha miradi mipya na kukarabati miradi ya zamani na hiyo itaipunguzia Serikali gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kazi zetu za Kamati tulitembelea kule Manyara tulikuta mradi mkubwa kabisa imetekelezwa na Wataalam wa Ndani, juzi tuliona Tabora kuna bwawa limekarabatiwa lilijengwa mwaka 1958 limetimia miaka 60 limekarabatiwa na watalaamu wa ndani. Hapa tunaiomba Serikali kusisitiza kutumia wataalam wa ndani ili waweze kuanzisha miradi mipya na kukarabati miradi ya zamani na hiyo itaipunguzia Serikali gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miradi mikubwa unakuta mkandarasi wa nje anaweka billions of money, hela nyingi Mzee wetu hapa anasema; “ma-bi” kwa “ma-bi” lakini wataalamu wa ndani wakifanya mradi ule inatumia labda robo ya fedha za mkandarasi wa nje. Kwa hiyo, ni muhimu kabisa hilo likasisitizwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)