Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana angalau kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mfumo mzima wa miradi ya REA. Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini alifika Jimboni kwangu, wakati anakuja kusuluhisha mgogoro wa Saza nashukuru sana angalau sasa hivi mgogoro umemalizika, japo yapo mambo madogo madogo ambayo nadhani mimi na wewe tunaendelea kuya-solve pole pole, kwa sababu migogoro ya wachimbaji wadogo wadogo, haiwezi kwisha leo wala kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mfumo wa REA, kwenye Jimbo langu la Songwe, kwanza Awamu ya Kwanza sikupata kijiji hata kimoja. Awamu ya Pili nimekuja kupata vijiji vinne; na sijajua hii Awamu ya Tatu, nitapata vijiji vingapi. Naweza kusema ni kama kuna upendeleo fulani hivi, kwa sababu wakati ule wana-sort kwenye Awamu ya Kwanza, walipokuwa wakiandika tu neno Chunya, basi REA vijiji vingi vilienda upande mmoja kwa Mheshimiwa Mwambalaswa, Mbunge wa Jimbo la Lupa. Jimbo la Songwe sikupata kijiji hata kimoja. Baadaye nikawa nimeenda pale Mkoani Mbeya nikaambiwa basi angalau utapata baadhi ya vijiji kwenye Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Pili mwaka 2012 Mheshimiwa Simbachawene alipokuwa Naibu Waziri wa Wizara hii, alitembelea Jimbo langu tukaja tukaandika vijiji kama 15, lakini mpaka hivi ninavyosema ni vijiji vinne ndiyo angalau kuna nguzo na waya lakini hata matransfoma bado na vijiji havijaanza kuwaka. Kwa hiyo, Jimboni kwangu niseme katika huu mradi, hata kijiji kimoja umeme haujaanza kuwaka; toka Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, leo tunakwenda kwenye Awamu ya Tatu. Jamani ninaposema kwamba kuna upendeleo katika baadhi ya maeneo, huo ni upendeleo wa waziwazi Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba hata kama kesho utakapokuwa unatoa majibu, hebu turidhisheni sisi ambao Awamu ya Kwanza tulikosa na Awamu ya Pili bado vijiji ni vichache. Basi kwenye Awamu ya Tatu mtujazie vijiji vingi tuweze kulingana na wenzetu ambao mliwapa Awamu ya Kwanza na Awamu ya Pili; kwa kweli inasumbua sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata yule Mkandarasi ambaye amekaa kule Mbeya, SINOTEC yule Mchina, sijui kama ameshindwa kazi, lakini Mheshimiwa Muhongo kwa namna ninavyokufahamu, Waziri uko makini na unachukua hatua pale pale unapoona mtu anakosa, njoo Mbeya utembelee maeneo yale ya Chunya, utakuta kabisa yule mkandarasi labda ameshindwa kazi. Si afukuzwe tu wapewe watu wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji 12 ni vijiji vinne tu na sijajua maeneo ya kwa mama Mbene kule Ileje kama nako kuna kazi zinafanyika. Wapeni wazawa basi hizi kazi kuliko kuwapa Wachina hizo tender. Wapeni wazawa, mbona wanaweza wakafanya kazi vizuri? Hali ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile niongelee upande wa madini. Nadhani kwa Mkoa wa Mbeya Jimbo langu ndiyo lenye migodi mingi kuliko sehemu nyingine, ama tuseme Mkoa mpya wa Songwe, nina migodi karibu 12. Naomba niongelee kitu fulani kinaitwa 0.03 ambayo inaenda kwenye Halmashauri, tunaita service levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hii inapokuwa calculated, watu wa Halmashauri wanakuwa hawapo, kwa sababu pale panakuwa pana TMAA, panakuwa na watu wa TRA, lakini vile vile panakuwa na mmiliki mwenyewe wa mgodi, kama kule kwangu niseme labda moja kwa moja Shanta. Mtu wa Halmashauri anayewakilisha kwamba sasa yule ndiye mzawa, mwenye mgodi mwenyewe anakuwa hayupo pale ambapo unakuta ndege inakuja, inachukua dhahabu, TRA yupo, TMAA yupo, lakini mtu wa Halmashauri anakuwa hayupo.
Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba turekebishe sheria hiyo, kwa sababu tunaibiwa. Mnatupa asilimia 0.03 lakini hatujui ni ya nini kutoka kwenye nini, kwenye mapato gani? Nadhani hata wenzangu wenye migodi kama mkiliangalia hilo, ni kama vile tunaibiwa. Labda Mheshimiwa Waziri uje utufafanulie vizuri juu ya hilo jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba niishauri Serikali, mtueleweshe vizuri, Ile service levy mnayotupa kwenye Halmashauri, ile ela imetoka kwenye mapato ya nini? Sasa kwa nini ndege inapokuja pale Saza, inachukua madini, TRA yupo, anawakilisha Serikali Kuu, TMAA yupo, naye anawakilisha Serikali Kuu, lakini mtu wa Halmashauri anakuwa hayupo, kama yupo labda yupo Afisa Madini ambaye naye sio mkazi wa maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka sisi wakazi, maana yake Baraza la Madiwani liteue labda Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha wa Halmashauri, awe anakuwepo pale ambapo ndege inakuja inachukua dhahabu na yeye yupo, tuweze kujua kwamba basi kama ni bilioni kadhaa, ndiyo una-calculate sifuri nukta sifuri tatu ndiyo imechukuliwa hapa, ndio inakuja kwenye Halmashauri, ningependa sheria hiyo kidogo tuweze kuirekebisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sikuwa hata nimesomwa kwamba nitaweza kuchangia leo, nimesomwa tu huku nimetoka kusalimia huko, nilikuwa natembea kidogo nimetoka nje, lakini nilikuwa nimejiandaa angalau mambo mawili haya niweze kuchangia Wizara hii. Ahsante sana.