Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia, nami mchango wangu utajielekeza katika Taarifa ya Kamati ya NUU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ningependa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo Tanzania imeendee kufunguka na jinsi ambavyo tunaimarisha diplomasia ya kiuchumi. Pia, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri January Makamba pamoja na Katibu Mkuu Ndugu Shelukindo na viongozi wote wa Wizara hii ya Mambo ya Nje kwa kazi kubwa wanayoifanya ili kuhakikisha azma ya Mheshimiwa Rais ya kuifungua Tanzania, kufungua uchumi wetu kwa kutumia diplomasia ya kiuchumi inafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii ya Mambo ya Nje jambo pekee ambalo ningependa kusisitiza na kuikumbusha Serikali ni kwamba suala zima la hadhi maalumu kwa diaspora wa Tanzania ni jambo ambalo kwanza tunaishukuru sana Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuridhia kwamba wenzetu diaspora wa Tanzania wapate hadhi maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati sasa umefika itamkwe rasmi hadhi maalumu itatolewa lini. Tumeshasikia kwamba itakuwa ni mwaka huu 2024 lakini lini bado hatujasikia. Vivyo hivyo ni vema Wizara hii ya Mambo ya Nje ikaweka wazi ni haki zipi ambazo diaspora wa Tanzania wataweza kupata, ni vitu gani ambavyo wanavihitaji wawe navyo ili waweze kujiandaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niendelee kusisitiza kwamba suala la ushiriki katika siasa, suala la ushiriki katika kupata ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama hilo ni jambo ambalo lazima libaki kwa ajili ya Watanzania na Watanzania pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitajielekeza katika eneo la pili la mchango wangu ambao utajikita kwenye eneo la masuala ya ulinzi na usalama. Kama ambavyo tunafahamu mapinduzi ya teknolojia yameleta mabadiliko makubwa kwenye namna ambavyo tunaendesha mambo yetu. Mapinduzi haya ya teknolojia yapo katika pande mbili, kuna pande ambayo ni ya mafanikio unaleta na unafungua fursa mbalimbali lakini kuna upande ambao ni changamoto ambao unaleta unaleta mambo hasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchukua fursa hii kuishauri sana Wizara yenye dhamana ya maswala ya ulinzi kwamba ni wakati sasa tujielekeze kuwekeza kwenye electronic warfare (EW) kwa sababu kadri teknolojia inavyokuwa ndivyo ambavyo watu wanatumia teknolojia kwa ajili ya kufanya vitendo vya kiuhalifu ambavyo vitahatarisha ulinzi na usalama wa Taifa letu, lakini pale ambapo tutawekeza katika electronic warfare (EW) ina maana tutawekeza fedha nyingi kwa Jeshi letu, ina maana Jeshi letu litaweza kuimarika na kupata mbinu za medani pamoja na mbinu za kivita zitakazoliwezesha Jeshi letu kukabiliana na athari zozote ama changamoto zozote, ama matukio yoyote ambayo yanaweza kupelekea kuhatarisha ulinzi na usalama wa Taifa letu kwa kutumia teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ningependa kupendekeza kwamba Serikali ifanye mapitio kwenye Sheria yetu ya Taifa ya Ulinzi ili kuona namna gani ambavyo tutaweza kuainisha na kujumuisha haya maeneo mapya ili kuhakikisha Serikali inatenga fedha za kutosha kwenye Jeshi letu ili tuweze kujilinda na athari mbalimbali kama ambavyo nimeshazitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuelezea na kurejea suala zima la athari ya kuendela kutegemea kuagiza mbegu za vyakula kutoka nje ya nchi. Hivi sasa takribani zaidi ya asilimia 60 ya mbegu ambazo tunatumia hapa nchi kuzalisha chakula zinatoka nje ya nchi. Hapa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa ambayo ameweka katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha sekta ya kilimo inapata bajeti kubwa, pia kwa kuweka kipaumbele kikubwa katika uzalishaji wa mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza pia sana TARI kwa kazi kubwa ambayo wanafanya ya kuzalisha mbegu, lakini kama tutaendelea kutegemea mbegu kwa asilimia zaidi ya asilimia 60 kutoka nje ya nchi tunaendelea kuliweka Taifa letu katika hatari, kwa sababu mfano mzuri ni mbegu za alizeti. Mbegu za alizeti tumekuwa tukitegemea Nchi ya Ukraine kwa kiwango kikubwa, wakati Ukraine inapitia vita sisi Tanzania tumepata athari kubwa ya kukosa upatikanaji wa mbegu za alizeti kama ambavyo tulikuwa tunapata awali. Nikienda mbali zaidi katika hizo takribani 60% ya mbegu ambazo tunategemea kutoka nje ya nchi, unakuta karibia 30% mpaka 40% ya mbegu hizo zinazalishwa na kuuzwa na kampuni kama nne tu kubwa duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa embu ona namna ambavyo kama Taifa tunaweka utegemezi wa mbegu zetu za chakula chetu, lishe yetu, afya yetu kula yetu kwenye takribani kampuni nne tu duniani. Pale ambapo kampuni hizi zinaweza zikatumiwa kutuhujumu na zile mbegu wakaacha kutuuzia au ghafla wakapandisha bei au chochote kile tunajiweka kama Taifa katika hali ya hatari kwa sababu chakula ni suala la ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa mara nyingine tena nirejee kuishauri Serikali waone namna ya kuliwezesha Jeshi letu hususani Jeshi la Kujenga Taifa – JKT ili iweze kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu kwenye mashamba yao. Jambo hili JKT wakiwezeshwa fedha za kutosha ina uwezo wa kuzalisha mbegu na nguvu kazi wanayo na hiyo itatuweka kama Taifa letu mahala salama zaidi ili kuondokana na huu utegemezi pia tutaokoa fedha ya kigeni ambayo hivi sasa inakwenda nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupitia mpango huo huo ambao utaelekezwa kwenye Jeshi letu la Kujenga Taifa, Jeshi linaweza likaanzisha mpango wa kulinda mbegu za asili, kwa maana ya kutengeneza mabenki mbalimbali katika mashamba hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la mwisho napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa amabyo ameweka ya kuimarisha upatikanaji wa haki hapa nchini. Kupitia jitihada hizo sasa tunaona kupitia taarifa ya Kamati kwamba idadi ya mahabusu sasa hivi imepungua kuliko idadi ya wafungwa. Hili ni jambo kubwa sana na ni mageuzi makubwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara yenye dhamana ya masuala ya Magereza ikiwemo ni Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na Jeshi la Magereza wenyewe kwa kazi kubwa ambayo wamefanya katika kufanikisha hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa Jeshi la Magereza limepunguza mzigo wake kwa maana idadi ya mahabusu imekuwa ni chini kutoka idadi ya wafungwa. Basi naamini pia Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Wizara husika wataona ni namna gani sasa wataimarisha lishe ambayo wafungwa wanapata ikiwemo wale wafungwa ambao ni wafungwa wanaishi kwa virusi vya UKIMWI, kwa sababu hata Sheria inatambua ya kwamba lazima wapate lishe iliyo tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo kwa kuwa sasa gharama ya kulisha mahabusu imepungua, naamini kabisaa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wataweza sasa kuweka mpango thabiti ambao utawezesha wanawake wenzetu ambao wapo magereza wanapokuwa kwenye hedhi waweze kupata taulo za kike ili wapate kujistiri kwa kuzingatia afya na usalama wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mimi naendelea kuipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa sana inayofanya kwenye maeneo haya, naipongeza sana Kamati chini ya Mwenyekiti Baba yangu Mheshimiwa Vita Kawawa kwa kazi kubwa ambayo ameifanya, naunga mkono hoja ya Kamati hii na kazi iendelee. (Makofi)