Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja zilizopo mezani. Nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti ambao wamewasilisha hoja zote na hasa nimpongeze Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kwa wasilisho zuri na hoja zote ambazo zimepitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaanza na Jeshi la Zimamoto; hakuna yeyote aliyopo hapa ama waliopo nje ya hapa hawajui umuhimu wa Jeshi hili na Zimamoto na Uokoaji. Jeshi hili lina umuhimu mkubwa sana, lina watendaji ambao wana weledi na wameweza kupatiwa mafunzo ambayo yanatakiwa kwa fani yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumza hivi kwa sababu tumeona kuna majanga mengi ambayo yanatokea. Tuliona majanga yalitokea Mkoa wa Manyara tunawapa pole wenzetu kwa yaliyowakuta, lakini tumeona majanga ambayo yametokea Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya mafuriko na tunaona mara nyingi majanga mbalimbali ya moto ambayo yanatokea kwenye masoko yetu na maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ndilo linatakiwa kuwa mstari wa mbele kufanya kazi hizi, lakini jeshi hili linakutwa na changamoto kubwa sana ya vitendea kazi. Jeshi hili lina upungufu wa Maafisa zaidi ya 3,519, hao Maafisa ni pungufu ambao wanatakiwa waende wakafanye kazi hizo kama nilivyoainisha. Pia, tuna upungufu wa kibajeti, kwa bajeti iiyopita hii ya mwaka huu ambayo walitengewa shilingi bilioni 9.9 kwa ajili ya fedha za maendeleo hadi ninavyozungumza hapa lakini mwezi Disemba kulikuwa ni sifuri, hakuna fedha iliyopelekwa mpaka mwezi Disemba! Sasa hawa watu watafanyaje kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana unakuta malalamiko yanakuwa mengi, hawa wanaonekana hawatendi kazi lakini wanashindwa kutekeleza wajibu wao kwa sababu fedha hizo hazipelekwi. Kwa hiyo, hiyo ni changamoto kubwa sana kwa Jeshi letu, wanakuwa na weledi mkubwa wa kutaka kufanya kazi lakini fedha haziendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona wana mahitaji makubwa ambayo yanatakiwa, kuna ukosefu wa magari ya zimamoto. Hapa Mheshimiwa Naibu Waziri kila siku anaulizwa maswali hapa lini tutapelekewa gari Zimamoto Wilaya kadhaa, Mikoa kadhaa. Tuna ukosefu wa magari ya zimamoto kwa Wilaya 120 za nchi yetu, lakini tuna ukosefu wa helikopta, tuna ukosefu wa boti 38 zinahitajika, tuna ukosefu wa magari ya ngazi haya ni muhimu sana zaidi ya 28 na mengine mengi na mitambo na kadhalika. Hivi vyote wanashindwa watavipataje kwa sababu hakuna fedha zinazokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe Serikali hasa Wizara ya Fedha, Wizara ya Fedha iweze kupeleka fedha katika Jeshi letu la Zimamoto ili tujenga taswira chanya ya Jeshi hili. Taswira iliyopo nje ni Jeshi halitekelezi wajibu wake lakini tunaomba Wizara ya Fedha ipeleke fedha jeshi letu lifanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala jingine ninalokwenda kuliongelea ni swala ambalo lipo kwenye ukurasa wa 34 wa taarifa ya Mambo ya Nje ambayo inahusu tathmini inaonesha kwamba kuna ongezeko kubwa la uhalifu dhidi ya binadamu ikiwepo ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Ninazungumza hili kwa uchungu mkubwa kabisa, kuna biashara ambayo imeanza na ipo kwa nchi yetu pia, kuna biashara kuu tatu haramu. Kuna biashara za madawa ya kulevya, kuna silaha lakini biashara ya binadamu ni biashara ya tatu kwa ukubwa. Hii inaonekana katika nchi yetu kwa maana kwamba kuna ma-agent ambao sijui kama Serikali inawatambua, kama inawatambua watuambie hao ma-agent wanakwenda kurubuni vijana wetu hasa mabinti na watoto hata watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawachukua kutoka vijijini wanawaleta mijini, wanawafanyisha kazi na wale ma-agent wanataka kupata pesa. Mfano Mkoa wa Dodoma kwa tafiti imeonyesha kwamba inatoa watoto wengi wanaokwenda kusaidia ombaomba kwa Mikoa mikubwa kama ya Dar es Salaam na mingine ambapo wanawasaidia kwa ajili ya kuomba na wanawalipa wale waliowabeba wanawekwa kwenye majumba ambayo hawako salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna Mkoa wa Simiyu unaongoza kwa kuchukua watu wenye ulemavu na kuwapeleka kwenye miji mikubwa ambapo wakiwafikisha kule wale wanawachukua wanawaweka kwenye nyumba; wanawapeleka asubuhi kwenda kuomba na jioni wanarudisha pesa kiasi kwa wale waliowapeleka. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwa kweli iangalie jambo hii ni jambo linaumiza, ni jambo linawaumiza vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo two-way traffic wengine wanatoka nje wanaletwa hapa nchini, tuliona wananchi kutoka Asia waliingia lakini kuna wanaowatoa pia hapa ndani na kuwapeleka nje ya nchi, wakifika huko nje ya nchi wananyang’anywa passport, wanatendewa matendo magumu sana. Niombe Serikali iwe na mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba suala hili linadhibitiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza majeshi yetu yanafanya kazi kubwa sana, wanafanya kazi kubwa sana. Tumeona nchi yetu ina amani, ninawapongeza Kikosi cha Mzinga ambacho wanafanya kazi kubwa mno. Wamefanya utafiti wa kutengeneza bomu ambalo litafukuza wanyama wakali wakiwemo tembo. Kikosi hiki kimefanya hiyo kazi niwaombe washirikiane na Wizara ya Maliasili kuhakikisha kwamba wanatumia mabomu hayo ili wananchi wetu waweze kunusurika na adha kubwa ya wanyama wakali ambao wanatuzingira huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Disemba mwaka jana waliomba bilioni nne hawakupata hata shilingi moja hawa. Kwa hiyo, ninawaomba Serikali pelekeni fedha majeshi yetu yafanye kazi kwa weledi mkubwa, wanafanya kazi lakini katika mazingira magumu. Mnajua hawa watu huwa hawawezi kuzungumza wenyewe lazima tuwazungumzie hapa ili muwape pesa wafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Jeshi la Magereza, Jeshi la Magereza wanafanya kazi kubwa. Nilikuwa najiuliza hivi Magereza nao wanakuwa treated kama wafungwa? Kwa sababu wanafanya kazi kubwa. Ukienda Magereza ukaona kazi wanayofanya Jeshi la Magereza, kwa wale wahalifu ambao ni wahalifu hasa unawahurumia hawa Jeshi, basi muwaangalie angalie muwalipe pesa zao, maslahi yao kwa wakati na stahiki zao kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafanya kazi ngumu sana na yenye kujitolea ziadi. Pia, tumeona Magereza muda wote tulikuwa tunasema kuna mlundikano lakini sasa hivi ina wafungwa 17,969 na mahabusu 9,154 ambao jumla yake ni 27,123, ukiangalia uwezo wa kuhifadhi wahalifu ni 29,902 kwa hiyo ina maana kuna upungufu. Tunamshukuru na tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuwafanya Mahakama kuhukumu kesi zao kwa wakati na kupunguza lile ombwe ambalo Magereza walikuwa wanapata shida sana ya kuweza kuwalisha wafungwa wakiwa mule ndani, kwa hiyo hilo ni la kuwapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC); kituo hiki kinafanya kazi kubwa na kipo pale, kina maeneo mengi lakini tumeona kwenye taarifa yetu maambo yaliyoainishwa. Mimi napenda kusema wanayo madeni takribani bilioni 5.2 ambayo wanaidai Serikali. Serikali mkawape hela ili hiki kituo kifanyekazi hata Wizara ya Mambo ya Nje inadaiwa, naomba mpeleke pesa katika kituo hiki ili kiweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)